Mtunzi Haji Gora Haji

Leo nimeamua kuongelea kifupi utunzi wa Haji Gora Haji wa Zanzibar, mmoja wa waandishi maarufu wa ki-Swahili wa zama zetu hizi. Nafurahi kuwa niliwahi kuonana naye mjini Zanzibar na kuzungumza naye. Panapo majaliwa, nitaandika taarifa ya mazungumzo yetu, ambayo yalihusu maisha yake katika sanaa. Ni muhimu kuutangazia ulimwengu kazi murua inayofanywa na watu wetu wenye vipaji kama Haji Gora Haji.

Nina vitabu vyake vinne: Kimbunga (Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press, 1994), Utenzi wa Visa vya Nabii Suleiman Bi Daudi (A.S.) (Zanzibar: Al-Khayria Press Ltd, 1999), Kamusi ya Kitumbatu (Zanzibar: Express Printing Services, 2006), na Siri ya Ging'ingi (Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam, 2009).

Kadiri siku zinavyopita, wasomaji na wahakiki wanajitokeza na kuongelea uandishi wa Haji Gora Haji. Mifano ya kutambuliwa huko ni taarifa ya Amanda Leigh Lichtenstein, ya Ridder Samson, na ya Pascal Bacuez. Nami nimetafsiri mashairi yake mawili nikayachapisha hapa, hapa, na hapa.

Haji Gora Haji, kama walivyo watunzi wengi, wa zamani hadi leo, wamejengeka katika jadi ya fasihi simulizi. Wanaitumia jadi hii katika utunzi wao, iwe ni mashairi kama walivyofanya W.B. Yeats na Derek Walcott, au riwaya, kama walivyofanya Charles Dickens na Chinua Achebe, au tamthilia, kama walivyofanya William Shakespeare, Wole Soyinka na Ebrahim Hussein, au hadithi fupi, kama walivyofanya Lu Hsun na Ama Ata Aidoo.

Ni hivyo hivyo kwa Haji Gora Haji, kama nilivyowahi kutamka. Utumiaji wa mbinu, miundo, na hata dhamira zitokanazo na fasihi simulizi kunachangia uwezo wa tungo kugusa fikra na hisia za hadhira kwa namna ya pekee kutokana na kwamba fasihi simulizi ni urithi wa wanadamu wote. Maudhui yatokanayo na fasihi simulizi ni ya thamani kwa wanadamu wote.

Kuthibitisha zaidi namna Haji Gora Haji alivyojengeka katika fasihi simulizi, sikiliza anavyosimulia hadithi ya Paa na Pweza.


Comments

Pascal Bacuez said…
Ukereketwa wako mpendwa Mbele umeiva sana wala huchoki kumtilia pondo HG ambaye naye bila shaka anajua matumizi ya pondo. Juhudi zako zinafaa kabisa ili kulikuza na kulitukuza jina la mshairi mwenzetu. Pengine ingefaa uwe "mfawidhi" na mwasisi katika kazi hiyo ya kukusanya michango ya wasomi mbalimbali, sijui makala kadhaa kuhusu kazi yake, baadhi ya mashairi yake na kadhalika, pamoja na tafsiri zake. Nina uhakika kwamba utapata mwangwi mkubwa, si katika nchi magharibi tu, bali Afrika pia.
Mbele said…
Ndugu Pascal Bacuez

Shukrani kwa ujumbe wako. Kwa kweli, watunzi kama Haji Gora Haji ni hazina kubwa. Kwa upande wangu ninashukuru kuwa ninayo fursa na mazoea ya kujisomea kazi za watunzi hao na hivyo kuitajirisha akili yangu kwa namna mbali mbali, ikiwemo kuboresha ufahamu wangu wa ki-Swahili.

Wazo lako la kukusanya michango ya wasomi ni wazo bora. Wenzetu katika mataifa mengine wana jadi hiyo tangu zamani. Kuna vitabu vingi ambavyo ni mkusanyo wa maandishi juu ya watunzi maarufu. Sisi tunao watunzi wetu, kama akina Muyaka, Shaaban Robert, Mgeni bin Faqihi, Embrahim Hussein, Haji Gora Haji na Kezilahabi. Wasomi na wahiki wa maandishi ya ki-Swahili bado tuna njia ndefu. Ninafahamu kuwa kazi hapa na pale imefanyika kuhusu waandishi kama Muyaka na Shaaban Robert, lakini haitoshi kabisa.

Labda, kwa kulianzisha na kuliongelea suala hili tutaweza kujizindua na kuwazindua wengine usingizini.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini