Sunday, March 15, 2009

Mbwa aliyezua tafrani Zanzibar apelekwa New York

Leo nimeona makala, "Mbwa aliyezua tafrani Zanzibar apelekwa New York," ambayo imenigusa kwa namna ya pekee, kwa vile inahusu tofauti baina ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani. Masuala hayo nayashughulikia sana, katika utafiti, ufundishaji, uandishi, warsha, na mazungumzo na watu mbali mbali.

Makala hii imenigusa kwa namna ya pekee kwa kuwa inahusu habari iliyotokea Zanzibar. Nilishaenda Zanzibar, kwa kuombwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kutoa mihadhara kuelezea jinsi mimi kama Mwafrika ninavyoiona Marekani. Mihadhara hiyo niliitoa Zanzibar na Pemba. Nilizungumzia tofauti za utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani, nikitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Suala la mbwa nimeliongelea katika kitabu hiki. Na niliposoma makala hii, nilipata hisia kuwa laiti kama hao wawekezaji wangekuwa wamekisoma, kwani walikuja kweye utamaduni ambao si wao, na walikuwa na wajibu wa kuzingatia utamaduni wa wenyeji. Makosa ya aina hii hutokea sana, na matokeo yake ni kutoelewana, hasira, vinyongo na majuto. Makala yenyewe ni hii hapa.

Waafrika nasi tunao wajibu wa kujielimisha kuhusu tamaduni za hao wageni. Unaweza kunisikia ninavyoongelea masuala haya hapa.

Vitabu vyangu vinapatikana Dar es Salaam, simu 0754 888 647 au 0717 413 073

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Kwa kweli nami nimeguswa sana na hii habari ya mbwa. Eti kuomba radhi kwa kumtishia au kumpiga mbwa yaani mbwa anaheshimiwa zaidi kuliko binadamu. Na zaidi nimefurahi sana kusikia mahojiano yako kuhusu mila na desturi, yaani mambo uliyoandika kwenye kitabu chako. Asante sana kwa yote nimependa sana

Mbele said...

Dada Yasinta, nafurahi kuwa umepata fursa ya kusikiliza yale mahojiano. Kweli hii tekinolojia ina uwezo wa kutupeleka mbali. Kwa vile nawe unaufahamu utamaduni wa huku ughaibuni, una mengi ya kuweza kuwaelimisha walioko kule nyumbani, na vile vile kuwaelimisha watu wa ughaibuni kuhusu mambo ya kwetu. Ndio shughuli mojawapo ninayofanya, kwa moyo mkunjufu.

Simon Kitururu said...

Maswala ya utamaduni ni magumu!


Wikiendi iliyopita nilishuhudia Muiraki mmoja akipandisha jazba kutokana na maswala ya Viatu!

Hapa nilipo kuna utamaduni wa kuvua viatu ukiingia nyumbani kwa mtu. Kwa bahati mbaya mmoja wa mgeni aligongwa na kiatu na kutafsiri katukanwa ingawa mimi ninauhakika ilikuwa bahati mbaya.

Pamoja na mimi kujua jinsi George Bush na Saddam walivyo tukanwa kwa kutumia viatu Iraki, lakini ilikuwa ni somo tofauti kushuhudia mtu ambaye mambo mengi ya maana mnaweza kujadili na kuelewana, alivyokuwa anashindwa kuelewa kuwa viatu tulipo havimaanishi chochote.

Yeye alichukulia kuwa ametukanwa na aliyemtukana ni Racist hata kama hakuelewa ni kosa gani kafanya zaidi ya bahati mbaya kumgonga na kiatu.

@Dada Yasinta: Hivi na wewe bado unavaa viatu fulani vya kike ambavyo ni shughuli kuvivua?

Yasinta Ngonyani said...

Sawa, Kuhusu kuwaelimisha watu huku niishiko na kule nitokako ni kweli hii kazi naifanya kuna wakati wananiomba niwaeleze jinsi utamaduni wetu ulivyo. na nikiwa nyumbni TZ huwa najaribu kuongea na watu kuwaeleza utadaduni wa hapa.

Simon:-) Hata kama navaa viatu ambavyo ni shughuli kuvivua ni lazima nitavivua tu nifikapo kwako kama ni sheria kuvua.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...