Posts

Showing posts from October, 2016

Black African Voices: Tungo za Afrika

Image
Pamoja na kwamba fasihi ya Afrika, kama ilivyo ulimwenguni kote, inastawi kwa kasi kadiri miaka inavyopita, na waandishi wapya hujijokeza na kujipambanua, ni lazima pia kukumbuka na kusoma uandishi wa zamani. Kwa yeyote anayependa fasihi, awe ni mwanafunzi, mwalimu au msomaji wa kawaida, usomaji wa aina hii ni jambo lisilohitaji mjadala. Fasihi inahitaji usomaji usio na kikomo, sio tu kwa kuwa ina historia ndefu, bali pia kwa kuwa inastawi ulimwenguni kote na daima inaendelea kuchanua kama maua. Mimi, mwalimu wa fasihi, ninazingatia umuhimu wa kufundisha kazi za tangu zamani hadi leo. Fasihi ya kila taifa au sehemu yoyote ya dunia ina historia, na fasihi inayoandikwa leo ni mwendelezo wa mkondo ulioanza zamani. Katika siku hizi chache, nimekuwa ninasoma Black African Voices , kitabu kilichohaririwa na James E. Miller na wenzake. Sikumbuki ni lini nilikinunua kitabu hiki, lakini mara kwa mara katika kuangalia vitabu vyangu, nilikuwa ninakichungulia kitabu hiki, nikawa ninakumbuk

Miaka 80 ya "The Snows of Kilimanjaro"

Image
Kwa mara nyingine tena, ninaandika ujumbe kuhusu kutimia kwa miaka 80 tangu hadithi ya Ernest Hemingway, 'The Snows of Kilimanjaro" ilipochapishwa kwa mara ya kwanza. Niliandika ujumbe wa aina hiyo katika blogu hii. Leo nimesoma tena ujumbe wangu, nikajiridhisha kwamba niliyosema ndiyo ninayoamini hadi sasa. Jambo moja kubwa kabisa ni kuwa wa-Tanzania tunajipotezea fursa za wazi za kutumia hazina kama hii hadithi ya Hemingway kuitangaza nchi yetu. Niliandika katika ujumbe wangu baadhi ya mambo ambayo tungeyafanya mwaka huu wa kumbukumbu. Lakini mwaka unaelekea ukingoni, na hakuna tulichofanya. Hii ni hasara ya kukosa utamaduni wa kusoma vitabu. Tunashindwa hata kutumia fursa zilizo wazi. Nimeona niandike ujumbe huu leo kwa sababu wiki hii, hapa katika Chuo cha St. Olaf ninapofundisha, litatokea jambo la pekee linalohusiana na Ernest Hemingway. Keshokutwa, tarehe 28, pataonyeshwa kwa mara ya kwanza filamu ya "Papa's Shadow," ambayo niliwahi kuielezea katika

Ninarekebisha Kitabu Nilichochapisha Mtandaoni

Image
Mara kwa mara, ninaongelea suala la kuchapisha vitabu mtandaoni, kutokana na uzoefu wangu. Ninatarajia kuwapa wengine uzoefu wangu wa kutumia tekinolojia za uchapishaji mtandaoni, ambazo zinatoa fursa tele kwa yeyote kujikomboa na taabu na vikwazo vya uchapishaji wa jadi. Faida mojawapo ya uchapishaji wa aina ninayotumia kuchapishia vitabu vyangu ni fursa isiyo na mipaka ya kurekebisha kitabu chako wakati wowote uonapo dosari ndani yake au fursa ya kukiboresha. Hilo linawezekana kwa kuwa mswada wako unakuwa umehifadhiwa kama faili la kielektroniki mtandaoni, hata kama hukuuhifadhi katika kompyuta, disketi, au kifaa kingine. Mimi ninatumia mtandao wa lulu.com. Hapo, ukishachapisha kitabu, nakala ya mswada inahifadhiwa hapo hapo mtandaoni. Unapotaka kurekebisha kitabu chako, unachofanya ni kuuingiza "(down-loading") mswada katika "flash drive" na kuufanyia marekebisho. Kisha unaurudisha ("up-loading") sehemu ya kuchapishia. Yeyote atakayekinunua baa

Siku ya Mashujaa wa Kenya, Rochester, Minnesota

Image
Jana nilikwenda mjini Rochester, Minnesota, kuhudhuria sherehe ya siku ya Mashujaa wa Kenya. Hii ni sikukuu ambayo wa-Kenya huifanya kila mwaka tarehe 20 Oktoba, kuwakumbuka mashujaa wa tangu enzi za kupigania uhuru hadi leo. Sherehe ya jana iliandaliwa na jumuia ya wa-Kenya waishio Rochester. Nilipata taarifa ya sikukuu hii kutoka kwa Olivia Njogu, m-Kenya aishiye Rochester, na mwanabodi wa  Rochester International Association . Anaonekana pichani hapa kushoto, wa pili kutoka kulia. Chama hiki huandaa tamasha la kimataifa kila mwaka, na Olivia tulifahamiana niliposhiriki tamasha hilo mwaka huu, kama nilivyoelezea  katika blogu hii.  Baada ya tamasha, Olivia alisoma kitabu changu  Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , na kisha akaniandikia kunielezea alivyokipenda. Taarifa hiyo niliiandika katika blogu hii.   . Hii haikuwa mara yangu ya kwanza kuhudhuria sherehe za wa-Kenya hapa Marekani. Daima nimependezwa kujumuika nao, kama nilivyowahi kuandika katika blog

Nimepata Vitabu Vipya vya Uislam

Image
Leo nimepata vitabu kadhaa vya u-Islam kutoka kwa profesa Nadia Mohamed wa Minneapolis Community and Technical College. Huyu profesa, mzaliwa wa Misri, tulifahamiana mwaka jana. Muhula uliopita nilimwalika kutoa mhadhara katika darasa langu, Muslim Women Writers. Nilimwalika tena, na amekuja leo. Katika vitabu alivyonipa leo, kuna nakala za Quran, yaani tafsiri tofauti. Kabla, nilikuwa na tafsiri mbili: moja ya Abdallah Yusuf Ali, yenye maelezo ya kina, ambayo nimekuwa nayo kwa miaka mingi, na ya pili aliyonipa Profesa Nadia Mohamed alipotembelea darasa langu muhula uliopita, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Lakini leo, amenipa The Message of the Quran , iliyotafsiriwa na kufafanuliwa na Muhammad Asad. Humo kuna Quran kwa hati ya ki-Arabu, na hicho ki-Arabu kipo pia kwa hati ya ki-Rumi. Na kuna tafsiri ya ki-Ingereza, pamoja na maelezo ya kina. Nakala ya Abdallah Yusuf Ali ina sura mbili: hati ya ki-Arabu na tafsiri ya ki-Ingereza. Profesa Nadia Mohammed amenipa nakala z

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Image
Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa. Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake: Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe . (Ukurasa 61) Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii: Nil

Ki-Ingereza Kama Lugha ya Ulimwengu

Image
Jana, katika blogu hii, nilikiongelea kitabu cha Charles Derber, Peo ple Before Profit , ambacho kinahusu utandawazi. Katika kukisoma kitabu hiki, nilivutiwa na maelezo yake, na nikapata hamasa ya kufuatilia mada ya utandawazi kwa namna nyingine. Nilikumbuka kwamba nina kitabu cha David Crystal, English as a Global Language , ambacho nilikinunua miaks michache iliyopita, ila nilikuwa nimekipitia juu juu tu. Leo nimeamua kukisoma, na ninaona jinsi maelezo yake kuhusu lugha ya ki-Ingereza yanavyofungamana na suala la utandawazi. Kwa mfano, katika utangulizi wake, mwandishi anasema, "We have as yet no adequate typology of the remarkable range of language contact situations which have emerged as a consequence of globalization, either physically (e.g. through population movement and economic development or virtually (e.g. through Internet communication and satellite broadcasting)." (xi) Kitu kimoja kilichonifanya nikumbuke kitabu cha David Crystal ni kuwa huyu ni mtaalam

People Before Profit: Kitabu Kuhusu Utandawazi

Image
Leo nimejipatia kitabu kiitwacho People Before Profit kilichoandikwa na Charles Derber. Nimeanza kukisoma leo hii hii. Kwanza, niseme kuwa kitabu hiki kina utangulizi ulioandikwa na Noam Chomsky. Hilo pekee ni ishara ya thamani ya kitabu hiki, kwani Chomsky ni mchambuzi maarufu wa masuala ya ulimwengu kwa mtazamo wa kimaendeleo. Ninamheshimu sana, kama ninavyowaheshimu wachambuzi kama Seymour Hersh na Amy Goodman. People Before Profit ni hazina ya elimu. Kinafafanua dhana ya utandawazi. Kwanza kinaelezea ukale wa utandawazi, na kwamba utandawazi una historia ndefu. Haukuanza zama zetu hizi, bali umekuwepo kwa miaka maelfu na maelfu, ukibadilika katika kila zama. Pili kitabu kinaelezea uhusiano wa utandawazi na tekinolojia, kama vile mapinduzi ya miundombinu na viwanda. Tatu, kitabu kinaelezea mahusiano ya utandawazi na utamaduni, na hasa katika mazingira ya leo, kuna suala la mahusiano ya utandawazi na itikadi, kama vile demokrasia. Kuna dhana kadhaa juu ya utandawazi ambazo

Tafsiri ya "Ye Tradefull Merchants," Shairi la Edmund Spencer

Image
Siku kadhaa zilizopita nilichapisha mashairi mawili ya Edmund Spencer katika blogu hii. Nilivutiwa na wazo la kuyatafsiri mashairi haya, ingawa magumu, ili kuchangamsha akili yangu na kujipima ufahamu wangu wa lugha. Siku ile ile, nilijaribu kutafsiri "Ye Tradefull Merchant," tangu mwanzo hadi mwisho, halafu nikaamua kuiweka kando tafsiri yangu, kwa kuwa sikuridhika na namna nilivyotafsiri vipengele viwili vitatu. Leo, bila kutegemea wala kupangia, nimepata hamu ya kurekebisha vipengele hivyo. Ninafahamu kwamba, kwa mujibu wa nadharia za tafsiri, tafsiri ni dhana tata. Kutafsiri ni sawa na kujaribu kukikamata kitu kinachoteleza sana. Kwa ujumla, tunajidanganya au tunadanganyana tunaposema tumetafsiri utungo wowote wa fasihi. Hata hivyo, kwa kuzingatia jadi yetu ya kujidanganya na kudanganyana, ninaleta tafsiri yangu ya "Ye Tradefull Merchants." --------------------------------------------------------------------------------------------- YE TRADEFULL MERCHAN

Wadau wa Vitabu Vyangu Kwenye Mkutano wa Africa Network

Image
Jana jioni nilirudi kutoka Ohio, katika Chuo cha Denison, ambako nilikwenda kushiriki mkutano wa Africa Network kama nilivyoripoti katika blogu hii. Nina mengi ya kusema kuhusu mkutano ule, na hapa napenda kusema neno juu ya maprofesa wanaoonekana nami pichani hapa kushoto, ambao wote walinigusa kwa namna walivyoongelea vitabu vyangu. Huyu aliyeko kushoto ni Stephen Volz, profesa wa Chuo cha Kenyon. Tumefahamiana miaka kadhaa katika mikutano ya Africa Network. Aliwahi kuishi Botswana akijitolea chini ya mpango wa Peace Corps. Juzi, nilipowasili kwenye ukumbi wa mkutano, ulikuwa wakati wa chakula cha jioni. Nilienda kukaa kwenye meza ambayo ilikuwa na kiti cha ziada. Mmoja wa watu waliokuwa wameketi hapo ni Profesa Volz. Baada ya kusalimiana, profesa Volz alianza hima kutuambia kuwa alikuwa anajiandaa kwenda Botswana na wanafunzi wa Associated Colleges of the Midwest (ACM), na kwamba atatumia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika pr

Mkutano wa Africa Network

Image
Wikiendi hii nilikuwa chuoni Denison, katika jimbo la Ohio, kuhudhuria mkutano wa Africa Network, mtandao wa vyuo vinavyoshughulikia masomo juu ya Afrika. Nimekuwa mwanabodi wa Africa Network tangu mwanzo, na nimeshuhudia historia yake hadi leo. Mtandao wa wanachama na washiriki wetu unaendelea kupanuka. Picha zote zinazoonekana hapa nilipiga mimi, ambaye naonekana hapa kushoto. Mikutano ya Africa Network ni fursa ya waalimu na watafiti kubadilishana mawazo na uzoefu katika taaluma na nyanja mbali mbali zinazohusu Afrika. Wikiendi hii, tulipata fursa ya kusikia na kujadili mada juu ya masuala kama uhifadhi na usambazaji wa kumbukumbu kidigitali, historia ya kale ya Afrika na umuhimu wake katika masomo juu ya Afrika, kuboresha viwango na ubora katika elimu ya juu, program za kupeleka wanafunzi Afrika. Mkutano wetu huo ulijumlisha washiriki kutoka Marekani na nchi kadhaa za Afrika. Kwa ujumla wetu, tuna uzoefu wa utafiti katika nchi nyingi za Afrika, kama vile Ghana