Showing posts with label tungo. Show all posts
Showing posts with label tungo. Show all posts

Thursday, September 27, 2018

Nimenunua Tena Tungo Zote za Shakespeare

Tarehe 24 Septemba, nimenunua tena kitabu cha tungo zote za William Shakespeare.  Nilikinunua katika duka la Half Price Books mjini Apple Valley nilipotoka Burnsville kuangalia kitabu changu kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Ingawa tayari nina vitabu vinne vyenye tungo zote za Shakespeare, sikuona tatizo kununua hiki pia. Kuwa na nakala mbali mbali za kitabu cha tungo za Shakespeare kuna mantiki nzuri kwa sababu tungo hizo zimehaririwa kwa namna mbali mbali. Hii imekuwa ni sehemu ya historia ya uchapishaji wa tungo za Shakespeare.

Mara kwa mara neno linaloonekana kwenye nakala fulani si lile linaloonekana kwenye nakala nyingine au limeandikwa kwa namna tofauti na lilivyo katika nakala nyingine. Hali hiyo ni ile inayoonekana katika miswada ya tungo za zamani, sehemu mbali mbali ulimwenguni, ikiwemo za huku kwetu, kama zile za Liongo Fumo.

Tofauti hazikwepeki, kwa sababu uandishi katika enzi za Shakespeare ulikuwa tofauti na wa leo. Leo kitabu kikichapishwa, tunategemea ni nakala sahihi ya mswada ulivyoridhiwa na mwandishi. Wakati wa Shakespeare, hapakuwa na utaratibu huo. Watu walikuwa wananakili andiko walivyoweza, na tofauti mbali mbali zilijidhihirisha kutoka kwa mnukuzi hadi mwingine.

Kadhalika waigizaji wa tamthilia majukwaani walikuwa wanatamka, pengine bila kujitambua, maneno yaliyofanana sauti, ingawa maneno ya mwandishi yalikuwa tofauti. Hiyo nayo ni sababu ya waandishi kuandika maneno tofauti.

Kwa hali hiyo, ni busara kuwa na nakala tofauti za kitabu hiki cha tungo zote za Shakespeare. Hata mtu ukiwa na kitabu cha tamthilia mojawapo tu, ni busara kuwa na nakala zilizohaririwa na wahariri tofauti wa kitabu hicho.

Faida nyingine ni kwamba baadhi ya nakala hizi zina maelezo ya wahariri juu ya mambo mbali mbali, yakiwemo maana za maneno na semi. Maelezo haya ni msaada mkubwa kwetu, kwani ki-Ingereza cha wakati wa Shakespeare kina tofauti nyingi na kiIngereza cha leo.

Thursday, March 8, 2018

Nimenunua Vitabu Vipya vya Mashairi

Katika siku chache zilizopita, nimenunua vitabu vipya viwili vya mashairi. Kimoja ni Collected Poems: 1974-2004  cha Rita Dove, ambacho nilikinunua mjini Moscow, Idaho. Kingine ni Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein ambacho nilikinunua mtandaoni Amazon.

Nilipokuwa Moscow katika tamasha la Hemingway, niliingia katika duka la Book People of Moscow. Niliangalia, nikaona kitabu hiki Collected Poems, ambacho sikukifahamu kabla. Nilivutiwa kwa sababu nilifahamu habari za Rita Dove, kwamba ni mshairi maarufu sana, aliyepata tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya Pulitzer.

Zaidi ni kuwa niliwahi kusoma insha yake "Either I'm Nobody, or I'm a Nation," ambayo ni uchambuzi wa mashairi ya Derek Walcott. Nilikuwa ninafundisha tungo za Walcott, nikaitafuta makala hii na niliona ilivyojaa tafakari na ilivyoandikwa kwa ustadi. Makala hii ilinithibitishia kuwa Rita Dove ana akili sana. Hii ikawa sababu kubwa ya mimi kununua Collected Poems.

Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein niliinunua baada ya kuiona imetajwa mtandaoni Amazon. Nilikuwa sifahamu kuwepo kwake, lakini kwa jinsi ninavyomwenzi Ebrahim Hussen ambaye nilimfahamu tulipokuwa wote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yeye akiwa mhadhiri wakati ninasoma, na hatimaye tukawa tunafundisha wote, niliona ninunue kitabu hiki. Mimi mwenyewe nimechapisha makala juu ya tungo za Ebrahim Hussein katika Encyclopedia of African Literature iliyohaririwa na profesa Simon Gikandi.

Nimeanza kuyasoma mashairi yaliyomo katika vitabu vyote viwili. Tayari nimeona kuwa Rita Dove anaandika kwa nidhamu ya hali ya juu, ya kutumia maneno yanayohitajika tu, na anatupeleka sehemu mbali mbali za dunia, tangu enzi za kale hadi leo, kama anavyofanya Derek Walcott katika tungo zake, iwe ni mashairi au tamthilia. Diwani ina washairi wengi chipukizi. Ni fursa yao kuonekana kwa wasomaji.

Sunday, February 19, 2017

Utungo wa Pushkin, "Eugene Onegin," Ni Mtihani

Siku chache zilizopita, niliandika katika blogu hii kuwa nilikuwa ninajiandaa kusoma Eugene Onegin, utungo maarufu wa Alexander Pushkin. Nilianza hima, na sasa ninaendelea.

Nilifahamu tangu zamani kuwa Pushkin alikuwa ameandika tungo zingine pia. Nilifahamu kuwa Eugene Onegin ndio utungo wake maarufu kuliko zingine. Nilifahamu kuwa utungo huo ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa kishairi.

Nilidhani kuwa ningesoma Eugene Onegin bila matatizo, kama ninavyosoma kazi za waandishi wengi. Baada ya kuanza kuusoma, na ninavyoendelea kusoma, ninajikuta kama vile niko katika mtihani. Eugene Onegin si rahisi kama nilivyodhani.

Pushkin ameusuka utungo wake kwa umahiri mkubwa, akitumia mbinu mbali mbali za kisanii, na pia taarifa za wasanii wa mataifa mbali mbali, kuanzia zama za kale, hadi zama zake. Humo kuna majina ya watunzi wa mataifa mbali mbali, kama vile Theocritus, Juvenal, Ovid, Racine, Chateaubriand, Lord Byron, pamoja na waandishi na waigizaji kadha wa kadha wa u-Rusi, wa wakati wa Pushkin na kabla yake, ambao hata mimi sikuwa ninawafahamu.

Kwa kufuatilia dondoo, dokezo, na maelezo yaliyomo, ninajifunza mambo mengi mapya. Mtindo huu wa Pushkin unanikumbusha ushairi wa Derek Walcott. Kusoma mashairi yake ni chemsha bongo. Unajikuta ukipelekwa sehemu nyingi katika historia, ikiwemo historia ya fasihi, sanaa, na falsafa.

Tafsiri ya Eugene Onegin ninayosoma ni ya Hofstadter. Katika kupambana na tafsiri yake, nimefikia uamuzi kuwa nikimaliza kusoma tafsiri, nisome tafsiri nyingine angalau moja ya mtu tofauti. Lakini ukweli utabaki kuwa ingekuwa bora zaidi kama ningekuwa ninakifahamu ki-Rusi, nikajisomea mwenyewe alichoandika Pushkin. Kama taaluma inavyotufundisha, hakuna tafsiri ambayo inaweza kuwa sawa na utungo unaotafsiriwa.

Mtu unaweza kujiuliza: Kwa nini ninajipitisha katika mtihani huu wa kusoma Eugene Onegin, badala ya kusoma vitabu rahisi? Jibu langu ni kuwa chemsha bongo ni muhimu kwa afya ya ubongo, kama vile mazoezi ya viungo yalivyo muhimu kwa afya ya binadamu. Utungo kama Eugene Onegin, kwa jinsi ulivyosheheni utajiri wa fikra na kumbukumbu za aina mbali mbali, ni njia bora ya kutajirisha akili. Nitajisikia mwenye furaha nitakapoweza kusema nimeusoma na kuutafakari kwa makini utungo huu mashuhuri wa Pushkin.

Saturday, November 19, 2016

"Ozymandias:" Shairi la Shelley na Tafsiri Yangu

Percy Bysshe Shelley ni mmoja kati ya washairi maarufu kabisa katika ki-Ingereza, ambaye nilimtaja jana katika blogu hii. Alizaliwa mwaka 1792 akafariki mwaka 1822. Ni mmoja wa washairi wanaojumlishwa katika mkondo uitwao "Romanticism," ambamo wanaorodheshwa pia washairi wa ki-Ingereza kama William Blake, William Wordsworth, Samuel Taylor Coleridge, na Lord Byron. "Romanticism" ni mkondo uliojitokeza katika mataifa na lugha zingine pia, kama vile Ujerumani na Ufaransa. Kwa waandishi wa Afrika au wenye asili ya Afrika waliotumia ki-Faransa, "Romanticism" ilijitokeza kama "Negritude," jambo ambalo nimeelezea katika mwongozo wa Song of Lawino.

"Ozymandias" ni shairi mojawapo maarufu la Shelley. Ninakumbuka kuwa nililisoma kwa mara ya kwanza nilipokuwa sekondari, miaka ya kuanzia 1967. Kitu kimoja kinacholitambulisha shairi hili kuwa ni la mkondo wa "Romanticism" ni ule mtazamo wake ambao Edward Said aliuita "Orientalism." Lengo langu hapa si kuongelea "Romanticism" wala "Orientalism," bali kutaja mambo mawili matatu yanayohusu shairi la "Ozymandias" na suala la tafsiri.

Suala la kutafsiri kazi za fasihi nimeliongea tena na tena katika blogu hii. Pamoja na ugumu wake, ninaona kuwa baada ya mahangaiko yote, inakuja raha ya aina yake. Sio raha au furaha inayotujia tunaposhinda shindano au mtihani, kwani katika kutafsiri hakuna ushindi. Kinachotokea ni kuwa mtu unafanikiwa kuuzalisha upya utungo unaowania kuutafsiri.

"Ozymandias" ni shairi ambalo ninalielewa vizuri kabisa lilivyo katika ki-Ingereza. Lakini, nilivyojaribu kulitafsiri, tangu jana, limenihangaisha. Nimejionea jinsi ufahamu wangu wa ki-Swahili unavyopwaya. Nimejikuta nikijiuliza iwapo madai yetu wa-Tanzania kuwa tunakifahamu vizuri ki-Swahili ni ya kweli au ni porojo. Nilipata taabu zaidi kutafsiri mstari wa tano na mistari mitatu ya mwisho. Pamoja na kwamba nimeweka tafsiri yangu hapa, siridhiki nayo.

Kuhusu dhamira, shairi la "Ozymandias" lina mengi ya kujadiliwa. Kwa mtazamo wa fasihi linganishi, dhamira ya kisa cha msafiri inajitokeza katika tungo nyingi za tangu zamani. Mfano moja ni hadithi ya Misri ya kale iitwayo "The Tale of the Shipwrecked Sailor." Kuna pia hadithi za baharia Sindbad. Pia kuna shairi la Samuel Taylor Coleridge, "The Rime of the Ancient Mariner." Tungo zote hizi zina mambo ya ajabu na mtazamo juu ya ulimwengu na tabia za binadamu.

Vile vile, "Ozymandias" ni shairi lenye ujumbe mzito. Ni onyo kwa wanadamu kuwa utukufu wa hapa duniani, uimara wa himaya au udikteta ni vitu ambavyo vina mwisho. Ujumbe huu umo pia katika tungo zingine maarufu, kama vile utenzi wa Al Inkishafi. Naishia hapo.
--------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ozymandias

Percy Bysshe Shelley, 1792-1822

I met a traveller from an antique land,
Who said: "Two vast and trunkless legs of stone
Stand in the desert.... Near them, on the sand,
Half sunk, a shattered visage lies, whose frown,
And wrinkled lip, and sneer of cold command,
Tell that its sculptor well those passions read
Which yet survive, stamped on these lifeless things,
The hand that mocked them, and the heart that fed;
And on the pedestal, these words appear:
'My name is Ozymandias, King of Kings;
Look on my Works, ye Mighty and despair!'
Nothing beside remains. Round the decay
Of that colossal Wreck, boundless and bare
The lone and level sands stretch far away."

Tafsiri

Nilimkuta msafiri kutoka nchi ya kale
Ambaye alisema, "Miguu miwili ya mawe mikubwa sana isiyo na kiwiliwili
Imesimama jangwani....Karibu nayo, mchangani,
Ukiwa umezama nusu, uso uliopasuka vipande umelala, mnuno wake,
Na mdomo uliokunyata, na dhihaka ya mamlaka yabisi
Vyabainisha kwamba mchongaji alizifahamu sawasawa hisia zile
Ambazo bado zimedumu, zikiwa zimebandikwa katika vitu hivi visivyo hai,
Mkono uliovidhihaki, na moyo uliovilisha,
Na kwenye sehemu ya kusimamia yanaonekana maneno haya:
'Jina langu ni Ozymandias, Mfalme wa Wafalme:
Yaoneni niliyofanikisha, enyi wenye mamlaka makuu, mkate tamaa!'
Hakuna kilichosalia, pembeni mwa uharibifu
Wa ile sanamu kuu iliyoporomoka, bila upeo bila chochote
Mchanga mpweke umetanda hadi mbali kabisa."

Friday, November 18, 2016

Mashairi Mazuri ya Ki-Ingereza

Tangu ujana wangu, nimebahatika kusoma na kuyafurahia mashairi mazuri ya ki-Ingereza. Ninakumbuka nilivyoingia kidato cha tano, Mkwawa High School, mwaka 1971, nikakutana na Mugyabuso Mulokozi na Kulikoyela Kahigi ambao nao walikuwa wanafunzi. Walikuwa na kitabu cha mashairi ya ki-Ingereza, tukawa tunayasoma na kuyafurahia. Mifano ni shairi la Thomas Hardy, "An Ancient to Ancients."

Mashairi ya Shakespeare yaitwayo "sonnets" yalituvutia. Mfano ni "Sonnet 18" ambayo mstari wake wa kwanza ni "Shall I compare thee to a summer's day?" Shairi la Samuel Taylor Coleridge, "The Rime of the Ancient Mariner," lilikuwa daima mawazoni mwetu. Shairi la W.B. Yeats, "The Second Coming," ni moja ya mashairi yaliyonigusa sana, kama nilivyoandika katika blogu hii. Shairi la Walter de la Mare, "The Listeners," limeng'ang'ania akili mwangu tangu enzi zile.

Mashairi mengine tulisoma darasani, kama vile yale ya Percy Bysshe Shelley na Alfred Lord Tennyson, ambao ni wa-Ingereza, na pia waandishi wa ki-Afrika kama vile Wole Soyinka, John Pepper Clark, Dennis Brutus, na Keorapetse Kgositsile. Hiyo ilikuwa ni miaka ya sabini na kitu.

Baada ya kuja masomoni katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, mwaka 1980, niliendelea kukutana na mashairi yenye mvuto mkubwa kwangu. Mifano ni shairi la William Wordsworth, "Lines Composed a Few Miles Above Tintern Abbey.'' Hilo tulilisoma kwa makini katika kozi ya "Poetry" iliyofundishwa na Profesa John Brenkman. Profesa Brenkman alitufundisha pia mashairi ya washairi wengine, kama vile Wallace Stevens.

Baada ya kuja kufundisha katika Chuo cha St. Olaf, mwaka 1991, nimepata fursa ya kusoma na kufundisha mashairi ya watunzi wengi zaidi, kuanzia wa Australia, kama vile Judith Wright na Oodgeroo Noonuccal hadi wa Marekani, kama vile Carl Sandburg na Lawrence Ferlinghetti, hadi wa Caribbean, kama vile Derek Walcott. Derek Walcott ni mshairi mojawapo ninayemwenzi sana, kwa uhodari wake wa kutumia lugha, kusisimua akili. na kuelezea hali halisi ya tabia na hisia za binadamu kwa upeo mpana wa historia na tamaduni mbali mbali.

Ninaendelea kusoma mashairi ya ki-Ingereza, ili kutajirisha akili yangu, na wakati mwingine ninayatafsiri kwa ki-Swahili. Kwa mfano nimetafsiri shairi la Stanley Kunitz, "The Layers," na shairi la Edmund Spencer, "Ye Tradefull Merchants." Ninajiona mwenye bahati kwa hizi fursa nilizo nazo za kufurahia kazi za watunzi maarufu. Jana, kwa mfano, nimesoma shairi la William Savage Landor, "To Wordsworth," nikaguswa sana.

Kuhitimisha ujumbe wangu, ninawazia ingekuwaje kama ningejua lugha nyingi zaidi, kama vile ki-Faransa, ki-Jerumani, ki-Hispania, na ki-Arabu, nikawa ninasoma tungo maarufu zilizomo katika lugha hizo.

Friday, February 19, 2016

"Tenzi Tatu za Kale:" Makala Inayosomwa Kuliko Zote

Mara kwa mara, ninaangalia takwimu zinazohusu blogu yangu hii: idadi ya watembeleaji, makala wanazozitembelea, na nchi walimo. Kuanzia wiki kadhaa zilizopita, makala inayotembelewa kuliko zote ni "Tenzi Tatu za Kale." Idadi ya watembeleaji iliongezeka ghafla pale Ndugu Michuzi alipoiweka makala hii katika blogu yake.

Ninajiuliza kwa nini makala hii inawavutia wasomaji namna hii. Je, hii ni ishara ya kupendwa kwa somo la fasihi ya ki-Swahili? Siamini kama ni hivyo, kwani ninaandika makala nyingi kuhusu fasihi, ambazo zinagusia tungo mbali mbali. Ingekuwa uwingi wa wasomaji unaonekana kwenye makala hizo pia, ningeamini kuwa kuna msisimko wa kupenda fasihi.

Ninapata hisia kwamba labda uhusiano na mahitaji ya shuleni au vyuoni. Ninahisi kuwa labda wanaosoma makala ya "Tenzi Tatu za Kale" ni wanafunzi ambao wanatakiwa kusoma Utenzi wa Al Inkishafi, au Utenzi wa Mwana Kupona, au Utenzi wa Fumo Liyongo: moja, mbili, au zote tatu.

Kama ni hivyo, si jambo la kuridhisha wala kufurahisha. Uwanja wa fasihi ya ki-Swahili ni mpana, na mwenye mapenzi na fasihi hii ninamtegemea awe anasoma tungo nyingi. Hata wanafunzi wa fasihi wanatakiwa kusoma tungo mbali mbali, si zile zilizomo katika mitaala tu.

Ningependa sana kuona mijadala ya fasihi ya ki-Swahili katika blogu hii. Ndio maana ninaweka taarifa mbali mbali kuhusu tungo za ki-Swahili. Tuienzi fasihi hii kwa kuisoma bila mipaka, kuichambua, na kuitangaza.
 

Wednesday, December 9, 2015

Mtunzi Haji Gora Haji

Leo nimeamua kuongelea kifupi utunzi wa Haji Gora Haji wa Zanzibar, mmoja wa waandishi maarufu wa ki-Swahili wa zama zetu hizi. Nafurahi kuwa niliwahi kuonana naye mjini Zanzibar na kuzungumza naye. Panapo majaliwa, nitaandika taarifa ya mazungumzo yetu, ambayo yalihusu maisha yake katika sanaa. Ni muhimu kuutangazia ulimwengu kazi murua inayofanywa na watu wetu wenye vipaji kama Haji Gora Haji.

Nina vitabu vyake vinne: Kimbunga (Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press, 1994), Utenzi wa Visa vya Nabii Suleiman Bi Daudi (A.S.) (Zanzibar: Al-Khayria Press Ltd, 1999), Kamusi ya Kitumbatu (Zanzibar: Express Printing Services, 2006), na Siri ya Ging'ingi (Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam, 2009).

Kadiri siku zinavyopita, wasomaji na wahakiki wanajitokeza na kuongelea uandishi wa Haji Gora Haji. Mifano ya kutambuliwa huko ni taarifa ya Amanda Leigh Lichtenstein, ya Ridder Samson, na ya Pascal Bacuez. Nami nimetafsiri mashairi yake mawili nikayachapisha hapa, hapa, na hapa.

Haji Gora Haji, kama walivyo watunzi wengi, wa zamani hadi leo, wamejengeka katika jadi ya fasihi simulizi. Wanaitumia jadi hii katika utunzi wao, iwe ni mashairi kama walivyofanya W.B. Yeats na Derek Walcott, au riwaya, kama walivyofanya Charles Dickens na Chinua Achebe, au tamthilia, kama walivyofanya William Shakespeare, Wole Soyinka na Ebrahim Hussein, au hadithi fupi, kama walivyofanya Lu Hsun na Ama Ata Aidoo.

Ni hivyo hivyo kwa Haji Gora Haji, kama nilivyowahi kutamka. Utumiaji wa mbinu, miundo, na hata dhamira zitokanazo na fasihi simulizi kunachangia uwezo wa tungo kugusa fikra na hisia za hadhira kwa namna ya pekee kutokana na kwamba fasihi simulizi ni urithi wa wanadamu wote. Maudhui yatokanayo na fasihi simulizi ni ya thamani kwa wanadamu wote.

Kuthibitisha zaidi namna Haji Gora Haji alivyojengeka katika fasihi simulizi, sikiliza anavyosimulia hadithi ya Paa na Pweza.


Thursday, November 26, 2015

Utendi wa Mikidadi na Mayasa

Wiki hii, bila kutegemea, nimevutiwa na wazo la kusoma Utendi wa Mikidadi na Mayasa. Ninazo tendi kadhaa, kuanzia za zamani kama vile Mwana Kupona, Fumo Liongo, na Ras il Ghuli, hadi za enzi zetu hizi. Ninapenda kuzisoma na kuzitafakari, sambamba na tungo za aina hiyo za mataifa mengine, kama vile Gilgamesh, Iliad na Odyssey, Sundiata, na Kalevala.

Nimeusikia Utendi wa Mikidadi na Mayasa tangu zamani. Sijui lini nilinunua nakala yangu ya utendi huu, lakini sikupata wasaa wa kuusoma. Kwa kuupitia haraka haraka, nimeona kuwa una mambo yanayofanana na yale yaliyomo katika tendi zingine maarufu za ki-Swahili kama Ras il Ghuli. Kwa mfano, dhamira ya mapigano kama njia ya kuthibitisha ushujaa imejengeka katika Utendi wa Mikidadi na Mayasa, kama ilivyo katika Utendi wa Ras il Ghuli.

Mayasa ni shujaa mwanamke anayenikumbusha shujaa mwanamke aitwaye Dalgha katika Utendi wa Ras il Ghuli. Wote wawili ni wapiganaji hodari na hatari sana, ambao yeyote anayetaka kuwaoa sherti kwanza apigane nao na kuwashinda. Hata ungekuwa mwanamme hodari na jasiri kiasi gani, kupambana nao ni kama kujitakia aibu au kifo.

Baada ya kuonja mvuto wa  Utendi wa Mikidadi na Mayasa, ninajizatiti kuusoma kikamilifu. Nikiweka nidhamu nikamaliza kuusoma, nitafurahi kuandika juu yake katika blogu hii, angalau kifupi, kama nilivyoandika juu ya Tenzi Tatu za Kale.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...