Posts

Showing posts from May, 2010

Warsha Kuhusu Utamaduni na Utandawazi, Juni 12, 2010

Hebu fikiria: hao wa-Tanzania wanaoondoka nchini kwenda kufanya kazi nchi za mbali au kutafuta biashara, kusoma, na kadhalika, wanakuwa wamejiandaa vipi kukabiliana na tamaduni za huko wanakoenda? Wageni wanaokuja Tanzania kwa shughuli mbali mbali, au kama wahamiaji, nao wanakuwa wamejiandaa vipi kuishi katika utamaduni wetu? Masuala ya aina hii yameanza kupata umuhimu wa pekee duniani, kutokana na kuimarika kwa utandawazi. Ni aina ya masuala ambayo ninayashughulikia sana, kama mwandishi, mtoa mada na mwendesha warsha, hasa huku Marekani. Ni muhimu wa-Tanzania nao wajipange na kujiandaa ipasavyo, kwani kama ninavyosema mara kwa mara katika blogu hii, ushindani unaendelea kushamiri duniani, na uwezo wa kukabiliana na ushindani huu unatokana na elimu, ujuzi na maarifa. Tarehe 12 Juni nitaendesha warsha Tanga, kuhusu utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nimeshaendesha warsha za aina hii kabla hapa Tanzania. Yeyote anakaribishwa. Kwa taarifa zaidi kuhusu warsha ya tarehe 12 Juni, som

Wa-Tanzania Hawana Hela za Kununulia Vitabu?

Image
Katika malumbano yetu kwenye hizi blogu, wakati mwingine tunajadili tatizo sugu na la kukera la wa-Tanzania kutokuwa na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Baadhi ya watu wanadai kuwa kipato cha m-Tanzania ni duni kiasi kwamba wazo la kununua vitabu haliwezi kuwa kichwani mwake. Anahangaika apate angalau mlo moja kwa siku. Hii hoja ina ukweli kwa baadhi ya wa-Tanzania. Lakini kuna maelfu ya wa-Tanzania wenye uwezo wa kununua vitabu ila hawana utamaduni huo. Ushahidi kuwa wana uwezo kifedha uko kila mahali, kuanzia baa hadi kwenye michango ya sherehe ambayo haiishi, na makamuzi mengine mengi. Nimeona picha leo kwenye blogu ya Michuzi ambayo imenikumbusha haya malumbano yetu. Inawaonyesha mashabiki katika ukumbi wa Arcade, Mikocheni, wakishangilia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha hii haihitaji maelezo zaidi, maana vyupa vya bia vinaonekana wazi vikiwa vimeota kama uyoga, na hapo pembeni kushoto vuvuzela linapigwa kwa nguvu kuboresha haya makamuzi.

Mteja wa Pili wa CHANGAMOTO

Kitabu cha Changamoto kimepata mteja wa pili leo, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Amenunua nakala tano. Kwanza ninamshukuru mteja huyu kwa imani yake juu ya kitabu hiki, kama nilivyomshukuru mteja wa kwanza . Jambo la pili ni kuwa nafurahi kuona kuwa habari za kitabu hiki zinaenea. Hii ni ndoto na mategemeo ya kila mwandishi. Kwa upande wangu, nangojea kwa hamu mijadala itakayotokana na changamoto niliyotoa katika masuala mbali mbali ya jamii ya Tanzania na dunia ya leo. Nikizingatia imani ya wateja, namalizia kwa kuahidi kuwa nitaendelea kujibidisha katika kuifahamu zaidi lugha hii ya ki-Swahili, ili niweze kuitumia kwa ufasaha zaidi na kuandika maandishi bora zaidi. Hii ndio shukrani yangu kwao.

