Tuesday, May 25, 2010

Warsha Kuhusu Utamaduni na Utandawazi, Juni 12, 2010

Hebu fikiria: hao wa-Tanzania wanaoondoka nchini kwenda kufanya kazi nchi za mbali au kutafuta biashara, kusoma, na kadhalika, wanakuwa wamejiandaa vipi kukabiliana na tamaduni za huko wanakoenda? Wageni wanaokuja Tanzania kwa shughuli mbali mbali, au kama wahamiaji, nao wanakuwa wamejiandaa vipi kuishi katika utamaduni wetu?

Masuala ya aina hii yameanza kupata umuhimu wa pekee duniani, kutokana na kuimarika kwa utandawazi. Ni aina ya masuala ambayo ninayashughulikia sana, kama mwandishi, mtoa mada na mwendesha warsha, hasa huku Marekani.

Ni muhimu wa-Tanzania nao wajipange na kujiandaa ipasavyo, kwani kama ninavyosema mara kwa mara katika blogu hii, ushindani unaendelea kushamiri duniani, na uwezo wa kukabiliana na ushindani huu unatokana na elimu, ujuzi na maarifa.

Tarehe 12 Juni nitaendesha warsha Tanga, kuhusu utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nimeshaendesha warsha za aina hii kabla hapa Tanzania. Yeyote anakaribishwa.

Kwa taarifa zaidi kuhusu warsha ya tarehe 12 Juni, soma hapa.

6 comments:

Fadhy Mtanga said...

Mimi nasubiri kwa hamu kubwa warsha itakayofanyika hapa Dar es Salaam. Naamini nitapata nafasi ya kutosha ya kujifunza mambo mengi.

Karibu sana Tanzania.

Katu said...

Profesa Mbele, nasikitika kwamba sitaweza kushiriki mjadala huo wa JUne wakati huo nitakuwa katika kilele cha kipindi cha mavuno ya mpunga..

Nategemea kusikia ama kuona kutoka vyanzo vingine vya kuwasilisha habari kwa wananchi hiyo semina ya Juni.

Nguvu ya teknolojia ya mwasailiano inaniwezesha kuwasilisha maoni na mawazo binafsi kutoka hapa kijijini kwangu Lungongole-Kikwawila-Ifakara

Mbele said...

Bado natafuta sehemu ya kufanyia warsha hapa Dar es Salaam. Kwa vile niko mbali, inakuwa vigumu kidogo hasa kwa vile mabadiliko ni mengi hapa Dar es Salaam kama ilivyo sehemu zingine.

Lakini bado muda ninao. Nategemea kupata sehemu muafaka, na nitatoa matangazo.

Yasinta Ngonyani said...

Kwa kweli hili ni jambo zuri sana. Nasikitika sipo nawe katika shughuli hii mana hata hapa niishipo pana utamaduni ambao ni tofauti sana. Nazidi kupata moyo na kufurahi kuona unawakirisha ila ipo siku nami nitafanya hili na najua nitaomba msaada wapi. Kila la kheri.

Mbele said...

Dada Yasinta, mimi naona kuwa tayari unafanya mambo hayo tunayoongelea. Unavyowapeleka watoto wako Songea, Mbambabay, na kadhalika, na kuwapa fursa ya kuishi maisha ya kule, pamoja na ndugu, jamaa, majirani, na wapita njia, kuona wanavyosalimia, wanavyoongea, na kadhalika, tayari unafanya kwa vitendo hayo ninayoyaongelea kwenye warsha au kuandika vitabuni.

Utakapoamua, utaweza bila tatizo kuwaeleza watu wa nyumbani tofauti za utamaduni wetu na ule wa Sweden. Na hata kitabu ningekushauri uanze kutunga. Mimi ninaufahamu utamaduni wa waMarekani, na ndio ninaouandikia. Kuhusu utamaduni wa Sweden ni lazima tukusikilize wewe. Kwa hivi, kazi kwako.

Mbele said...

Leo nimeona tangazo la ajira ambalo linawataka waomba ajira wawe na sifa kadhaa. Sifa mojawapo ni kufahamu suala la tofauti za tamaduni duniani, na kufahamu namna ya kushughulika na watu wa tamaduni mbali mbali. Bofya hapa

Haya ndio masuala ninayoyaongelea katika warsha zangu na katika blogu zangu. Wenye masikio watasikia. Huku ughaibuni hakuna tatizo, kwani watu wananitafuta wenyewe na wanasikiliza kwa makini, kama inavyoonekana katika blogu zangu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...