Showing posts with label wa-Somali. Show all posts
Showing posts with label wa-Somali. Show all posts

Saturday, April 20, 2013

Binti Zangu Wamewajibika Leo Minneapolis

Leo binti zangu wawili wameshiriki mbio za kuchangia taasisi ya mafunzo iitwayo ThreSixty Journalism. Mbio hizi zimefanyika asuhubi leo mjini Minneapolis.

Mwaka 2009, binti huyu mwenye kitambaa kichwani alichaguliwa kusoma katika taasisi hiyo. Huchaguliwa vijana kadhaa kutoka shule mbali mbali. Wakiwa kwenye taasisi hiyo husomea masuala ya uandishi katika magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla. Ni fursa inayothaminiwa sana. Vijana hupata mafunzo bora kitaaluma, na pia fursa ya kukutana na waandishi na wanahabari maarufu. Kama sehemu ya mazoezi, binti yangu alipelekwa kwenye jamii ya wa-Somali hapa Minneapolis kufanya nao mahojiano, akachapisha makala hii hapa. Makala yake hiyo, na nyingine, zilichapishwa pia katika Twin Cities Daily Planet na Star Tribune, ambayo ni magazeti maarufu hapa Minnesota.

Nimefurahi binti zangu wamechukua uamuzi kulipia ushiriki wa mbio hizo, kuchangia taasisi hiyo. Napenda waendelee katika moyo huo.

Sunday, December 19, 2010

Kitabu Kimetua St. Cloud, Minnesota

Wasomaji wa blogu zangu, hii na ile ya ki-Ingereza, wanafahamu ninavyopenda kujishughulisha na masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa leo.

Nafanya shughuli hizi si kwa ajili ya kutafuta umaarufu, bali naamini ni wajibu kwa wanadamu kusaidiana katika maisha na kuifanya dunia iwe bora kuliko ilivyo.

Miezi ya karibuni nimejishughulisha sana na matatizo yanayowapata wahamiaji wa ki-Somali katika jimbo la Minnesota, ambalo linaongoza kwa idadi ya wahamiaji wa ki-Somali. Wasomaji wa blogu zangu watakumbuka taarifa za shughuli zangu katika mji wa Faribault.

Matatizo kama haya ya Faribault yako pia katika miji mingine, kama vile St. Cloud. Kutokana uzoefu nilioupata Faribault, nimeanzisha mawasiliano na ndugu Mohamoud Mohamed, mkurugenzi wa SASSO, jumuia inayoshughulikia masuala ya wa-Somali mjini St. Cloud.

Nilimpelekea nakala ya kitabu cha Africans and Americans, kama mchango wangu na changamoto. Jana ameniambia kuwa kitabu amekipata, anaendelea kukisoma, na anakipenda. Atawaonyesha wadau wa St. Cloud: halmashauri ya mji, shule na vyuo, idara ya polisi, mahospitali, na kadhalika. Nami nilimhakikishia kuwa ni jambo bora. Badala ya watu kununiana tu au kugombana, ni vema wakaanza utaratibu wa kuzungumzia matatizo kama ilivyofanyika Faribault, na ikapokelewa vizuri.

Kama ninavyosema katika mihadhara, blogu na maandishi mengine, matatizo ya aina hii yanayoikumba miji ya Faribault na St. Cloud yanajitokeza katika miji na jamii nyingine duniani: Afrika, Asia, Australia, Marekani, Ulaya, na kwingineko, na yataongezeka, kutokana na mwenendo wa utandawazi wa leo. Ninapokuwa Dar es Salaam, kwa mfano, nasikiliza na kutafakari minong'ono na majungu kuhusu wa-China, ambao wanaendelea kuja katika mji ule. Niliwahi pia kuongelea tafrani iliyotokea Zanzibar. Kinachobaki ni sisi kujizatiti kwa kuelimishana kuhusu tofauti zetu na kutafuta namna ya kuishi bila matatizo.

Najiandaa kushiriki katika masuala ya St. Cloud. Mbali ya umuhimu wake kwa jinsi hali ilivyo, ni fursa ya mimi kujiongezea ujuzi na uzoefu nitakaoutumia katika kuwasaidia wengine.

Saturday, August 28, 2010

Maonesho Faribault, Minnesota

Nimerejea muda mfupi uliopita kutoka Faribault, kwenye maonesho ya utamaduni ambayo hufanyika mara moja kila mwaka, chini ya kamati ya Faribault Diversity Coalition. Mimi ni mwanakamati.

Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu.

Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania.
Baada ya meza yangu kukamilika, niliketi nikingojea wateja na watu wa kuongea nao kuhusu shughuli zangu za uandishi na ushauri juu ya masuala ya elimu na tamaduni. Picha hii, na jinsi nilivyokaa imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu uuzaji wa vitabu. Kijuu juu naonekana nimekaa kama muuza dagaaa. Ukweli ni kuwa hapa huwa ni darasa zito siku nzima.

Walikuwepo wacheza ngoma za kabila la Aztec. Hao wamekuwa wakishiriki maonesho haya mwaka hadi mwaka, na huwa ni kivutio kikubwa.




Watu walileta vitu mbali mbali vya kuuza, kama vile vyakula, vinywaji, na kazi za sanaa. Katika maonesho haya, huwa napata fursa ya kukutana na watu wengi wapya.


Leo, kwa mfano, nimekutana na huyu mama, ambaye aliniambia kuwa alisoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hii ilikuwa ni ajabu, kwani nami nilisoma katika Chuo hicho hicho, miaka ya kabla yake. Halafu, aliniambia kuwa alishachukua kozi moja ya Profesa Harold Scheub iliyohusu fasihi hadithi za Afrika. Profesa huyu ndiye aliyesimamia tasnifu yangu ya shahada ya udaktari. Kweli milima haikutani, binadamu hukutana.
Huyu kijana hapa kushoto, baada ya kununua kitabu hiki alichoshika, aliomba tupige picha. Akanipa kitabu changu kingine nishike, na rafiki aliyekuja naye akatupiga picha.

Tabia hii si ngeni kwa wa-Marekani. Huwa wanapenda kumbukumbu za aina hii. Wengi wanapenda mwandishi atie sahihi kwenye kitabu wanachonunua. Nami leo nimefanya hivyo kwa wateja wangu.
Katika mji wa Faribault kuna wa-Somali wengi, ambao wamefika miaka ya karibuni. Leo hapo kwenye maonesho nilikutana na hao wa-Somali wawili. Huyu aliyeko kushoto anaishi kwenye mji mwingine. Lakini huyu wa kulia ni rafiki yangu, ambaye anafuatilia maandishi na shughuli zangu kuhusu masuala ya tamaduni. Ni kijana makini, na tunapangia kushirikiana katika shughuli hizo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...