Posts

Showing posts from December, 2014

Vitabu vya Kukumbukwa Nilivyosoma Mwaka 2014

Leo, siku ya mwisho ya mwaka 2014, napenda kujikumbusha vitabu nilivyosoma mwaka huu ambavyo nitavikumbuka kwa namna ya pekee. Sitavitaja vitabu tulivyovisoma darasani. Kwanza, napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushuhudia mwaka 2014 ukiisha, huku zikiwa zimebaki saa nne tu hadi kuanza kwa mwaka 2015. Ingawa huu umekuwa mwaka mgumu kwangu kuliko miaka yote ya maisha yangu kwa sababu ya kuugua, nashukuru nimefikia hapa nilipo, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, huduma za madaktari, wauguzi na familia yangu, na maombi ya ndugu na marafiki. Kutokana na hali yangu hiyo, sikuweza kusoma kama ilivyo mazoea yangu. Hata hivi, kila nilipojisikia nafuu, nilishika kitabu na kusoma, hata nilipokuwa nimelazwa hospitalini. Vitabu ni moja ya vitulizo vyangu, na madaktari na wauguzi walitambua jambo hilo. Nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Abbott Northwestern, mjini Minneapolis, nilikwenda na kitabu cha mashairi ya Robert Frost kiitwacho Robert Frost: Selected Poems , ambacho binti yangu

Benki ya Mkombozi na Mabilioni Kubebwa Katika Viroba, Magunia, na Mifuko ya Rambo

CHANZO: MKOMBOZI COMMERCIAL BANK Taarifa Kwa Umma Kuhusu Akaunti Ya VIP Engineering And Marketing Iliyopo Katika Benki Ya Biashara Ya Mkombozi Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP) Kampuni ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa akaunti husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo. Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho la kampuni kumruhusu moja kati ya wanahisa wake ku

"As You Like It:" Kitabu cha Kumalizia Mwaka

Image
Nimeanza kusoma As You Like It , moja ya tamthilia za Shakespeare. Ni wazi kuwa, nikizingatia kwamba leo ni tarehe 28 Desemba, hiki kitakuwa kitabu cha kumalizia mwaka. Kama zilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, As You Like It ni hazina kubwa ya mafundisho kuhusu mahusiano baina ya wanadamu na kuhusu maisha kwa ujumla. Tamthilia yoyote ya gwiji huyu, sawa na mashairi yake, ni hazina ya lugha ya ki-Ingereza. Ningefurahi kama ningekuwa nimesoma angalau kitabu kimoja kwa kila wiki. Padre Lambert Doerr, OSB, mwalimu wetu wa ki-ingereza tulipokuwa tunasoma seminari ya Likonde, ambaye sasa ni abate askofu mstaafu, alitushinikiza kusoma angalau kitabu kimoja kwa wiki. Kila mmoja wetu alipewa daftari ambamo alitakiwa kuorodhesha vitabu alivyosoma, na alitegemewa kuweza kutoa maelezo mafupi kuhusu kila kitabu. Ningefurahi kama ningeweza kuendeleza jadi hii miaka yote. Nirudi tena kwenye As You Like It . Simulizi inapoanza, tunamsikia Orlando akilalamika kuwa amedhulumiwa na kaka yake

Kitabu Changu Katika Jalada Gumu

Image
Leo nimepata nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kikiwa katika jalada gumu ("hard cover"). Wiki iliyopita, kwa kutumia tekinolojia ya uchapishaji vitabu mtandaoni, niliuchapisha upya mswada wa kitabu changu, ili kitabu kipatikane pia katika jalada gumu. Nilipomaliza tu kuchapisha, niliagiza nakala, ambayo nimepata leo. Ni nakala ya kwanza kabisa, nami nimeridhika nayo. Ni jambo la kawaida, huku ughaibuni, kwa kitabu kupatikana katika jalada jepesi ("paperback") na pia katika jalada gumu. Kuna vitabu vingine ambavyo hupatikana katika jalada jepesi tu, au katika jalada gumu tu. Ninaamini, tangu zamani, ingawa sijafanya utafiti, kwamba maktaba ndizo zinazohitaji sana vitabu hivi vyenye jalada gumu, kwani vinaweza kuhimili vizuri zaidi misukosuko ya kuazimwa azimwa na wasomaji. Lakini kuna pia watu binafsi wanaopenda vitabu vya aina hiyo, hata kama nakala zenye jalada jepesi ziko pia. Mimi mwenyewe nina vitabu vingi

