Najiuliza kama njia ya kufanikiwa katika jamii yetu ya kiTanzania ni ya kushirikiana au ni ya kila mtu na lwake.
Mara moja moja huwa nahudhuria mikutano ya wajasiriamali na wafanya biashara hapa Marekani, ingawa mimi ni mwalimu. Huwa nasoma pia vitabu na majarida kuhusu ujasiriamali na uendeshaji wa biashara. Kwenye hii mikutano, watu wanaongelea shughuli zao, wanabadilishana uzoefu na kuelimishana. Baada ya hapo, watu hupenda kubadilishana anwani na simu, ili waweze uwasiliana zaidi.
Mimi mwenyewe nimewahi kuombwa nielezee shughuli zangu, maana ninajaribu kujiimarisha kama mjasiriamali, kwenye shughuli ya kutoa ushauri katika masuala yahusuyo tamaduni ili kuwawezesha wafanya biashara, wajasiriamali, na wengine kufanikiwa wanaposhughulika na watu wa tamaduni mbali mbali. Ni jambo la kufurahisha kwamba, baada ya kujieleza, nimeona watu walivyo wepesi kunipa ushauri, kuniunganisha na wengine, na kadhalika.
Kitu wanachozingatia katika shughuli hizi ni kujenga na kutumia mtandao. Hii dhana wanaiita "networking." Vitabu ninavyosoma navyo vinasisitiza umuhimu wa "networking." Wazo la msingi ni kuwa kila mtu ana uwezo fulani au uzoefu fulani ambao wengine hawana. Watu hao wakishirikiana, wote wanafaidika. Biashara na shughuli zingine zinapanuka na kustawi kwa mmsingi huo. Kufanikiwa kwako ndio kufanikiwa kwangu, na kufanikiwa kwangu ndio kufanikiwa kwako.
Lakini je, hii dhana ya "networking" iko katika jamii yetu ya kiTanzania? Au sisi tunafuata sera ya kila mtu na lwake? Kwa ufahamu wangu, waTanzania wanafuata sera ya kila mtu na lwake. Ni sera ya kufa na kupona, hadi watu wengine kutumia ushirikina, badala ya kutafuta elimu, ikiwemo hii elimu ya "networking," ujuzi na maarifa, ambazo ndizo dira za maendeleo zinazotumiwa na wenzetu. Je, tutafika?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
7 comments:
Ni swali nzuri Kama kweli tutafika? kwani nimekuwa najiuliza mara nyingi kwa nini tunapenda sana ushirikiana. Nina maana mtu akiona mmoja ameendelea basi ni chuki mtupu. Na mambo mengine mengi mengi. hawajui kwamba "Kufanikiwa kwako ndio kufanikiwa kwangu, na kufanikiwa kwangu ndio kufanikiwa kwako".
Shukrani kwa mchango wako. Napenda kuongezea kidogo, mfano wa tatizo la "kila mtu na lwake." Huku ughaibuni, inapotokea misiba, mara nyingi tunawajibika kuchanga hela kusafirisha maiti Tanzania. Kwa kuwa huku ughaibuni hakuna hela inayopatikana bila jasho, hii ni shughuli nzito.
Kama tungefuata sera ya "kufanikiwa kwako ni kufanikiwa kwangu, na kufanikiwa kwangu ni kufanikiwa kwako," tungekuwa tunaelezana mbinu za kufanikiwa na kunyanyuana. Aliyefanikiwa angewafundisha wenzake. Tungefanikiwa kama jumuia, kwa namna mbali mbali, iwe ni kielimu, kijamii, na kiuchumi. Kama ni suala la michango wakati wa matatizo, tungeimudu kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa.
Lakini kwa sera ya "kila mtu na lwake," mwenzetu akianzisha kabiashara, kwa mfano, sisi tunaenda kununua bidhaa sehemu nyingine, sio kwake. Na huko tunakoenda kununua ni kwa mtu baki. Siku ya msiba, huyu mtu hatuletei chochote. Tunabaki kuangaliana sisi wenyewe.
Na Tanzania ni hivyo hivyo. Mtu anapiga chenga ili asimnufaishe mwenzake. Wakati mwingine inaonekana watu hata hawajitambui kuwa wanafanya hivyo. Kwa mfano, mtu anaenda kununua juisi ya maembe au machungwa kutoka kwenye duka la wawekezaji wageni, badala ya kwenda Kariakoo au Ubungo kununua maembe au machungwa yaliyowasili leo hii kutoka shambani. Kwa namna hii, tunamtajirisha na kumwongezea biashara huyu mwekezaji mgeni.
Siku inapotokea shida, kama vile msiba, tunajikuta hatuna uwezo mkubwa. Yule mwekezaji mgeni tunayemtajirisha haonekani hapo kwenye msiba. Yuko Kunduchi anaogelea. Tungekuwa na sera ya kunyanyuana, hatungeteseka namna hii. Hayo ndio mawazo yangu.
Tatizo haliishii hapa. Mtanzania aliyeko nchini na yule aliyeko ughaibuni hawashirikiani. Malamiko na majungu hayaishi, badala ya kutafuta njia za kushirikiana kwa mafanikio ya wote.
Ni wazi, nimetia chumvi kidogo katika maelezo yangu, na wako ambao hawafanyi niliyosema, au hawafanyi kwa kiwango nilichosema, lakini kuna ukweli fulani katika hayo niliyosema.
Huku nyumbani tatizo hili ndio kubwa sana maana watu wakiona unafanya kitu badala ya kukunga mkono ili uendelee basi wao wanakuvunja moyo kwa maneno na hata kuwa-support washindani wako ili wewe uwe na wakati mgumu
Mfano mzuri ni kwenye bidhaa zetu, watu badala ya kununua bidhaa zinazozalishwa nchini wao wanakazania bidhaa za nje na hata sijui sababu nini?
vitu kama siagi ya blue band, colgate ya Jirani zetu, maziwa, sabuni za kufulia, vyombo vya chakula, body za malory na mabasi, nyama ya ngombe na kuku n.k ni moja ya vitu ambavyo vinapatikana nchini katika ubora wa hali ya juu, lakini utakuta kuna upinzani mkubwa toka kwa nchi jirani.
Mimi natoa wito kwa wa Tanzania ndani na nje ya nchi tuwe na tabia ya kupenda vyetu na kupendana wenyewe kwani mwenzio akifanikiwa basi na wewe kwako ni faraja.
kuna watu wanaodhani wanaweza kuishi bila wenzao na ndio maana wanajenga nyumba zenye fensi ndefu harafu moto ukitokea wanakufa wote. ndio maan wanamiliki bastola harafu zinafyatuka na kuwaua wawapendao huku vibaka wakitesa.
kila mtu na lwake, kila dini na lwake na Mungu wake ni mzuri kuliko li-Mungu la dini nyingine.
kila mtu na lwake inaanzia mbali ndio maana tunaona watoto wamelanda landa mitaani eti hawana wazazi.l enzi za ujamaa mambo yalikuwa shwari kwani kila kitu kilikuwa ni chetu na ndivyo ilivyo kwa asili.
lakini nikuulize Prof mabele, mke wako ni wako tu au wetu/wenu nyote? yaani ukimkuta na bwaya au kitururu utasema ni wetu sote? si tunapaswa kufurahia sote kwa pamoja? au kuna mahali ambapo inabidi kila mtu awe na lwake?
Ndugu Bennet na Ndugu Kamala, shukrani kwa changamoto yenu. Hoja yako Ndugu Bennet ya hao wanaoagiza bidhaa za nje hata pale ambapo si lazima, imenigusa. Katika safari zangu za Tanzania, na wanafunzi, huwa tunatumia huduma mbali mbali, zikiwemo hoteli. Huwa nachukia nikiona wana sabuni au vitu vingine kutoka nje za nje ambavyo Tanzania inavyo pia. Nimeamua kuwa siku zijazo nitakuwa nawasusia na kwenda kwa wale wanaotumia vitu vya Tanzania. Wakiniuliza kwa nini siendi kwao, itabidi niwaeleze ukweli.
Ndugu Kamala, hizo hoja ulizotoa ni nzuri, na nimejikuta nacheka kwa jinsi ulivyoelezea ujinga huu wa kujiona sisi ni sisi, halafu kujenga hiyo nyumba na geti kubwa na kisha kuungua wote moto ukija. Ni hoja ya kufikirisha, laiti watu wangekuwa wanaelezwa hayo kila siku.
Unavyoulizia suala la mke au mume, inatukumbusha kuwa, pamoja na wazo la umuhimu wa kushirikiana, bado tutakuwa na mambo ya binafsi.
Nafurahia hizi tafakari.
Pasipo na ushirikiano,
hakuna maendeleo,
kwani kila mmoja hatapenda kuona mwingine anasonga mbele,
hivyo wote wanaishia kuwa wa hali moja na wenye mawazo yanayofanana,
miongoni mwa watu wasio na ushirikiano,chuki ni lazima, na kila mmoja anafikiri namna ya kujihami na mwingine kuliko kufikiri mambo ya maendeleo.
Watu kupenda bidhaa za nje inategemea na ubora wa bidhaa zenyewe wakati mwingine na bei.Hili la ubora nafikiri ni changamoto kwa wale wanaozalisha bidhaa.Nadhani wakitengeneza bidhaa zenye ubora natumai zitapendwa na kununuliwa kwa wingi.Tatizo letu ni kwamba tunazitengeneza bidhaa zetu kwa gharama ndogo matokeo yake zinakuwa hazina ubora, halafu tunazipeleka sokoni kwa gharama kubwa.
Ninapopita mjini huwa nawaonea huruma sana "wamachinga" kwani huwa wanafanya kazi ktk mazingira magumu. Binafsi nilikwisha azimia kununua vitu kwao kuliko kununua kwa mtu ambaye kwa kiasi chake ameshayapatia maisha. Lakini nilikuja kugundua kitu fulani. Bidhaa ya shilingi mia tano atataka kuiuza kwa shilingi elfu mbili.
Sasa mimi ninayetafuta kama yeye ,"loss" yote hii ya elfu na miatano si ningeweza kuendeshea maisha kabisa!
Kwa hiyo watanzania tuna kazi kubwa,mtu anataka akiuza bidhaa mara moja basi hata akikaa siku tatu bila kuuza asione shida kwani kuna bidhaa moja ilishanuua bidhaa nyingine zote.
Kwa hali hii wa kipato cha chini tunakandamizwa kupita maelezo.
Ndugu Kissima, shukrani kwa kukumbushia suala la ubora. Naafiki hoja yako kuwa mteja anahitaji bidhaa bora.
Kama kuna ushahidi kuwa kitu hicho cha nje ni bora zaidi, basi sina malumbano na mwenye duka au hoteli anayewawekea vitu hivi wateja wake.
Hata hivi, kuna watu wengi wana imani kuwa kitu kinachotoka nje, hasa "majuu," ni bora kuliko cha nchini. Watanunua juisi kutoka "majuu," badala ya kununua machungwa Kariakoo.
Ninaishiwa nguvu ninapokuwa hotelini, kwa mfano, na kuona wameweka sabuni au vikorokoro vingine kutoka nje wakati vitu hivyo vinatengenezwa pia Tanzania, na ninavifahamu ubora wake, na navitumia bila matatizo. Hapo ndipo ninapoishiwa nguvu.
Post a Comment