Sunday, March 28, 2010

Biashara Mtandaoni

Kadiri siku zinavyopita, neno tekinolojia linazidi kusikika miongoni mwa wa-Tanzania, kama ilivyo duniani kwa ujumla. Tekinolojia ya leo imetuletea mambo mengi, mojawapo likiwa ni mtandao. Ulimwengu unazidi kuunganishwa kwa tekinolojia ya mawasiliano ambayo kifupi tunaiita mtandao.

Lakini kuna hatari kuwa hizi dhana zinabaki kuwa dhana tu miongoni mwa wa-Tanzania wengi. Ukweli ni kuwa, ingawa una dosari za hapa na pale, na athari mbaya za hapa na pale, huu mtandao umekuja kama baraka. Mtandao umepunguza au kuondoa tofauti zilizokuwepo kabla katika uwezo wa watu mbali mbali kusambaza taarifa na maoni, au kutangaza shughuli zao kama vile biashara.

Kwa mfano, kwa kutumia nyenzo kama blogu, tovuti, au Facebook, mfanyabiashara mdogo, auzaye mahindi mjini Songea au Tunduma, au yule auzaye vinyago Mtwara, anaweza kutangaza biashara yake kwa ulimwengu.

Mtandao umeleta urahisi wa aia nyingine pia. Leo hii, umuhimu wa kujenga jengo linaloitwa duka, au kukodi chumba cha kukitumia kama duka, umepungua sana. Mtu unaweza ukawa na bidhaa zako nyumbani mwako au katika ghala yako, na ukafungua duka mtandaoni.

Mimi, kwa mfano, ni mwandishi wa vitabu. Ninauza hivi vitabu. Lakini sina nyumba au chumba kinachoitwa duka. Vitabu ninavichapisha mtandaoni. Bofya hapa. Au, kwa usahihi zaidi, niseme kuwa miswada ya vitabu hii nimeihifadhi mtandaoni, na mtu anapoagiza nakala, ndipo mitambo inachapisha nakala iliyoagizwa au nakala zilizoagizwa tu. Sivioni hivi vitabu wanavyoagiza wateja, lakini nimefungua duka huko huko mtandanoni. Bofya hapa. Wateja wananunua bila mimi kuwaona au kuwafahamu.

Katika maduka ya jadi, mwuzaji na mteja wanakutana, au wanasiliana kwa simu au barua. Mteja wa duka la mtandaoni kama hili langu, hahitaji kuwasiliana na mwenye duka. Yeye anafungua kompyuta, anaingia hapo dukani na kununua anachotaka, kwa kutumia "credit card" na kwenda zake. Wewe mwenye duka unapofungua kompyuta na kuangalia duka lako la mtandaoni, utaona kuwa bidhaa imenunuliwa, bila kumjua aliyenunua. Lakini malipo yako yanakuwa yameshaingia.

Siku hizi, watu wengi wenye maduka ya jadi au biashara za jadi wanaziweka mtandaoni pia. Ni njia ya kuwafikia wateja duniani kote. Mtu akiangalia duka hili la mtandaoni akapenda kununua kitu, anawasiliana na mwenye duka, kwa njia itakayokuwa imetajwa, iwe ni barua pepe, simu, au faksi. Au, kufuatana na utaratibu alioweka mwenye duka, mteja anatoa malipo hapo hapo anapoamua kununua kitu fulani. Jukumu la mwenye duka ni kumfungashia na kumpelekea mteja hicho alicholipia.

Kwa maana hiyo, biashara ya aina hii inahitaji uaminifu. Hili si jambo la kuongelewa. Ni ukweli usiopingika. Mwenye biashara makini anazingatia umuhimu wa kumridhisha mteja daima, kwani hii ndio siri ya mafanikio katika biashara. Mteja aliyeridhika na kufurahia huduma mahali fulani anawaambia wenzake. Huduma bora huzaa wapiga debe na kumneemesha mwenye biashara. Lakini mteja asiyeridhika naye atawaeleza wengine, na kusambaa kwa habari hii ni sumu kwa biashara. Wafanya biashara wetu wengi hawaelewi madhara ya kumnyanyasa mteja. Biashara yao inapoanguka, wanatoa visingizio kama vile kurogwa na washindani wao.

Ni muhimu sana wafanyabiashara wetu Tanzania waangalie suala hili la kuingia mtandaoni. Baadhi, kama vile kwenye sekta ya utalii, wanazo tovuti. Lakini kwa jinsi tekinolojia ya mtandao inavyozidi kupanuka na kusonga mbele, na kwa jinsi ilivyo na manufaa, ni vizuri wengine wajiunge na kuwa nayo sambamba.

Saturday, March 20, 2010

"Lonely Planet" Waidhalilisha Arusha

Leo nimeona taarifa mtandaoni kuwa Lonely Planet hivi karibuni ilitoa taarifa ikiutaja mji wa Arusha katika orodha ya miji isiyofaa duniani. Arusha imeshika namba nane. Bofya hapa. Sikujua kuwa kuna taarifa ya namna hii, hadi leo, nilipoiona katika Jamii Forums. Bofya hapa.

Inaeleweka kwa nini wahusika wa mji wa Arusha na labda wa-Tanzania wengi wanaishutumu taarifa hii ya Lonely Planet. Mji wa Arusha unajulikana kwa utalii, na katika ushindani uliopo duniani, wahusika wote wanajitahidi kuwa na jina zuri, ili wafanikiwe kibiashara.

Pamoja na yote hayo, sisi wa-Tanzania tunapaswa kujifunza kutokana na makosa. Hii si mara ya kwanza watu wa nje kutangaza habari za nchi yetu kwa namna ambayo haitupendezi. Kwa mfano, tumelalamika kwa muda mrefu kuwa nchi jirani inatangaza kuwa Mlima Kilimanjaro uko kwao. Na sasa tunalalamikia hii taarifa ya Lonely Planet kuhusu Arusha. Je, tutalalamika mpaka lini? Je, tutaweza kushindana na hao wapinzani wetu kwa kulalamika tu?

Katika blogu zangu, na za wengine, na pia katika kitabu changu cha Changamoto, nimeandika tena na tena kuwa wa-Tanzania tuache uzembe. Tujibidishe katika elimu, ambayo ni pamoja na elimu ya lugha. Tuwe na uwezo wa kujieleza, kwa ufasaha na viwango vya juu kabisa, iwe ni kwa ki-Swahili au ki-Ingereza. Tuwe na tabia ya kununua na kusoma vitabu, kujiongezea maarifa na ujuzi, pamoja na ujuzi wa lugha.

Njia madhubuti ya kupambana na propaganda hizi tunazozilalamikia ni sisi wenyewe kuandika habari za nchi yetu na kuzisambaza duniani. Katika dunia ya leo, ya utandawazi na tekinolojia ya mawasiliano ya mtandaoni, uwanja uko wazi kwetu sote. Tutumie fursa hizi kama wanavyozitumia hao tunaowalalamikia.

Kama kweli tunaudhika na yale tunayofanyiwa, njia iliyopo ni hii ya kujibu mapigo. Binafsi, najitahidi kuandika habari zetu, kama njia moja ya kuipa dunia mtazamo wa m-Tanzania. Ninaandika kuhusu wa-Tanzania na wa-Afrika, kuhusu u-Tanzania na u-Afrika, ili kupambana na hao waliojivika kofia ya kuwa wasemaji wetu, wakati hatujawapa wadhifa huo.

Kampuni ya Lonely Planet ni kubwa sana duniani, ambayo vitabu vyake vinasomwa na watu zaidi ya 900,000. Mimi ni mtu moja tu, na sina mtandao na nguvu za kiuchumi namna hiyo. Lakini, hii sio sababu ya kukata tamaa. Cha msingi ni kujiamini. Wahenga walituachia busara katika methali zao. Walituambia, kwa mfano, kuwa mwanzo wa makubwa ni madogo na pia bandu bandu humaliza gogo.

Juzi tu kwenye blogu hii, bofya hapa, nilimnukuu msomaji wangu mmoja akisema kuwa kitabu cha Africans and Americans alikiona kuwa bora zaidi kuliko cha Lonely Planet. Pamoja na hali yangu ya chini sana nikifananisha na Lonely Planet, sina wasi wasi kuwa kadiri siku zinavyopita, nitalipunguza hili gogo liitwalo Lonely Planet.

Walichoandika Lonely Planet kuhusu Arusha kiwe ni changamoto kwetu wa-Tanzania, kwamba tusikae tunalalamika tu. Tupambane nao kwa vitendo.