Maana ya Krismasi Inavyopotoshwa

Kimsingi, Krismasi ni siku ambayo sisi wa-Kristu tunakumbuka kwa namna ya pekee kuzaliwa kwa Yesu. Au labda niseme, ni siku ambayo wa-Kristu tunategemewa kukumbuka kwa namna ya pekee kuzaliwa kwa Yesu. Ni siku muhimu katika dini yetu, nasi tunategemewa kuwa tumejiandaa kiroho kwa kumpokea Yesu. Ni siku ambapo tunakumbushwa kuhusu utukufu wa Mungu, uokovu wetu, na amani duniani. Wanataaluma tuna mazoea ya kutafiti mambo, na tunajua kuwa Krismasi ina historia ndefu, na sio vipengele vyake vyote vinatokana au kuhusiana na dini ya u-Kristu. Lakini ninachozingatia hapa ni kuwa, pamoja na hiyo historia ndefu, Krismasi kama tunavyoijua leo, ni siku takatifu, ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu, siku ambayo wa-Kristu tunapaswa kuizingatia kwa misingi hiyo. Lakini, kwa hali ilivyo, mtazamo huu wa kuiona Krismasi kama siku takatifu unazidi kupungua, na wengi wameshasau jambo hilo. Badala yake, maana ya Krismasi inapotoshwa. Badala ya kuzingatia kuwa maandalizi ya Krismasi ni ya kiroho, watu tunaj

Mkutano na Wanachuo wa Gustavus Adolphus Unakaribia

Image
Siku zinakwenda haraka. Tarehe 5 Januari, ambayo imekaribia, ndio siku nitakayokutana na wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus, kama nilivyoandika hapa . Hao ni wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya Tanzania, kujiongezea elimu kuhusu masuala ya afya na matibabu katika mazingira tofauti na ya Marekani, hasa kwa upande wa utamaduni. Profesa wao aliniomba nikaongee nao kuhusu masuala ya aina hiyo kwa mapana kufuatia yale niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho watakuwa wamekisoma kabla ya mimi kukutana nao. Kutokana na kusoma hiki kitabu, wanachuo hao watakuwa wameandaa masuali. Kama ilivyotokea siku zilizopita, masuali mengine yatazuka hapo hapo. Jukumu hili linanifanya nikipitie tena kitabu changu, angalau kijuujuu, kwani sina mazoea ya kusoma sana yale ambayo nimeshayaandika na kuyachapisha. Napendelea kutumia muda wangu na akili yangu katika kutafiti, kutafakari na kuandika mambo mapya. Ingawa yale yaliyomo kitabuni sija

Kitabu Kingine: "A Goal is a Dream With a Deadline"

Image
Usiku wa kuamkia leo, nimemaliza kusoma kitabu kiitwacho A Goal is a Dream With a Deadline , ambacho nilikinunua siku za karibuni. Mwandishi wake, Leo B. Helzel, amekusanya kauli za watu mbali mbali wenye ujuzi na uzoefu, ili kuwaelimisha wajasiriamali, mameneja, na watu werevu kwa ujumla, wenye mitazamo ya kimaendeleo. Kitabu hiki ni tofauti na vingine kwani ni mkusanyo wa misemo ya busara kuhusu mambo kama kujiwekea malengo, kustahimili matatizo, kutafuta masoko au wateja, kujiwekea maamuzi na kuyatekeleza kwa dhati na bila kuchelewa, kuwasikiliza wateja kwa makini na kuwahudumia vizuri, kuzingatia ubunifu, kupunguza urasimu, na kujiamini. Hayo ni baadhi ya yaliyomo katika kitabu hiki. Sura zote za kitabu hiki zina mambo muhimu. Kwa vile mimi ninashughulika na kutoa ushauri kwa jumuia, taasisi, makampuni, na watu binafsi kuhusu tofauti za tamaduni na athari zake, nimevutiwa sana na sura ya kitabu hiki iitwayo "Going Global." Baadhi ya mawaidha yaliyomo katika sura hii

Kitabu Sasa Kinapatikana Katika "Kindle"

Image
Baada ya kujaribu jaribu, jana nimefanikiwa kukichapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differeces katika "Kindle." Yeyote, sehemu mbali mbali za dunia, mwenye kifaa cha kuingizia na kusomea vitabu pepe anaweza kukipata mtandaoni, kwenye duka la Amazon Kindle . Kwa miezi mingi nilikuwa nawazia kukiweka kitabu hicho katika Kindle, lakini sikujituma vya kutosha na kufanya kazi hiyo. Wiki hii, nilipania kuitekeleza, na nimefanikiwa. Katika kuhangaika kwangu, nimejifunza mambo ya ziada kuhusu tekinolojia hii, ambayo nilianza kujifunza kwa vitendo wakati nilipochapisha kitabu hiki hiki katika lulu.com. Kuna sababu zilizonifanya niingie huko Kindle. Kwanza, ninafahamu kuwa kadiri tekinolojia inavyosonga mbele na kuenea, shughuli nyingi zinahamia mtandaoni, kuanzia elimu, biashara na mawasiliano ya aina mbali mbali. Nami najaribu kwenda na wakati. Vile vile, ninalikumbuka tukio lililonitokea siku moja katika tamasha la vitabu la Twin Cities, mjini St. P

Mwaliko Mwingine

Leo nimepata mwaliko mwingine wa kwenda kuzungumza na wanachuo wa chuo cha South Central ambao wanajiandaa kwa safari ya masomo Afrika Kusini. Mwaliko umetoka kwa mwalimu wao, Becky Djelland Davis. Hii ni mara pili yeye kunialika. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka jana, naye baadaye aliandika kuhusu mazungumzo yale katika blogu yake . Nami nimeguswa kwa namna alivyoniandikia leo: I will be taking students to South Africa again in May. This coming semester, we will again be reading your book Africans and Americans . I hope that perhaps you can talk with my students again? They loved you last time! Huu ni mwaliko wa tatu kwa siku za hivi karibuni, na yote inangojea utekelezaji katika miezi michache ijayo. Wa kwanza niliuelezea hapa , na wa pili hapa . Mialiko hii ninayopata sio jambo jepesi au la mteremko. Inahitaji tafakari katika kujiandaa ili nitoe mawazo na mitazamo ya kiwango kinachokidhi mahitaji ya hao wanaonialika, na bora zaidi ni kufanya vizuri kuliko wanavyotegemea. H

Zawadi ya Vitabu

Image
Nimeona picha hii hapa kushoto katika Mjengwablog . Maggid Mjengwa (kulia) anaonekana akikabidhi vitabu kwa mzee wa kijiji cha Mahango, Madibira, kwa ajili ya maktaba ya kijiji. Nimeguswa na taarifa hii, kwani vitabu ni sehemu muhimu ya maisha yangu. Hii sio tu kwa kuwa mimi ni mwandishi na mwalimu, bali pia kwa kuwa nathamini sana kitendo cha kupeleka vitabu popote vinapohitajika. Kwa mtazamo wangu, kitabu cha maana kina thamani isiyopimika. Nikipata fursa ya kuchagua kati ya kitabu cha aina hiyo na kreti ya bia, nitachagua kitabu, kwa furaha kabisa. Mimi mwenyewe hupeleka vitabu Tanzania. Nimeshapeleka kwenye maktaba mbali mbali, zikiwemo za Mbinga, vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Makumira, na Tumaini,  na pia kwa watu binafsi. Kuna wakati niliwahamasisha wanadiaspora wanachama wa jumuia ya mtandaoni ya Tanzanet wakachangia dola 500 kuendeleza jukumu hilo. Mbali na hilo, kila ninapokwenda Tanzania, kwa kadiri ya uwezo wangu, nabeba vitabu kwa madhumuni hayo. Siandiki makala hii

Sitafundisha Mwezi Januari, 2015

Awali, kwa ratiba iliyopangwa, nilitarajiwa kufundisha mwezi Januari, kozi iitwayo "The Hero and the Trickster." Hiyo ni kozi ambayo nimefundisha karibu kila mwaka, mwezi Januari. Tuna utaratibu, katika chuo hiki cha St. Olaf kuwa na kozi za mwezi Januari ambazo zinaitwa "interim." Kozi yangu ya "Hemingway in East Africa" ambayo nilifundishia Tanzania, ilikuwa ya aina hiyo. Pamoja na kwamba ilipangwa kwamba Januari ijayo nifundishe, hivi karibuni, viongozi wa chuo wameonelea nisifundishe bali nipumzike, ili niendelee kupona vizuri. Kwa hali yangu ilivyo, nina hakika ningeweza kufundisha, lakini uongozi wa chuo umeamua kunipa hii likizo ambayo sikuitegemea. Ninashukuru sana. Ninaona ni mipango ya Mungu, kwani kwa miezi niliyokuwa na hali mbaya kiafya, hadi nikashidwa kufanya kazi nilizozizoea, nilikuwa katika majaribu makubwa. Kutoweza kufundisha, kufanya utafiti, kuandika au kurekebisha makala za kitaaluma ulikuwa ni mtihani mkubwa kisaikolojia. Kw

Uhuru wa Tanganyika na Ukoloni Mamboleo

Image
Siku hii ya leo, ambayo ni ya kumbukumbu ya siku ambapo Tanganyika ilijipatia Uhuru, nilitaka kuandika makala, "Uhuru wa Tanganyika na Ukoloni Mamboleo." Nilianzza kuandika, lakini nilijikuta naandika insha ndefu, sio makala fupi ambayo nadhani inatakiwa katika blogu. Kutokana na jambo hilo, nimeifuta ile makala na badala yake nimeandika kwa ufupi mambo yafuatavyo. Uhuru tulipata tarehe 9 Desemba, 1961. Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, na ninakumbuka msisimko, hata kule kijijini kwangu. Waalimu wetu, Charles Kinunda, John Pantaleon Mbonde, na Alois Turuka, walikuwa chanzo kikubwa cha ufahamu wetu wa mambo yaliyokuwa yanatokea. Kati ya kumbukumbu ambazo haziwezi kutoweka akilini mwangu ni picha ya askari Alexander Nyirenda akiweka mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro. Sambamba na tukio hili la kihistoria ni hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, ambamo alisema: Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ul

Vitabu Nilivyonunua Juzi

Image
Juzi, Jumamosi,  nilienda Minneapolis, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation , ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la Half Price Books, ambalo nimeliongelea mara kadhaa katika blogu hii . Ingawa ilikuwa jioni sana,  watu walikuwa wengi humo dukani: watu wazima, vijana, na watoto. Nami nilijichanganya nao, nikaangalia angalia sehemu zenye vitabu vya fasihi. Nilinunua vitabu vinne, ambavyo nitavielezea leo. Lakini kabla ya kuelezea vitabu hivi, napenda kujikumbusha kitu kimoja kilichonigusa, wakati nimesimama katika foleni ya kulipia vitabu. Mbele yangu walikuwepo baba na mama na watoto wadogo wawili wasichana. Walikuwa wameshaweka vitabu vyao kwenye kaunta ya kulipia, huku wakiwaelezea wale watoto jinsi watakavyowasomea vitabu. Kati ya vile vitabu kwenye kaunta, niliviona viwili vikubwa vikubwa vya Harry Potter . Muda wote wale watoto walikuwa na furaha na msisimko. Kwa mara nyingine tena, nilishuhudia jinsi wen

