Posts

Showing posts from October, 2018

Nimepeleka Vitabu kwa wa-Matengo

Image
Mwezi Julai mwaka huu nilikwenda Tanzania, nikiwa nimechukua vitabu vingi. Baadhi ni vile nilivyoandika mwenyewe, ambavyo niliviwasilisha katika maduka ya Kimahama, na A Novel Idea. Nilichukua pia nakala 16 za Matengo Folktales kwa ajili ya kuzipeleka kwa wa-Matengo, wilayani Mbinga, katika mkoa wa Ruvuma. Ninasema hivyo, na kutaja kabila langu, nikijua kwamba kwetu wa-Tanzania, hii ni kauli tata, isiyopendeza, kwani inaashiria upendeleo au ubaguzi kwa msingi wa kabila. Utamaduni wa Tanzania, uliojengwa na chama cha TANU, hauafiki ubaguzi wa makabila au wa aina nyingine. Sasa kwa nini nimetoa kauli hiyo? Kwa nini niliamua kupeleka nakala hizi za Matengo Folktales kwa wa-Matengo? Napenda kuthibitisha kwamba nilifanya jambo muafaka. Matengo Folktales ni mkusanyo wa hadithi za jadi ambazo nilizirekodi nyumbani u-Matengo miaka ya sabini na kitu. Nilizirekodi katika kaseti, kisha nikachagua hadithi kumi na kuzitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliandika uchambuzi wa kila hadithi na nika

Minnesota Black Authors Expo Imekaribia

Image
Bado siku sita tu hadi maonesho yaitwayo Minnesota Black Authors Expo yatakapofanyika. Hii ni mara ya pili kwa maonesho haya kufanyika. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana. Waandaaji waliniomba niwemo katika jopo la waandishi watakaoongelea masuala mbali mbali ya uandishi wa vitabu. Nilikubali. Jopo linategemewa kuwa kivutio kikubwa katika tamasha hilo.

Waandishi Marafiki Tumekutana

Image
Tarehe 13 mwezi huu, nilishiriki tamasha la vitabu liitwalo Deep Valley Book Festival mjini Mankato, jimbo hili la Minnesota. Nilishahudhuria mara tatu tamasha hili linalofanyika mara moja kwa mwaka. Nilijua kuwa mmoja wa waandishi ambao walikuwa mbioni kushiriki ni rafiki yangu Becky Fjelland Brooks anayeonekana pichani kushoto. Becky ni mwalimu katika South Central College hapa Minnesota. Tulianza kufahamiana wakati yeye na Profesa Scott Fee wa Minnesota State University Mankato waliponialika kwenda kuongea na wanafunzi waliokuwa wanawaandaa kwa safari ya masomo Afrika Kusini. Watu wengi walihudhuria mhadhara wangu kuhusu tofauti za tamaduni, na nakala nyingi za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences zilinunuliwa. Baada ya hapo, nimepata mialiko ya kwenda kuongea na wanafunzi hao kila mara wanapoandaliwa safari ya Afrika Kusini. Mwalimu Becky ni mmoja wa wale wa-Marekani ambao wanaipenda Afrika na wanajibidisha kuwaelimisha wenzao kuhusu Afri

Kitabu Bado Kiko Dukani Barnes and Noble

Image
Juzi nilienda Apple Valley na Burnsville kuangalia maduka ya vitabu, kama nilivyoandika katika blogu hii. Kule Burnsvile, mji jirani na Apple Valley, nilitaka kuingia katika duka la Barnes and Noble ambamo kitabu changu kilikuwa kimewekwa sehemu maalum ya vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Sikujua kama ningekikuta, kwani sijui utaratibu wanaofuata katika kuvionesha vitabu hivyo sehemu hiyo. Nilidhani labda vinawekwa kwenye kabati hili kwa wiki moja hivi. Nilishangaa kukiona kitabu changu bado kipo, na kimewekwa juu zaidi ya pale kilipokuwepo kabla. Hapa kushoto ni picha niliyopiga wiki iliyopita, na kulia ni picha niliyopiga juzi. Ninafarijika na kufurahi kukiona hapa. Ninasubiri siku ya kwenda kukiongelea, kama nilivyodokeza.

