
Nimefundisha riwaya ya
Things Fall Apart ya Chinua Achebe tangu yapata mwaka 1976, sehemu kama
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Burundi, na vyuo vya
Colorado na
St. Olaf.
Kutokana na uzoefu huu, na mengi niliyojifunza, na kwa lengo la kuweka kimaandishi mawazo yangu juu ya riwaya hii, niliandika mwongozo. Nimeshaongelea kidogo kuhusu mwongozo huu katika
blogu hii, lakini napenda kueleza zaidi habari zake.
Aliyenisukuma kuandika mwongozo huu kwa wakati niliofanya hivyo ni rafiki yangu A.S. Muwanga, aliyekuwa katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yeye na mimi tulikubaliana kuwa niandike pia mwongozo kuhusu kitabu cha
The African Child, kilichoandikwa na Camara Laye. Muwanga alifanya mpango na kitabu kilichapishwa mwaka 1988 na Nyanza Publications Agency kama inavyoonekana katika picha hapo juu. Lengo mahsusi lilikuwa ni hasa kuwasaidia wanafunzi wa sekondari waliokuwa wanasoma riwaya hizo.
Miaka hiyo, 1976 hadi 1991, nilikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka huo 1991, niliondoka pale mwaka 1991, nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf, katika idara ya kiIngereza.

Mwaka 1997, bodi ya
South Dakota Humanities Council iliyokuwa ikiratibu mradi wa usomaji katika jimbo la South Dakota iliniomba kuandika mwongozo kuhusu
Things Fall Apart. Katika utaratibu wao, walikuwa wanachagua kitabu ili kisomwe na vikundi mbali mbali katika jimbo zima.
Ili kuchangia zoezi hili, walikuwa wana utaratibu wa kutafuta mtu wa kuandika mwongozo kuhusu kitabu husika, na mwongozo huu ulikuwa unatumiwa sambamba na kitabu husika. Kila kikundi kilikuwa kinajadili kitabu kweye mji wao, au eneo lao, na kisha walikuwa wanajumuika na wenzao wa sehemu zingine katika mjadala kwa njia ya barua pepe.
Mwaka huo 1997 kitabu kimojawapo walichokuwa wamekichagua ni
Things Fall Apart. Ndio maana nikaombwa kuandika mwongozo. Nilitumia fursa hii kurekebisha ule mwongozo niliouchapisha Dar es Salaam. Kwa vile ilikuwa imepita miaka mingi nami nilikuwa nimetafakari zaidi riwaya ya
Things Fall Apart niliweza kuweka marekebisho na kuuboresha mwongozo ule.
Kitabu kingine kilichokuwa kinajadiliwa ni
Crimes of Conscience cha Nadine Gordimer, na aliyeombwa kuandika mwongozo ni profesa Karen A. Kildahl. Kazi yake na yangu zilichapishwa katika kijitabu kimoja, kama inavyoonekana katika picha hapo juu. Yeye na mimi tulialikwa kwenda kuendesha warsha kuhusu hivi vitabu viwili, katika mji wa Brookings, warsha ambayo ilihudhuriwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za jimbo la South Dakota.
Mpango huu wa kuhamasisha usomaji katika jimbo zima ulinivutia sana, nikaona kuwa kama tungeweza kufanya jambo kama hili Tanzania, kuwafanya watu wajadili kitabu kimoja baada ya kingine, katika mkoa mzima au nchi nzima, tungefika mbali sana. Hatimaye, wahusika katika bodi hii ya
South Dakota Humanities Council waliuweka mwongozo wangu wa
Things Fall Apart mtandaoni, ukatumiwa na watu kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Nilianza kuwazia umuhimu wa kuufikisha huu mwongozo Tanzania, ukiwa umeboreshwa zaidi. Niliurekebisha, nikauchapisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwaka 2003, kwa gharama ya dola 520 za Marekani.
Wakati huo nilikuwa nimeanzisha kijikampuni, na kukisajili hapa Minnesota, kwa jina la Africonexion. Shughuli zake ni masuala ya elimu, kama vile kutoa ushauri, warsha, uandishi na uchapishaji. Nilivyochapisha mwongozo huu Dar e Salaam, nilitumia jina la Africonexion kama kampuni husika.
Hata hivi, lazima niseme ukweli. Pamoja na juhudi hizi zote, sikuona mwamko wa kuridhisha miongoni mwa wa-Tanzania, wa kutumia fursa niliyowaletea. Lakini, naridhika kwamba sina lawama. Kama vijana wa shule wa Rukwa, Pemba, Morogoro na Kondoa hawana kitabu kama hiki, kosa ni la wananchi na serikali. Mimi kama mwalimu nawajibika kusema kuwa serikali inapotosha ukweli inaposema haina hela, wakati kila mtu anaona jinsi inavyofuja hela, kwa magari ya fahari, na kadhalika. Tabia hiyo na wananchi wanayo pia, kama nilivyoeleza
hapa.

Harakati za mwongozo huu ziliendelea. Mwaka 2005 nilikuwa nimechapisha kitabu mtandaoni, kiitwacho
Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Baada ya kuvutiwa na uchapishaji wa aina hii, niliamua kuchapisha mwongozo wangu wa
Things Fall Apart kwa njia hiyo hiyo. Niliufanyia marekebisho na kuuboresha, na hatimaye niliuchapisha, kama inavyoonekena katika picha kushoto.
Mwongozo wangu huu unawafaidia wengi. Nilifurahi, kwa mfano, nilipoona umechaguliwa na Chuo Kikuu cha Cornell kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokuwa wanatakiwa kusoma
Things Fall Apart.
Huo ni utaratibu wao, kwamba wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza wasome kitabu fulani, na vitabu hubadilika mwaka hadi mwaka. Kwa jinsi Chuo Kikuu cha Cornell kilivyo maarufu duniani, na kwa kuwa kuna vijitabu vingi na machapisho mengine kuhusu riwaya hii, kuchaguliwa mwongozo wangu ni heshima ya pekee.
Soma hapa. Niliumiza kichwa kwa miaka mingi kuufikisha mwongozo huu kwenye kiwango hiki na nilijua ubora wake, kwani hilo ni somo langu, lakini inapendeza pia kuwasikia wataalam wengine wanaonaje.
Ninaendelea na shughuli ya kuandika miongozo kwa vitabu vingine. Kwa mfano, ninataka kurekebisha mwongozo wangu wa
The African Child, ili niuchapishe kama kijitabu. Vile vile, kwa miaka kadhaa nimejishughulisha na uandishi wa mwongozo wa utungo maarufu wa
Song of Lawino, uliandikwa na Okot p'Bitek. Nikijaliwa uzima, nitaandika sana siku za usoni. Kwani kazi na wajibu wa mwalimu ni nini?