Nimepita Tena Kwenye Duka la Vitabu
Leo nilikuwa Minneapolis nikihudhuria kikao cha kuandaa mkutano wa waAfrika, Wamarekani Weusi na wengine wenye asili ya Afrika ambao tutafanya Oktoba tarehe 9, 2010. Nilihudhuria pia kikao cha bodi ya Afrifest . Nilipokuwa narudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaingia kwenye duka la vitabu la Half Price Books. Duka hili nimelitembelea mara nyingi na nilishawahi kuandika habari zake katika blogu hii . Niliyoyaona leo ni yale ambayo nayaona daima ninapotembelea maduka ya vitabu hapa Marekani. Watu wengi walikuwemo, watoto, vijana, wazee, wake kwa waume. Wazazi wengine walikuwemo na watoto wadogo sana, na hata watoto wachanga. Duka ni kubwa, lakini watu walikuwa wanapishana kila sehemu, wakiangalia vitabu, wakivisoma, na kuvinunua. Wengine walikuwa wanawasomea watoto wao hadithi. Watoto wadogo sana niliwasikia wakiongea na wazazi au kujibizana nao kuhusu vitabu. Ni jambo la kugusa sana moyoni unapomwona mama ameketi akijibizana na mtoto wake kuhusu kitabu ambacho mtoto anaangalia. N