Posts

Showing posts from February, 2013

Mhadhara Wangu Leo Umekuwa Mzuri

Mhadhara wangu leo katika chuo cha South Central umekwenda vizuri sana. Nilijua hali ingekuwa hivyo, kwani nilikuwa naongelea masuala ambayo nina uzoefu nayo kwa miaka mingi. Niliongea na wanafunzi wakiwa mbele yangu na wengine wakiwa mji wa Mankato ila tunaonana nao kwenye skrini ya televisheni. Walimu wao walijigawa sehemu hizo mbili. Mhadhara ulikuwa juu ya kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho maprofesa waliwaelekeza wanafunzi wakisome kabla ya mhadhara wangu. Niliibua masuala mengi, kwa muhtasari, nikianzia na uzoefu wangu kama mshauri wa programu zinazopeleka wanafunzi na watu wengine Afrika. Nilielezea nilivyoandika kitabu hiki , na changamoto zake. Hatimaye, nilitoa nasaha kuhusu mambo ya msingi ya kukumbuka tunapokutana watu wa tamaduni mbali mbali. Kipindi cha masuali na majibu kilifana sana. Nilifurahi kuona jinsi wanafunzi na maprofesa walivyokuwa wanakinukuu kitabu, hata kunikumbusha vipengele ambavyo sikuvikumbuka. Mwishoni

Mhadhara Kesho Kuhusu Kitabu Changu

Image
Miezi kadhaa iliyopita, niliandika kuhusu mwaliko niliopewa na maprofesa Scott Fee na Becky Davis wa Mankato, Minnesota, kwenda kuongea na wanafunzi wao ambao walikuwa wanawaandaa kwa safari ya Afrika Kusini. Ombi lilikuwa kwamba nikaongee na wanafunzi hao kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, ambayo nimeyaongelea katika kitabu cha cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Siku zimeenda kasi, maana kesho ndio siku ya mhadhara huo. Badala ya kwenda Mankato, nitatoa mhadhara wangu katika chuo cha South Central kilichopo Faribault. Mhadhara wangu utarushwa kwa televisheni kuwawezesha wanafunzi watakaokuwa Mankato kuufuatilia. Nimepangia nikawape mhadhara wa kuelimisha na kusisimua. Profesa Becky Davis atakuwepo nami Faribault na ndiye atakayenipokea na kunitambulisha. Profesa Fee atakuwa Mankato, pamoja na wanafunzi, wakinisikiliza. Kama kawaida, nafurahi kupata fursa ya kuongelea masuala ya tofauti za tamaduni. Kama kawaida, nafurahi kuona kitabu changu kina

Maonesho Yamefana St. Paul, Minnesota

Image
Maonesho kuhusu watu weusi yaliyofanyika jana mjini St. Paul, yalifana sana, hasa ukizingatia kuwa hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa maonesho haya kufanyika. Watu wengi walihudhuria na kushiriki kwa namna mbali mbali. Wajasiriamali na watoa huduma kwa jamii walijitokeza kwa wingi, wakionesha na kuelezea shughuli zao. Walimu, wasanii, waandishi, na viongozi mbali mbali wa jamii walikuwepo. Wauza bidhaa mbali mbali walikuwepo, kuanzia kazi za sanaa hadi vitabu. Hapa niko na waandaaji wa maonesho, wamiliki wa Liberation Clothing & Gifts. Mgeni rasmi, aliyetoa hotuba ya ufunguzi wa maonesho, alikuwa Dr. Julianne Malveaux , ambaye ni msomi aliyebobea, hasa katika masuala ya uchumi, na aliwahi kuwa rais wa Chuo cha Bennett . Hapa vijana wanaopiga ngoma na kucheza. Niliwapiga video kwa dakika kadhaa. Siku nzima, watu walikuwa wanafika, kwa wakati wao. Huu ni ukumbi ambamo mambo mengi yalifanyika, kama vile hotub

Maonesho Makubwa St. Paul, Minnesota, Kuhusu Watu Weusi

Tarehe 23 Februari hii, yaani keshokutwa, kutakuwa na maonesho makubwa mjini St. Paul, Minnesota, kuhusu historia, utamaduni, na mambo mengine ya watu weusi, kuanzia wale wa Afrika hadi wale walioko diaspora, yaani sehemu mbali mbali za dunia. Nitashiriki, kama mwandishi na mwalimu. Nimeshalipia meza na hapo nitaweka machapisho yangu . Nangojea kwa hamu kuongea na watu siku nzima kuhusu masuala ninayoyashughulikia, kama vile utafiti katika mila, desturi, na fasihi; tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani, masuala ya kuwapeleka wanafunzi Afrika, faida na changamoto zake. Kila yanapotokea maonesho ya aina hii, huwa ni fursa ya kukutana na watu wengi na kuelimishana. Nawakaribisha wote watakaopenda kuonana nami. Muhimu zaidi ni kuwa nawahimiza wote wanaoishi maeneo haya ya Minnesota kuhudhuria. Ni fursa nzuri na ya pekee kielimu kwa watu wazima, vijana na watoto. Kwa taarifa zaidi kuhusu maonesho haya, soma hapa na hapa .

Shule Ngorongoro

Image
Nilipiga picha ya shule hii, tarehe 10 Januari mwaka huu, katika kijiji kimojawapo cha wa-Maasai sehemu ya Ngorongoro. Yawezekana kuna wa-Tanzania ambao hawajui kuwa wa-Maasai wanajitahidi kuwapa watoto wao elimu ya shuleni. Hayo nimeyaona katika pita pita zangu sehemu mbali mbali katika nchi ya wa-Maasai. Yawezekana pia wako ambao watasikitika kuona kuwa shule hii ni ya miti na nyasi, badala ya matofali na bati au vigae. Hilo ni suala la kujadiliwa, kwani ni tata. Nami niliwahi kusema machache kuhusu suala hili. Niliandika makala kuhusu darasa chini ya mti. Soma hapa .

Bia na Mafanikio ya m-Tanzania

Image
Siku moja, mwezi Januari huu, nilikuwa katika baa fulani Mto wa Mbu. Sijui ni kwa nini, ila nilipata dukuduku ya kuona ujumbe kwenye chupa ya bia. Nilisoma, nikaona ni ujumbe wa kusisimua: Bia pekee inayowaleta Watanzania pamoja na kuwaburudisha, ikiwapa ari na hamasa ya kufika kilele cha mafanikio.

Profesa Anapoyaruka Majoka

Image
Katika safari zangu za Tanzania na wanafunzi, huwa najitahidi kwa uwezo wangu wote kuwafundisha vizuri. Papo hapo, najitahidi kuwaburudisha. Ikipatikana fursa ya kuyaruka majoka, ninawajibika vilivyo, na wanafunzi wanabaki hawana mbavu. Mbali ya kwamba burudani ni muhimu katika maisha, napenda kufanya mambo ya aina hii ili kuwaweka wanafunzi sawa kisaikolojia kwa kazi ya kitabu inayowakabili. Hizo picha zilipigwa Longido, tarehe 27 Januari, siku ya mwisho ya kozi yetu. Mchana wa siku hiyo, wanafunzi walishafanya mtihani wa mwisho, ikabaki sasa kujiburudisha jioni hadi usiku. Palikuwa hapatoshi.

Mdau Niliyemkuta Katika Ndege

Image
Tarehe 3 Januari, katika mazingira ya aina yake, nilimkuta mdau wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Nilipanda ndege Minneapolis, kwa safari ya Amsterdam, kisha Tanzania. Baada ya kuketi kitini, akina mama waliokaa karibu yangu waliniomba iwapo inawezekana kubadilishana viti, ili rafiki yao aje akae pale nilipokaa. Nilikubali kwa roho moja, nikaenda kukaa ile sehemu nyingine.  Baada ya kuketi tu, tulisalimiana na dada aliyekuwa amekaa kiti cha pembeni yangu. Naye, katika kuitikia, aliniangalia mara moja tu akasema, "wewe uliandika kitabu." Nilihisi alimaanisha kitabu cha Africans and Americans , kwani nyuma kuna picha yangu. Hapo alichukua kibegi chake kilichokuwa chini ya kiti, akafungua na kunitolea nakala ya kitabu hicho. Ilikuwa ni ajabu kukutana na mdau katika mazingira ya aina hiyo. Lakini hii si mara ya kwanza, kama nilivyoelezea hapa . Mdau huyu aliniambia kuwa yuko katika ndege ile na wenzake kadhaa ambao wanaenda Ken

Nashukuru Kumaliza Kozi ya Hemingway

Image
Nashukuru kuwa safari ya Tanzania, mwezi Januari mwaka huu, nikiwa na wanafunzi 29, ilienda vizuri sana. Wanafunzi kadhaa walinipiga picha nikiwa kazini. Hapa ni pembeni mwa Ziwa Manyara. Nawasomea wanafunzi maneno murua kutoka Green Hills of Afric a, ambayo yanahusu sehemu hiyo. Ni pembeni mwa Ziwa Manyara. Nawasomea wanafunzi vifungu kutoka Green Hills of Africa kuhusu sehemu hiyo. Hapa ni Namanga. Naonekana nikisoma kitabu cha Hemingway, True at First Light, ambacho kilikuwa ni andiko mojawapo muhimu katika kozi yetu. Hapa ni Karatu, nikiwa na kitabu cha Hemingway, Green Hills of Africa . Ni matayarisho ya kipindi.   Darasa kuhusu Green Hills of Africa limekolea. Ni Karatu hapo. Darasa kuhusu Green Hills of Africa linaendelea, Karatu. Hapa ni Babati. Darasa linaendelea. Hapa niko katika maandalizi ya kipindi, katika Colobus Mountain Lodge, pembeni m

Mnadani Karatu, 7 Januari 2013

Image
Mwezi Januari tarehe 7, mwaka huu, nilitembelea mnada mjini Karatu. Mnada huu hufanyika kila mwezi, tarehe 7, kama nilivyoandika hapa . Hao vijana wanaoonekana pichani ni wachuuzi wa vitu mbali mbali mitaani. Waliniomba niwapige picha nikawatangaze, ili wapate wateja kutoka Marekani.

Wanafunzi Wangu Wameipenda Tanzania

Image
Kuanzia tarehe 3 hadi 28 Januari, nilikuwa Tanzania na wanafunzi 29 wa Chuo cha St. Olaf , kwenye kozi juu ya mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Niliitunga kozi hii kwa makusudi, ili kuwapa wanafunzi fursa ya kuyaelewa mambo ya mwandishi huyu ambayo hayajulikani sana au hayajulikani vizuri, hata miongoni mwa wasomi. Tulisafiri katika maeneo kadhaa nchini Tanzania, ambamo Hemingway alipita mwaka 1933-34, tukiwa tunasoma maandishi yake kuhusu sehemu hizo. Wanafunzi walipata fursa tele ya kukutana na wa-Tanzania, kuanzia watoto wadogo hadi wazee. Walipata fursa ya kukutana na wa-Tanzania wa dini mbali mbali. Walipata fursa ya kuona maisha ya mijini na vijiji. Walipata ufahamu mpana na wa kina kuhusu maandishi na falsafa ya Hemingway. Kitu kimoja muhimu ni jinsi wanafunzi wote walivyopendezwa na hali waliyoiona Tanzania, hali ya ukarimu mkubwa kila walipopita. Walishangaa kuona kuwa wa-Tanzania wanajisikia raha kabisa kuwakaribisha wageni. Wamefurahi sana kupata fursa ya kuif

Baada ya Arusha, Niko Dar es Salaam

Image
Niliondoka Arusha tarehe 3 Februari, nikaja Dar. Hapa kushoto naonekana nimevaa vazi la Arusha. Kilichobaki hapo ni magwanda ya CHADEMA. Natania, kwani mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Isipokuwa, niliwahi kununua suti moja kule Burundi mwaka 1980 ambayo ningeivaa leo, watu wangesema mimi ni CHADEMA. Kazi kweli.

