
Jana nimeona taarifa mtandaoni kuwa Jumamosi hii, tarehe 23, mjini Faribault, Minnesota, kutakuwepo na
tamasha la kimataifa la tamaduni. Hapo hapo nilipiga simu kwa waandaaji, ili kuona kama bado kuna nafasi ya mimi kushiriki.
Leo mratibu mkuu wa tamasha, amenipigia simu. Tumeongea kwa muda, nami nikamwulizia kama bado kuna nafasi ya kushiriki katika tamasha. Hapo hapo aliniambia kuwa nafasi bado iko, na kwamba tukimaliza maongezi atanitumia fomu ya kujisajili.
Tuliongelea shughuli nifanyazo katika jamii, ikiwemo kushiriki matamasha ya aina hii kama mwandishi na mwelimishaji, hasa kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake. Tuligusia pia ushiriki wangu katika masuala ya Faribault, kama ilivyotamkwa katika
taarifa hii hapa.
Wakati tunaendelea na mazungumzo, aliniuliza kama nina bendera ya nchi yangu, yaani Tanzania. Alifafanua kwamba kwenye jukwaa kuu, zitakuwepo bendera za nchi wanakotoka washiriki wa tamasha, na kuna kipindi ambapo wawakilishi wa nchi hizo watakuwepo jukwaani wakiwa na bendera zao. Watapata dakika kadhaa za kuongelea mbele ya kadamnasi kuhusu nchi zao na hizo bendera. Hapo nilijisikia vibaya, kwani sina bendera ya Tanzania ya ukubwa utakiwao, ambao ni angalau futi tatu kwa tano. Nilikiri kuwa sina, ila nikasema nitajitahidi katika siku hizi mbili tatu kutafuta.
Baada ya maongezi, nimeangalia mtandaoni nione wapi naweza kuipata bendera ya aina hiyo. Nimeona sehemu kadhaa, ambapo naweza kuagiza bendera hiyo. Nimepiga simu sehemu tatu, nikaambiwa kuwa hatawezekana kuipata kabla ya tamasha.
Kwa maana hiyo, nimekwama. Nimekosa fursa ya kuelezea habari za Tanzania na bendera yetu, mbele ya wote watakaohudhuria tamasha. Nimejifunza. Niko mbioni kuagiza bendera, niweze kuitumia siku za usoni.
Mji wa Faribault uko umbali wa maili kama 25 tu kutoka hapa ninapoishi. Nami si mgeni katika mji ule, kwani, kwa miaka iliyopita, nimeshafanya shughuli nyingi za jamii katika mji ule, kama ilivyoelezwa
hapa,
hapa, na
hapa.
Lakini, pamoja na yote, hili suala la kutokuwa na bendera limenikera na papo hapo limenigutua. Mimi kama m-Tanzania, tena sio m-Tanzania wa uraia pacha, ningejisikia vizuri sana kuwepo kwenye jukwaa kuu na bendera yangu, nikasema mawili matatu kuhusu nchi yangu na bendera yake. Dosari hii ni lazima irekebishwe hima.