Tarehe 13 mwezi huu, nilishiriki tamasha la vitabu liitwalo Deep Valley Book Festival mjini Mankato, jimbo hili la Minnesota. Nilishahudhuria mara tatu tamasha hili linalofanyika mara moja kwa mwaka. Nilijua kuwa mmoja wa waandishi ambao walikuwa mbioni kushiriki ni rafiki yangu Becky Fjelland Brooks anayeonekana pichani kushoto.
Becky ni mwalimu katika South Central College hapa Minnesota. Tulianza kufahamiana wakati yeye na Profesa Scott Fee wa Minnesota State University Mankato waliponialika kwenda kuongea na wanafunzi waliokuwa wanawaandaa kwa safari ya masomo Afrika Kusini.
Watu wengi walihudhuria mhadhara wangu kuhusu tofauti za tamaduni, na nakala nyingi za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences zilinunuliwa. Baada ya hapo, nimepata mialiko ya kwenda kuongea na wanafunzi hao kila mara wanapoandaliwa safari ya Afrika Kusini.
Mwalimu Becky ni mmoja wa wale wa-Marekani ambao wanaipenda Afrika na wanajibidisha kuwaelimisha wenzao kuhusu Afrika. Kuandaa programu za kupeleka watu Afrika ni kazi ngumu, yenye changamoto nyingi. Inahitaji ujasiri na uvumilivu. Nina uzoefu wa shughuli hizo, na ninawaenzi watu wa aina ya mwalimu Becky.
Mwalimu Becky ni mwandishi mwenye kipaji. Tayari ameshachapisha vitabu kadhaa, kwa ajili ya watoto, vijana, na watu wazima. Umaarufu wake unaongezeka mwaka hadi mwaka, na ameshatambuliwa na tuzo kama Midwest Book Awards. Ni faraja kwangu kwamba mwalimu Becky, mwandishi maarufu, anakipenda sana kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na anaipenda mihadhara yangu, kama inavyonekana hapa na hapa.
Hii tarehe 13, kwa kuwa mwalimu Becky na mimi tulifahamu kuwa tungekutana, nilichukua nakala yangu ya kitabu chake kiitwacho Slider's Son ili anisainie. Ninavyo vitabu vyake vingine ambavyo alivisaini siku zilizopita. Tulifurahi kukutana. Ninajiona nimebarikiwa kuwa na rafiki kama huyu. Picha hiyo hapa juu aliiweka Facebook akiwa ameambatisha ujumbe huu: "With my dear friend Joseph Mbele, author of the enlightening and humorous book, "Africans and Americans," sharing stories and friendship at the Deep Valley Book Festival today...."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment