Showing posts with label usomaji. Show all posts
Showing posts with label usomaji. Show all posts

Saturday, July 1, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ninaamini kuwa kila mtu ana kitu anachokipenda sana. Kuna watu wanaopenda sana soka. Ni mashabiki ambao daima wanafuatilia mechi. Wako tayari kukopa hela ili waende uwanjani kuangalia mechi. Wengine wanapenda bia. Katika baa za Tanzania, nimeona watu wanaokunywa na kuandikiwa deni walipe baadaye. Kama huku kupenda kitu namna hii ni ugonjwa, basi vitabu ndio ugonjwa wangu. Ndio maana katika blogu hii ninaandika mara kwa mara habari za vitabu.

Mtu anaweza kuuliza, inakuwaje katika ulimwengu huu wa vitabu pepe, tuko watu ambao tunaendelea kung'ang'ania vitabu vya jadi? Je, hatuoni udhia wa kubeba vitabu hivyo, na pia udhia wa kuvitafutia sehemu ya kuviweka, badala ya kutumia kifaa cha kuhifadhia vitabu pepe, ambacho kinaweza kubeba mamia ya vitabu au zaidi? Ukweli ni kwamba, mazoea yana taabu. Sio rahisi kuachana na mazoea.

Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi, nilipita katika duka la vitabu la Half Price Books, mjini Apple Valley. Kama kawaida, niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Ernest Hemingway au vitabu juu ya Hemingway. Sikuona kipya, nikaelekea sehemu vinapouzwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Hapo nilichagua vitabu vinne.

Kitabu kimoja ni Gilgamesh: A Verse Narrative, cha Herbert Mason. Wafuatiliaji wa fasihi simulizi za kale wanafahamu juu ya Gilgamesh, mtu maarufu katika masimulizi ya watu wa himaya ya Sumer, katika nchi ambayo leo inaitwa Iraq, na pia nchi zingine za Mashariki ya Kati. Masimulizi haya hatimaye yaliandikwa, katika lugha kadhaa za wakati ule, kwa hati iitwayo "cuneiform," ambayo ni tofauti kabisa na hizi hati tunazotumia leo, kama vile ya ki-Rumi, au ki-Arabu. Ugunduzi wa maandishi yale ulitokana na juhudi za wana akiolojia.

Lakini baada ya ugunduzi, hakuna aliyeweza kusoma hati ya "cuneiform." Baadaye sana siri ya hati hii iligunduliwa na usomaji wake ukawezekana. Tafsiri za masimulizi ya Gilgamesh zikaanza. Kwa upande wangu, kwa miaka mingi nimefundisha masimulizi ya Gilgamesh kwa kutumia tafsiri ya N. K. Sandars. Nilifahamu, hata hivyo, kwamba ziko tafsiri zingine pia. Kwa hivyo, leo niliona ninunue hii tafsiri ya kishairi ya Herbert Mason.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni A Play of Giants, ambayo ni tamthilia ya Wole Soyinka. Nimesoma na kufundisha maandishi ya Soyinka kwa miaka mingi, kuanzia tamthilia, riwaya, mashairi na insha. Ninavyo vitabu vyake kadhaa, lakini si A Play of Giants. Hata hivyo, nilifahamu tangu zamani kuwa tamthilia hii inawaumbua madikteta wa Afrika. Sasa nitaisoma.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Theban Plays of Sophocles. Ni tafsiri ya David R. Slavitt ya tamthilia tatu za Sophocles. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa u-Griki ya kale. Ninazo tatsiri tofauti za tamthilia hizo, lakini niliamua kununua hii pia. Ni jambo bora kusoma tafsiri mbali mbali za kazi ya fasihi, kwani kila tafsiri inaleta ladha tofauti na hata tofauti za ujumbe.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Speaking of Books: The Best Things Ever Said About Books and Book Collecting, kilichohaririwa na Rob Kaplan na Harold Rabinowitz. Hicho sikuwahi hata kukisikia, lakini nilivyoangalia ndani, nilivutiwa. Ni mkusanyiko wa kauli za watu mbali mbali kuhusu vitabu, usomaji, uandishi, waandishi, wasomaji, na kadhalika. Nilikuwa ninafahamu baadhi ya mambo ambayo yamewahi kusemwa kuhusu vitabu, kama vile kauli ya Ernest Hemingway, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Kutokana na kupendezwa kwangu na mambo hayo, niliona ninunue kitabu hiki.

Saturday, March 11, 2017

Mashairi ya Robert Frost

Leo nina jambo la kusema, kuhusu mashairi ya Robert Frost, ambayo nimekuwa nikiyasoma sambamba na kazi zingine za fasihi au taaluma. Ni mazoea yangu kusoma kiholela, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Mashairi ya Frost ninayoongelea yamo katika kitabu kiitwacho Robert Frost: Selected Poems, ambacho binti yangu alininunulia. Wakati ule, nilijitahidi kuyasoma, lakini ninayafurahia zaidi wakati huu, labda ni kwa kuwa akili yangu imetulia kuliko wakati ule.

Leo, kwa mfano, nimesoma shairi liitwalo "The Black Cottage." Tunaelezwa kuhusu watu wawili wanavyoijongea nyumba ndogo iliyofichika nyuma ya miti na nyasi mbali na barabara. Wanaikaribia na kuchungulia ndani. Mmoja wao, ambaye ni mchungaji, anafahamu habari za nyumba hii ambayo sasa haina watu.

Anamweleza mwenzake kuwa bibi kizee aliyeishi humu alifariki, na watoto wake, wote wanaume, wanaishi mbali, ila hawataki kuiuza nyumba wala chochote kilichomo. Walipangia kuwa wanakuja mara moja kwa mwaka, lakini mwaka huu hawajaja. Baba yao alikufa katika vita ya wa-Marekani wenyewe kwa wenyewe ("Civil War"), eneo la Fredericksburg au Gettysburg.

Sehemu kubwa inayobaki ya shairi hili inaelezea fikra za marehemu bibi kizee kuhusu masuala mbali mbali yatokanayo na vita ile, kama vile malengo ya vita, na usawa wa binadamu. Mchungaji anaonesha kuwa fikra na mitazamo ya bibi kizee yule ilikuwa ya pekee na pia ya kutatanisha.

Hata mimi siwezi kusema nimeelewa vizuri mtazamo wa bibi kizee huyu, ingawa nimelisoma shairi hili na kulirudia. Itanibidi nilisome tena na tena. Vile vile, nimeona itakuwa jambo jema kufanya utafiti ili nione kama kuna tahakiki za shairi hili ambazo zimechapishwa. Daima, hii njia bora ya kujipanua upeo kuhusu utungo wa fasihi.

Kama kawaida, Frost anaandika kwa mtindo unaokufanya msomaji ujisikie kuwa anafanya nawe maongezi ya kina. Unawajibika kumsikiliza huku ukitafakari asemayo. Kusoma shairi hili, kama mashairi mengine ya Frost kunahitaji akili  tulivu.

Jambo moja linalonivutia katika kusoma mashairi haya ya Frost ni kuwa ninasoma alichoandika yeye mwenyewe, sio tafsiri. Ni bahati kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mwandishi namna hiyo. Ninakuwa na fursa kamili ya kuguswa na umahiri wa mwandishi katika kuelezea mambo, kuanzia hisia na fikra zake na za wahusika, hadi vitu na mazingira.

Friday, December 2, 2016

Ndugu wa Uganda Anataka Kitabu

Kama ilivyo kawaida katika blogu hii, ninapenda kujiwekea kumbukumbu mbali mbali. Jana niliwatembelea akina mama wawili wa-Kenya waishio Brooklyn Park, Minnesota, ambao walitaka tukutane ili niweze kuwapa ushauri kuhusu fursa za kujiendeleza kielimu ya juu na katika ajira. Wakati tulipokuwa katika maongezi, waliwasiliana na bwana mmoja wa kutoka Uganda, wakamwita kuja kuungana nasi.

