Showing posts with label maonesho. Show all posts
Showing posts with label maonesho. Show all posts

Thursday, March 23, 2017

Mpiga Debe wa Vitabu Amenifuata

Jana niliandika katika blogu hii kuhusu programu inayowapeleka watu wa Nebraska Tanzania, ambao wanashauriwa kusoma Africans and Americans Embracing Cultural Differences. Nilikiri kuwa niliandika kama vile ninajipigia debe, lakini nilipendekeza utamaduni huo.

Ilikuwa kama nimeota, kwani leo nimepigiwa simu na kuletewa ujumbe na kampuni ya Readers Magnet inayojishughulisha na utangazaji wa vitabu. Mama aliyenipigia alisemaa kuwa wanakifahamu kitabu changu kutokana na taarifa za wasomaji katika mtandao wa Amazon. Wangependa kukijumlisha katika orodha ya vitabu wanavyovitangaza, akafafanua mipango yao, ikiwemo kuwakilisha katika maonesho ya vitabu ya Frankfurt.

Kwa kuwa maelezo yalikuwa mengi, nilimwuliza kama anaweza kuniletea kwa maandishi, akakubali. Ameniandikia ujumbe, ambao unaanza hivi:

Your book, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, was recommended to us by our Book Scouts. We believe and we have validated that your unique book has the potential and our goal for your book is to be recognized or acquired by specific decision makers like book store owners, librarians, and traditional publishers who have connections and contacts to help you reach out to your target audience and increase your returns. Your book is sure to capture a lot of attention this coming 2017 Frankfurt International Book Fair in Frankfurt, Germany dedicated for titles like yours and positively we will be able to give them the same impression as we have realized to entice investors for your book.

Baada ya kusoma na kutafakari maelezo yote, nimekubali kushiriki mpango huo. Katika mazungumzo ya simu, Sophia alivyoniulizia mikakati yangu ya kutangaza vitabu vyangu, nilimjibu kwa uwazi kuwa mimi ni mwalimu na mwandishi. Sina uzoefu wa biashara, wala mkakati maalum wa kutangaza vitabu vyangu, bali kwa ujumla vinatangazwa na wasomaji wenyewe katika maongezi yao, mawasiliano yao, mitandaoni, kama vile blogu, na kama alivyojionea hapo Amazon. Kutokana na kwamba sina mkakati wala uzoefu wa kibiashara, nimeona kuwa sina hasara kuipa kampuni hiyo wadhifa wa kutangaza kitabu changu. Zaidi ya kwamba sina cha kupoteza, nimevutiwa na maelezo ya faida za kufanya hivyo.

Nimejisikia vizuri kutokana na mawasiliano ya leo na Sophia. Alivyonieleza namna walivyokifahamu kitabu changu, na nikatambua kuwa wanakihitaji, nilijikuta nikimhoji na kumwekea vizingiti. Sikutaka kuweka hata chembe ya fununu kwamba ninahitaji huduma yao. Ni wazi kuwa kama mtu una kitu cha thamani, una uwezo wa kuonyesha kuwa unajiamini. Utamaduni wa kujiamini na kujithamini ni muhimu kwa mtu binafsi, kwa jamii, na kwa taifa. Ndio maana, bila kusita, nilimwambia Sophia kuwa aniletee ujumbe wa maandishi ili nitafakari.

Nimeelezea ujumbe huu hapa kwa kuwa ninaamini unaweza kuwa na manufaa kwa waandishi wengine. Vile vile, ni jadi yangu kuandika katika blogu hii mambo yanayotokana na uzoefu wangu na ninayojifunza kuhusu masuala ya vitabu.

Sunday, May 22, 2016

Leo Nimemwandikia Mzee Patrick Hemingway

Leo nimemwandikia barua pepe Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Nilipiga naye picha inayoonekana hapa kushoto tarehe 27 Aprili, 2013, nyumbani pake mjini Craig, katika jimbo la Montana.

