Friday, May 21, 2010

Mteja wa Pili wa CHANGAMOTO

Kitabu cha Changamoto kimepata mteja wa pili leo, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Amenunua nakala tano.

Kwanza ninamshukuru mteja huyu kwa imani yake juu ya kitabu hiki, kama nilivyomshukuru mteja wa kwanza. Jambo la pili ni kuwa nafurahi kuona kuwa habari za kitabu hiki zinaenea. Hii ni ndoto na mategemeo ya kila mwandishi. Kwa upande wangu, nangojea kwa hamu mijadala itakayotokana na changamoto niliyotoa katika masuala mbali mbali ya jamii ya Tanzania na dunia ya leo.

Nikizingatia imani ya wateja, namalizia kwa kuahidi kuwa nitaendelea kujibidisha katika kuifahamu zaidi lugha hii ya ki-Swahili, ili niweze kuitumia kwa ufasaha zaidi na kuandika maandishi bora zaidi. Hii ndio shukrani yangu kwao.

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Furaha ya mtu awaye yeyote yule ni kuona matunda ya jitihada zake. Ni jambo lenye kupendeza na kutia moyo mno kwa hatua kubwa uliyoifikia. Hadi sasa umeweza kuuza nakala sita. Si jambo dogo hata kidogo. Ni jambo lenye kuchochea hamasa ya uandishi.

Kuna wakati hapa nchini waandishi hawakuwa wakiandika sana vitabu. Hawakufanya hivyo si kwa sababu hawakuwa tayari kuandika, la hasha. Bali ilitokana na vitabu kutokuwa na soko. Tulishalijadili suala hili la watu kutopenda kusoma machapisho makini.

Lakini kwa jambo la kuandika kitabu na kupata wateja ni ndoto ya mwandishi, na ni hamasa aendelee mbele.

Napenda kukuongeza kwa dhati kwa mambo mawili. Mosi, kupata mafanikio kwa kitabu chako kununulika.

Pili, kwa changamoto unayotupatia sisi wengine.

Kila la kheri.

Mbele said...

Ndugu Mtanga, shukrani kwa ujumbe wako. Nikijiuliza kwa nini naandika, napata jawabu kwamba msingi mkubwa ni hamu yangu ya kutaka kujieleza. Nina jambo akilini na lazima nilieleze kimaandishi, nipate kuliona lilivyo. Ninachoandika kinakuwa kama kioo cha kuniwezesha kuona kilichomo katika nafsi au akili yangu.

Na nikishakitoa namna hiyo, najisikia faraja fulani, kama vile nimetua mzigo niliokuwa nabeba au nimeondoa nafsini mwangu kitu kilichokuwa kinanisongasonga. Najisikia huru, tayari kuwazia mambo mengine.

Suala la kuuza vitabu linakuja baadaye. Angalia, kwa mfano, nilivyofurahi baada ya kuchapisha kitabu cha CHANGAMOTO. Soma hapa

Sikuongelea mauzo, kwani furaha yangu ilikuwa katika kufanikiwa kuandika kitabu. Hiyo furaha peke yake ni motisha tosha ya kunifanya niendelee kuandika, hata kama watu hawatanunua. Ninajiridhisha mimi mwenyewe. Na ninataka niandike kwa ubora zaidi ili niendelee kujitazama kwenye haya maandishi na kuona hatua ninayopiga.

Ukiwa na moyo huu, huwezi kukata tamaa. Mauzo ni mengineyo.

Hata hivyo, ikiwa unaandika kwa namna ya kuelezea ukweli ulio ndani ya nafsi na akili yako, ni lazima utawagusa binadamu wenzako. Uhalisia na ukweli ni msingi wa kuwagusa wanadamu wenzako. Vitabu vinavyoandikwa kwa msingi huu havina msimu. Vinaendelea kuwagusa watu miaka na miaka, kama vile vya akina Shakespeare na Shaaban Robert.

Lakini vitabu vya udaku wa leo na jana, vitavuma msimu huu na vitatoweka msimu ujao.

Kuhusu kuuza vitabu, nimewahi kuelezea kiasi hisia na uzoefu wangu. Jambo la msingi ni kuwa siwabambikizi watu vitabu vyangu, hata kama wamesogea kwenye meza yangu wakati wa tamasha la vitabu. Huwa nawaelezea shughuli zangu kama mwalimu, mtafiti, na kadhalika, na umuhimu wa shughuli hizo, na jinsi ninavyozipenda.

Wanavutiwa na maelezo haya mambo muhimu ninayofanya, na hapo wanakuwa na duku duku ya kupata kitabu ili wakaendelee kunisikia zaidi. Ni muhimu uwavutie watu kwa namna hiyo kwanza, kama nilivyoelezea hapa.

Kuhusu umuhimu wa kuwaelezea watu shughuli zako na kuwaelezea fikra, mtazamo na mengine yanayokugusa katika nafsi yako, badala ya kuwabamibikizia vitabu vyako, angalia mfano kwenye video hii, ambayo nilikuwa najieleza wakati wa tamasha hapa Marekani, nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Niliongelea umuhimu wa tamasha lile, na mchango wangu kwenye tamasha lile, bila kutaja vitabu vyangu. Sikiliza hapa.

Kwa vile tumekubaliana kuwa wa-Tanzania hawana utamaduni wa kununua vitabu, labda viwe vya udaku, kilichopo ni kuendelea kuandika ukizingatia kuwa dunia nzima ndio uwanja wako.

Kama unaandika kwa ki-Swahili, kumbuka kuwa wako watu wanaotumia ki-Swahili Kenya, Ulaya, pande za Arabuni, Marekani, na sehemu nyingine nyingi. Kama unaandika kwa ki-Ingereza, ni hivyo hivyo. Dunia ya leo imeunganishwa na tekinolojia za mawasiliano kiasi cha kuwa kama kijiji kidogo. Hakuna mipaka. Kazi tuliyo nayo ni kuendelea kujielimisha kwa dhati na kuandika.

Christian Bwaya said...

Ninatamani sana niwe mteje wako wa tatu. Kwa bahati mbaya itanibidi nisubiri mpaka kitakapoanza kupatikana madukani.

Mbele said...

Ndugu Bwaya, shukrani kwa ujumbe. Najitahidi vitabu vyangu viwe vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0717 413 073 au 0788 888 647. CHANGAMOTO nacho kitapatikana mwezi ujao. Siku za usoni, nataka vipatikane sehemu zingine, zikiwemo nchi jirani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...