Nimempata Msomaji na Mpiga Debe Mpya

Siku chache zilizopita nimefahamiana na mama mmoja mzee m-Marekani ambaye amekuja kuishi hapa mjini Northfield. Ilikuwa bahati tu kuwa tulisalimiana na tukaongea nakuanza kufahamiana. Katika maongezi na kutambulishana, tuligundua kuwa kazi ambayo tumeipenda maishani ni ya ualimu. Yeye amestaafu ila mimi ninaendelea kufundisha katika Chuo cha St. Olaf.

Katika kuongea zaidi, tuligundua kwamba mitazamo yetu kuhusu elimu, ufundishaji, na mahitaji ya wanafunzi, hasa wenye matatizo inafanana. Tangu hapo tumekuwa tunangea kila siku, kwani tunazidi kugundua jinsi tunavyopenda ualimu na tunavyopenda kuwalea wanafunzi kitaaluma na kimaadili.

Katika maongezi yetu hayo, suala la mimi kama mwandishi lilijitokeza. Nilimtajia vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales, akavinunua hima. Tangu alipovipata, alianza kusoma Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na kila tunapokutana amekuwa akinielezea mambo anayojifunza humo, na jinsi yanavyofanana na utamaduni wa Wa-Marekani wa Asili ("Native Americans"). Papo hapo amekuwa akinieleza anavyofananisha tamaduni hizi na utamaduni wa wa-Marekani wazungu.
Huyu mama amenishangaza kwa jinsi anavyolichukulia suala hili kwa dhati. Anasoma kitabu changu kwa makini sawa na mwanafunzi anayejiandaa kwa mtihani. Katika nakala yake, amechora mistari chini ya sentensi na vifungu vingi karibu katika kila ukurasa. Vifungu vingine amevizungushia mduara kwa msisitizo. Kurasa karibu zote amezipamba namna hiyo.

Zaidi ya hayo, amekuwa akiandika katika karatasi tofauti dondoo mbali mbali za kufananisha au kupambanua vipengele vya utamaduni wa wa-Afrika, wa-Marekani wa Asili, na Wamarekani Wazungu. Leo amenipa karatasi tatu alizoandika, ambazo nimezipiga picha zinazoonekana hapa.

Pamoja na juhudi yake hiyo ya kutafakari yaliyomo na yatokanayo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, mama huyu amekuwa akinunua nakala za kuwapelekea ndugu na marafiki zake. Ingawa Krismasi bado iko mbali, ameshaniambia kuwa atahitaji kununua vitabu hivi kama zawadi za sikukuu. Hapo amenikumbusha makala niliyowahi kuhusu utamaduni wa kununua vitabu kama zawadi ya sikukuu. Ni utamaduni uliojengeka hapa Marekani.

Nimeona niandike habari hii kuhusu mdau wa vitabu vyangu, kama ilivyo desturi katika blogu hii. Kwa kuwa mdau huyu mpya anafuatilia habari zangu katika Facebook and blogu yangu ya ki-Ingereza, ninapangia kumwomba tupige picha ili wadau wangu wengine wapate kumwona mtandaoni.


Comments

Popular posts from this blog

Tenzi Tatu za Kale

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania