Posts

Showing posts from March, 2017

Tangazo la Mhadhara Chuo Kikuu cha Minnesota Rochester

Image

Mpiga Debe wa Vitabu Amenifuata

Image
Jana niliandika katika blogu hii kuhusu programu inayowapeleka watu wa Nebraska Tanzania, ambao wanashauriwa kusoma  Africans and Americans Embracing Cultural Differences . Nilikiri kuwa niliandika kama vile ninajipigia debe, lakini nilipendekeza utamaduni huo. Ilikuwa kama nimeota, kwani leo nimepigiwa simu na kuletewa ujumbe na kampuni ya Readers Magnet inayojishughulisha na utangazaji wa vitabu. Mama aliyenipigia alisemaa kuwa wanakifahamu kitabu changu kutokana na taarifa za wasomaji katika mtandao wa Amazon.  Wangependa kukijumlisha katika orodha ya vitabu wanavyovitangaza, akafafanua mipango yao, ikiwemo kuwakilisha katika maonesho ya vitabu ya Frankfurt. Kwa kuwa maelezo yalikuwa mengi, nilimwuliza kama anaweza kuniletea kwa maandishi, akakubali. Ameniandikia ujumbe, ambao unaanza hivi: Your book, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , was recommended to us by our Book Scouts. We believe and we have validated that your unique book has the potential an

Kitabu kwa Wasafiri Watokao Nebraska

Image
Leo nimeona taarifa kutoka sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, kuhusu maandalizi ya safari za kwenda Tanzania. Safari hizo zimefanyika tangu miaka iliyopita. Kuna sehemu iitwayo "Preparatory Reading," na kama miaka iliyopita, katika sehemu hiyo kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimependekezwa kwa wasafiri hao: For those persons wanting to more deeply explore cultural differences between Africans and Americans, the book Africans and Americans: Embracing Cultural Differences by Joseph Mbele is recommended. The book is available at www.africonxion.com. Kwangu kama mwandishi, hii ni habari njema, ingawa si mpya. Viongozi wa programu kama hiyo ya Nebraska wana uzoefu wa miaka mingi wa kwenda Tanzania. Wana uzoefu wa utamaduni wa Tanzania. Kuendelea kwao kukipendekeza kitabu changu ni ushahidi kuwa wameona kinawafaa wa-Marekani wanaowapeleka Tanzania. Watu kutoka Nebraska wanaosairi kwenda Tanzania nimewahi kuwataja k

Nimenunua "Two Thousand Seasons" (Ayi Kwei Armah)

Image
Leo nilienda St. Paul, na wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley kuangalia vitabu katika duka la Half Price Books, kama ilivyo kawaida yangu. Hilo duka lina maelfu ya vitabu, na wateja wanapishana humo tangu asubuhi hadi jioni. Kila ninapoingia katika duka la vitabu, ninajikuta nikianza kuangalia kama kuna vitabu vipya juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Leo sikuona kitabu kipya juu ya Hemingway, nikaenda sehemu nyingine humo dukani, kwenye kona kabisa, ambapo sikosi kupitia. Hapo, katikati ya msitu wa vitabu, niliona kitabu cha Ayi Kwei Armah, Two Thousand Seasons . Sikutegemea kukuta kitabu cha Armah. Nilikichukua hima, huku nikikumbuka enzi za ujana wangu Tanzania, kwani ni wakati ule ndipo nilianza kusikia habari za Ayi Kwei Armah. Tangu nikiwa mwanafunzi sekondari, nilikuwa nafuatilia sana fasihi ya ki-Ingereza. Somo la fasihi ni somo nililolipenda na kuliweza sana. Nilipoingia Chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973, ndipo nilipofahamu kuwa Ayi Kwei Armah alikuwa anai

Maktaba ya Chuo Kikuu cha Minnesota

Image
Mara kwa mara, ninaandika kuhusu maktaba ninazozitembelea, hapa Marekani na Tanzania. Mifano ni maktaba ya John F. Kennedy,   ya Brookdale,   ya Southdale,   ya Moshi,   ya Tanga,   ya Iringa,   ya Dar es Salaam, na ya Songea. Jana, nilikuwa Minneapolis kwa shughuli binafsi. Baadaye niliingia katika maktaba ya Wilson. Nimezoea kwenda kusoma katika maktaba hii, ambayo ni moja ya maktaba za Chuo Kikuu cha Minnesota. Kati ya hizo, hii ndio inayonihusu zaidi, kwa sababu humo ndimo kuna majarida, vitabu, na hifadhi za lugha na fasihi. Ingawa chuoni St. Olaf ninapofundisha pana maktaba kubwa, ambayo imeunganishwa na maktaba ya chuo cha Carleton,   maktaba ya Wilson ni kubwa zaidi. Picha zinazoonekana hapa nilipiga jana. Hiyo ya juu ni ubavuni mwa maktaba, na hiyo ya chini ni sehemu ya mbele, kwenye mlango. Ardhini inaonekana theluji, kwani ni bado kipindi cha baridi.

