Posts

Showing posts from January, 2016

Mungu ni Mmoja Tu

Dini ni kati ya masuala ninayopenda kuyaongelea katika blogu hii. Kwa kitambo sasa, nimekuwa nikielezea imani yangu kwamba kuna Mungu mmoja tu. Nimekuwa nikielezea ulazima wa kuziheshimu dini zote. Nilikuwa nikisema hayo yote nikiwa najitambua kuwa ni m-Katoliki. Sijui wa-Katoliki wenzangu walinionaje, na sijui wa-Kristu wenzangu walinionaje. Sijui watu wa dini zingine walinionaje. Ninafurahi kwamba mkuu wa kanisa Katoliki, Papa Francis, ana mwelekeo huo huo. Dalili za mwelekeo wake zilianza kujitokeza tangu mwanzo wa utumishi wake kama Papa. Aliongeza kasi ya kujenga mahusiano baina ya dini mbali mbali, akifuata mkondo ulioanzishwa na mapapa waliotangulia. Leo nimeona taarifa kuwa Papa Francis ameweka msimamo wake kuhusu dini mbali mbali kwa uwazi kuliko siku zilizopita. Amesema kuwa dini zote ni njia mbali mbali za kumwelekeza binadamu kwa Mungu. Nimeona kuwa msimamo huu ni changamoto kubwa ambayo inahitaji kutafakariwa. Kwa kuzingatia mtazamo huu wa Papa Francis, ninaona k

Nimemkumbuka Shakespeare

Image
Leo, bila kutegemea, nimemkumbuka Shakespeare. Nimeona niandike neno juu yake, kama nilivyowahi kufanya. Nimekumbuka tulivyosoma maandishi yake tukiwa vijana katika shule ya sekondari. Katika kiwango kile, tulisoma tamthilia tulizozimudu, kama  The Merchant of Venice na Julius Caesar .  "High school," ambayo kwangu ilikuwa Mkwawa, tulisoma tamthilia ngumu zaidi, kama Othello na Hamlet .   Othello ilikuwa katika silabasi ya "Literature." Nakumbuka sana kuwa hapo hapo Mkwawa High School tuliangalia filamu ya Hamlet , ambamo aliyeigiza kama Hamlet alikuwa Sir Lawrence Olivier. Huyu ni mmoja wa waigizaji maarufu kabisa wa wahusika wakuu wa Shakespeare. Niliguswa na uigizaji wake kiasi cha kujiaminisha kwamba sitaweza kushuhudia tena uigizaji uliotukuka namna ile. Nilipoteza hamu ya kuangalia filamu yoyote baada ya pale, kwa miaka mingi. Ninavyomkumbuka Shakespeare, ninajikuta nikikumbuka mambo mengi. Kwa mfano, nakumbuka tafsiri murua za Mwalimu Julius Nyere

Kupigwa Marufuku kwa Gazeti la "Mawio"

Nimesoma taarifa kuwa serikali ya Tanzania imelifuta gazeti la "Mawio." Taarifa hizi nimezisoma mitandaoni, kama vile blogu ya Michuzi. Napenda kusema kwamba siafiki hatua hii ya serikali. Msimamo wangu tangu zamani ni kutetea haki na uhuru wa kutoa mawazo. Ninatetea uhuru wa waandishi na uhuru wa vyombo vya habari. Nimewahi kugusia suala hili katika blogu hii.   Msimamo wangu unaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu, ambalo limetamka: Everyone has the right to freedom of opinion and expression; this right includes freedom to hold opinions without interference and to seek, receive and impart information and ideas through any media and regardless of frontiers . Kupiga marufuku gazeti ni kuhujumu haki ya waandishi na wamiliki wa gazeti kueneza habari na mawazo, na ni kuhujumu haki ya wasomaji kupata habari na mawazo. Kwa msingi huu, ninapinga hatua ya serikali ya kulipiga marufuku gazeti la "Mawio." Serikali ya CCM inapiga marufuku magazeti kwa

