Tuesday, November 22, 2016

Ninaendelea Kusoma "Hamlet"

Miaka miwili iliyopita, niliandika katika blogu hii kuwa nina tabia ya kusoma vitabu kiholela. Wakati wowote nina vitabu kadhaa ninavyovisoma, bila mpangilio maalum, na pengine bila nia ya kufikia mwisho wa kitabu chochote.

Kusoma kwa namna hii hakuna ubaya wowote, bali kuna manufaa. Nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari, katika seminari ya Likonde, mwalimu wetu, Padri Lambert OSB alituhimiza tuwe na mazoea ya kusoma sana vitabu, na pia mazoea ya kuvipitia vitabu kijuu juu, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "browsing."

Nikiachilia mbali vitabu ninavyofundisha, wakati huu nimezama zaidi katika kusoma Hamlet, kama nilivyoandika katika blogu hii. Ninasoma Hamlet pole pole, ili kuyanasa vizuri akilini yaliyomo, hasa maudhui kuhusu maisha, maadili, na tabia za binadamu. Kusoma pole pole kunaniwezesha kukifurahia ki-Ingereza cha Shakespeare, ingawa si rahisi kama ki-Ingereza tunachotumia leo.

Tofauti kati ya ki-Ingereza cha leo na kile cha Shakespeare ninaifananisha na tofauti kati ya ki-Swahili cha leo na kile cha mashairi ya zamani kama yale ya Muyaka au Utenzi wa Rasi lGhuli. Kwa msingi huo, kusoma utungo kama Hamlet ni chemsha bongo inayoboresha akili, sawa na mazoezi ya viungo yanavyoboresha afya ya mwili.

Mwandishi maarufu Ernest Hemingway alielezea vizuri thamani ya vitabu aliposema, "There is no friend as a loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Ujumbe uko wazi, nami sina la kuongeza. Kitabu bora ukishakinunua, ni rafiki wa kudumu.


  

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...