Wednesday, March 3, 2010

Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad

Mwaka jana, nilipokuwa Dar es Salaam, niliingia katika duka la vitabu, Dar es Salaam Bookshop, nikanunua vitabu kadhaa vya ki-Swahili. Vitatu vilikuwa vya Shaaban Robert, na kingine ambacho sikuwa nimewahi kusikia habari zake, kilikuwa juu ya Siti Binti Saad.
Kitabu hiki Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad Malkia wa Taarab, kimeandikwa na Nasra Mohamed Hilal wa Malindi, Zanzibar, ambaye alikuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Zanzibar kwa miaka 27. Kimechapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, 2007.

Kwa mujibu wa taarifa iliyo ukurasa wa nyuma ya kitabu, Bibi Nasra "(a)mefanya utafiti wa historia ya wanawake wa makabila mbali mbali walioishi mjini Zanzibar na kuacha nyayo zao juu ya mila, utamaduni na sanaa. Hivi sasa anakamilisha vitabu vingine viwili. Zaidi ya uandishi Bibi Nasra ni mtengenezaji wa filamu wa kujitegemea na amekwishatoa filamu tano fupi, zote katika Kiswahili."

Natoa pongezi na shukrani kwa juhudi za mama huyu. Kitabu chake hiki kinathibitisha juhudi yake katika utafiti, kwani amekusanya habari na kumbukumbu nyingi kutoka kwa watu mbali mbali waliomfahamu Siti Binti Saad, wakiwemo ndugu zake.

Amekusanya nyimbo mbali mbali za Siti Binti Saad, nyingine zikiwa mpya kwetu ambao ufahamu wetu wa Siti Binti Saad unatokana na maandishi. Tuna bahati ya kuzipata taarifa na nyimbo nyingi namna hii katika kitabu kimoja.

Kuna mengi ya kujifunza kutokana na maisha na tungo za Siti Binti Saad, ambaye alipambana na matatizo mengi katika maisha yake, lakini akawa shujaa mwenye kujiamini muda wote. Alituachia mafundisho mengi murua. Kwa mfano, katika wimbo wake moja alisema

Ukicha kutajwa
Hutotenda jambo....

Alimaanisha kuwa kama unaogopa maneno ya watu, hutafanya kitu cha maana maishani.

Kama tunavyofahamu, msingi wa utafiti juu ya Siti Binti Saad uliwekwa na Shaaban Robert, katika kitabu chake cha Wasifu wa Siti Binti Saad. Katika kufuatilia habari za Shaaban Robert, nimeshangazwa na vipaji vyake. Kwa mfano, ingawa hakuwa na elimu kubwa ya shuleni, ikiwemo elimu ya utafiti wa masuala ya aina hii, Shaaban Robert alifanya kazi nzuri, akizingatia maadili ambayo leo tunafundisha vyuoni. Bibi Nasra ameutaja vizuri mchango wa Shaaban Robert na amemtolea sifa na shukrani ipasavyo.

Nategemea kupata wasaa wa kukichambua kitabu hiki cha Mfinyanzi Aingia Kasri siku zijazo na kuelezea maoni yangu vizuri. Kwa leo nimeona nikitaje tu, ili walimwengu wapate kufahamu uwepo wake.


















6 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Shaaban Robert alikuwa na kipaji cha pekee na mimi nahisi kwamba hatujaweza kusoma vitabu vyake kwa makini, kuvichambua vizuri na kumwelewa ipasavyo - yeye pamoja na falsafa yake. Na pengine ndiye mwandishi aliyeweza kuitumia lugha ya Kiswahili katika maandishi yake kwa ufundi wa ajabu. Wasifu wa Siti Binti Saad, bila kutaja Kusadikika na Kufikirika, ni kitabu ambacho kimeandikwa kwa ufasaha mno pengine kuliko vyote katika Fasihi ya Kiswahili.

Hiki ulichokitaja hapa nilikuwa sikijui. Nategemea kwenda huko muda si mrefu ujao na bila shaka nitajaza sanduku wakati wa kurudi.

Umeshajaribu kuzisoma novela za Kezilahabi - Nagona na Mzingile? Kama umeshawahi kuvisoma, una maoni gani? Wahakiki bado wanahangaika wakijaribu kufahamu kinachoongelewa humo na wengine (mf. Wamitilla - mchambuzi mashuhuri kutoka Kenya) wamefikia hata kumshutumu Kezilahabi kwamba ameiua riwaya ya Kiswahili.

bibi Alesha said...

Nimesoma pambio lako limenifurahisha lakini limenipa mawazo sana. Kuna mabishano makubwa nyumbani kuhusu vitabu vya kutumia mashuleni wakati tuna hazina kubwa ya vitabu. Wanasiasa wamekuwa wakichagua vitabu ambavyo havina mvuto wala vionjo vya kumfanya mwanafunzi kufikiri. Je, Mzee Hapa kwetu ulishaombwa kutoa mihadhara kwa walimu wa Sekondari nchini Tanzania?

Mbele said...

Mwalimu Matondo, pamoja na kwamba mimi ni mwalimu wa ki-Ingereza, na fasihi katika lugha hiyo, nimekuwa nikifurukuta sana kujiimarisha katika lugha na fasihi ya ki-Swahili. Pamoja na kufanya utafiti na katika tungo za kale za ki-Swahili, kwa miaka zaidi ya ishirini, nimekuwa nikisoma maandishi ya mabingwa wa enzi zetu, kama vile Shaaban Robert, Ahmad Sheikh Nabhani, Amiri Andanenga, na Haji Gora Haji.

Nimeona ni lazima nijielimishe namna hiyo, na kuonyesha mfano wa kuienzi lugha ya ki-Swahili, kama walivyoienzi hao mabingwa.

Kuhusu Shaaban Robert, ni kama unavyosema. Maandishi yake ni ya kiwango cha juu sana kwa upande wa fani, falsafa na maudhui. Nakubaliana nawe kabisa kuwa WaTanzania tunababaisha, wala hatujazama katika kutafiti na kutafakari urithi aliotuachia.

Baada ya kununua vitabu vyake vitatu mwaka jana, niliangalia ndani nikaona kuwa kuna taasisi nchini Tanzania ambayo inatoa idhibati kwa vitabu kutumika mashuleni. Kitabu kimoja cha Shaaban Robert kilikuwa kimepigwa muhuri wa idhibati hiyo.

Nilishtuka. Je, kuna mtu anayeweza kusema ana wadhifa wa kukiwekea idhibati kitabu cha Shaaban Robert? Yaani hatujui kuwa andiko lolote la Shaaban Robert ni dhahabu? Ulisikia wapi Mwingereza akathubutu kutoa idhibati kwa kitabu cha Shakespeare?

Wa-Tanzania ndivyo tulivyo. Hatujui hata thamani ya urithi aliotuachia Shaaban Robert.

Kezilahabi nimemfahamu tangu mwaka 1971 nilipoenda kusoma Mkwawa High School. Alikuwa mwalimu pale. Kisha tulikuwa wote Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison kwenye masomo ya juu. Maandishi yake nayafahamu, ila sijayasoma kwa makini bado. Yeye anapenda kutumia au kuanzisha mitindo yake mwenyewe na pia anatumia falsafa mbali mbali, zikiwemo za nchi za Magharibi. Hayo majaribio ndio yanayochangia ugumu katika kuyaelewa au kuyaelezea maandishi yake.

Mbele said...

Ndugu Milembe, shukrani kwa ujumbe wako. Elimu haithaminiwi sana Tanzania. Watu wanachangia mamilioni ya shilingi kwa ajili ya sherehe, lakini hawachangii kununulia vitabu mashuleni, au kuweka vitabu majumbani mwao, wajisomee na watoto wao wavisome.

Vitabu vya Shaaban Robert vinapatikana, hasa baada ya kampuni ya Mkuki na Nyota kuamua kuvichapisha upya. Kwa mtazamo wangu, serikali ingepaswa kuhakikisha viko katika mashule yote. Fedha ziko, tena nyingi. Kwa mfano, CCM imenunua magari 200 kwa shughuli za uchaguzi wa mwaka huu.

Wazazi wangepaswa kuhakikisha vitabu hivi viko majumbani, kwani ni hazina kubwa kwao na kwa watoto. Lakini wazazi hao wanatumia shilingi zao kwenye baa au kwenye michango ya sherehe.

Vitabu vya Mwalimu Nyerere ni hazina kubwa. Navyo serikali ingepaswa iviweke katika shule zote, na wazazi wangekuwa navyo majumbani. Ni kama unavyosema, kwamba vitabu viko.

Hata mimi mwenyewe nimeandika vitabu, ambavyo vinatumika katika vyuo mbali mbali huku Marekani. Lakini sina uwezo wa kununua nakala za kuzisambaza katika mashule yetu. Ningefurahi iwapo, baada ya uchaguzi, CCM ingenipa gari moja kati ya hayo 200 niliuze, na pesa ninunulie vitabu vyangu nivilete mashuleni Tanzania.

Huwa napata mialiko ya kuzungumza sehemu mbali mbali huku ughaibuni. Labda kwa vile safari zangu Tanzania huwa nazipanga mwenyewe na ninakuwa na shughuli zangu, haijawa kawaida mimi kualikwa kutoa mihadhara.

Isipokuwa, kuanzia mwaka juzi, nimejipangia utaratibu wa kuendesha warsha ninapokuwa Tanzania. Warsha hizi ni kuhusu masuala ambayo nayaona ni muhimu katika dunia ya leo, kwa mujibu wa taaluma zangu.

Kwa mfano tarehe 3 Julai, nitaendesha warsha Arusha, katika ukumbi wa Arusha Community Church, kuhusu "Culture and Globalization" ("Utamaduni na Utandawazi").

Ratiba kamili ya warsha za mwaka huu bado ninaiandaa.

Sisulu said...

Hongera wataalamu kwa haya hii ni dalili tosha kwamba angalau kuna watu wanao kisemea kiswahili chetu chenyewe tu ni urithi na utambulisho wetu watanzania kama wakaazi wa bara hili upande wa afrika mashariki na kati.naunga mkono hii kauli ya matondo na hapa na namnukuru "hatujaweza kusoma vitabu vyake kwa makini, kuvichambua vizuri na kumwelewa ipasavyo" TUFANYE HIMA tuilinde na tuibebe lugha yetu

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Milembe - ni jina la Kisukuma au? Nina dada mwenye jina hili na nimefurahi kuliona hapa!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...