Posts

Showing posts from March, 2018

Kitabu Kinaendelea Kupigiwa Debe Nebraska

Image
Mfanya biashara au mtoa huduma hufarijika anapoona wateja wakija tena kufuata kile walichokipata kabla. Imekuwa hivyo kwangu kama mwandishi. Mimi si mfanyabiashara, bali ni mwalimu. Uandishi ni sehemu ya ualimu. Ninafarijika na kufurahi ninapoona watu wakifaidika na maandishi yangu. Ninaandika ujumbe huu kuelezea ujumbe juu ya kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences  kutoka Nebraska, jimbo mojawapo la Marekani. Waumini wa kanisa la ki-Luteri la Marekani, ELCA, wa sinodi ya Nebraska wana programu ya kuzuru Tanzania iitwayo vision trip , kujifunza masuala ya utamaduni na maisha ya wa-Tanzania na kubadilishana uzoefu, ili kujenga mahusiano na maelewano. Mwaka hadi mwaka, waratibu wa programu wamekipendekeza kitabu changu hicho. Leo nimeona chapisho la mwongozo kwa ajili safari ya mwaka 2018. Humo, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, kitabu changu kimeendelea kupendekezwa kwa wasafiri: For those persons wanting to more deeply explore cultural differences

Nimenunua CD za "Hamlet"

Image
Leo niliingia katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf kununua vitabu ambavyo nilikuwa nimepangia tangu jana. Lakini wakati naangalia vitabu, niliona kifurushi cha CD za Hamlet , tamthilia ya Shakespeare. Hiyo niliiona kama bahati ya pekee, kwa sababu siku chache zilizopita niliandika katika blogu hii kuwa tunasoma Hamlet. Ilikuwa ni wazi kuwa CD hizi nimeziona wakati muafaka. Nilichukua hicho kifurushi cha CD, nikakijumlisha na vitabu nilivyopangia kununua nikalipia vyote. Jioni hii nimefungua kifurushi nikaona ziko CD tatu. Zimeandaliwa na Folger Theatre, ambacho ni kitengo cha Folger Shakespeare Library,  ambayo ndio makataba kubwa kuliko zote duniani za kazi za William Shakespeare na machapisho juu yake. Watafiti kutoka duniani kote wanafanya utafiti katika maktaba hii. Hamlet , kama ilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, inapatikana katika matoleo mbali mbali. Folger Shakespeare Library ina toleo lake. Kama nilivyosema, nimeanza kusikiliza jioni hii. Nimevutiwa sana

Tunasoma "Hamlet"

Image
Muhula huu nina mwanafunzi mwingine aliyeamua kujitungia kozi yake mwenyewe na kuifanya chini ya usimamizi wangu. Utaratibu huu uko hapa chuoni St. Olaf, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Kwa kushauriana nami, mwanafunzi alijitungia kozi juu ya "The Living and the Dead: Folklore and Tragedy." Tulikubaliana kusoma  Agamemnon (Aeschylus), Beowulf (translated by Seamus Heaney), Inferno (Dante Alighieri), Hamlet (William Shakespeare), Othello (William Shakespeare), Love in the Time of Cholera (Gabriel Marcia Marquez), na As I Lay Dying (William Faulkner). Tumeshasoma Beowulf , na sasa tuna soma Hamlet . Napenda kusema neno kuhusu Hamlet katika mkabala wa kozi yetu hii. Kwanza napenda kusema kuwa niliwahi kuongelea Hamlet katika blogu hii. Nilifanya hivyo kwa kujikumbusha tamthilia hii maarufu. Lakini sasa tunaisoma tukiwa na lengo la kuihusisha na mada ya kozi "The Living and the Dead: Folklore and Tragedy." Hamlet ni tamthilia ya tanzia ("

Nimenunua Vitabu Vipya vya Mashairi

Image
Katika siku chache zilizopita, nimenunua vitabu vipya viwili vya mashairi. Kimoja ni Collected Poems: 1974-2004  cha Rita Dove, ambacho nilikinunua mjini Moscow, Idaho. Kingine ni Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein ambacho nilikinunua mtandaoni Amazon. Nilipokuwa Moscow katika tamasha la Hemingway, niliingia katika duka la Book People of Moscow.  Niliangalia, nikaona kitabu hiki Collected Poems , ambacho sikukifahamu kabla. Nilivutiwa kwa sababu nilifahamu habari za Rita Dove, kwamba ni mshairi maarufu sana, aliyepata tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya Pulitzer. Zaidi ni kuwa niliwahi kusoma insha yake "Either I'm Nobody, or I'm a Nation," ambayo ni uchambuzi wa mashairi ya Derek Walcott. Nilikuwa ninafundisha tungo za Walcott, nikaitafuta makala hii na niliona ilivyojaa tafakari na ilivyoandikwa kwa ustadi. Makala hii ilinithibitishia kuwa Rita Dove ana akili sana. Hii ikawa sababu kubwa ya mimi kununua Collected Poems . Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibr

Mdau wa Kitabu Amekuja Tena

Image
Hapa pichani ninaonekana na De'Vonna, mmoja wa waandaaji wa maonesho ya waandishi yaliyoitwa Minnesota Black Authors Expo, ambayo niliyaelezea katika blogu hii. Anaonekana ameshika kitabu changu, Africans and American:Embracing Cultural Differences .  Picha tulipiga wakati wa maonesho. Amenilitea ujumbe kuwa anahitaji nakala nyingine ya hiki kitabu. Kwa kuzingatia jinsi mama huyu alivyo na ushawishi katika jimbo hili la Minnesota, hasa miongoni mwa wenzake wa-Marekani Weusi, nimeguswa na ujumbe wake kwa namna ya pekee. Tangu nilipoandika kitabu hiki, nilikuwa na dukuduku ya kujua wa-Marekani Weusi watakuwa na maoni gani kuhusu yale ninayosema juu ya mahusiano yao na sisi wa-Afrika. Nilielezea dukuduku hiyo katika blogu ya ki-Ingereza. Kama inavyoeleweka, mahusiano hayo yanawatatiza baadhi ya watu. Kwa hivyo ninapopata mrejesho kutoka kwa hao wenzetu, ninauchukulia kwa uzito wa pekee. Nimefarijika na kufurahi kwamba De'Vonna anataka nakala nyingine ya kitabu changu. Sijui