Kupigwa Marufuku kwa Gazeti la "Mawio"

Nimesoma taarifa kuwa serikali ya Tanzania imelifuta gazeti la "Mawio." Taarifa hizi nimezisoma mitandaoni, kama vile blogu ya Michuzi. Napenda kusema kwamba siafiki hatua hii ya serikali. Msimamo wangu tangu zamani ni kutetea haki na uhuru wa kutoa mawazo. Ninatetea uhuru wa waandishi na uhuru wa vyombo vya habari.

Nimewahi kugusia suala hili katika blogu hii.  Msimamo wangu unaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu, ambalo limetamka:

Everyone has the right to freedom of opinion and expression; this right includes freedom to hold opinions without interference and to seek, receive and impart information and ideas through any media and regardless of frontiers.

Kupiga marufuku gazeti ni kuhujumu haki ya waandishi na wamiliki wa gazeti kueneza habari na mawazo, na ni kuhujumu haki ya wasomaji kupata habari na mawazo. Kwa msingi huu, ninapinga hatua ya serikali ya kulipiga marufuku gazeti la "Mawio."

Serikali ya CCM inapiga marufuku magazeti kwa kutumia sheria kandamizi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa miaka na miaka. Serikali inadai kuwa hatua zake ni sahihi kisheria. Lakini msimamo huu una matatizo.

Kwanza hii sheria haitendi haki, bali inahujumu haki. Ni kama zilivyokuwa sheria za utawala wa kikaburu Afrika Kusini, ambazo zilikuwa halali kwa misingi ya sheria lakini si za haki. Mfumo mzima wa ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini haukuwa wa haki.

Pili, kazi ya kutafsiri sheria si ya serikali wala mamlaka nyingine yoyote, bali ni ya mahakama. Kama serikali inaona gazeti limekiuka sheria, wajibu wake ni kulipeleka gazeti mahakamani. Tufanye hima kuondoa sheria za kikaburu ili mahakama ziwe zinatoa haki.

Kwa mtazamo wangu, kufungia au kupiga marufuku gazeti ni dharau kwa jamii. Ni kusema kuwa jamii haina akili ya kuweza kusoma na kuchambua kilichoandikwa. Kama wa-Tanzania wameridhika kutukanwa namna hiyo, mimi simo. Ninajitambua kuwa nina akili timamu, na ninatetea, ninaheshimu na kutumia haki na uhuru wangu wa kusoma nitakacho.

Hoja ya serikali kwamba gazeti la "Mawio" linaandika taarifa za uchochezi haina mashiko. Serikali inadai kwamba tangu mwezi Juni mwaka 2013 gazeti la "Mawio" limekuwa likiambiwa libadili mwelekeo likakaidi. Sasa basi, kama gazeti limeandika linavyoandika kwa miaka yote hii na jamii imeendelea kuwa na amani, hili wazo la uchochezi linatoka wapi na lina ushahidi gani?

Serikali au mamlaka yoyote inayotumia ubabe ndio inahatarisha amani. Uvunjifu wa haki ndio uchochezi. Gazeti likiripoti hayo halifanyi uchochezi, kwani jamii inayoumia haihitaji kuambiwa na gazeti kuwa inaumia. Jamii hiyo ikizuiwa hata kusema, na machungu yakabaki yanafukuta moyoni, ni hatari ya kutokea mlipuko. Hilo ni jambo linaloeleweka katika taaluma ya saikolojia. Ni bora watu wawe huru kuelezea mawazo na hisia zao. Wanaozuia uhuru huo wakumbuke kauli ya wahenga kuwa kimya kingi kina mshindo mkuu.

Comments

Shukran Prof, kwa kujenga hoja zenye mashiko. Naomba ukipata muda utueleze uchambuzi wako juu ya uchaguzi kufutwa wote na kurejewa Zanzibar. Vipi taswira ya nchi ya Tz katika jambo hili ukizingatia maoni ya mh membe kuwa dunia inatushangaa.

Ahsante na niwie radhi iwapo nakusukuma katika eneo tata.
Mbele said…
Ndugu Khalfan Abdallah Salim,

Shukrani kwa ujumbe wako. Samahani sikuweza kuliongelea suali lako kuhusu mambo ya Zanzibar. Nina mawazo mengi na hisia nyingi na pia kumbukumbu nyingi. Ila jambo moja nina hakika nalo, ni kwamba jina la Tanzania limekuwa likichafuliwa kutokana na mambo ya uchaguzi. Tangu zamani imekuwa hivyo. Sio rahisi kwangu kujua undani wake. Hata wakati huu ninapoandika, ni baada ya kusikia tamko la BAKWATA kuwa wanaunga mkono kurudiwa kwa uchaguzi. Itabidi niwe msikilizaji; labda nitajifunza kitu.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini