Nimenunua Webster's Concise Dictionary and Thesaurus

Jana nilinunua nakala ya Webster's New World Concise Dictionary and Thesaurus, iliyochapishwa mwaka 2014. Hili ni toleo jipya la kitabu hiki ambacho kimekuwa kikichapishwa kwa miaka mingi. Kitabu hiki ni hazina ya pekee kwa kuwa kinajumlisha kamusi na "thesaurus."

Kwa wale wasiofahamu tofauti za vitu hivi viwili, napenda kusema kwa kifupi kwamba kamusi hutoa tafsiri za maneno. "Thesaurus," badala ya kutoa tafsiri ya neno, huorodhesha maneno ambayo maana zake zinafanana au kukaribiana na neno hilo.

Kwa mfano, katika kitabu nilichonunua leo, sehemu ya thesaurus, neno "docile" limewekewa maneno yafuatayo: "meek, mild, tractable, pliant, submissive, accommodating, adaptable, resigned, agreeable, willing, obliging, well-behaved, manageable, tame, yielding, teachable, easily influenced, easygoing, usable, soft, childlike."

Mfano huu unaonyesha wazi ubora na upekee wa "thesaurus." Kwa kuyaorodhesha maneno yenye maana zinazofanana au kukaribiana, mtu unakumbushwa msamiati wa lugha. Kama ni mzoefu wa kusoma unayeyatambua maneno hayo na unapenda kuchagua neno la kulitumia, kazi yako inakuwa imerahisishwa. Inatakiwa uwe na ufahamu wa tofauti ndogo ndogo za maana au msisitizo zilizomo katika maneno kama zile ambazo kwa ki-Ingereza huitwa "denotation" na "connotation" ili uweze kuchagua neno lifaalo kuliko mengine katika muktadha wa uandishi wako.

Nimenunua Webster's New World Concise Dictionary and Thesaurus ingawa ninazo "thesaurus" tangu zamani, nilipokuwa sekondari, ambapo niliifahamu Roget's Thesaurus. Kwa nini nimenunua "thesaurus" nyingine leo? Ni kwa kuwa ni toleo jipya. Vile vile, mara kwa mara ninanunua kitabu ambacho nakala yake ninayo, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii.

Nakala za ziada za vitabu muhimu ni baraka. Ninapokwenda Tanzania, huwa sikosi kuchukua vitabu kadhaa kuzigawa kwenye maktaba za jamii au vyuo. Kwa miaka mingi, nimekuwa na wazo kwamba ukipeleka kamusi ya ki-Ingereza, kwa mfano, kwenye shule yoyote, ni kama unaanzisha mapinduzi katika ufundishaji wa somo la ki-Ingereza katika shule hiyo. Unakuwa umemwezesha mwalimu kufahamu uandishi sahihi wa maneno ya ki-Ingereza. Vile vile, kwa kuwa kamusi kwa kawaida hutoa pia mifano ya matumizi ya maneno, unakuwa umemjengea mwalimu fursa ya kujiongezea ufahamu wa lugha. Unakuwa umeweka msingi wa kuboresha somo la ki-Ingereza kwa wanafunzi.

Kitabu ni rasilimali na pia ni mtaji. Kupeleka kitabu muhimu popote nchini kikasomwe ipasavyo ni aina ya uwekezaji. Hilo ni jambo linaloeleweka kwa yeyote anayefahamu kuwa dunia inaingia zaidi na zaidi katika enzi za uchumi unaoendeshwa na elimu na maarifa. Hiyo ndiyo dhana ya "knowledge economy." 

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini