Suluhu ya Maandamano
Ni muhimu kila mtu awe huru kutoa mawazo yake, kuliko kunyamazishwa. Wanataaluma katika saikolojia wanatufundisha kuwa ukandamizaji au unyamazishaji, kwa maana ya "repression," una madhara makubwa. Sigmund Freud, Carl Jung, na wafuasi wao ni kati ya wanataaluma hao. Watu wakiwa huru kujieleza, wanapata ahueni kisaikolojia, na hii ni muhimu kwa afya ya mtu binafsi na kwa afya ya jamii. Kuhusu madhara ya "repression," hata wahenga walitahadharisha, waliposema "kimya kingi kina mshindo mkuu." Wakati huu, wa-Tanzania wanapita katika kipindi kigumu sana, kutokana na mvutano uliozuka baina ya wapinzani wanaotaka kufanya maandamano nchi nzima kupinga kile wanachoita udikteta, na papo hapo, polisi, serikali, na baadhi ya raia hawataki maandamano haya yafanyike. Wengine wamesema watafanya maandamano yao ili kuyapinga yale mengine. Ninaona hili si suala gumu. Wote wanaotaka kuandamana wapewe fursa ya kufanya hivyo, ili mradi wahakikishe kuwa maandamano yao n