Nimekutana na Mdau Wangu Mkubwa wa Arusha

Image
Juzi, tarehe 31, nilikutana na Mama Linda, mMarekani anayishi Arusha. Ni mdau mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences .  . Niliwahi kumtaja hapa Mama huyu tumefahamiana kwa miaka mingi kidogo, na tumekuwa na kukutana Arusha na pia Marekani, anapotembelea kule. Tuna mawazo yanayofanana kuhusu umuhimu wa watu kuzitafakari tofauti za tamaduni, ili kuboresha mahusiano yao. Yeye ni mshauri wa jumuia ya wageni, hasa wa-Marekani hapa Arusha, kama vile mimi ninavyofanya kwa wa-Marekani na wa-Afrika kule Marekani. Tangu nilipochapisha kitabu changu, Mama huyu amekuwa akikitumia na kukipigia debe. Namheshimu kama mmoja wa wadau wangu wakubwa. Kila tunapokutana, inakuwa ni furaha sana kwetu, na tunabadilishana mawazo na uzoefu. Kwa miezi kadhaa tumekuwa tukitafakari wazo la kuendesha warsha hapa Arusha kuhusu masuala haya ya tofauti za tamaduni. Tunapangia kufanya hivyo nitakapokuja tena Tanzania.

Arusha: Nimekutana na Mbunge Godbless Lema

Jana, nilienda kujipatia chakula cha mchana sehemu fulani hapa Arusha. Baada ya kuketi, jamaa niliyetanguzana naye alinikonyeza niangalie meza ya kushoto kwangu. Kulikuwa na watu yapata watao, na nilipoangalia zaidi nilimwona Mheshimiwa Godbless Lema, mbunge wa Arusha kwa tiketi ya CHADEMA. Sikuwa nimewahi kumwona kabla, ila sura yake ni ile ile ninayoiona mitandaoni. Nilifurahi. Nilisimama nikaenda kumsalimia. Nilimwambia "pole na majukumu" na nikamtajia jina langu. Nilimwambia pia kuwa mbunge mwenzake wa CHADEMA, Profesa Kulikoyela Kahigi, ni rafiki yangu wa tangu tuliposoma dara moja Mkwawa High School. Sikumsalimia kwa vile ni Godbless Lema, bali kwa vile ni mwakilishi wa Arusha. Nilikuwa natoa heshima kwa wapiga kura wa Arusha. Wakati anaondoka, na watu wake, Mbunge alisogea nilipokaa, akaniaga. Nami nilimweleza kuwa mimi si mwanachama wa CHADEMA, bali ninaunga mkono harakati za CHADEMA za kulikwamu Taifa hili ambalo CCM imelizamisha katika ufisadi. Nilimwambia kuw

Nimeleta Wanafunzi Tanzania

Image
Nimekuwa kimya kwa karibu mwezi mmoja. Kisa? Nilileta wanafunzi Tanzania, kutoka Chuo cha St. Olaf ambapo nafundisha. Niliwaleta wanafunzi hao ili kuwafundisha kozi ambayo niliitunga, kumhusu mwandishi maarufu Ernest Hemingway, ambaye alisafiri na kuishi hapa Afrika Mashariki, hasa Kenya na Tanganyika, mwaka 1933-34 na 1953-54. Tulifika Tanzania tarehe 3 Januari, tukapitia maeneo kadhaa aliyopitia mwandishi huyu hapa nchini petu, tukisoma maandishi yake kuhusu safari zake na matukio mbali mbali sehemu hizo. Maandishi hayo ni riwaya, hadithi fupi, insha, na barua. Ingawa kazi hii ni nzito, yenye vipengele vingi, nina uzoefu nayo. Nilishaendesha kozi ya aina hii siku zilizopita, kwa wanafunzi wa Chuo cha Colorado, kama nilivyoelezea hapa Hapo pichani wanaonekana wanafunzi niliowaleta mwaka huu. Ilikuwa ni jioni ya tarehe 28 January, wakati nilipowafikisha uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, tayari kwa safari ya Marekani. Insha Allah nitaweka picha na maelezo mbali mbali katika blogu