Posts

Showing posts from September, 2012

Tamasha la Vitabu "Twin Cities" Linakaribia

Image
Tamasha la vitabu liitwalo Twin Cities Book Festival litafanyika tarehe 13 Oktoba mjini St. Paul, Minnesota. Litafanyika kwenye sehemu maarufu iitwayo State Fairgrounds. Hii ni mara ya kwanza kwa tamasha hili kufanyika nje ya mji jirani wa Minneapolis. Nimeshiriki tamasha hili kwa miaka kadhaa, kama nilivyoelezea hapa na hapa . Mimi kama mwandishi wa vitabu nimeshalipia meza. Hapa pichani ni vitabu vyangu nitakavyopeleka kwenye tamasha. Sasa nangojea tu siku ije, nikajumuike na wadau mbali mbali katika nyanja za uandishi, uchapishaji, uuzaji, na uchambuzi wa vitabu.  Nangojea kuwashuhudia tena maelfu ya watu wa hapa wakiwa katika heka heka za kuangalia vitabu, kuvinunua, kuongea na waandishi, wachapishaji, wauza vitabu, na kadhalika.

Tanzania Inaendelea Kufedheheka

Image
Hapa kuna ujumbe kutoka Jumuia ya Nchi za Ulaya. Ujumbe unalalamikia mauaji ya mwanahabari Daud Mwangosi. Papo hapo, kati ya mambo mengine, ujumbe unaikumbusha serikali ya Tanzania umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari, uhuru ambao umeendana na uhuru wa watu kujieleza. Ujumbe unaikumbusha serikali ya Tanzania kufanya kila liwezekanalo kudumisha na kuendeleza uhuru huo. Suali langu ni hili: Kwa nini serikali ikumbushwe umuhimu wa kulinda haki za binadamu, kama vile hili ni suala gumu sana kulielewa na kulizingatia? Na kwa nini serikali yenyewe haikutambua mara moja umuhimu huo ikawa imechukua hatua muafaka, hadi ikumbushwe na nchi za nje? Hii ni fedheha kwa nchi yetu. Hapa nimeongezea tu taarifa ya suala ambalo nililiongelea siku chache zilizopita katika ujumbe huu hapa . Ujumbe wa  Jumuia ya Nchi za Ulaya ni huu hapa:

Tamko Dhidi ya Serikali ya Tanzania Kuhusu Uvunjwaji wa Haki za Binadamu

Nadhani wengi wetu tunafahamu kuwa kuna tamko linalosambaa mitandaoni dhidi ya serikali ya Tanzania, ambalo watu sehemu mbali mbali duniani wanasaini ili hatimaye lipelekwe serikalini, kuishinikiza kuheshimu haki za binadamu. Tamko lenyewe ni hili hapa . Heshima ya Tanzania inaendelea kuchafuka ulimwenguni kutokana tabia ya serikali hii. Hiyo ni habari ya kweli, sio uzushi. Leo, nimesoma taarifa kuwa mkurugenzi mkuu wa UNESCO ametoa tamko kuitaka serikali ya Tanzania iwajibike katika kuchunguza tukio la kuuawa mwanahabari Daud Mwangosi. Taarifa ni hii hapa .

Mwenyekiti Mjengwa Amtembelea Mjane wa Daud Mwangosi

Image
Ndugu zangu, Leo jioni nilifunga safari kwenda kumwona mjane wa marehemu Daud Mwangosi. Anakoishi ni maeneo ya Mwanyingo hapa Iringa. Mjane amerudi juzi jioni kutoka msibani Tukuyu. Itika, jina la mjane wa marehemu, anawashukuru kutoka ndani ya moyo wake, wale wote waliomchangia na wanaoendelea kumchangia fedha kama pole ya msiba mkubwa uliomkuta. Na wote waliokuwa naye katika wakati huu mgumu. " Mungu ndiye atakayewalipa"- Anasema Itika Mwangosi, mjane wa marehemu. Amerudi kutoka msibani akiwa hana cha kuanzia. Leo pekee tumefanya jitihada ya ziada kuhakikisha maji hayakatwi kutokana na bili iliyochelewa kulipwa kutokana na msiba wa ghafla wa Daud Mwangosi . Kutokana na michango yenu, kesho Jumatatu familia italipa deni la maji lisilozidi shilingi laki moja na nusu. Nilichokiona kwa mjane wa Daud Mwangosi ni uhalisia wa hali aliyo nayo sasa. Anafikiria jinsi atakavyomudu kuishi na kuitunza familia. Alifarijika sana aliposikia amechangiwa kiasi cha fedha ki