Tulizungumza kuhusu masuala mbali mbali, yakiwemo masuali waliyoniuliza juu ya ufundishaji na uandishi wangu. Mmoja wa hao akina mama nilikuwa nimemwahidi kumpa nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Huyu jamaa wa Uganda aliniulizia namna ya kukipata kitabu kile, nikamweleza kuwa anaweza kukipata mtandaoni Amazon.com au lulu.com/spotlight/mbele, au kutoka kwangu. Nikamshauri kwamba kwa upnde wa gharama, ni rahisi zaidi kukinunua Amazon.com. Lakini yeye alisisitiza kuwa nimpelekee, akanipa na anwani yake.
,
M-Ganda huyu amenikumbusha wa-Ganda wengine niliokutana nao hapa Minnesota, wakajiptia kitabu changu. Mmoja ni Steven Kaggwa ambaye alikuwa anamiliki mgahawa wa Tam Tam. Baada ya kukisoma kitabu hiki, aliniambia kuwa aliwaelezea wafanya kazi wake. Mmoja wao, Sally, hakuishia tu kujinunulia nakala, bali alinunua nakala nyingine ambayo aliniambia alikuwa anampelekea mkuu wake wa kazi, ambaye ni m-Marekani. Niliguswa na taarifa ya huyu mama, kama nilivyoguswa miaka michache baadaye, wakati mama mmoja kutoka Togo alivyonunua nakala za kitabu hiki kwa ajili ya wakuu wa kazini kwake, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

M-Ganda mwingine ninayemkumbuka nilikutana naye katika tamasha la vitabu ambalo nilikuwa ninashiriki. Alikuwa amefika kikazi hapa Minnesota, lakini alikuja kwenye tamasha hilo, na ndipo tulipofahamiana. Bila kusita alinunua kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differenes, akaenda zake. Yeye na hao wengine wameniacha nikitafakari jinsi hao wenzetu walivyo. Ninaona kuwa sio tu wameenda shule, bali wameelimika, kwani uthibitisho wa kuelimika ni kuwa na hamu ya kutafuta elimu hata baada ya kumaliza shule.

Monday, October 10, 2016

Ki-Ingereza Kama Lugha ya Ulimwengu

Jana, katika blogu hii, nilikiongelea kitabu cha Charles Derber, People Before Profit, ambacho kinahusu utandawazi. Katika kukisoma kitabu hiki, nilivutiwa na maelezo yake, na nikapata hamasa ya kufuatilia mada ya utandawazi kwa namna nyingine.

Nilikumbuka kwamba nina kitabu cha David Crystal, English as a Global Language, ambacho nilikinunua miaks michache iliyopita, ila nilikuwa nimekipitia juu juu tu. Leo nimeamua kukisoma, na ninaona jinsi maelezo yake kuhusu lugha ya ki-Ingereza yanavyofungamana na suala la utandawazi. Kwa mfano, katika utangulizi wake, mwandishi anasema,

"We have as yet no adequate typology of the remarkable range of language contact situations which have emerged as a consequence of globalization, either physically (e.g. through population movement and economic development or virtually (e.g. through Internet communication and satellite broadcasting)." (xi)

Kitu kimoja kilichonifanya nikumbuke kitabu cha David Crystal ni kuwa huyu ni mtaalam maarufu ulimwenguni wa masuala ya lugha. Nilipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973, nikisomea "Literature" na "English," ndipo niliposoma maandishi ya Crystal, sambamba na mabingwa wengine, kama vile Frank R. Palmer, John Lyons, Noam Chomsky, Sydney Greenbaum, na Randolph Quirk. Kumbukumbu hiyo ndiyo ilinifanya ninunue kitabu cha Crystal, English as a Global Language miaka michache iliyopita. Sasa, kwa kuwa ninafuatilia suala la utandawazi, ninaona nilifanya vizuri kununua kitabu hiki.

Pamoja na kuelezea jinsi ki-Ingereza kilivyofanikiwa kuenea duniani na kinavyoendelea kuiteka dunia kama lugha ya mawasiliano ulimwenguni iliyo muhimu kuliko zote, Crystal anabainisha pia kuwa hatuwezi kuwa na uhakika kama hali hii itaendelea hivi siku za usoni. Kama nilivyoeleza katika ujumbe wa jana, nikinukuu kitabu cha People Before Profit, utandawazi hausambai bila upinzani kutoka katika jamii na tamaduni mbali mbali zinazotaka kulinda jadi na misingi yao.

Ni hivi hivi katika kuenea kwa ki-Ingereza. Crystal anatuelekeza kwenye kitabu cha Tom McArthur, The English Language, na anatumabia kuwa McArthur

"adopted a more synchronic perspective, moving away from a monolithic concept of English. His primary focus was on the kinds of variation encountered in the language as a consequence of its global spread. He suggested that English was undergoing a process of radical change which would eventually lead to fragmentation into a 'family of languages.'" (x)

Hilo wazo la ki-Ingereza kugawanyika katika vilugha mbali mbali linasisimua akili. Lakini, hata kama ki-Ingereza kitaishia kuwa vilugha vingi, ninategemea kuwa bado kutakuwa na misingi itakayodumu katika vi-Ingereza hivyo na kuendelea kuwawezesha watumiaji kuwasiliana na kuelewana. Hata wakati huu, tayari ki-Ingereza kina lahaja nyingi, sawa na ki-Arabu, ki-China, ki-Swahili, na lugha zingine.

Jambo la muhimu la kuzingatia, kwa nchi kama Tanzania, ni hoja ya msingi ya English as a Global Language, kwamba hakuna namna ya kukizuia ki-Ingereza kutawala dunia kama lugha ya mawasiliano. Tupende tusipende, lazima tutafute namna ya kuhakikisha kuwa tunaijua lugha hiyo. Tusipumbazwe na siasa reja reja zilizovaa gwanda la utaifa, tukasahau kwamba ki-Ingereza ndiyo nyenzo na silaha itakiwayo katika mapambano ya ulimwengu wa utandawazi wa leo na kesho.

Friday, February 19, 2016

"Tenzi Tatu za Kale:" Makala Inayosomwa Kuliko Zote

Mara kwa mara, ninaangalia takwimu zinazohusu blogu yangu hii: idadi ya watembeleaji, makala wanazozitembelea, na nchi walimo. Kuanzia wiki kadhaa zilizopita, makala inayotembelewa kuliko zote ni "Tenzi Tatu za Kale." Idadi ya watembeleaji iliongezeka ghafla pale Ndugu Michuzi alipoiweka makala hii katika blogu yake.

Ninajiuliza kwa nini makala hii inawavutia wasomaji namna hii. Je, hii ni ishara ya kupendwa kwa somo la fasihi ya ki-Swahili? Siamini kama ni hivyo, kwani ninaandika makala nyingi kuhusu fasihi, ambazo zinagusia tungo mbali mbali. Ingekuwa uwingi wa wasomaji unaonekana kwenye makala hizo pia, ningeamini kuwa kuna msisimko wa kupenda fasihi.

Ninapata hisia kwamba labda uhusiano na mahitaji ya shuleni au vyuoni. Ninahisi kuwa labda wanaosoma makala ya "Tenzi Tatu za Kale" ni wanafunzi ambao wanatakiwa kusoma Utenzi wa Al Inkishafi, au Utenzi wa Mwana Kupona, au Utenzi wa Fumo Liyongo: moja, mbili, au zote tatu.

Kama ni hivyo, si jambo la kuridhisha wala kufurahisha. Uwanja wa fasihi ya ki-Swahili ni mpana, na mwenye mapenzi na fasihi hii ninamtegemea awe anasoma tungo nyingi. Hata wanafunzi wa fasihi wanatakiwa kusoma tungo mbali mbali, si zile zilizomo katika mitaala tu.

Ningependa sana kuona mijadala ya fasihi ya ki-Swahili katika blogu hii. Ndio maana ninaweka taarifa mbali mbali kuhusu tungo za ki-Swahili. Tuienzi fasihi hii kwa kuisoma bila mipaka, kuichambua, na kuitangaza.
 

Saturday, December 19, 2015

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii, na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni. Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi.

Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu.

Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika kumi kumaliza shughuli hii na kitabu kikawa tayari kununuliwa na watu popote ulimwenguni.

