Friday, March 20, 2009

Vitabu kwa Watalii

Leo nimepata ujumbe kutoka Longitude Books, kampuni maarufu ya kiMarekani inayouza vitabu kwa watalii na wasafiri wengine. Wanaulizia namna ya kupata vitabu vyangu. Wanasema wameambiwa na jumuia ya Stanford Alumni Travel waviweke vitabu hivi katika orodha yao kwa ajili ya wasafiri wanaokwenda Tanzania.

Longitude Books wanahitaji vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales na katika ujumbe wao wanasema "we'd like to be able to include Africans and Americans and Matengo Folktales in our mix of recommendations for travelers to Tanzania....We're working on more family and exchange programs and both books will enhance our offerings."

Kwangu hii ni habari njema. Ni faraja kuona kuwa kazi ninayofanya inatambuliwa. Hilo si jambo geni hapa Marekani. Vitabu vyangu vinatambuliwa na kutumika sehemu mbali mbali.

Kinachosikitisha ni kuwa kwa miaka kadhaa nimejaribu kuwasiliana na waTanzania wanaohusika na sekta ya utalii, kuwaarifu kuwa nina vitabu ambavyo vingeweza kuwafaa, lakini sijaona msisimko wowote, na hata kujibiwa barua ni bahati nasibu. Wazo la vitabu liko mbali kabisa na mawazo yao. Huu ni ushahidi mwingine wa jinsi elimu ilivyodhoofika au kufifia nchini.

Ingekuwa elimu haijadhoofika au kufifia kiasi hicho, watu wangekuwa na duku duku ya kufuatilia wazo wanalopewa, ili kujifunza zaidi. Kwa kufanya hivyo, wangeweza kuelewa, kwa mfano, kwamba kwa ujumla, Wamarekani wanapenda kusoma vitabu. Wanapokuja kwetu kama watalii, wanakuwa wamejizatiti kwa kusoma vitabu kuhusu nchi wanayoitembelea, kuhusu watu wake, utamaduni, na mambo mengine kadha wa kadha. Kama hawajanunua huko wanakotoka, wanategemea wavikute huko wanakoenda.

Ufahamu huu inaonekana haumo katika jamii ya waTanzania, kama hao niliowasiliana nao. Kwa vile wao wenyewe hawatilii vitabu maanani, wanapofanya biashara ya utalii, hawawazii vitabu. Katika maduka wanaweka vinyago, bangili, na vitu vingine ambavyo wanaamini watalii watavipenda, lakini si vitabu. Katika blogu yangu hii, nimeandika na nitaendelea kuandika, kuhusu tatizo hilo la waTanzania kutovithamini vitabu, na athari zake. Sitachoka kuandika, na kutetea elimu, kwani huu ni wajibu wangu kama mwalimu.

Kwa hivi, kichwani mwangu leo kuna mawazo mazito. Natambua kuwa vitabu vyangu vitaiongezea biashara kampuni ya kiMarekani ya Longitude Books, wakati mimi nilijaribu kuwapa waTanzania mwanya huo, bila mafanikio.

3 comments:

Albert Kissima said...

Hongera sana Profesa Mbele kwa kazi zako nzuri za vitabu vinavyojuza watu juu ya tamaduni za watu tofauti hususani za Amerika na Afrika.

Swala la hawa watanzania wanaodili na watalii kuonyesha uitikio mdogo ktk kuchukua vitabu vyako mbali na maswala mengine lakini thana hii ya "kwa nini yeye afaidi" yani kuto penda kuona wengine wanafanikiwa, ni kati ya mambo yanayochangia sana.

Kijijini kwangu nimeshuhudia hivihivi nikikosa huduma ya maji baada ya wanakijiji kutokutoa ushirikiano wa kutosha kwani ili kufanikisha project hiyo nguvu kazi ya watu ilikuwa ni muhimu.
Watu hawakutoa ushirikiano kisa wanakijiji wachache walikuwa na miradi ya umwagiliaji, hoja yao kubwa ni kwamba hata maji yakiletwa wachache watayatumia kwa miradi yao.Wakati uhalisia ni kwamba maji hayo ndio uhai wa kila mmoja pale kijijini.

Christian Bwaya said...

Kusema ukweli, hivi sasa katika Tanzania tunajenga taifa la watu wanaotegemea zaidi masimulizi badala ya vitabu. Watu wanatumia masaa kwenye luninga lakini si kusoma. Na ndio maana waswahili wanathamini umbeya. Kwa nini wasipende vijiwe wakati hawana muda na kujielimisha?

Leo hii usomaji unaotia fora, ni ule wa udaku na habari nyepesi nyepesi. Blogu zinazopendwa ni zile zenye kujadili watu na matukio.

Maana yake nini? Kusoma kwa bidii imekuwa dhahama katika Tanzania.

Ndio maana sishangai kwamba hao jamaa walijivuta vuta. Watachangamkia nini kama wao wenyewe hawajisomei? Hivi ingekuwa 'udaku unaolipa' wasingetokwa na macho hao?

Inauma kwamba nchi yetu imejaaliwa watu wenye maarifa makubwa, wabobevu wanaoachwa waifaidishe dunia. Wanakatishwa tamaa na serikali isiyo na habari na utamaduni wa kujisomea.

Ni habari njema kwamba umeahidi kutokukata tamaa. Nami, kama mfuatiliaji wa kazi zako, nakuunga mkono. Usikome kupaza sauti yako nyikani. Hata kama wanajidai hawasikii, angalau tunajua wanasikia.

Mbele said...

Ndugu Kissima na Ndugu Bwaya, shukrani kwa changamoto murua.

Pamoja na matatizo yote, wajibu wa mwalimu ni kuendelea kufundisha, kwa mujibu wa utafiti, ufahamu, na dhamiri yake.

Yeyote mwenye ufahamu angalau kidogo wa maana ya elimu, atatambua kuwa ualimu ni kazi ya kuwafaidia na kuwatajirisha wengine, kwani hakuna utajiri unaozidi elimu.

Sasa, kwa vile katika Tanzania elimu imeporomoka kiasi cha kuwa mahututi, ndio tunao hao watu ambao wakielezwa kuhusu vitabu, hawafanyi juhudi ya kufuatilia ili angalau kupata fununu zaidi, bali wanawazia kuwa mwalimu anataka kuwatoa upepo. Nchi ikifikia hapo, ujue iko taabani.

Hata hivi, ukiwa kama mimi, huyumbishwi na fikra kama hizo, unaendelea na wajibu wako. Faraja ni kuwa, kidogo kidogo matunda ya juhudi zako unaweza kuyaona. Kwa mfano, miaka hii michache iliyopita, nimejenga uhusiano na kikundi cha vijana wa pale Mto wa Mbu, ambao wanashughulika na utalii. Hao ni vijana wenye mwamko wa kutaka kujifunza ili kuboresha shughuli zao.

Unaweza kusoma taarifa kidogo za uhusiano wetu huu hapa na hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...