Sunday, March 29, 2009

Watanzania Wanaoishi Baa

Watanzania wengi wanaishi baa. Ingawa wana nyumba, au wamepanga vyumba, wanatumia muda mwingi zaidi baa kuliko kwenye makazi hayo. Wakitoka ofisini au sehemu nyingine ya kazi, wanaelekea baa. Wanakaa hapo hadi usiku, wakati baa inapofungwa. Wanakwenda nyumbani kulala tu, na asubuhi sana wanaamka tena na kwenda kazini. Jioni wanapotoka kazini, wanaelekea baa. Siku hadi siku, maisha yao ni hayo.

Kwa nini watu wanaishi baa? Bila shaka kila mtu anayeishi baa ana sababu zake. Katika kuongea na watu kijuu juu, inaonekana wako wanaoamini kuwa baa ni mahali pa kubadilishana mawazo ya maana. Sina hakika kuwa ulabu unaboresha mawazo. Wengine inaonekana wanaishi baa kwa vile nyumbani hakukaliki. Wako baa kama wakimbizi.

Hata kama sina ufahamu wa kutosha, naona kuna haja ya kulitafakari suala hili la Watanzania wanaoishi baa.

9 comments:

Zainab Mrisho Mwatawala said...

Mwalimu Mbele,
Mimi nashindwa kuchangia kwa uzamifu katika makala ya wanaoishi baa kwa sababu hiki ni kitu kigeni kwangu binafsi japo nafahamu fika kwamba si mmoja wala wawili wenye tabia hiyo.

Labda niseme tu kuwa watu kama hao ndio ambao huwaambia wenzao wamelishwa limbwata. Wale ambao hawana tabia za kuishi Baa. Ambao wanajali familia zao, wanashauriana na wenza wao, wanawajali watoto wao, hawaoni msingi wa kwenda kusambaza ofa kwa meza; kwa dhamira ya kujionyesha kuwa wao kwa siku ile ndio wana pesa za matumizi!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

yaani vitu vingine bwana. kuna katuni moja ilichorwa, mama kaondoka na mtoto, wamefika karibu na baa katoto kaliposikia harufu ya pombe, kakauliza mama mbona hapa pananuka babababa? yaana baba yake huwa ananuka urabu muda wote!

hata hivyo watu kama hawa wanahitaji msaada kwani ni ugigili zaidi ya starehe. kazini bosi noma, nyumbani famiia inabana nk.

Mbele said...

Bi Zainab, umetukumbusha jambo la msingi, namna shinikizo la jamii linavyoweza kuchangia tatizo hili. Kijamii na kisaikolojia, watu wengi tunayumbishwa na wasi wasi au hofu ya kueleweka hivi au vile na watu wengine. Kwa hivi, tunafanya mambo kufuata mkumbo badala ya kujiamini na kujitegemea kifikra. Mwanamme akikaa nyumbani analea watoto, anaambiwa amelishwa kitu na mkewe.


Ndugu Kamala, hoja yako kuwa watu wanaoishi baa wanahitaji msaada ina ukweli. Kipengele kimoja ni kuwa inawezekana watu wanaoishi baa wamechukua njia isiyo sahihi kuhusu matatizo yao ya kazini, nyumbani, au maisha kwa ujumla. Tunahitaji kuelimishana kuwa ulabu si dawa ya matatizo, bali ni kujiongezea matatizo.

Kipengele kingine nimekifahamu huku ughaibuni. Huku wanatambua kuna ugonjwa unaoitwa "alcoholism." Mtu anayeonekana hawezi kujizuia kunywa ulabu, anayeonekana kuhitaji ulabu kila mara, wanamwona kwa mtazamo tofauti. Wanakuwa na hisia kuwa ana huu ugonjwa uitwao "alcoholism," ambao unahitaji kushughulikiwa.

Sikuwahi kusikia walevi wa kwetu au watu wengine wanaopiga sana ulabu wakihisiwa kuwa na tatizo la "alcoholism." Wanaendelea kula ulabu kadiri wanavyoweza bila wasi wasi. Hili nalo ni tatizo.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndio tunhahitaji kuwasaidia mimi ninao kadhaa kwenye familia yetu na nilikutana na shirika moja la nchini sweden linajishughulisha na walevi jinsi ya kuwasaidia ili wasiendelee kuwa walevi tena japo idadi ya wanywaji inatsha na inazidi kushika kasi

Christian Bwaya said...

Watanzania wanaoishi baa.

Tunapojadili, hebu tuangaze mpaka vijiweni. Wapo watanzania wenzetu wanaoishi vijiweni. Si kwamba hawana kazi, la. Wanazo. Ila wanazitumia kama sehemu ya soga. Wanaahirisha kutoa huduma wanazodai kuzitoa, ili wapate muda wa soga.

Hawanywi pombe wengine. Kwa hivyo, baada ya 'kazi' ya kupiga soga ofisini wanaelekea kijiweni.

Kwa nini?

Hivi kwa wastani, ni masaa mangapi Mtanzania anakuwa makini kazini?

Mbele said...

Ni kweli, wako pia maelfu, au labda malaki, ya waTanzania wanaoishi vijiweni. Kazi tunayo.

Simon Kitururu said...

Nakiri mim ni mmoja wawaishio Baa! Na navyoandika nimetoka baa! Lakini nipo hapa nayi vilevile. Halafu sina Mtoto wala Mke na sidhani kuwa sipendwi. Na kanisani kesho asubuhi utanikuta kabla sijaenda tena baa.

Tupo tuishio pote kumbukeni msio enda baa !:-(

Nipo na nitajibu nikiwa baa au kanisani ikibidi .:-(

Simon Kitururu said...

katika comment hapo juuu , nayi ni NANYI.

Nani kawahakikishia wasioenda baa kwa kuwa nyumbani maana yake ndio kuna kitu cha muhimu wanafanya nyumbani?



Nyie msieenda baa leo mnauhakika ni nini cha maana mlichofanya nyumbani leo zaidi ya siye wa baa?

Mimi kwa kuwa baa naweza kukujulisha mambo kadhaa leo hii niliojifunza baa .

Daima usijaji kama wewe ni UNAYEJALI.

Mbele said...

Lo, Ndugu Kitururu, hapo umetupa changamoto nyingine, ambayo naitafsiri kama ifuatavyo.

Kwamba mtu anaishi nyumbani badala ya baa isitufanye tutoe hukumu kimoja kuwa huko nyumbani anafanya mema. Ndio, inawezekana mtu huyu anafanya mema huko nyumbani, kama vile kulea watoto, kufua nguo za watoto au kuosha sahani. Lakini inawezekana pia mtu akakaa nyumbani lakini anapiga bia yake hapo kwenye kochi na kuangalia televisheni saa zote bila kusaidia kazi yoyote ya nyumbani. Au inawezekana akawa ni mkorofi wa kutupwa hapo nyumbani. Kwa upande mwingine, inawezekana kuwa hao wanaoishi baa wanaepusha shari huko majumbani, yaani bora waishi baa kuliko nyumbani.

Na kama unavyosema, huyu anayeishi baa anaweza akaambulia moja mawili ya manufaa huko huko baa :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...