"The Fear:" Shairi la Robert Frost

Image
Leo nimesoma "The Fear," shairi la Robert Frost, kwa mara ya kwanza. Limenigusa kwa namna ya pekee. Shairi linavyoanza, tunaona kuwa ni usiku, na kuna watu wawili, mwanamme na mwanamke, nje ya nyumba, na kuna mwanga kiasi wa taa. Lakini giza imetamalaki. Mwanamke anaingiwa na hofu baada ya kuona uso wa mtu gizani, lakini kwa sababu ya giza, hajulikani ni nani. Wakati mwanamme anasisitiza kuwa hajasikia wala kuona chochote, mwanamke anataka kwenda kuangalia. Si vizuri niandike muhtasari, bali ni bora niliweke shairi hapa. Baada ya kulisoma, nimeangalia namna wahikiki walivyolichambua, nikaona linavyowakanganya. Hatimaye, nimeona mtandaoni jinsi mama moja anavyolisoma shairi hili, nikavutiwa sana na usomaji wake, kama unavyosikika hapa: The Fear A LANTERN light from deeper in the barn Shone on a man and woman in the door And threw their lurching shadows on a house Near by, all dark in every glossy window. A horse’s hoof pawed once the hollow floor, And the back of

Mashairi ya Robert Frost

Image
Leo nina jambo la kusema, kuhusu mashairi ya Robert Frost, ambayo nimekuwa nikiyasoma sambamba na kazi zingine za fasihi au taaluma. Ni mazoea yangu kusoma kiholela, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Mashairi ya Frost ninayoongelea yamo katika kitabu kiitwacho Robert Frost: Selected Poems , ambacho binti yangu alininunulia. Wakati ule, nilijitahidi kuyasoma, lakini ninayafurahia zaidi wakati huu, labda ni kwa kuwa akili yangu imetulia kuliko wakati ule. Leo, kwa mfano, nimesoma shairi liitwalo "The Black Cottage." Tunaelezwa kuhusu watu wawili wanavyoijongea nyumba ndogo iliyofichika nyuma ya miti na nyasi mbali na barabara. Wanaikaribia na kuchungulia ndani. Mmoja wao, ambaye ni mchungaji, anafahamu habari za nyumba hii ambayo sasa haina watu. Anamweleza mwenzake kuwa bibi kizee aliyeishi humu alifariki, na watoto wake, wote wanaume, wanaishi mbali, ila hawataki kuiuza nyumba wala chochote kilichomo. Walipangia kuwa wanakuja mara moja kwa mwaka, lakini mw

Vitabu Nilivyonunua Leo

Image
Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi nilipitia Apple Valley nikaingia katika duka la Half Price Books. Kama kawaida, nilitaka kuona vitabu mbali mbali, lakini nilikuwa hasa na dukuduku ya kuona kama kuna vitabu juu ya Ernest Hemingway. Kwa hivyo, nilivyoingia tu dukani, nilienda moja kwa moja kwenye sehemu vinapowekwa vitabu vya Hemingway, yaani vilivyoandikwa naye au juu yake. Tofauti na siku zingine, leo nilikuta vitabu vichache, na vyote ni vile alivyoandika Hemingway mwenyewe. Nilikiona kitabu ambacho sikumbuki kama nimewahi kukiona kabla, The Fifth Column and Four Stories of the Spanish Civil War , nikakiangalia. Niliona kuwa "The Fifth Column" ni tamthilia, ambayo sina katika maktaba yangu. Papo hapo nilihisi kuwa hadithi zilizomo katika kitabu ziko katika kitabu cha The Complete Short Stories of Ernest Hemingway , ambacho ninacho. Nimethibitisha hivyo baada ya kuja nyumbani. Nilipotoka sehemu vinapowekwa vitabu vya Hemingway, nilienda sehemu ambapo

Nimemsikiliza Angela Davis Leo

Image
Leo hapa chuoni St. Olaf tumepata fursa ya kutembelewa na Angela Davis, profesa na mwanaharakati maarufu. Kwangu imekuwa siku ya kumbukumbu. Mara ya kwanza kumsikiliza Angela Davis ni siku alipotoa mhadhara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1974, kama sikosei. Nilikuwa mwanafunzi na ninakumbuka jinsi mwanaharakati huyu mrefu mwenye Afro kubwa kichwani alivyotusisimua kwa hotuba yake katika ukumbi wa Nkrumah. Leo ameongelea hali ya ulimwengu kwa kuzingatia majanga yanayotokana na mfumo wa ubepari na mikakati ya kukabiliana yao.  Hotuba yake hii hapa: https://www.stolaf.edu/multimedia/play/?e=1816