Tembo wa Hifadhi ya Tarangire, Tanzania

Tarangire ni moja ya hifadhi maarufu Tanzania, yenye wanyama mbali mbali. Nimefika katika hifadhi hii mara nne, kwa miaka tofauti. Mwezi Januari, mwaka juzi, 2013, nilipiga picha mbali mbali. Baadhi ni picha za tembo zinazoonekana hapa. Nilikuwa naongoza darasa la wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf , katika kozi ambayo nilikuwa nimeitunga, kumhusu Ernest Hemingway. Mwandishi Ernest Hemingway aliitembelea hifadhi hii mwaka 1933. Aliandika hayo katika kitabu chake cha Green Hills of Africa ambamo amezitaja na kuzielezea sehemu nyingi za Tanganyika alimopita. Green Hills of Africa , kwa mtazamo wangu, ni kitabu bora sana, ambacho kiliitangaza nchi yetu vizuri kabisa, kuliko ambavyo sisi wenyewe tumefanya, kuliko tunavyoweza. tunaendekeza uzembe katika lugha na katika nidhamu ya uandishi kama ille ya Hemingway.. Kila ninapofika sehemu kama Tarangire, ninamkumbuka Hemingway na maandishi yake, hasa hiki kitabu chake cha Green Hills of Africa . Haiwezekani kujizuia.