Mteja wa Uingereza Kanunua Kitabu

Leo kwenye tovuti ninapochapisha vitabu vyangu nimeona kuwa mteja aliyeko Uingereza amenunua nakala ya Notes on Achebe's Things Fall Apart. Uzuri wa uchapishaji wa namna hii ninayotumia ni kuwa mwandishi unaweza kufuatilia taarifa kama hizi za mauzo, ukajua kitabu kimenunuliwa sehemu gani ya dunia, nakala ngapi, na malipo yako ni kiasi gani.

Kwa miaka yote tangu nilipoanza kuchapisha vitabu kwenye tovuti ya lulu.com maelfu ya wateja walionunua vitabu vyangu wamefanya hivyo kutokea hapa Marekani. Nilikuwa na hisia kuwa hii ni kwa kuwa utamaduni wa kununua vitu mtandaoni ulikuwa bado kujengeka sehemu zingine za dunia.

Ninahisi kuwa huyu mteja aliyenunua Notes on Achebe's Things Fall Apart ni mwalimu wa fasihi. Kama ni hivyo, ninafurahi kuwa atapata mawazo mapya juu ya Things Fall Apart. Ingawa kuna miongozo mingi ya Things Fall Apart, mwongozo wangu umepata umaarufu hata ukateuliwa kama mwongozo kwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Cornell, ambacho kina jina kubwa katika masomo ya lugha na fasihi ya ki-Ingereza.

Vile vile, hivi karibuni, nilipohudhuria mkutano wa Africa Network, profesa Eric Michael Washington wa chuo cha Calvin aliniambia jinsi anavyotumia mawazo yaliyomo katika mwongozo huo, katika ufundishaji wake wa Things Fall Apart. Alisema anavutiwa zaidi na jinsi ninavyomwelezea mhusika aitwaye Unoka.

Mambo hayo yananipa hamasa ya kuendelea kuandika miongozo ya kazi za fasihi, azma ambayo niliwahi kuielezea katika blogu hii. Mimi kama mwalimu wa fasihi ninafarijika kuyaweka hadharani mawazo yangu kuhusu fasihi, ambayo yatadumu. 

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini