Tuesday, October 16, 2018

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo niliamua kutembelea maduka ya vitabu kwenye miji ya Apple Valley na Burrnsville hapa Minnesota. Apple Valley, kwenye duka la Half Price Books,  nilinunua vitabu vitatu bila kutegemea. Nilipita sehemu ya vitabu vya Hemingway, ambapo sikuona kitabu kigeni kwangu. Nilienda sehemu ya bei nafuu, nikanunua vitabu vitatu.

Kimoja ni Essays and Poems cha Ralph Waldo Emerson, kilichohaririwa na Tony Tanner. Kwa miaka mingi nimefahamu jina la Emerson. Nilifahamu kuhusu insha yake "Self Reliance," ingawa sikuwa nimewahi kuisoma. Nilifahamu pia kuwa ameathiri sana falsafa na uandishi, sio tu Marekani, bali kwingineko. Kwa hali hiyo, sikusita kununua kitabu hiki, hasa baada ya kuona kuwa kina mashairi ya Emerson. Sikujua kuwa alitunga mashairi.

Kitabu kingine nilichonunua ni Collected Poems cha Edna St. Vincent Millay. Huyu ni mwandishi ambaye sidhani kama niliwahi kusikia hata jina lake. Lakini nilipoona hiki kitabu kikubwa sana chenye kurasa 757 na nyongeza ya kurasa 32, na halafu nikasoma taarifa za huyu mwandishi, kwamba alikuwa mwanamke mwenye kujiamini na uthubutu katika utunzi wa ma shairi, na mwanaharakati ambaye katika mazingira ya miaka ya 1920 kuelekea 1930 alikuwa akitetea uhuru wa mtu binafsi na hasa wanawake, na halafu nikaona alipata tuzo maarufu ya uandishi iitwayo Pulitzer Prize mwaka 1923, niliona lazima ninunue kitabu hiki, ili nifaidi utunzi wa mama huyu.

Si kawaida kukutana na tungo za wanawake wa zamani namna hiyo hapa Marekani. Tungo ya mwanzo kabisa ambayo nimewahi kusoma na kuifundisha ni The Awakening, ya Kate Chopin. Hiyo ni riwaya ya mwanzo mwanzo inayotambulika kama ya kifeministi. Kutokana na kufahamu kiasi fulani harakati za wakati ule, nilivutiwa na kitabu hiki cha mashairi ya Edna St. Vincent Millay, ambaye alikuja baada ya Kate Chopin.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni The Mother, cha Maxim Gorky, kilichotafsiriwa na Hugh Aplin. Maxim Gorky ni mwandishi wa zamani wa Urusi. Nilipoona kitabu hiki, nilikumbuka enzi zangu kama mwanafunzi katika idara ya "Literature" ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, ambapo mwalimu wetu Mofolo Bulane alitufundisha nadharia ya fasihi kwa mtazamo wa ki-Marxisti.

Katika mafundisho yale alituwezesha kufahamu kuhusu waandishi wengi, wakiwemo wa Urusi, kama vile Leo Tolstoy, Fyodor Dostoyevsky, Maxim Gorky, Vladimir Mayakovsky, Anna Akhmatova, na Mikhail Sholokhov. Tulijifunza kuwa Gorky ni moja wa waandishi waanzilishi wa mkondo wa "Socialist Realism," ambao ulifuatwa baadaye na akina Mayakovsky na Ana Akhmatova na wengine. Kutokana na kumbukumbu hizi za ujana wangu, niliamua kununua kitabu hiki ili niweze kukisoma nitakapopata wasaa. Baada ya kununua vitabu hivyo, nilielekea kwenye mji jirani wa Burnsville, kwenye duka la vitabu la Barnes Noble. Nitaandika juu ya safari hiyo wakati mwingine.

1 comment:

eddyshaw9272711 said...

Nice post. I learn something more challenging on different blogs everyday. It can always be stimulating to learn content from other writers and observe just a little something from their store. I’d prefer to make use of some with the content on my blog whether you don’t mind. Natually I’ll give you a link on your internet blog. Thanks for sharing. online casino games

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...