Zawadi ya Vitabu

Nimeona picha hii hapa kushoto katika Mjengwablog. Maggid Mjengwa (kulia) anaonekana akikabidhi vitabu kwa mzee wa kijiji cha Mahango, Madibira, kwa ajili ya maktaba ya kijiji.

Nimeguswa na taarifa hii, kwani vitabu ni sehemu muhimu ya maisha yangu. Hii sio tu kwa kuwa mimi ni mwandishi na mwalimu, bali pia kwa kuwa nathamini sana kitendo cha kupeleka vitabu popote vinapohitajika.

Kwa mtazamo wangu, kitabu cha maana kina thamani isiyopimika. Nikipata fursa ya kuchagua kati ya kitabu cha aina hiyo na kreti ya bia, nitachagua kitabu, kwa furaha kabisa.

Mimi mwenyewe hupeleka vitabu Tanzania. Nimeshapeleka kwenye maktaba mbali mbali, zikiwemo za Mbinga, vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Makumira, na Tumaini,  na pia kwa watu binafsi. Kuna wakati niliwahamasisha wanadiaspora wanachama wa jumuia ya mtandaoni ya Tanzanet wakachangia dola 500 kuendeleza jukumu hilo. Mbali na hilo, kila ninapokwenda Tanzania, kwa kadiri ya uwezo wangu, nabeba vitabu kwa madhumuni hayo.

Siandiki makala hii kwa kuwa tu nimeona hii taarifa katika Mjengwablog. Wazo la vitabu kama zawadi nimekuwa nalo kwa muda mrefu. Niliwahi kuongelea jambo hili katika blogu hii. Mimi mwenyewe hufurahi nikipewa kitabu, kama nilivyoandika hapa, na hapa.

Kama ambavyo ninasema mara kwa mara katika blogu hii, ninapenda kununua vitabu. Sio kwamba nina pesa sana, bali ni kutokana na kuviona vitabu kuwa ni muhimu zaidi ya mambo mengi ambayo wengine wanayathamini zaidi. Kwa mfano, kama wewe ni mnywaji wa bia, ukiachana na bia, utagundua kuwa kumbe hela unazo. Ninasema hivyo kutokana na uzoefu wangu.

Nikirudi tena kwenye hii taarifa ya Mjengwablog, napenda kusema kuwa ni jambo jema sana kuanzisha na kuboresha maktaba vijijini. Ingetakiwa katika nchi yetu tuwe na mwamko wa namna hiyo. Kuna wageni ambao wanajitahidi kupeleka huduma ya vitabu vijijini. Mifano ni shirika la TETEA na Friends of African Village Libraries. Ingetakiwa sisi wenye nchi yetu tuwe mstari wa mbele katika kutimiza majukumu hayo, badala ya kuwaachia au kuwaangalia tu wageni wakifanya hivyo.

Kwa miaka mingi kidogo, nimewazia kuanzisha maktaba kijijini kwangu, lakini bado sijafanya hivyo. Kitu kimoja kinachonisukuma ni kuona jinsi wanakijiji wanavyotumia muda wao mwingi kwenye kilabu cha pombe. Papo hapo, kuna shule kadhaa jirani na kijiji, zikiwemo shule za sekondari, ambazo zingefaidika na kuwepo kwa maktaba kijijini. Wazo hili sio lazima alitekeleze mtu mmoja. Ni wajibu kwetu wote tunaotambua umuhimu wa vitabu.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini