Posts

Showing posts from June, 2012

Kugombana na Madaktari ni Uchuro

Mgomo wa madaktari umeanza tena, siku chache zilizopita. Inasikitisha kuona kuwa tumefikia hali hiyo. Ukiniuliza nani namhesabu kama mwajibikaji mkuu aliyesababisha tatio hili, nitakuambia kuwa ni serikali ya CCM. Huo umekuwa msimamo wangu tangu pale ulipotokea mgomo wa mwanzo wa madaktari wiki kadha zilizopita. Nilieleza msimamo huo hapa . Siku chache zilizopita, nilimsikiliza mwenyekiti wa madaktari wanaogoma, Dr.Stephen Ulimboka, akiongelea jinsi uhaba wa vitendea kazi ulivyo. Alitaja mfano wa kifaa cha "CT-scan" ambacho kimeharibika Muhimbili yapata miezi mingi iliyopita. Kama nilivyosema katika makala yangu ya mwanzo, sera za serikali ya CCM zinasabisha upotevu mkubwa wa mali ya Tanzania, kama vile madini. Serikali yenyewe imekiri kuwa mikataba ya madini ya siku zilizopita ilikuwa ni ya hasara kwa Taifa. Lakini je, serikali imeshamwajibisha yeyote aliyehusika katika kusaini mikataba hiyo? Je, ni kweli kuwa nchi hii haiwezi kununua hicho kifaa cha "CT-scan"

Nimetua Bondeni, kwa Madiba

Tarehe 14, nilitua Johannesburg, kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na American Council of Learned Societies (ACLS). Mkutano tumefanyia katika chuo Kikuu cha Witwatersrand, ukiwa umehudhuriwa na watafiti kutoka Afrika Kusini, Ghana, Marekani, Nigeria, na Tanzania. Tulijadili mada za utafiti zilizowasilishwa na watafiti mbali mbali. Utafiti huo hugharamiwa na ACLS, kwa wale ambao miradi yao ya utafiti inaonekana kuwa ya kiwango kinachotakiwa. Mada zote zilikuwa katika nyanja mbali mbali za sayansi ya jamii.

Mama Shakila, Mwimbaji Maarufu

Image
Mama Shakila ni mwimbaji maarufu wa taarab. Imepita miaka yapata 22 tangu nilipobahatika kumtembelea na kuongea naye kuhusu maisha yake na masuala ya sanaa na jamii. Laiti ningekuwa nimepata fursa zaidi ya kuongea naye hadi kuandika makala za kiwango cha juu kitaaluma, au hata kitabu  cha aina hiyo. Mama Shakila, sawa na wasanii wetu wengi, ametoa mchango mkubwa kwa jamii yetu na ulimwengu kwa ujumla. Lakini, jamii yetu ina tatizo la kutowaenzi watu hao ipasavyo. Kufanya utafiti na kuandika habari zao na tathmini ya mchango wao ingekuwa namna moja ya kuwaenzi, pia kuhakikisha kuwa wanapata kipato wanachostahili kutokana na kazi zao. Ingebidi wasomi wawe wanaandika makala na vitabu kuchambua kazi za wasanii hao; wanafunzi vyuoni wawe wanaandika tasnifu, na pawe na mijadala, makongamano, ya kuchambua mchango wa watu hao. Lakini jamii yetu, pamoja na kufaidika kutokana na juhudi za watu hao, ina jadi ya kutowajali kimaslahi, na kisha kuwasahau.

Mahojiano: Jacton Manyerere na wana-Uamsho (Zanzibar)

Image
Mwandishi wa gazeti la JAMHURI, Manyerere Jackton (pichani katikati), amefanya mahojiano ya ana kwa ana na Amiri Mkuu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed, aliyeeleza lengo kuu la Jumuiya hiyo ya Kiislamu. JAMHURI: Ni nini chanzo cha vurugu za Mei 26? Sheikh Farid: Kilichotokea hapa kwa muda mrefu, japo inasikika Jumuiya ya Uamsho ndiyo inayofanya mihadhara, lakini ni Umoja na Jumuiya za Kiislamu ambazo zimekuwa zinaendesha mihadhara. Tumefanya mihadhara zaidi ya mia moja hadi sasa - mikutano zaidi ya mia pamoja na makongamano tofauti. Na lengo zaidi hapo awali lilikuwa ni kuwaelimisha watu kujua Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuona ni jinsi gani inawabana Wanzibari na haijawapa ile haki yao ya kuujadili Muungano. Na baada ya hapo kilichokuwa kinazungumzwa zaidi ni kuwaelimisha wananchi kujua haki yao, kujua mustakabali wa nchi yao na umuhimu wa kuuhoji Muungano au kuujua Muungano. Wazanzibari wao kama washirika na Watanganyika wana haki ya kuuhoji Muungano.

Kanisa Lilivyoungua Zanzibar

Image
Kati ya uharibifu uliofanyika Zanzibar wakati wa vurugu za hivi karibuni makanisa yalichomwa moto. Hapa kushoto ni picha ya kanisa likiungua. Nimeipata hapa . Kutokana na kauli mbali mbali mtandaoni, ni wazi kuwa wako watu ambao wamefurahishwa na uchomaji moto wa haya makanisa, pamoja na vitabu vilivyokuwemo humo, kuanzia vya sala hadi Biblia. Wako ambao wanasema kuwa Zanzibar ni nchi ya ki-Islam na u-Kristo hautakiwi kule. Kwa maana hiyo, kuchoma moto makanisa ni kuwakomoa wa-Kristo. Maajabu ya dunia hayaishii hapa, kwani wako pia watu ambao wanauchukia u-Islam na wanataka kuwakomoa wa-Islam. Wangeikaribisha fursa ya kuichoma moto misikiti. Miezi kadhaa iliyopita, tulipata taarifa za kikundi cha wa-Marekani waliotangaza kuwa watachoma moto Quran. Kabla ya hapo, tulisikia kwamba kule kwenye jela ya Guantanamo, kulikuwa na kitendo cha kuikojolea Quran. Bila shaka, lengo ni kuwakomoa wa-Islam. Wenzetu ndio hao. Kweli, dunia ina mambo.

Watafiti wa ki-Tanzania Tumekutana Ughaibuni

Image
Kila siku ni ya pekee, lakini kuna siku ambazo ni za pekee zaidi. Leo nilienda Luther Seminary , St. Paul, kuonana na wachungaji wawili, ambao ni Rev. Dr. Falres Ilomo (aliye katikati pichani) na Rev. Dr. Andrea Mwalilino (hapo kulia). Mchungaji Mwalilino, ambaye tumefahamiana kwa miaka kadhaa, alikuwa ameniarifu kuwa kuna huyu mgeni kutoka Tanzania, ambaye yuko kwa kipindi tu hapa Luther Seminary . Tulitafuta fursa ya kuonana, na leo imewezekana. Mchungaji Mwalilino, ambaye alihitimu shahada ya uzamifu Luther Seminary , tuko wote hapa Minnesota, ingawa miji mbali mbali. Mgeni wetu, ambaye alihitimu shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Augustana, Ujerumani , ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa . Mimi mwenye blogu hii nilihitimu shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison . Mjadala wetu ulikuwa wa kiwango cha juu kitaaluma. Tumeongelea utafiti katika tamaduni na dini za jadi za wa-Afrika, lengo moja muhimu likiwa ni kutafakari namna ya kuziweka dhana

Tamko la Maaskofu Kuhusu Machafuko na Hali ya Vitisho Zanzibar

Sisi Maaskofu, Mapadre, Wachungaji na Waumini tunaoishi Zanzibar, tumekutana leo tarehe 30 Mei 2012 kufutia hali ya machafuko, uvunjifu wa amani, uchomaji wa Makanisa, uharibifu wa mali za Kanisa na vitisho dhidi ya Wakristo na mali zao. Tumekutana na tunatoa tamko baada ya muda mrefu wa kimya na uvumilivu tuliosafiri nao kwa takribani miaka 11, kwa kumbukumbu zetu tangu mwaka 2001. Tunajua na tunauambia umma wa wapenda amani kuwa matukio ya tarehe 26 hadi 28 Mei 2012 ni matokeo ya mahubiri na mihadhara ambayo imekuwa ikiendeshwa iliyolenga kwa makusudi kuutukana na kuukashifu Ukristo hapa visiwani Zanzibar na hivi kupandikiza hofu miongoni mwa waumini wa dini ya Kikristo. Tunashawishika kusema kuwa ufadhili na ushawishi wa vurugu na vitisho hivi vina udhamini wa ndani au nje ya nchi yetu. Tumefikia hatua hiyo baada ya matukio mbalimbali yaliyokuwa yanafanywa dhidi ya Kanisa na mali zake tangu mwaka 2001 hadi hivi majuzi yalikuwa yakitolewa taarifa kwenye vyombo vya Ul