Mapitio ya Kitabu

Image
Kama mwandishi, huwa nina hamu ya kujua maoni ya wasomaji kuhusu vitabu vyangu. Nawashukuru kwa lolote wanalosema baada ya kusoma na kutafakari yaliyomo kitabuni. Kama kitabu kimewaridhisha au kuwafurahisha, nami nafurahi. Wakiona dosari wakazibainisha, nitawashukuru kwa kunielimisha. Leo nimeona mtandaoni kuwa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , kimefanyiwa mapitio katika "The Zumbro Current," jarida la kanisa la ki-Luteri la Zumbro , lililopo kusini mashariki mwa Minnesota, Marekani: Book Review Africans and Americans: Embracing Cultural Differences The Abner Haugen Library at Zumbro Lutheran Church has a copy of this extremely helpful book on cultural differences between Americans and Africans. It is written by Joseph L. Mbele, a Tanzanian scholar who currently is a professor of English at St. Olaf College. Anyone traveling to another country or continent would find this short book well worth reading. A few of the topics covered are

Kitabu cha "Siasa Hapo Kale"

Image
Ninasoma Siasa Hapo Kale , kitabu ambacho nilikifahamu na kukipenda tangu nilipokuwa nasoma shule ya msingi kule nyumbani kwangu Litembo , katika mkoa wa Ruvuma. Mtunzi wa kitabu hiki ni Lucius Mabasha Thonya. Kama sikosei, nilikuwa na nakala ya kitabu hiki miaka ile kijijini kwangu. Ingawa sijui kilienda wapi, mara moja moja nimekikumbuka, hasa kwa vile mimi ni mtafiti katika fasihi simulizi. Hilo ni jambo moja katika utangulizi wa makala ya leo. Jambo jingine ni kuwa kwa miaka kadhaa, nimevutiwa na juhudi za Dada Yasinta katika kudumisha lugha ya ki-Ngoni kwa kuanzisha na kuendesha blogu ya Vangoni . Ingawa ki-Ngoni sio lugha yangu, ninaielewa kiasi fulani nikiisikia au kuisoma, kwa vile inakaribiana na lugha yangu ya ki-Matengo. Katika kusoma blogu ya Vangoni , nilipata wazo la kumwambia Dada Yasinta kuhusu kitabu hiki cha Siasa Hapo Kale . Hatimaye, nilimpelekea ujumbe, nikijua kuwa atapenda kusikia habari zake, na ndivyo ilivyokuwa. Kupitia maktaba ya hapa chuoni ninapofundish

Wazo la Kutafsiri Kitabu

Image
Kwa wiki kadhaa, nimekuwa nikiwazia kutafsiri kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii . Siku chache zilizopita, niliandika kuhusu kitabu hiki katika blogu hii . Nawazia kuzirekebisha insha zilizomo, na kuchapisha kitabu cha ki-Ingereza. Kufanya hivyo kutakipa kitabu hadhira kubwa zaidi kuliko ile ya wajuao ki-Swahili. Nina hakika, kwa mfano, kuwa wa-Marekani watakitafuta na kukisoma. Kwa ujumla wasomaji wa vitabu vyangu ni wa-Marekani. Ninaposhiriki matamasha hapa Marekani, watu kadha wa kadha huja kwenye meza yangu na kuangalia vitabu, kuvinunua, au tu kuongea nami. Wako wanaoniuliza kama nimechapisha kitabu kingine, kwani vile vilivyopo mezani, vya ki-Ingereza, wanavyo au wamevisoma. Kauli hizi hata binti zangu, ambao hushirikiana nami, wamezisikia tena na tena. Kwa miaka kadhaa, sijachapisha kitabu kipya. Sababu kubwa ni kuwa kuandika kitabu huchukua muda. Yaweza kuwa miezi au miaka. Kwa mfano, ilichukua miaka 23 hivi kuandaa kitabu cha Matengo Folktales . Vile vile, muda mwing

Nilivyohojiwa Katika Kombolela Show Kuhusu Utamaduni

Siku kadhaa zilizopita, nilileta mahojiano niliyofanyiwa na Radio Butiama . Hapa naleta mahojiano niliyofanyiwa katika Kombolela Show miaka michache baadaye: https://archive.org/details/KombolelaShowOctober22010