Maonesho Faribault, Minnesota
Nimerejea muda mfupi uliopita kutoka Faribault, kwenye maonesho ya utamaduni ambayo hufanyika mara moja kila mwaka, chini ya kamati ya Faribault Diversity Coalition . Mimi ni mwanakamati. Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu. Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania. Baada ya meza yangu kukamilika, niliketi nikingojea wateja na watu wa kuongea nao kuhusu shughuli zangu za uandishi na ushauri juu ya masuala ya elimu na tamaduni. Picha hii, na jinsi nilivyokaa imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu uuzaji wa vitabu . Kijuu juu naonekana nimekaa kama muuza dagaaa. Ukweli ni kuwa hapa huwa ni darasa zito siku nzima.