Wednesday, March 17, 2010

Naishangilia Zanzibar

Siku kadhaa zilizopita nilipata fursa ya kusikiliza hotuba aliyotoa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff, kule Uingereza, akielezea makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Karume. Bofya hapa.

Nimeipenda sana hotuba ile, kwa jinsi ilivyojaa kumbukumbu, mawazo, tathmini na mawaidha kuhusu siasa Zanzibar. Nimevutiwa na jinsi Zanzibar ilivyofikia hatua ya kutathmini maana ya mfumo wa siasa ambao umetumika kwa yapata nusu karne na wakauona kuwa una dosari na ni chanzo cha matatizo. Mfumo huo ni wa vyama vya siasa.

Mimi mwenyewe nimehoji sana mantiki ya dhana nzima ya chama au vyama vya siasa. Mwaka jana niliandika makala nikihoji kama chama cha siasa au vyama vya siasa ni kitu cha lazima katika kujenga demokrasia. Nilisema kuwa tumeiga hii dhana kikasuku, na tunashinikizwa na mataifa mengine. Nilitamka kuwa labda kuna umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kujenga demokrasia bila chama au bila vyama. Bofya hapa. Mawazo yangu, ambayo yanahoji mambo tuliyozoea, katika siasa, uchumi, utamaduni, elimu na kadhalika, yamo katika kitabu cha Changamoto.

Nimefurahi kusikia maelezo ya Maalim Seif kuhusu tathmini waliyoifanya Zanzibar, hadi wakafikia hatua ya kujenga ushirikiano baina ya CUF na CCM, na kuondokana na historia ya uhasama, kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar. Wamefanya uamuzi wa maana, na nimefurahi kuona jinsi wanavyojipanga kuunganisha nguvu za wa-Zanzibar wote, walioko nchini na nje ya nchi, ili wajenge Zanzibar, ambayo zamani ilikuwa na historia na heshima kubwa duniani.

Naamini kuwa kwa Zanzibar kuchukua uamuzi huu, sote tutafaidika. Kuimarika kwa Zanzibar ni neema kwa Muungano. Wale waliokuwa wanaitumia Zanzibar kwa manufaa yao, wakawa wanaendekeza siasa za mfarakano, ndio pekee watakaoambulia patupu. Wale waliokuwa wanaendekeza ubabe wa kutumia nguvu ya chama au vyama, wamepewa somo kubwa. Nategemea watajifunza.

Hotuba hii ya Maalim Seif nimeona ni muhimu kuliko zote ambazo nimewahi kuzisikia kutoka kwa wanasiasa wetu tangu aondoke Mwalimu Nyerere.

Wednesday, March 10, 2010

Mteja Anapofurahi

Leo mama moja Mmarekani ameniandikia ujumbe kwenye ukurasa wangu wa Facebook. Anaelezea kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans, na jinsi kilivyomsaidia alipokuwa Afrika Mashariki:

I remember being glad I had read it. Observations from someone who has lived in both Minnesota and East Africa, and a scholar no less, were a lot more insightful than my Lonely Planet.

Ni faraja kwangu kupata maoni ya wasomaji. Ni furaha kuwasikia kuwa wameridhika. Niliandika kitabu kwa sababu niliona kuna tatizo duniani lililohitaji ufumbuzi, tatizo la maelewano baina ya watu wa tamaduni mbali mbali. Lengo langu halikuwa kujipatia pesa. Hii Lonely Planet anayoitaja ni kampuni maarufu inayochapisha vitabu kwa ajili ya wasafiri. Vitabu hivi vinaelezea taarifa za nchi mbali mbali. Basi, nimetabasamu kusoma kauli ya huyu mama, kuwa kitabu changu ni tishio kwa Lonely Planet. Wakae chonjo.

Ni kweli kuwa watu wananunua kitabu hiki. Na mimi nazingatia hilo. Lakini jambo la msingi zaidi kwangu ni kuwa mteja aridhike. Asione kuwa alipoteza hela zake au kitu alichonunua hakikumridhisha. Mteja anapofurahi kama huyu wa leo, nami nafurahi.

Mara kwa mara, huwa naalikwa kwenda kutoa mihadhara kuhusiana na kitabu hiki au maandishi yangu mengine. Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, wanaonialika wananiuliza gharama ya mihadhara yangu ni kiasi gani.

Ningekuwa mtu ninayeweka pesa mbele, ningesema hii ni fursa yangu ya kuwakomoa na kutajirika. Lakini mimi, pamoja na mahitaji mengi ya pesa ambayo sote tunayo, siwezi kufanya hivyo. Kwa nini nifanye jambo ambalo haliendani na dhamiri yangu? Sipendi makuu, na sikulelewa katika mkondo wa kujilimbikizia utajiri.

Ninaridhika na malipo ya wastani. Vile vile, hata kama taasisi au jumuia inayonialika haina pesa, mimi huwa naenda kuwapa mhadhara. Akili niliyo nayo nilipewa na Mungu, haikuwa haki yangu, wala siwezi kujivunia. Nina wajibu wa kuitumia kwa manufaa ya wanadamu, si kwa manufaa yangu binafsi. Ninaamini kuwa nikifanya ubinafsi, Mungu anaweza kuninyang'anya.

Furaha ya mteja ni malipo tosha kwa juhudi zangu, na ni njia ya kumtukuza Mungu aliyenipa uwezo.

Wednesday, March 3, 2010

Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad

Mwaka jana, nilipokuwa Dar es Salaam, niliingia katika duka la vitabu, Dar es Salaam Bookshop, nikanunua vitabu kadhaa vya ki-Swahili. Vitatu vilikuwa vya Shaaban Robert, na kingine ambacho sikuwa nimewahi kusikia habari zake, kilikuwa juu ya Siti Binti Saad.
Kitabu hiki Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad Malkia wa Taarab, kimeandikwa na Nasra Mohamed Hilal wa Malindi, Zanzibar, ambaye alikuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Zanzibar kwa miaka 27. Kimechapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, 2007.

Kwa mujibu wa taarifa iliyo ukurasa wa nyuma ya kitabu, Bibi Nasra "(a)mefanya utafiti wa historia ya wanawake wa makabila mbali mbali walioishi mjini Zanzibar na kuacha nyayo zao juu ya mila, utamaduni na sanaa. Hivi sasa anakamilisha vitabu vingine viwili. Zaidi ya uandishi Bibi Nasra ni mtengenezaji wa filamu wa kujitegemea na amekwishatoa filamu tano fupi, zote katika Kiswahili."

Natoa pongezi na shukrani kwa juhudi za mama huyu. Kitabu chake hiki kinathibitisha juhudi yake katika utafiti, kwani amekusanya habari na kumbukumbu nyingi kutoka kwa watu mbali mbali waliomfahamu Siti Binti Saad, wakiwemo ndugu zake.

Amekusanya nyimbo mbali mbali za Siti Binti Saad, nyingine zikiwa mpya kwetu ambao ufahamu wetu wa Siti Binti Saad unatokana na maandishi. Tuna bahati ya kuzipata taarifa na nyimbo nyingi namna hii katika kitabu kimoja.

Kuna mengi ya kujifunza kutokana na maisha na tungo za Siti Binti Saad, ambaye alipambana na matatizo mengi katika maisha yake, lakini akawa shujaa mwenye kujiamini muda wote. Alituachia mafundisho mengi murua. Kwa mfano, katika wimbo wake moja alisema

Ukicha kutajwa
Hutotenda jambo....

Alimaanisha kuwa kama unaogopa maneno ya watu, hutafanya kitu cha maana maishani.

Kama tunavyofahamu, msingi wa utafiti juu ya Siti Binti Saad uliwekwa na Shaaban Robert, katika kitabu chake cha Wasifu wa Siti Binti Saad. Katika kufuatilia habari za Shaaban Robert, nimeshangazwa na vipaji vyake. Kwa mfano, ingawa hakuwa na elimu kubwa ya shuleni, ikiwemo elimu ya utafiti wa masuala ya aina hii, Shaaban Robert alifanya kazi nzuri, akizingatia maadili ambayo leo tunafundisha vyuoni. Bibi Nasra ameutaja vizuri mchango wa Shaaban Robert na amemtolea sifa na shukrani ipasavyo.

Nategemea kupata wasaa wa kukichambua kitabu hiki cha Mfinyanzi Aingia Kasri siku zijazo na kuelezea maoni yangu vizuri. Kwa leo nimeona nikitaje tu, ili walimwengu wapate kufahamu uwepo wake.


Money in African and American Culture