Mteja Wangu wa Kwanza

Image
Tarehe 8 Mei, 2010, mteja alinunua kitabu changu cha Changamoto , hapo mtandaoni kinapochapishwa. Niliguswa na kitu hicho, nikasema itabidi nikiongelee hapa kwenye blogu. Nimechapisha vitabu kadhaa, na wateja ninao. Siri moja ya uchapishaji vitabu mtandaoni kama ninavyofanya ni kuwa ninaweza kufuatilia mauzo ya vitabu saa yoyote. Ndio maana niliweza kuona kuwa mteja wa kwanza wa Changamoto amepatikana. Kitabu hiki ni cha pekee kwangu kwa sababu ni kitabu changu cha kwanza cha ki-Swahili. Mimi si mwandishi bora wa ki-Swahili, lakini naona nina haki ya kujipongeza kwa juhudi niliyofanya, hasa nikizingatia kuwa sisi wasomi ni wavivu katika kutumia ki-Swahili, na wengi tunaamini kuwa ki-Swahili hakina utajiri kama ki-Ingereza. Kwa vile nilisomea taaluma ya lugha na isimu ya lugha, ninaelewa kuwa dhana kama hii ni potofu. Hakuna lugha maskini. Kama mimi, ambaye ni mwalimu wa ki-Ingereza, nimeweza kujibidisha hadi kuandika kitabu kwa ki-Swahili, sioni kwa nini wasomi wengine wasiweze kufany

Tamaduni Zinapogongana

Yeyote anayefuatilia blogu zangu na maandishi mengine ataona kuwa ninashughulika sana na masuala ya tofauti za tamaduni hapa duniani. Ninatoa ushauri kwa taasisi, vyuo, makampuni, na watu binafsi kuhusu masuala hayo. Ninaendesha warsha hapa Marekani na Tanzania, na ninapangia kufanya hivyo katika nchi zingine za Afrika na duniani kwa ujumla. Haya ninayoongelea si mambo ya kinadharia tu wala ya kuyafanyia mchezo. Yasipoeleweka na kushughulikiwa ipasavyo, yanaweza kuwa na athari kubwa katika jamii na katika dunia yetu. Mifano ni mingi, nami naitaja katika warsha zangu. Napenda kuongelea kisa kimoja kilichosababisha niitwe kwenye mji wa Faribault, Minnesota, katikati ya mwezi Aprili mwaka huu, kutatua mgogoro uliokuwa unafukuta baina ya wa-Marekani ambao ni wafanyabiashara katika mji ule na wa-Somali ambao wamehamia katika mji ule, wengi wao wakiwa ni wakimbizi. Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro kati ya jamii hizi mbili. Wa-Somali, kama ilivyo kwetu Afrika wana jadi ya kuwa wanapokut

Vitabu Pepe

Kadiri siku zinavyopita na mabadiliko ya aina aina kutokea, yakiwemo mabadiliko ya tekinolojia, lugha nayo inawajibika kukabiliana na mabadiliko haya. Katika kuyamudu mabadiliko katika uwanja wa uandishi wa barua, kwa mfano, leo hii tuna kitu kiitwacho barua pepe. Zamani tulizoea barua ya karatasi na bahasha. Lakini leo tunaandika barua pepe, bila karatasi. Kama ninavyoeleza hapa na katika kitabu cha Changamoto , ulimwengu wa vitabu nao unabadilika kufuatana na mabadiliko ya tekinolojia. Leo vitabu vinaandikwa na kusomwa bila karatasi, sawa na barua pepe. Sasa sijui vitabu hivi tutaviita vitabu pepe au vipi.

Utalijua Jiji

Tangu kuanza kwa miji katika historia, wanadamu wamekuwa na hisia na fikra kuhusu miji na maisha ya mijini. Wametofautisha maisha ya mjini na maisha ya shamba, kama inavyojulikana. Kwa ujumla miji inachukuliwa kuwa sehemu ya maendeleo na usasa, na shamba ni sehemu iliyo nyuma au iliyolala usingizi. Mitazamo hii imeelezwa vizuri katika semi mbali mbali, hata katika utamaduni wetu. Kwa mfano, kuna usemi kuwa jogoo la shamba haliwiki mjini. Nakumbuka pia wimbo mmoja wa Mbaraka Mwishehe, mwanamuziki maarufu wa Tanzania, ambao una maneno ya kumbeza mtu wa shamba, kwamba "ulipotoka shamba kuingia mjini, mimi nilikuona...." Siti binti Saad yule mwimbaji maarufu wa zamani wa taarab alibezwa sana na wwashindani wake alipoingia mjini Unguja akitokea shamba alikokuwa mfinyanzI. Siku hizi Tanzania, mtu ukipata matatizo mjini, unaambiwa "utalijua jiji." Matapeli na wajanja wengine wa mjini wakikuibia, unaambiwa "umeingizwa mjini." Kutokana na mitazamo na itikadi