Vitabu vya Kozi: Waandishi Wanawake wa ki-Islam

Jana, kama ninavyofanya kila siku, niliingia katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, kuona kama vitabu vya kozi zangu za muhula ujao vimefika. Ni utaratibu wetu kwamba miezi au wiki kadhaa kabla ya kuanza masomo, tunapeleka dukani orodha ya vitabu tunavyotaka kutumia, na idadi yake, ili wanafunzi wavinunue. Lengo langu hasa lilikuwa kuona kama vitabu vya kozi yangu mpya, "Muslim Women Writers," vimefika. Nimeona kuwa vyote vimefika, na hapa naleta orodha ya waandishi na vitabu, na majina ya wachapishaji: 1. Aboulela, Leila. Minaret . Grove.  2. Ali, Monica. Brick Lane . Scribner. 3. Ba, Mariama. So Long a Letter . Waveland Press, Inc. 4. el Saadawi, Nawal. The Fall of the Imam . Telegram Books. 5. Hossein, Rokeya S. Sultana's Dream . Feminist Press. 6. Mattu, Ayesha. & Nura Maznavi. Love, InshAllah . Soft Skull Press. 7. Nafisi, Azar. Reading Lolita in Tehran . Random. Nimekuwa nikiandika kuhusu kozi hii mpya katika blogu hii, kuelezea ninavyoj

Kitabu "Qur'an and Woman" Kimewasili

Image
Ninafurahi kwamba kitabu nilichoagiza hivi karibuni, Qur'an and Woman, kilichotungwa na Amina Wadud, nilikipata jana. Siku chache zilizopia, katika blogu hii, niliandika kuwa nimeagiza kitabu hiki. Niliagiza kitabu hiki ili nikisome, kama sehemu ya maandalizi ya kufundisha kozi mpya, "Muslim Women Writers" hapa chuoni St. Olaf, juu ya fasihi iliyoandikwa na wanawake wa ki-Islam kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mara nilipokipata, nilisoma utangulizi, ambao umenivutia, kwa jinsi ulivyoelezea mambo yaliyomo kitabuni. Mwandishi alifanya utafiti wa miaka kadhaa katika kuandaa kitabu hiki, ambacho kinaweka wazi vigezo vya kutathmini nafasi ya mwanamke katika u-Islam. Mwandishi anasema kuwa aliamua kusimama na kuzama katika Qur'an , kwa kuwa hiki ni kitabu kinachokubalika na kuheshimiwa na wa-Islam wote, pasipo wasi wasi wala ubishi. Kwa hivi, ili kuelezea nafasi ya mwanamke katika u-Islam, aliona ni muhimu kujikita katika Qur'an . Mwandishi anasema kwamb

Qur'an na Mwanamke

Image
Siku chache zilizopita, niliandika kuhusu maandalizi ninayofanya kwa ajili ya kufundisha kozi mpya "Muslim Women Writers," hapa chuoni St. Olaf. Niliandika maelezo mafupi ya lengo la kozi hii katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Katika maandalizi ya kozi hiyo, na wakati wa kuifundisha, na siku za baadaye, ninawazia kuisoma Qur'an . Lakini, mbali na fasihi nitakayofundisha, fasihi iliyoandikwa na wanawake wa-Islam, nimeona itakuwa vizuri pia nikitafuta maandishi ya wanawake yanayoichambua Qur'an . Kwa bahati nzuri, nimeona kuwa maandishi haya yako, vikiwemo vitabu. Baada ya kuzipitia taarifa za vitabu hivi, nimeagiza kitabu cha Amina Wadud,  Qur'an and Woman: Rereading the Sacred Text From a Woman's Perspective . Kwa mujibu wa maelezo niliyosoma, kitabu hiki kinafuatilia historia ya maandishi kuhusu Qur'an na mwanamke, historia inayothibitisha jinsi wanaume walivyopotosha mafundisho ya  Qur'an na kuhalalisha mfumo unaowapendelea wanaume na kuwa

