Kitabu Kingine: "A Goal is a Dream With a Deadline"

Usiku wa kuamkia leo, nimemaliza kusoma kitabu kiitwacho A Goal is a Dream With a Deadline, ambacho nilikinunua siku za karibuni. Mwandishi wake, Leo B. Helzel, amekusanya kauli za watu mbali mbali wenye ujuzi na uzoefu, ili kuwaelimisha wajasiriamali, mameneja, na watu werevu kwa ujumla, wenye mitazamo ya kimaendeleo.

Kitabu hiki ni tofauti na vingine kwani ni mkusanyo wa misemo ya busara kuhusu mambo kama kujiwekea malengo, kustahimili matatizo, kutafuta masoko au wateja, kujiwekea maamuzi na kuyatekeleza kwa dhati na bila kuchelewa, kuwasikiliza wateja kwa makini na kuwahudumia vizuri, kuzingatia ubunifu, kupunguza urasimu, na kujiamini. Hayo ni baadhi ya yaliyomo katika kitabu hiki.

Sura zote za kitabu hiki zina mambo muhimu. Kwa vile mimi ninashughulika na kutoa ushauri kwa jumuia, taasisi, makampuni, na watu binafsi kuhusu tofauti za tamaduni na athari zake, nimevutiwa sana na sura ya kitabu hiki iitwayo "Going Global." Baadhi ya mawaidha yaliyomo katika sura hii ni haya: "Never assume that business is conducted in a foreign country just as it is at home" (uk. 146), "Learn about your host's people by reading about their history and culture" (uk. 147), " "Always assume that time will be handled differently in a foreign country" (uk. 147), "Latin Americans may refuse to do business with you if you are too serious. So lighten up and slow down" (uk. 151), "In Asia, learn when "maybe" really means "no" (uk. 151).

Mawaidha haya yanafanana na yale ninayotoa na kuyafafanua katika mihadhara na warsha zangu. Yamo katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na pia mara moja moja katika blogu hii.

Nimejifunza mambo kadhaa muhimu katika kusoma A Goal is a Dream With a Deadline, na nakipendekeza kwa yeyote anayetaka mabadiliko yenye manufaa katika fikra, shughuli, maisha yake na ya jamii.

Comments

Mfuko said…
Shikamoo Prof Mbele nimevutiwa na simulizi fupi juu ya yaliyomo kwenye kitabu hiki cha mwandishi Leo, kama una utamaduni wa kutoa zawadi kitabu ningependekeza kwangu zawadi ya kitabu hiki A Goal is a Dream with a Deadline natanguliza shukrani na pia nakutakia afya njema unapoendelea kurudisha nguvu baada ya maumivu Asante
Mbele said…
Ndugu Mfuko,

Shukrani kwa ujumbe wako. Nafurahi kwamba una hamu ya kitabu hiki. Ndio lengo langu, kwamba nikiona kitu kiachoweza kuwafaa wengine, huwa sifichi bali nasema hadharani.

Kuhusu ombi lako, inabidi tuwasiliane zaidi. Kwa mfano, ningependa kujua uko wapi katika dunia hii. Anwani yangu ni africonexion@gmail.com.

Kila la heri kwa msimu huu wa Krismasi na Mwaka Mpya.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini