Posts

Showing posts from April, 2016

Ninajiandaa Kushiriki Tamasha Rochester

Image
Jioni hii, ninajiandaa kwenda Rochester, Minnesota, kushiriki tamasha la kimataifa kesho. Nitaondoka asubuhi sana ili nikawahi kabla ya saa nne litakapoanza tamasha. Nimeshalipia meza. Nitapeleka vitabu vyangu kama kawaida. Meza ya vitabu katika tamasha ni kivutio kwa watu, sawa na meza za bidhaa na vitu vingine mbali mbali vinavyokuwepo. Watu wanapenda kuangalia vitabu, kuuliza masuali juu ya vitabu hivi, na wengine kuvinunua. Mimi mwenyewe ninapenda kuongelea mambo yanayonisukuma kuandika, hasa fasihi, tamaduni, na changamoto zitokanazo na tofauti za tamaduni. Nitabeba pia bendera ya Tanzania. Nilishawahi kuelezea katika blogu hii namna nilivyofikia uamuzi wa kununua bendera hii, kwa ajili ya matamasha na maonesho mbali mbali. Huku ughaibuni, bendera ya Taifa ina mguso wa pekee moyoni. Kwa vile tamasha la kesho ni la kimataifa, bendera hii itakuwa mahali inapohitajika. Tamasha la kimataifa hufanyika kila mwaka mjini Rochester. Mji huu una wakaazi kutoka sehemu mbali mbali z

Nimekwama Kutafsiri "Kibwangai."

Jana nilichapisha katika blogu hii shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai," nikasema kuwa ninataka kulitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliamini kabisa kuwa ningeweza kulitafsiri kwa kiwango cha kuniridhisha. Baada ya kulichapisha, nilianza jana hiyo hiyo kujaribu kulitafsiri. Tofauti na mategemeo yangu, nilikumbana na hali ngumu tangu mstari wa kwanza. Nilifanya kila juhudi kuutafsiri ubeti wa kwanza, lakini niligonga mwamba. Tafsiri ya kila sentensi katika ubeti huo haikutokea vizuri. Ilikuwa ya ovyo. Nilivunjika moyo, nikaacha kuendelea. Tatizo liko wapi? Kiswahili ninakijua vizuri. Kiswahili kilichotumika katika shairi la "Kibwangai" nimekielewa vizuri. Ninaamini kuwa shairi nimelielewa vizuri, angalau kwa namna yangu, kuanzia mbinu za kisanaa zilizotumika hadi dhamira zake. Sawa na msomaji mwingine yeyote makini ninaweza kulichambua shairi hili, ingawa, kwa hali yoyote, uchambuzi wangu utakuwa tofauti na ule wa msomaji mwingine yeyote. Hili ni jambo lisilo

"Kibwangai:" Shairi la Haji Gora Haji

Ninaleta hapa shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai," ambalo limechapishwa katika diwani yake iitwayo Kimbunga . Shairi la "Kibwangai" ni chemchemi ya mambo mengi yanayosisimua akili. Mwenye ujuzi wa nadharia za fasihi na uchambuzi wa fasihi atajionea utajiri uliomo katika shairi hili. Nitalitafsiri shairi hili kwa ki-Ingereza katika siku chache zijazo, ili kuwapa fursa watu wasiojua ki-Swahili fununu ya umahiri wa Haji Gora Haji kama mshairi. Nimeshatafsiri mashairi yake mawili: "Kimbunga" na "Nyang'au." Kutafsiri shairi au kazi yoyote ya fasihi ni mtihani mgumu. Lakini ni njia ya mtu kupima ufahamu wako wa lugha na ufahamu wa lugha ya kifasihi. Kwa kuwa lugha inabeba hisia na mambo mengine yanayofungamana na tamaduni, kutafsiri ni mtihani ambao unahitaji umakini usio wa kawaida. KIBWANGAI 1.    Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya        Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya        Nilikuwa mwanakele, hayo nikazin

Kumbukumbu ya Kifo cha Shakespeare

Image
Wiki hii ni ya kumbukumbu ya kifo cha William Shakespeare. Ingawa siku ya kufariki kwake haijulikani kwa uhakika, mapokeo yameiteua tarehe 23 April, 1616, kuwa ndio siku ya kufariki kwake. Alizikwa tarehe 25 Aprili. Sisi tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu tuliweza kusoma maandishi ya Shakespeare na kuyafurahia. Tulisoma tamthilia kama Julius Caesar na The Merchant of Venice . Baada sekondari, sisi tuliokwenda "high school" tulipata fursa ya kusoma na kutafakari tamthilia zake ngumu zaidi, kama vile Hamlet na Othello . Mwandishi maarufu wa ki-Swahili, Shaaban Robert, alimwenzi Shakespeare. Alisema kwamba akili ya Shakespeare ilikuwa kama bahari ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe duniani kote. Laiti kama wa-Tanzania tungefuata nyayo za Shaaban Robert, tukaachana na ufinyu wa fikra kuhusu umuhimu wa lugha mbali mbali na fasihi za ulimwengu, kwa kisingizio cha kukienzi ki-Swahili. Maandishi ya Shakespeare yana kauli nyingi maarufu. Sijui kama kuna msomaji

Ujumbe Mzuri Kutoka kwa Mwanafunzi

Leo nimepata ujumbe mzuri kutoka kwa m-Tanzania ambaye simfahamu. Amejitambulisha kwamba alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Namtumbo, alisoma mwongozo wangu juu ya Things Fall Apart na Song of Lawino . Nimefurahi kusikia habari hii ya kusomwa maandishi yangu sehemu ya mbali kama Namtumbo ambayo iko njiani baina ya Songea na Tunduru. Inawezekana kuwa huyu mtu alimaanisha kijitabu changu ambacho kilikuwa na mwongozo wa Things Fall Apart na The African Child , ambao niliuelezea katika blogu hii.  Ni hivi karibuni tu nimechapisha mwongozo wa Song of Lawino . Si hoja, ili mradi watu wasome ninayoandika. Mimi ni mwalimu, na dhana yangu ya ufundishaji ni pana. Inajumlisha ninavyofundisha darasani, ninavyoandika na kuchapisha vitabu na makala, ninavyoblogu, ninavyoshiriki matamasha ya vitabu na utamaduni, ninavyoongea na watu ana kwa ana, kama vile mitaani, ninavyoendesha warsha, ninavyoshiriki mijadala mitandaoni, na kadhalika. Mwalimu si mtu wa k

Nawazia Mwongozo wa "The African Child"

Image
Tangu miaka ya sabini na kitu, nilivutiwa na wazo la kuandika miongozo ya kazi maarufu za fasihi ya Afrika. Nilianza kujijengea uzoefu kwa kuandika mwongozo wa tamthilia ya Arthur Miller, A View From the Bridge . Niliandika mwongozo ule, ambao niliutaja katika blogu hii, kwa kuombwa na mwalimu Egino Chale, ambaye alikuwa mratibu katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Tanzania. Baadaye, kutokana na mashauriano na ndugu A.S. Muwanga wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, niliandaa mwongozo wa Things Fall Apart na The African Child . Hiyo miongozo miwili ilichapishwa kama kitabu kimoja. Hatimaye, niliamua kuushughulikia upya mwongozo wa Things Fall Apart , na kuuchapisha peke yake, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Wazo langu lilikuwa kwamba hatimaye niushughulikie pia mwongozo wa The African Child na kuuchapisha peke yake. Lakini badala ya kuushughulikia mwongozo wa The African Child , niliamua kuandika mwongozo wa Song of Lawino . Taarifa za shughuli hiyo nimeandika sik

"Song of Lawino" Yatimiza Miaka 50

Image
Mwaka huu, Song of Lawino , utungo maarufu wa Okot p'Bitek wa Uganda, unatimiza miaka hamsini tangu uchapishwe. Utungo huu, ambao unafahamika kama wimbo, ulichapishwa na East African Publishing House mwaka 1966 ukapata umaarufu tangu mwanzo. Ulisomwa mashuleni na katika jamii kote Afrika Mashariki na sehemu zingine. Ulileta msisimko na upeo mpya katika dhana ya ushairi katika ki-Ingereza, na ulichochea washairi wengine kutunga kwa mtindo aliotumia Okot p'Bitek, ambao ulijaa athari za ushairi wa jadi wa ki-Afrika. Siku chache zilizopita, niliandika katika blogu hii kuwa nimechapisha mwongozo wa Song of Lawino . Kitu ambacho sikusema ni kuwa nilikuwa na sababu ya kuchapisha mwongozo huu wakati huu, na sababu yenyewe ni hayo maadhimisho ya miaka 50. Nilisoma taarifa, zaidi ya mwaka mmoja uliopita, kwamba idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Makerere ilikuwa inaandaa maadhimisho ya kumbukumbu hii, ambayo yangehusisha mihadhara na shughuli zingine. Ingekuwa n