Hotuba ya Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa wa-Tanzania, Washington DC

Image

Kanisa Katoliki Latoa Zawadi ya Miaka 50 ya Uhuru

Image

Waalimu wa Idara Yangu, Chuoni St. Olaf

Image
Hapa ni picha iliyopigwa siku chache zilizopita ya walimu wa idara ya ki-Ingereza katika Chuo cha St. Olaf . Nimefundisha katika idara hii tangu mwaka 1991. Kuanzia mwaka 1976 hadi huo mwaka 1991 nilikuwa mwalimu katika idara ya Literature, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Chuo cha St. Olaf kinatoa shahada ya kwanza katika masomo mbali mbali. Walimu wengi niliowakuta katika idara hii hapa St. Olaf wamestaafu. Waliobaki, ambao wamo pichani, ni watano tu, na mwingine, wa sita, hayupo katika picha hii. Nimekuwa mwalimu pekee kutoka Afrika tangu ule mwaka 1991, na sasa nami nimeanza kuwazia suala la kustaafu, ili nirudi Tanzania nikiwa bado na umri wa kuendelea na kazi za taaluma.

Ziara Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki, Songea

Image
Kama nilivyoelezea tena na tena, napenda kutembelea vyuo ninapokuwa Tanzania. Soma kwa mfano, hapa . Ni fursa ya kujiweka sawa katika ufahamu wa nini kinachoendelea, changamoto zilizopo, mikakati ya kuboresha elimu ya juu. Napata fursa ya kujadiliana na wahusika namna ya kushirikiana na kuchangia vyuo hivi. Tarehe 21 mwezi Julai, mwaka huu, nilitembelea tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin, mjini Songea. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin ni mradi wa Kanisa Katoliki Tanzania. Ni mtandao ambao tayari una vituo sehemu mbali mbali za nchi. Kwa taarifa zaidi, soma hapa . Hapa kushoto naonekana na Profesa Donatus Komba, makamu wa mkuu wa chuo hicho mjini Songea. Yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu siku ya ziara yangu, akinitembeza kila mahali na kunipa maelezo. Hapa kushoto naonekana nikitia sahihi katika kitabu cha wageni. Hapa kushoto ni jengo la utawala. Chuo cha Mtakatifu Augustin kina mipango mikubwa ya kupanua mtandao wake. Kwa upande wa Songea, tayari Semina

Mwangosi Aliuawa Hivi: Simulizi ya Shahidi

Image
Mwangosi aliuawa hivi •  SIMULIZI YA SHAHIDI na Mwandishi wetu SEPTEMBA 2, 2012, polisi waliua kikatili mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa. Alikufa mbele ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, wakati polisi hao walipovamia ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kuwatawanya wasifungue tawi la chama chao katika kijiji hicho. Mmoja wa watu walioshuhudia tukio zima, ni mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah Khamis. Ifuatayo ni simulizi ya kile alichokiona wakati polisi wanaondoa uhai wa Mwangosi. SIKU hiyo asubuhi tulipata taarifa kuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo (RPC), Michael Kamuhanda, alipanga kukutana na waandishi wa habari majira ya saa 2.30 ambapo waandishi walifika akiwemo Daudi Mwangosi. Tukiwa katika chumba cha mikutano katika jengo la polisi Mkoa wa Iringa, Kamanda wa mkoa huo, alifika akiongozana na maafisa wake wawili na kuanza ku

Mchezo wa "Pool," Lizaboni, Songea

Image
Tarehe 21 Julai, wakati natoka Peramiho kurudi Songea, dala dala ilisimama kidogo kwenye kitongoji cha Lizaboni, ambacho ni sehemu ya Songea. Hapo niliona mchezo wa "pool" unaendelea, nikapiga picha hii nikiwa ndani ya dala dala.

Kanisa Kuu la Peramiho

Image
Hii ni picha ya kanisa kuu la Peramiho, ambayo nilipiga tarehe 21 Julai. Safari yangu ya Peramiho niliielezea hapa .