Vitabu Nilivyonunua Leo

Image
Leo niliamua kutembelea maduka ya vitabu kwenye miji ya Apple Valley na Burrnsville hapa Minnesota. Apple Valley, kwenye duka la Half Price Books,   nilinunua vitabu vitatu bila kutegemea. Nilipita sehemu ya vitabu vya Hemingway, ambapo sikuona kitabu kigeni kwangu. Nilienda sehemu ya bei nafuu, nikanunua vitabu vitatu. Kimoja ni Essays and Poems cha Ralph Waldo Emerson, kilichohaririwa na Tony Tanner. Kwa miaka mingi nimefahamu jina la Emerson. Nilifahamu kuhusu insha yake "Self Reliance," ingawa sikuwa nimewahi kuisoma. Nilifahamu pia kuwa ameathiri sana falsafa na uandishi, sio tu Marekani, bali kwingineko. Kwa hali hiyo, sikusita kununua kitabu hiki, hasa baada ya kuona kuwa kina mashairi ya Emerson. Sikujua kuwa alitunga mashairi. Kitabu kingine nilichonunua ni Collected Poems cha Edna St. Vincent Millay. Huyu ni mwandishi ambaye sidhani kama niliwahi kusikia hata jina lake. Lakini nilipoona hiki kitabu kikubwa sana chenye kurasa 757 na nyongeza ya kurasa 32, na h

Nimeshiriki Tamasha la Vitabu la Deep Valley

Image
Leo nilienda Mankato, Minnesota, kushiriki tamasha la vitabu liitwalo Deep Valley Book Festival. Hii ilikuwa mara yangu ya nne kushiriki tamasha hilo. Ilikuwa fursa ya kuongea na watu kwa undani kuhusu mambo mbali mbali. Kuna watu kadhaa ambao nawakumbuka zaidi. Mmoja aliniambia kuwa ana binti yake ambaye anafundisha ki-Ingereza kama lugha ya kigeni. Hapa Marekani somo hilo linajulikana kama English as a Foreign Language. Hufundishwa kwa wahamiaji ambao wanahijtaji kujia lugha hiyo, ambayo ndio lugha rasmi ya hapa Marekani. Nilichangia mada hiyo kwa kuelezea jinsi sgughuli ya kufundisha ESL inavyofungamana na suala la tamaduni. Hufundishi tu muuno, sarufi, istilahi, bali pia utamaduni wa mazungumzo. Mama mmoja mzee, mwandishi, ambaye meza yake ilikuwa mbele yangu, alifika kunisalimia na kuongea. Nilimwuliza ameandika kuhusu nini, akaniambia kitabu chake kinahusu changamoto aliyopitita kufuatia binti yake kujitokeza kama mwenye silika ya mapenzi ya jinsia yake. Nilivyomwelewa huyu

Mchakato wa Kwenda Kuongelea Kitabu

Image
Leo nimepata ujumbe kutoka kwa Dan, ambaye hivi majuzi alikipigia debe kitabu changu,  Africans and Americans: Embracing Cultural Differences,  katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Anaendelea na juhudi yake. Ameandika: Happy to spread the word about your book. Let me know if you are ever interested in doing a talk at our store. I can connect you with our manager. Tafsiri yangu : Ninafurahi kukitangaza kitabu chako. Nijulishe iwapo utapenda kuja kukiongelea katika duka letu. Nitaweza kukuunganisha na meneja wetu. Kuwaalika waandishi kuongelea vitabu vyao ni utamaduni wa kawaida hapa Marekani. Ni fursa ya mwandishi kukutana na watu wanaotaka kujua mambo kama  historia ya mwandishi, changamoto za uandishi, falsafa na mawaidha yake kuhusu uandishi, na kadhalika. Vinakuwepo vitabu vya mwandishi, kwa watu kuvinunua na yeye kuvisaini. Wa-Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Naambiwa Niongeze Bei ya Kitabu

Image
Katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki, ninakutana na mambo mengi, zikiwemo tabia na mitazamo ya wateja. Moja ambalo linanigusa zaidi ni pale mteja anaposhauri niongeze bei ya kitabu changu. Hiyo imetokea mara kadhaa, kuhusiana na vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultual Differences na Matengo Folktales . Vitabu hivi ninaviuza kwenye matamasha kwa dola 14 kila kimoja. Kwa kujua kwamba watu wengine wanatoa  noti ya dola 20 au noti mbili za dola kumi kumi, ninajitahidi kuwa na chenji. Ajabu ni kwamba watu wengine hawasubiri chenji, na wengine wanakataa. Wanachotaka ni kitabu waende zao. Ninakumbuka watu waliowahi kutoa noti ya dola 20 bila kutaka chenji. Mmoja wa hao, nilipojiandaa kumpa chenji, alisema hiyo chenji ni shukrani yake kwangu kwa kuandika kitabu. Tarehe 4 mwezi huu nilikutana na jambo jingine kabisa. Mama moja, Jackie, ambaye nimemfahamu miezi michache iliyopita na akasoma hivi vitabu vyangu viwili, alinialika kwenye mhadhara wa rafiki yake Mar