Nilifahamu habari zake kwa miaka mingi kabla ya kufahamiana naye na halafu tukakutana. Ni mzee mwenye maongezi ya kusisimua kuhusu baba yake Ernest Hemingway na waandishi wengine wa wakati wake. Pia ana kumbukumbu nyingi za Tanganyika, na kisha Tanzania, ambako aliishi kwa miaka yapata 25 kabla ya uhuru na baada ya uhuru, akiendesha kampuni ya utalii, na hatimaye akiwa mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mwika.

Tangu tulipoanza kufahamiana, ameguswa na ari yangu ya kutafiti maandishi, falsafa, na maisha ya Ernest Hemingway, na amevutiwa na msimamo wangu kuwa Ernest Hemingway ni mwandishi aliyetuenzi sana sisi watu wa Afrika Mashariki, na tunapaswa kujielimisha kuhusu mchango wake, na kisha kuutumia katika kujitangaza kama alivyotutangaza.

Hayo yamemfanya Mzee Patrick Hemingway awe tayari kunisaidia kwa dhati katika juhudi zangu za kujielimisha na kuuelimisha ulimwengu juu ya Ernest Hemingway. Miezi kadhaa iliyopita, nilivyomweleza kuwa napangia kutembelea hifadhi ya Ernest Hemingway katika John F. Kennedy Library, aliniambia kuwa nitakapokuwa tayari nimfahamishe ili anitambulishe kwa wahusika.

Nilipoongea naye tarehe 19 mwezi huu na kumtajia tarehe nilizopangia kwenda kwa shughuli hiyo, aliniagiza nimpelekee maelezo yangu kwa barua pepe, ili aweze kuandaa utambulisho huo. Aliniambia kuwa ninakwenda wakati mzuri, kwani kuna maonesho maalum juu ya Hemingway, ambayo yameanza siku chache zilizopita na yatadumu kwa miezi kadhaa.

Basi, leo nimemwandikia. Kilichobaki sasa ni kuandaa safari, nikajionee hiyo hifadhi kubwa kuliko zote duniani juu ya Ernest Hemingway. Hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kuitembelea hifadhi hiyo, lakini sitegemei kuwa itakuwa ni mara ya mwisho.

Friday, April 29, 2016

Ninajiandaa Kushiriki Tamasha Rochester

Jioni hii, ninajiandaa kwenda Rochester, Minnesota, kushiriki tamasha la kimataifa kesho. Nitaondoka asubuhi sana ili nikawahi kabla ya saa nne litakapoanza tamasha. Nimeshalipia meza. Nitapeleka vitabu vyangu kama kawaida.

Meza ya vitabu katika tamasha ni kivutio kwa watu, sawa na meza za bidhaa na vitu vingine mbali mbali vinavyokuwepo. Watu wanapenda kuangalia vitabu, kuuliza masuali juu ya vitabu hivi, na wengine kuvinunua. Mimi mwenyewe ninapenda kuongelea mambo yanayonisukuma kuandika, hasa fasihi, tamaduni, na changamoto zitokanazo na tofauti za tamaduni.

Nitabeba pia bendera ya Tanzania. Nilishawahi kuelezea katika blogu hii namna nilivyofikia uamuzi wa kununua bendera hii, kwa ajili ya matamasha na maonesho mbali mbali. Huku ughaibuni, bendera ya Taifa ina mguso wa pekee moyoni. Kwa vile tamasha la kesho ni la kimataifa, bendera hii itakuwa mahali inapohitajika.

Tamasha la kimataifa hufanyika kila mwaka mjini Rochester. Mji huu una wakaazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kufanyika kwa tamasha la kimataifa katika mji huu ni jambo lenye mantiki bora. Watu wanaonesha tamaduni za nchi zao, na wote wanajifunza kutoka kwa wenzao.

Mwaka jana nilihudhuria tamasha la Rochester kwa mara ya kwanza, na niliandika habari zake hapa, na hapa. Ninangojea kwa hamu kukutana tena kesho na baadhi ya watu niliokutana na kufahamiana mwaka jana.

Kwangu mimi mwalimu, matamasha ya aina hii ni kama darasa. Kila ninapohudhuria, ninajikuta nikifundisha na pia kujifunza siku nzima. Nategemea kuandika taarifa za tamasha la kesho hapa katika blogu yangu.

Monday, August 10, 2015

Bendera ya Tanzania Itapepea Faribault, Minnesota, 22 Agosti

Tarehe 22 Agosti, nitashiriki tamasha la kimataifa mjini Faribault, Minnesota. Nimeshalipia gharama. Nitakuwa na meza ambapo nitaweka vitabu vyangu na machapisho mengine.

Hapo nitaongea na watu siku nzima kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, uandishi, na utoaji ushauri kuhusu athari za tofauti za tamadauni, ushauri ambao ninautoa kwa wanafunzi na waalimu wa vyuo vya Marekani na watu wengine waendao Afrika, taasisi na jumuia zenye mahusiano na wa-Afrika, na kadhalika.

Nitaweka pia mabango ya filamu ya "Papa's Shadow." Filamu hiyo, ambayo ni ya maelezo ("documentary"), kwa kiasi kikubwa ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Tunajadili maisha na maandishi ya Ernest Hemingway, hasa yale yanayohusu Afrika. Filamu hii itaanza kuonyeshwa hivi karibuni katika majumba ya sinema na itakuwa inapatikana katika DVD na kadhalika. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti ya Ramble Pictures.

Jambo jingine la pekee ni kuwa, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tamasha la kimataifa mjini Faribault, bendera ya Tanzania itapepea, sambamba na bendera za mataifa mengine. Siku chache zilizopita, nilipeperusha bendera hii katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

Ninapokuwa Tanzania, ninaweza kuiangalia bendera ya Tanzania nikawa ninaguswa kwa namna fulani, lakini hisia hizo huwa za pekee zaidi huku ughaibuni. Ingekuwa natoka Dar es Salaam kwenda kushiriki tamasha Mtwara, Chake Chake au Mbeya nisingeona sababu ya kubeba bendera ya Tanzania, labda kama tamasha ni la kimataifa. Na hata ningebeba, watu hawangekuwa na duku duku nayo au mshangao. Ni kitu walichozoea.

Lakini mambo ni tofauti huku ughaibuni. Sina namna ya kuelezea vizuri ninachomaanisha. Labda kwa kuwa niko mbali, nina hisia za pekee kuhusu kijiji changu cha Lituru, kata yangu ya Litembo, wilaya yangu ya Mbinga, mkoa wangu wa Ruvuma, na nchi yangu ya Tanzania.

Isipokuwa, jambo moja ni wazi, na linaelezeka: watu watakaohudhuria tamasha mjini Faribault wataiona bendera ya Tanzania. Bendera hii itatokea katika picha mbali mbali watakazopiga siku hiyo na kuzihifadhi, kuwapelekea marafiki au kuziweka mitandaoni.

Wednesday, May 6, 2015

Leo Nimepata Bendera ya Tanzania

Leo nimepata bendera ya Tanzania. Niliwahi kuandika katika blogu hii kuwa mara kwa mara ninashiriki matamasha hapa Marekani ambapo watu huja na bendera za nchi zao, nami nilijisikia vibaya kwa kutokuwa na bendera kubwa ya nchi yangu. Nilifanya uamuzi muafaka, nikaagiza, na leo nimeipata.

Mwaka jana, nilipoandika ujumbe wangu, nilikuwa napeleleza katika tovuti kadhaa zinazouza bendera. Lakini safari hii, kwa kubahatisha tu, nimeingia katika tovuti ya Amazon nikaona bendera ziko, tena kwa bei rahisi sana.




Nimejionea hapa Marekani jinsi wa-Kenya walivyo hodari kwa suala hilo, na hapa naleta picha niliyopiga katika tamasha la Afrifest, tarehe 2 Agosti, mwaka jana, mjini Brooklyn Park, Minnesota. Inamwonyesha m-Kenya akitamba na bendera ya nchi yake.

Jiulize mwenyewe, ungejisikiaje kuwepo mahali ambapo wenzako wanatamba na bendera za nchi zao, nawe huna. Kwa nini ukae mahali hivyo, kama vile huna nchi? Hisia hizi ni kubwa unapokuwa ughaibuni. Sikutaka kuendelea kudhalilika namna hiyo.



Picha nyingine, inayoonekana hapa kushoto, nilipiga tarehe 11 Aprili, 2015, mjini Rochester, Minnesota, kwenye tamasha la tamaduni za ulimwengu. Inaonyesha meza ya wa-Kenya na bendera yao.

Kuna matamasha yanayokuja ambayo nitashiriki, kama vile tamasha la Afrifest, tarehe 1 Agosti, 2015. Nitakapokuwa naandika taarifa za matamasha hayo na maonesho, wadau mtajionea wenyewe bendera ya Tanzania ikipepea kwenye eneo la meza ya vitabu vyangu.

Saturday, August 28, 2010

Maonesho Faribault, Minnesota

Nimerejea muda mfupi uliopita kutoka Faribault, kwenye maonesho ya utamaduni ambayo hufanyika mara moja kila mwaka, chini ya kamati ya Faribault Diversity Coalition. Mimi ni mwanakamati.

Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu.

Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania.
Baada ya meza yangu kukamilika, niliketi nikingojea wateja na watu wa kuongea nao kuhusu shughuli zangu za uandishi na ushauri juu ya masuala ya elimu na tamaduni. Picha hii, na jinsi nilivyokaa imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu uuzaji wa vitabu. Kijuu juu naonekana nimekaa kama muuza dagaaa. Ukweli ni kuwa hapa huwa ni darasa zito siku nzima.

Walikuwepo wacheza ngoma za kabila la Aztec. Hao wamekuwa wakishiriki maonesho haya mwaka hadi mwaka, na huwa ni kivutio kikubwa.




Watu walileta vitu mbali mbali vya kuuza, kama vile vyakula, vinywaji, na kazi za sanaa. Katika maonesho haya, huwa napata fursa ya kukutana na watu wengi wapya.


Leo, kwa mfano, nimekutana na huyu mama, ambaye aliniambia kuwa alisoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hii ilikuwa ni ajabu, kwani nami nilisoma katika Chuo hicho hicho, miaka ya kabla yake. Halafu, aliniambia kuwa alishachukua kozi moja ya Profesa Harold Scheub iliyohusu fasihi hadithi za Afrika. Profesa huyu ndiye aliyesimamia tasnifu yangu ya shahada ya udaktari. Kweli milima haikutani, binadamu hukutana.
Huyu kijana hapa kushoto, baada ya kununua kitabu hiki alichoshika, aliomba tupige picha. Akanipa kitabu changu kingine nishike, na rafiki aliyekuja naye akatupiga picha.

Tabia hii si ngeni kwa wa-Marekani. Huwa wanapenda kumbukumbu za aina hii. Wengi wanapenda mwandishi atie sahihi kwenye kitabu wanachonunua. Nami leo nimefanya hivyo kwa wateja wangu.
Katika mji wa Faribault kuna wa-Somali wengi, ambao wamefika miaka ya karibuni. Leo hapo kwenye maonesho nilikutana na hao wa-Somali wawili. Huyu aliyeko kushoto anaishi kwenye mji mwingine. Lakini huyu wa kulia ni rafiki yangu, ambaye anafuatilia maandishi na shughuli zangu kuhusu masuala ya tamaduni. Ni kijana makini, na tunapangia kushirikiana katika shughuli hizo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...