Showing posts with label Macbeth. Show all posts
Showing posts with label Macbeth. Show all posts

Monday, April 25, 2016

Kumbukumbu ya Kifo cha Shakespeare

Wiki hii ni ya kumbukumbu ya kifo cha William Shakespeare. Ingawa siku ya kufariki kwake haijulikani kwa uhakika, mapokeo yameiteua tarehe 23 April, 1616, kuwa ndio siku ya kufariki kwake. Alizikwa tarehe 25 Aprili.

Sisi tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu tuliweza kusoma maandishi ya Shakespeare na kuyafurahia. Tulisoma tamthilia kama Julius Caesar na The Merchant of Venice. Baada sekondari, sisi tuliokwenda "high school" tulipata fursa ya kusoma na kutafakari tamthilia zake ngumu zaidi, kama vile Hamlet na Othello.

Mwandishi maarufu wa ki-Swahili, Shaaban Robert, alimwenzi Shakespeare. Alisema kwamba akili ya Shakespeare ilikuwa kama bahari ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe duniani kote. Laiti kama wa-Tanzania tungefuata nyayo za Shaaban Robert, tukaachana na ufinyu wa fikra kuhusu umuhimu wa lugha mbali mbali na fasihi za ulimwengu, kwa kisingizio cha kukienzi ki-Swahili.

Maandishi ya Shakespeare yana kauli nyingi maarufu. Sijui kama kuna msomaji wa Shakespeare ambaye hakumbuki ile hotuba ya Hamlet inayoanza hivi:

To be, or not to be: that is the question:
Whether 'tis nobler in the mind to suffer
The slings and arrows of outrageous fortune,
Or to take arms against a sea of troubles,
And by opposing end them? To die: to sleep;
No more; and by a sleep to say we end
The heart-ache and the thousand natural shocks
That flesh is heir to, 'tis a consummation
Devoutly to be wish'd.

Sijui kama kuna msomaji wa Shakespeare ambaye hakumbuki ile hotuba ya Mark Antony iliyomo katika Julius Caesar, inayoanza hivi:

Friends, Romans, countrymen, lend me your ears;
I come to bury Caesar, not to praise him.
The evil that men do lives after them;
The good is oft interréd with their bones;
So let it be with Caesar. The noble Brutus
Hath told you Caesar was ambitious:
If it were so, it was a grievous fault,
And grievously hath Caesar answer'd it.

Kuna pia kauli maarufu katika tamthilia ya As You Like It, ambayo ni ya mhusika aitwaye Jaques. Anasema kuwa dunia ni jukwaa, ambapo kila binadamu ni kama mwigizaji:

All the world’s a stage,
And all the men and women merely players;
They have their exits and their entrances,
And one man in his time plays many parts,
His acts being seven ages.

Shakespeare aliona mbali. Kwa mfano, unaposoma The Merchant of Venice, unajionea jinsi Shakespeare alivyokuwa na upeo wa fikra wa kutambua tabia ya ubepari mapema kabisa, wakati ulipokuwa unachimbuka. Haishangazi kwa nini Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa katika harakati za kupambana na ubepari na kujenga ujamaa aliamua kuitafsiri tamthilia hii, akaiita Mabepari wa Venisi.

Shakespeare alizielezea kwa umakini tabia za binadamu, njema au mbaya. Katika tamthilia ya Macbeth, kwa mfano, tunashuhudia jinsi binadamu anavyoweza kuwa mbaya, na kama wewe ni msomaji wa Shaaban Robert utakumbuka jinsi naye alivyoielezea dhamira hii, kwa mfano katika Adili na Nduguze.

Shakespeare alikuwa mtunzi wa tamthilia na mashairi. Alitunga mashairi mengi, na baadhi ya hayo yako katika tamthilia zake. Haiwezekani kumtendea haki Shakespeare kwa kuelezea mchango wake katika makala ndogo kama hii. Kuna makala nyingi na vitabu juu yake na kazi zake, na maandishi yanaendelea kuchapishwa katika lugha nyingi. 

Kama Shaaban Robert alivyosema, akili ya Shakespeare ni kama bahari, ambayo mawimbi yake yanatua kwenye fukwe duniani kote. Ni miaka mia nne imepita tangu Shakespeare afariki, lakini mawimbi ya akili yake yataendelea kumwagika duniani kote.

Wednesday, December 31, 2014

Vitabu vya Kukumbukwa Nilivyosoma Mwaka 2014

Leo, siku ya mwisho ya mwaka 2014, napenda kujikumbusha vitabu nilivyosoma mwaka huu ambavyo nitavikumbuka kwa namna ya pekee. Sitavitaja vitabu tulivyovisoma darasani.

Kwanza, napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushuhudia mwaka 2014 ukiisha, huku zikiwa zimebaki saa nne tu hadi kuanza kwa mwaka 2015. Ingawa huu umekuwa mwaka mgumu kwangu kuliko miaka yote ya maisha yangu kwa sababu ya kuugua, nashukuru nimefikia hapa nilipo, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, huduma za madaktari, wauguzi na familia yangu, na maombi ya ndugu na marafiki.

Kutokana na hali yangu hiyo, sikuweza kusoma kama ilivyo mazoea yangu. Hata hivi, kila nilipojisikia nafuu, nilishika kitabu na kusoma, hata nilipokuwa nimelazwa hospitalini. Vitabu ni moja ya vitulizo vyangu, na madaktari na wauguzi walitambua jambo hilo.

Nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Abbott Northwestern, mjini Minneapolis, nilikwenda na kitabu cha mashairi ya Robert Frost kiitwacho Robert Frost: Selected Poems, ambacho binti yangu Zawadi alikuwa amenipa, kama nilivyoelezea hapa. Nilijitahidi kusoma mashairi mengi yaliyomo. Kabla ya kitabu hiki, nilikuwa nimesoma mashairi machache ya Frost wakati wa ujana wangu, na kati ya mashairi hayo, moja ambalo nimelikumbuka daima ni "The Road Not Taken."

Ninafurahi kuwa nimepata fursa ya kusoma mashairi mengi ya Frost mwaka huu 2014, ingawaje, kwa ujumla, yanahitaji tafakari sana, na kama mtu ni mvivu, hatafika mbali katika kuyasoma. Hata hilo shairi la "The Road Not Taken" linatuacha njia panda.

Kwa sababu kama hizi nilizotoa hapa juu, nitamkumbuka Robert Frost kwa namna ya pekee kama mmojawapo wa waandishi niliowasoma mwaka 2014. Nimeweza kupanua upeo wangu wa kumfahamu mshairi huyu maarufu.

Kitabu kilichonigusa kwa namna ya pekee ni The Pearl, riwaya ya John Steinbeck, ambayo niliielezea hapa. Ni riwaya inayosomeka kirahisi na inavutia kama sumaku kwa mtiririko wa matukio yake na jinsi inavyoelezea  tabia za binadamu, kama vile upendo na wivu, wema na ubaya. Ni riwaya ambayo sitaweza kuisahau.

Nimepata fursa ya kujiongezea ufahamu wa Shakespeare kwa kusoma Macbeth, tamthilia yake mojawapo ambayo sikuwa nimeisoma. Niliiongelea tamthilia hii katika blogu hii. Sina matumaini ya kusoma tamthilia zote 37 za Shakespeare. Ni nani amezisoma zote? Hii ndio hali halisi katika ulimwengu wa fasihi. Hata usome saa nyingi kila siku na kwa miaka yote ya maisha yako, utakachokuwa umefanya ni kama kuchota maji ndoo moja katika bahari inayoendelea kujaa maji. Kuna waandishi wengi maarufu, wa zamani, wa siku hizi, na wanaochipuka muda wote.

Lakini, hii isiwe sababu ya kukata tamaa, bali changamoto ya kukufanya ujitahidi kuvuna kila uwezacho katika hazina hii isiyo na mwisho. Nami, tunapoingia katika mwaka mpya, nina viporo vya vitabu ambavyo nilianza kuvisoma na napangia kuendelea navyo katika huu mwaka mpya, na papo hapo, nina shauku kubwa ya kusoma vitabu vingi zaidi, kwa kuwa afya yangu inaendelea kuimarika.

Sunday, November 30, 2014

Kuhusu "Macbeth"

Makala hii nilianza kuiandika mara tu baada ya kuanza kusoma Macbeth, tamthilia ya Shakespeare, ambayo niliitaja hapa na hapa. Jana usiku nimefika mwisho wake. Inafurahisha kujisomea namna hii, bila msukumo kutoka popote.

Hapa na pale katika Macbeth nimejikuta nikiyakumbuka maandishi mengine ya Shakespeare ambayo niliyasoma zamani, kama vile The Merchant of Venice, Othello, The Tempest, na Twelfth Night. Hii ni kwa sababu kuna mawazo ambayo yanajitokeza tena na tena katika maandishi ya Shakespeare. Wazo mojawapo ni kwamba dunia ni jukwaa ambapo sisi wanadamu ni waigizaji. Kuna misemo pia ambayo inajitokeza tena na tena.

Kwa mfano, nilivyosoma katika Macbeth kauli ya mchawi kuhusu meli kukumbwa na dhoruba (I, III, 25-26) nimekumbuka The Tempest. Nilivyokutana na usemi huu wa mfalme kwa kapteni shujaa: "So well thy words become thee as thy wounds; They smack of honor both," (I, II, 47-48) nimekumbuka hotuba ya Portia katika The Merchant of Venice, ambamo anaelezea thamani ya huruma.

Kati ya mambo anayosema kuhusu thamani ya huruma ni kwamba "It becomes the throned monarch better than his crown." Kwa tahadhari, niseme kuwa neno "becomes" anavyolitumia Shakespeare, lina maana tofauti kabisa na ile tunayoijua. Jambo hilo nilishaligundua katika kusoma tamthilia za Shakespeare.

Unaposoma Macbeth, sawa na kazi nyingi maarufu za fasihi, mahusiano ya namna hii hujitokeza, sio tu baina ya maandishi ya mwandishi mmoja, bali pia baina ya maandishi ya waandishi mbali mbali. Katika nadharia ya fasihi, mahusiano hayo huitwa "intertextuality" kwa ki-Ingereza.

Kufafanua zaidi wazo hili, napenda kusema kuwa jambo moja lililonistua katika Macbeth ni pale Fleance anaposema, "The moon is down; I have not heard the clock" (II, I, 2). Hapo nilikumbuka riwaya ya John Steinbeck, The Moon is Down, nikapata shauku ya kufuatilia kama kuna uhusiano. Lo, nimegundua kuwa Steinbeck alipata jina la riwaya yake hapo kwenye tamthilia ya Macbeth.

Ni wazi kuwa kusoma vitabu kunasisimua akili. Unaposoma masimulizi ya aina hii, ubongo unafanya kazi muda wote, kukumbuka hiki au kile, kuelewa kile unachosoma, na pia kubashiri kinachofuata katika mtiririko wa matukio.Kuelewa huko na kukumbuka vimefungamana. Akili hailali; inapata mazoezi, sawa na mazoezi ya viungo vyovyote vya mwili. Manufaa yake ni makubwa.

Ninavyosoma Macbeth, nakumbuka vizuri taarifa niliyosoma miaka kadhaa iliyopita kuhusu onesho la Macbeth lililofanywa Uingereza na kikundi cha waigizaji cha wa-Zulu. Niliisosoma makala hiyo, "The Zulu Macbeth," katika jarida la The New African, kama sikosei. Kuna ripoti kadhaa mtandaoni kuhusu onesho hilo la tamthilia ya Macbeth ya ki-Zulu, ambayo ilitungwa na Welcome Msomi na kupewa jina la "Umabatha." Kwa mfano, soma makala hii.

Ningeweza kuandika makala ndefu kuhusu Macbeth, nikijadili masuala kama dhamira, wahusika, mawaidha, falsafa, na umahiri wa Shakespeare katika kutumia lugha. Pamoja na mengine yote, Shakespeare ni mwanafalsafa anayefikirisha. Kwa mfano, tafakari kauli hii maarufu ya Macbeth mwenyewe, mhusika mkuu wa tamthilia hii, anapoambiwa kuwa mke wake amefariki:

She should have died hereafter;
There would have been a time for such a word.
Tomorrow, and tomorrow, and tomorrow
Creeps in this petty pace from day to day
To the last syllable of recorded time;
And all our yesterdays have lighted fools
The way to dusty death. Out, out, brief candle!
Life's but a walking shadow, a poor player,
That struts and frets his hour upon the stage
And then is heard no more. It is a tale
Told by an idiot, full of sound and fury,
Signifying nothing (V, V, 19-30).

Kwa kuhitimisha, napenda kusema kuwa nimefurahi sana kuisoma Macbeth hadi mwisho. Najisikia raha kuwa nimeongeza kitu cha thamani katika akili yangu. Ndivyo inavyokuwa katika kusoma vitabu vyenye thamani.

Tuesday, November 25, 2014

Tuna Likizo Fupi ya "Thanksgiving"

Leo hapa chuoni tunaanza likizo fupi itakayokwisha mwisho wa wiki. Ni wakati wa sikukuu maarufu hapa Marekani iitwayyo "Thanksgiving." Kwa mwaka huu, "Thanksgiving" ni keshokutwa, tarehe 27.

Kwa upande wangu, nilianza hayo mapumziko jana mchana, baada ya kufanyisha mtihani katika somo langu la "South Asian Literature." Kwa hivi, kipindi hiki ambacho ni cha mapumziko sitapumzika, bali nitakuwa nasahihisha huo mtihani.

Vile vile, wakati huu ambapo hatufundishi, ninaendelea kujisomea maandishi mbali mbali, hasa tamthilia ya Macbeth. Ninangojea kwa hamu kuandika ripoti yake wiki hii hii katika blogu hii. Pamoja na jukumu la kusahihisha mtihani, naona akili yangu imetulia vizuri, kiasi cha kuniwezesha kuitafakari tamthilia ya Macbeth na kuifaidi vilivyo.

Nikirudi kwenye hii sikukuu ya "Thanksgiving," ningeweza kusema mengi kuhusu historia yake, pia malumbano na migogoro ya kiitikadi ambayo imeigubika sikukuu hii hasa miaka ya hivi karibuni.

Kifupi ni kuwa hii ni sikukuu ambayo ni kumbukumbu ya ujio wa wazungu katika nchi hii ya Marekani. Historia wanayoisimulia ni kuwa wale wazungu wa mwanzo waliwakuta wenyeji, tunaowaita Wahindi Wekundu, na hao wenyeji waliwakaribisha wageni hao, na ndio waliowawezesha hao wahamiaji kustawi katika mazingira ya nchi hii.

Kwa mujibu wa masimulizi hayo, hiyo "Thanksgiving" ni kumbukumbu na fursa ya kutoa shukrani. Batamzinga ndio chakula rasmi kwa siku hiyo, kiasi kwamba wa-Marekani wanapowazia sikukuu hii, wanaiunganisha moja kwa moja na mlo huo. Historia yake nayo ni ndefu.

Lakini, hasa miaka ya karibuni, wanaharakati wa hilo taifa la Wahindi Wekundu na wengine, wanaikosoa historia inayosimuliwa kuanzia katika vitabu vya watoto hadi katika media zingine, kwa msingi kuwa inapotosha ukweli kwamba wale wazungu waliingia nchi hii kwa mabavu, wakafanya maovu mengi dhidi ya wenyeji, yakiwemo mauaji na kupora ardhi. Wanaharakati wanaona hii sikukuu ya "Thanksgiving" kama ni tusi kwao. Wanaiona kama siku ya maombolezo.

Ni vema kwetu ambao hatukukulia nchi hii kujielimisha ili angalau tuelewe huu mgogoro wa kiitikadi. Tuelewe hisia za wenyeji wa asili wa nchi hii. Tusiwe watu wa kusherehekea tu, na kula batamzinga, kama wanavyosherehekea wengine hapa Marekani, bali angalau tufahamu utata wa suala zima la hii sikukuu.

Kwa upande mwingine, kila kabila au taifa hapa duniani lina wakati ambapo wanasherehekea na kutoa shukrani, hasa wakati wa mavuno. Dhana ya kutoa shukrani sio dhana ya Marekani pekee. Ingawa mimi si m-Marekani na hii si nchi yangu, ninaamini kuwa kinachotakiwa ni wao kutafuta njia za kutatua huu mgogoro wa kiitikadi niliouelezea.

Thursday, November 20, 2014

Ninasoma Vitabu Kiholela

Jana, baada ya kufundisha darasa langu la South Asian Literature, nilikuwa ofisini kwa muda, nikawa napekuapekua bila lengo maalum katika makabati ya vitabu vyangu. Niliamua, kiholela tu, kuchukua tamthilia ya Macbeth ya Shakespeare, nikarudi nayo nyumbani na kuanza kuisoma.

Nilikuwa na hamu ya kujikumbusha enzi za ujana wangu, nilipokuwa nasoma sekondari hadi chuo kikuu. Nilipenda kusoma vitabu vya waandishi mbali mbali, kama vile Shakespeare na Charles Dickens.

Leo asubuhi, nilipoamka, niliendelea kusoma Macbeth, lakini nikakumbuka kuwa kuna vitabu kadhaa ambavyo nilianza kuvisoma au nilikuwa navisoma siku kadhaa zilizopita, au wiki kadhaa zilizopita, au miezi kadhaa iliyopita, ambavyo sikuvimaliza. Mifano ni A Moveable Feast na Islands in the Stream, vilivyoandikwa na Ernest Hemingway; Lost For Words, kilichoandikwa na J.W. Patrick Creber, na Nomad, kitabu cha Ayaan Hirsi, yule dada m-Somali anayetishiwa maisha yake kwa vile anaukosoa u-Islam. Hiyo ni mifano tu ya viporo.

Wakati kuna viporo, inatokea mara kwa mara kuwa naanza kusoma kitabu kingine kabisa na kukimaliza. Hivi ndivyo ilivyokuwa niliposoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Nilikiongelea kitabu hiki katika blogu hii, hapa na hapa. Nilikianza nikakimaliza, huku viporo kadhaa ninavyo.

Pamoja na yote hayo, jana nimekurupuka na kuanza kusoma Macbeth. Kwa hakika, nimepania kumaliza kuisoma tamthilia hii, ingawa nimeichagua kiholela tu. Hakuna uhakika kuwa kesho na keshokutwa sitaanza kusoma kitabu kingine tofauti kabisa. Kusema kweli, jana hiyo hiyo nilianza pia kusoma kitabu cha Postcolonial Criticism, kilichohaririwa na Bart Moore-Gilbert na wengine ambacho nilikinunua miaka kadhaa iliyopita, nikawa nimechunguliachungulia tu kurasa zake, bila kukisoma.

Leo nimejikuta nikitafakari tabia yangu hii kama msomaji. Siongelei vitabu ninavyofundisha darasani. Hivyo huwa navisoma kwa nidhamu, tangu ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, kama impasavyo mwalimu, na ninawaongoza wanafunzi katika kuvijadili. Hii tabia ya kusoma vitabu kiholela inahusu vitabu ambavyo ninajisomea mwenyewe, bila msukumo kutoka kokote. Najiuliza kama ni jambo jema kusoma vitabu kiholela.

Lakini, papo hapo, sioni ubaya wake. Wakati huja ambapo napata hamu ya kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikiweka kando siku zilizopita. Ajabu ni kuwa, ninapoamua kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikianza siku zilizopita nikakiweka kando, kumbukumbu hunijia kuhusu yale niliyosoma kabla.

Naamini kila msomaji wa vitabu ana tabia yake katika usomaji. Nimeona nitafakari tabia yangu na kuieleza kama nilivyofanya. Labda hii itawapa wasomaji wengine fursa ya kujitafakari pia.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...