Posts

Showing posts from October, 2008

Mwalimu Nyerere na Elimu

Image
Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwalimu. Naamini ni sahihi kusema kuwa silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na hatimaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa, na daima alikuwa anafundisha. Ninachotaka kuongelea hapa ni mchango wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa elimu. Elimu ni suala mojawapo ambalo Mwalimu Nyerere alilishughulikia sana. Katika kuelezea suala la elimu, Mwalimu aliweka na kufuata misingi kadhaa muhimu. Tanganyika ilipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa ameshajizatiti kubadilisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni, ambao ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Kulikuwa na shule za wazungu, za Wahindi, na za watu weusi. Mara tulipopata Uhuru, Nyerere alifuta ubaguzi na kuwachanganya wanafunzi mashuleni. Tangu mwanzo, Mwalimu Nyerere aliamini dhana ya usawa wa binadamu. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu. Alifanya kila juhudi kutoa elimu kwa watu wote, kuanzia watoto hadi watu wazima. Mwalimu alij

Watoto wa Marekani

Image
Ingawa kazi yangu kuu hapa Marekani ni kufundisha katika kiwango cha chuo kikuu, kufanya utafiti katika taaluma zangu, na kutoa mchango wa mawazo na uzoefu kwa walimwengu kwa ujumla, napenda sana kukutana na kuongea na watoto, kuwasilimulia hadithi za Afrika, na kuwaeleza kuhusu maisha ya Afrika na masuala mengine ya maisha kwa ujumla, katika nchi yao na duniani. Nimeshaongea na watoto kwenye miji mbali mbali, katika mikoa ya Colorado, Minnesota, Pennyslvania, na Wisconsin. Watoto ni watoto. Kitu kimoja wanachopenda ni hadithi. Nami nimekuwa na fursa nyingi za kuwasimulia hadithi za Kiafrika. Kitu kimoja kinachofurahisha ni jinsi watoto walivyo na akili ya kufuatilia hadithi na kuzichambua. Hata watoto wanaodhaniwa kuwa hawana akili sana au hawana moyo wa kupenda masomo, wanaonyesha msisimko wanaposimuliwa hadithi. Hapa kuna taarifa kuhusu nilivyokutana na watoto wa shule ya LeTort, Pennsylvania. Soma hapa Jambo hili limenifanya nikumbuke habari moja

Wasomaji wa Maandishi Yangu

Image
Uandishi ni shughuli inayohitaji juhudi na ustahimilivu. Inaweza kuleta mema au mabaya katika jamii. Kwa hivi, mwandishi anapaswa kuwa makini. Uandishi unaweza kuwa na manufaa mengi, kwa mwandishi mwenyewe na kwa jamii. Kuandika kunatupa fursa ya kutumia akili katika kupanga mawazo na lugha. Ni zoezi la kuchangamsha na kuboresha akili. Kitu kimoja kinachonipa faraja sana na motisha pia, ni kufahamiana na watu mbali mbali, kwa njia ya maandishi yangu. Najifunza mengi kutokana na maoni ya wasomaji. Napenda kwenda sehemu mbali mbali kuwaonyesha watu maandishi yangu na kuongelea shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, na uandishi. Napenda pia kuelezea ninavyojishughulisha katika kutoa ushauri kwa wageni mbali mbali, hasa Wamarekani, wanaokwenda Afrika, kama wanafunzi, watafiti, watalii, na washiriki katika shughuli za kujitolea. Baadhi ya picha zinazoonekana hapa zilipigwa Minneapolis, tarehe 4 Oktoba, 2008, wakati wa sherehe za kumbukumbu ya Uhuru wa Nigeria. Nilipata fursa ya kushiriki

Mwalimu Julius Nyerere

Image
Nimeona kuwa andiko la kwanza liwe juu ya Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu Nyerere ni mtu maarufu katika historia ya Tanzania. Katika ukumbi huu athari za mawazo na siasa za Mwalimu Nyerere zitajitokeza mara kwa mara, kwani alichangia kuiwezesha Tanzania kupitia hatua ilizopitia, akishirikiana na wazalendo wenzake, ambao nao watakuwa wanatajwa hapa ukumbini, kila itakapobidi. Mwalimu Nyerere anastahili kukumbukwa, kwa mchango wake mkubwa, sio tu kwa nchi yetu bali kwa dunia. Tunapaswa kusoma maandishi yake na kuyajadili, kuyatathmini, na kuyakarabati inapobidi, ili yaendelee kuwa mwongozo wetu. Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa fikra, ambaye daima alikuwa anaangalia maslahi ya nchi yetu, na jitihada alizofanya katika kubadilisha siasa, uchumi, utamaduni, na vipengele vingine vya nchi yetu ilikuwa ni kwa nia ya kuikomboa na kuijenga katika misingi ya uhuru, usawa, haki, na kujitegemea. Yako makosa ambayo alifanya, lakini alikuwa mzalendo, aliyeamini kuwa aliyokuwa anafanya ni kwa maslahi

Karibu, hapa kwetu

Karibu. Hapa ni kwetu--Watanzania, Waafrika, na wengine wanaotumia kiSwahili. Ninategemea kuwa huu utakuwa ukumbi wa masuala yanayotuhusu: katika siasa, uchumi, utamaduni, na jamii kwa ujumla. Namshukuru sana ndugu Freddy Macha, ambaye alinipa wazo la kuanzisha blogu. Freddy ni Mtanzania mwenye uwezo wa pekee katika fani mbali mbali, hasa muziki na uandishi. Anafanya kazi kubwa ya kuwaelisha na kuwaunganisha walimwengu. Namshukuru sana pia ndugu Jeff Msangi kwa kunihamasisha kwa namna mbali mbali. Jeff ni hodari katika kuelimisha umma kwa namna mbali mbali. Karibuni.