Posts

Showing posts from December, 2010

Mafisadi Wanaufurahia Mwaka Mpya

Mwaka unaoisha leo, mafisadi wanaoihujumu Tanzania walikuwa na sababu ya kukosa usingizi, kutokana na kampeni kali iliyofanyika dhidi yao. Ingekuwa vipi, mwaka huu mpya ungekuwa ni mgumu kwa mafisadi, lakini moto uliowashwa dhidi yao umeendelea kuwa hafifu, kwa juhudi za zimamoto. Tumerudi katika amani na utulivu.

Utamaduni na Utandawazi: Tunawafahamu wa-Turuki?

Image
Wasomaji wa blogu zangu wanafahamu kuwa suala la utamaduni na utandawazi ni moja ya masuala ninayoyatafakari sana. Ninaelezea umuhimu wa suala hili kwa namna ya pekee katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii . Dhana ya utamaduni ina maana nyingi, na ni muhimu kwa mtumiaji wa dhana hii kuelezea anaitumia kwa maana ipi. Ili nieleweke vizuri na kiurahisi, singependa kuleta nadharia na mambo ya kufikirika. Badala yake, nimeamua kuuliza suali: Tunawafahamu wa-Turuki? Leo hii, Tanzania na u-Turuki zinajenga uhusiano kwa kiwango ambacho hatujawahi kuona kabla, katika nyanja kama biashara, utalii, na elimu. Shirika la ndege la u-Turuki linapiga hatua katika kuimarisha safari baina ya Tanzania na u-Turuki. Ni wazi kuwa watu wa nchi hizi mbili wataendelea kuwa na mahusiano ya karibu katika nyanja mbali mbali. Kama ninavyosema mara kwa mara, naamini kuwa mahusiano yoyote baina ya watu wa tamaduni mbali mbali yanaathiriwa moja kwa moja na tofauti za tamaduni hizo. Ndio maana ninauli

Kitabu Kimetua St. Cloud, Minnesota

Image
Wasomaji wa blogu zangu, hii na ile ya ki-Ingereza , wanafahamu ninavyopenda kujishughulisha na masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa leo. Nafanya shughuli hizi si kwa ajili ya kutafuta umaarufu, bali naamini ni wajibu kwa wanadamu kusaidiana katika maisha na kuifanya dunia iwe bora kuliko ilivyo. Miezi ya karibuni nimejishughulisha sana na matatizo yanayowapata wahamiaji wa ki-Somali katika jimbo la Minnesota, ambalo linaongoza kwa idadi ya wahamiaji wa ki-Somali. Wasomaji wa blogu zangu watakumbuka taarifa za shughuli zangu katika mji wa Faribault . Matatizo kama haya ya Faribault yako pia katika miji mingine, kama vile St. Cloud . Kutokana uzoefu nilioupata Faribault, nimeanzisha mawasiliano na ndugu Mohamoud Mohamed, mkurugenzi wa SASSO , jumuia inayoshughulikia masuala ya wa-Somali mjini St. Cloud. Nilimpelekea nakala ya kitabu cha Africans and Americans , kama mchango wangu na changamoto. Jana ameniambia kuwa kitabu amekipata, anaendelea kukisoma,

Nimenunua Kitabu Kipya cha Chimamanda Ngozi Adichie

Image
Leo nimenunua, The Thing Around Your Neck , kitabu kipya cha Chimamanda Ngozi Adichie. Huyu dada ni mwandishi wa ki-Nigeria, mwenye kipaji sana cha kuandika riwaya na hadithi fupi. Pia ana mawazo ya kusisimua na kufikirisha kuhusu simulizi . Umaarufu wake unakua kwa kasi. Amepata tuzo mbali mbali, ikiwemo ya Taasisi ya MacArthur Riwaya yake ya kwanza, Purple Hibiscus , niliifundisha hapa chuoni St. Olaf . Inavutia sana kwa dhamira, maudhui, na matumizi ya lugha. Inaongelea maisha ya familia ya profesa wa chuo kikuu cha Nsukka, Nigeria, kwa namna ya kukufanya msomaji ujisikie uko sehemu hiyo. Matukio na migogoro baina ya wahusika imeelezwa kwa uhalisi wa kuvutia. Mwaka 2006 nilipata bahati ya kumwona Chimamanda Ngozi Adichie, alipofika mjini Minneapolis kwenye tamasha la vitabu . Alikuja kuzindua kitabu chake cha pili, Half of a Yellow Sun . Nilinunua nakala, ambayo aliisaini, na tulipata muda wa kuzungumza kiasi, hata akaniambia kuhusu anavyoendesha blogu. Tulipiga picha inayoonekan

Laiti Ningekuwa Kama Hemingway

Image
Laiti ningekuwa kama Hemingway , mwandishi maarufu sana duniani. Ningeandika kuhusu nchi yangu na watu wake kwa umakini, ubunifu, na ukweli wa kumgusa kila msomaji. Ningeandika kuhusu maziwa, mito, milima na mabonde. Ningeandika kuhusu fukwe, nyanda na visiwa. Ningeandika kuhusu miji na vijiji, mitaa na vitongoji. Nimetamka hayo , na nimeanza kufanya mazoezi . Lakini bado njia ni ndefu mbele yangu. Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyeangalia mazingira, matukio, na tabia za wanadamu kwa macho na akili yote, aliyejawa nidhamu ya kutumia lugha, akiangalia kila neno, tena na tena, akibadili na kusahihisha tena na tena, akitafuta namna ya kuandika sentensi sahihi yenye ukweli mtupu. Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyetufundisha kuwa kazi ya mwandishi ni kujitoa mhanga ili nafsi yake yote ibakie katika kitabu tu, asibakishe hata chembe nje ya kitabu. Kila kitabu kiwe ni mauti ya mwandishi, vinginevyo kitabu hiki ni mzaha na udanganyifu. Je, nitayaweza hayo? Hemingway aliandika kuhus

Nimekutana na Mratibu wa Chuo Kikuu cha Njombe

Image
Tarehe 9 Oktoba nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Bill, akisema kuwa angependa kumleta kwangu mgeni kutoka Tanzania, kwa mazungumzo. Alimtaja mgeni kuwa ni Dr. Peter Kimilike. Basi, tarehe 11 walifika hapa Chuoni St. Olaf . Tulifurahi kufahamiana. Dr. Kimilike ni mchungaji m-Tanzania ambaye anaratibu shughuli za kuanzisha Chuo Kikuu cha Njombe . Tulifurahi kutambua kuwa kuna watu maarufu ambao yeye na mimi tunafahamiana nao, kama vile Danford Mpumilwa , afisa habari wa Mahakama ya ki-Mataifa inayoshughulikia mauaji ya Rwanda (ICTR) , na Rev. Dr. Anneth Munga, mkuu wa Chuo cha Sebastian Kolowa Maongezi yetu yalilenga zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Njombe . Nilimweleza Dr. Kimilike kuwa ninafuatilia kwa karibu maendeleo ya vyuo Tanzania. Kila ninapoenda kule, ninatembelea vyuo. Nikampa mifano ya vyuo nilivyotembelea: Tumaini (Iringa), Makumira (Arusha), na Sebastian Kolowa (Lushoto). Ninaelimika sana ninapoongea na walimu na wengine kuhusu hali halisi ya vyuo vyet