Nilizuru Nyumba za Ibada za wa-Hindu, India

Image
Mwaka 1991 nilipata fursa ya kwenda India, kwa utafiti wa mwezi moja. Nilifikia katika taasisi ya American Studies Research Center, ambayo ilikuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Osmania, mjini Hyderabad. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishi na wa-Hindi. Siku moja, Afande Rana, mstaafu wa jeshi la India, alinichukua kwa piki piki yake, tukazunguka maeneo kadhaa ya Hyderabad. Alinipitisha katika nyumba kadhaa za ibada za wa-Hindu, kama inavyoonekana katika ukurasa huu.   Hapa kushoto tunaonekana mbele ya nyumba mojawapo ya ibada, tukiwa tumevaa vilemba. Kwa bahati nzuri, ninasoma misahafu na maandishi mengine ya u-Hindu. Ninafahamu kiasi cha kuridhisha kuhusu historia ya dini hii, imani yake. Ni dini yenye miungu wengi, baadhi wanafahamika kwa kila muumini na kuabudiwa, na wengine hawafahamiki na kila muumini. Baadhi ya miungu hao wanachorwa wakiwa na umbo la wanyama. Kwa mfano mungu aitwaye Ganesha anawakilishwa na tembo, na mungu aitwaye Hanuman anawakilishwa na umbo la

Itafakari Katuni Hii

Image
Katuni hii nimeiona katika mtandao wa Facebook. Inamwonyesha mchora picha na mteja wake. Huyu mteja ni mu-Islam anayeonekana amekaa kwenye kochi, akiwa ameshika ua. Mwangalie mteja huyu na halafu angalia picha iliyochorwa. Nimeitafakari picha hii na bado naitafakari. Ninaona ina mengi ya kutufundisha. Je, mdau una maoni gani?

Nimekutana na Wanablogu Songea

Image
Mwaka huu, kwa mara nyingine, nilifanikiwa kufika Songea, nikaonana na Ndugu Christian Sikapundwa, mmiliki na mwendeshaji wa blogu ya Tujifunze Kusini . Hii ilikuwa ni mara pili kukutana, kwani tulishakutana mwaka jana pia, kama nilivyoripoti hapa . Tulifurahi kukutana tena, tukabadilishana mawazo na kupiga michapo kuhusu mambo mbalimbali. Kwa vile sisi wote ni walim, tulikuwa na mengi ya kuongelea. Hapa kushoto tunaonekana tukijipongeza na kushukuru kwa kukutana. Hapa kushoto tunaonekana tukiwa na mdogo wangu na binti yake. Katika pita pita yangu kwenye eneo la Chuo Kikuu kipya cha Mtakatifu Augustin (SAUT),  tarehe 21 Julai, nilikutana na jamaa ambaye alijitambulisha kuwa ni Willy Migodela, mmiliki na mwendeshaji wa blogu ya mtandao-net . Nilifurahi kukutana naye, kwani mimi ni mmoja wa wadau wa blogu yake. Ni yeye aliyenitambua tulipoonana. Alisema kuwa alikuwa mwanafunzi katika darasa la uzamili la Profesa Mugyabuso Mulokozi, ambamo niliwahi kutoa mhadhara

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Makala hii nimeshaichapisha mara kadhaa katika hii blogu yangu, na imewahi kuchukuliwa na kuchapishwa na mitandao mingine pia. Nimeona niiweke tena hapa.  -------------------------------- Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa. Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:   Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu wa

Ziara Kwenye Kanisa Kuu Peramiho

Image
Tarehe 21 Juni nilitembelea Peramiho, mkoani Ruvuma. Peramiho ni kituo kikuu kimojawapo cha Kanisa Katoliki nchini Tanzania, tangu enzi za m-Jerumani, ambapo wamishenari walijenga kanisa hapa. Walianzisha hospitali, shule, vyuo vya ualimu, ufundi na uuguzi; shirika la uchapishaji, na mambo mengine muhimu kwa jamii. Hapa kushoto ni picha ya Kanisa Kuu linavyoonekana leo. Pembeni mwa Kanisa kuna nyumba za mapadri na masista, na pia ofisi. Hata Abate/Askofu mstaafu anaishi hapa. Nilienda Peramiho ili kumwona, kwani sijawahi kumwona tangu mwaka 1970, nilipomaliza kidato cha nne katika Seminari ya Likonde, ambapo alikuwa mwalimu wangu wa Historia na ki-Ingereza. Niliambiwa amesafiri. Nje ya makazi yake nilipiga picha inayoonekana hapa kushoto, kwa kuvutiwa na sanamu ya Mtakatifu Benedikt. Maaskofu, mapadri, masista, na mabruda walioleta dini ya Katoliki Peramiho ni wa shirika la Mtakatifu Benedikt. Pamoja na dini, walijishughulisha na masuala ya afya, elimu, na ustawi