Yule Binti Bukola Ametua Ikulu ya Marekani Leo

Image
Siku kadhaa zilizopita, niliandika kuhusu binti Bukola Oriola katika blogu hii. Huyu ni binti kutoka Nigeria ambaye alipatikana na mkasa wa kutumikishwa na kunyanyaswa huku Marekani kwa miaka miwili na mtu ambaye alikuwa ni mume wake, ambaye naye alikuwa m-Nigeria. Hatimaye, kwa bahati nzuri, aliokolewa, na katika ujumbe wangu nilitoa taarifa ya kuteuliwa kwake kama mjumbe katika tume ya serikali ya Marekani ya kutoa ushauri kuhusu majanga haya ya watu kusafirishwa kwa ghilba, kutumikishwa na kunyanyaswa. Leo, Bukola na wanatume wenzake wamekutana kwa mara ya kwanza katika Ikulu ya Marekani, kama inavyoonekana pichani, wakiwa na Mheshimiwa John Kerry, "Secretary of State," wa tano kutoka kulia. Bukola anaonekana amevaa kilemba chekundu. Nimeona nilete taarifa hii hapa kuonyesha hatua hii ya safari ya Bukola. Vile vile, nataka kusema kwamba tatizo tunaloongelea hapa ni la dunia nzima. Tusijiziuke, hata wa-Tanzania wanakumbana nalo. Ni tatizo lisilojali jinsia, umri, dini

Nawazia Dini na Uandishi wa Wanawake wa ki-Islam

Muhula ujao, kuanzia mwezi Februari hadi Mei, nitafundisha kozi mpya hapa chuoni St. Olaf ambayo nimeiita "Muslim Women Writers." Ni kozi ya fasihi kwa ki-Ingereza, ambamo tutasoma maandishi ya wanawake wa-Islam kutoka Bangladesh, India, Iran, Misri, Sudan, Senegal, na Marekani. Taarifa fupi ya kozi hiyo  nimeandika hapa. Wakati huu ninapongojea kufundisha kozi hii katika mazingira ya leo ambamo maelewano miongoni mwa waumini wa dini na madhehebu mbali mbali yanatatanisha, ninajikuta nikiwazia mara kwa mara masuala ya dini. Katika siku zijazo, labda kwa miezi kadhaa, ninategemea kuandika tena na tena katika blogu hii kuhusu dini na kozi yangu. Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu dini. Nimeandika kuhusu umuhimu wa mijadala ya dini, umuhimu wa kuziheshimu dini zote, na  nilivyozuru nyumba za ibada za dini nyingine. Sioni mantiki kwa dini yoyote kuwafundisha waumini wake kwamba Muumba anawapenda wao zaidi kuliko watu wa dini nyingine. Msimamo wangu ni kwamba Mungu (Allah)

Kitabu Kinaposainiwa

Image
Leo napenda kuirejesha mada ya kusainiwa vitabu, ambayo nimewahi kuileta katika blogu hii.  Wanablogu wengine nao wameiongelea. Kwa mfano, Christian Bwaya amelielezea suala la kusaini vitabu kama jambo la ajabu, akatumia dhana ya muujiza. Nakubaliana na dhana hiyo, kutokana na uzoefu wangu kama mwandishi ambaye nimesaini vitabu vyangu mara nyingi, na pia mnunuaji wa vitabu ambaye nimesainiwa vitabu mara kwa mara. Hapa kushoto ninaonekana nikisaini kitabu changu mjini Faribault, Minnesota. Huyu ninayemsainia ni binti kutoka Sudan. Ninafahamu muujiza huu unavyokuwa kwa pande zote mbili, mwenye kusaini kitabu chake na mwenye kusainiwa. Ninadiriki kusema kuwa kitendo cha kusainiwa kitabu kinafanana na ibada. Natumia neno ibada kwa maana ile ile ya dhana ya ki-Ingereza ya "ritual." Hapo kushoto anaonekana mwandishi Seena Oromia akinisainia kitabu chake mjini Minneapolis. Ibada ni sehemu ya kila utamaduni, na kila ibada ina utaratibu wake, iwe ni misa kanisani, mazishi,