Jambo moja linalovutia sana katika kuchapisha vitabu mtandaoni kwa namna nifanyavyo ni kwamba vitabu hupatikana bila kikomo. Vinahifadhiwa kama mafaili ya kielektroniki, na huchapishwa kama kitabu halisi pale tu mdau anapoagiza nakala. Akiagiza nakala moja, inachapishwa hiyo hiyo. Akiagiza mia au elfu ni hivyo hivyo. Hakuna udhia wa kutunza shehena ya vitabu ghalani na kungojea wateja, huku vikiwa katika hatari ya kuharibiwa na unyevu, mende, au panya.

Hata hivi, nimeona kuna matatizo. Kwanza kwa upande wa mnunuzi. Ni lazima awe na namna ya kununua mtandaoni. Kwa kawaida hii inamaanisha awe na "credit card" kama vile VISA na Mastercard. Jambo la pili ni bei. Nikiangalia vitabu vyangu, naona wazi kuwa kama vingechapishwa mahali kama Tanzania kwa mtindo wa jadi, vingekuwa na bei nafuu kuliko ilivyo sasa.

Lakini, kwa upande mwingine, kama kitabu kinachapishwa kama kitabu pepe, yaani "e-book," kinaweza kuuzwa kwa bei ndogo sana, kuliko bei ya kuchapisha kwa mtindo wa jadi. Mdau anatakiwa awe na kifaa cha kuhifadhia na kusomea kitabu pepe, yaani "e-reader" au "e-book reader," kama vile Kindle au Nook.

Pamoja na kuwepo kwa vitabu pepe na vifaa vya kuhifadhia na kusomea vitabu hivyo, imethibitika tena na tena kwamba wadau wengi bado wanavitaka vitabu vya jadi, yaani vya karatasi na majalada. Mazoea haya na mapenzi ya vitabu vya jadi yamejengeka na hayaonekani kutoweka mioyoni mwa wengi.

Tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni inawaathiri wachapishaji wa jadi kwa namna mbali mbali. Kadiri siku zinavyopita, wengi wao wanaona faida ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Tekinolojia hii mpya inawasukuma kwenda na wakati ili wasipoteze biashara katika mazingira ya ushindani na mabadiliko yasiyoisha.

Sunday, June 21, 2015

Niliyoyaona Maktabani Brookdale, Minnesota

Jana, kama nilivyoandika katika blogu hii, nilihudhuria mkutano Brooklyn Park, ambao tulifanyia katika maktaba ya Brookdale. Hapa kushoto ni picha ya upande wa Mbele wa maktaba hii, inavyoonekana kabla hujaingia ndani. Jana ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika hapa, na niliona jinsi jengo lilivyo tofauti na majengo ya maktaba zingine ambazo nimeingia hapa Minnesota.



Nilivyoingia ndani, nilijikuta sehemu hii inayoonekana kushoto, ingawa ni kubwa na pana zaidi ya hii inayoonekana pichani. Wakutubi wengi wapo katika eneo hilo, tayari kuwasiaida wateja, na sehemu ya maulizo ambayo ni kubwa pia, iko eneo hili. Unapokuwa sehemu hii, kwa mbele yako na pembeni kuna maeneo yenye vitabu, majarida, kompyuta nyingi na hifadhi mbali mbali za taarifa, kama vile CD, DVD na na kaseti.

Niliulizia kilipo chumba cha mkutano, nikapita katikati ya makabati ya vitabu vya kila aina hadi mwishoni kabisa.




Baada ya mkutano, nilirejea tena sehemu hii na kuchungulia katika makabati mbali mbali, hasa ya fasihi. Kuna utajiri mkubwa wa vitabu, vya masomo na taaluma mbali mbali, vya watoto na watu wazima, na vitu vingine vingi. Inapendeza kuona wenzetu wanavyowekeza katika vitu vya namna hii, kuelimisha jamii.

Hiyo jana ilikuwa ni Jumamosi, na ilikuwa ni alasiri. Jua lilikuwa linawaka vizuri, na walikuwepo watu wengi katika maktaba, watu wa kila rangi, na kila rika. Wwnginw walikuwa wanasoma vitabu, wengine wanaazima, wengine wanatumia kompyuta, na wengine walikuwa wanarudufu maandishi.

Nilivyoangalia hali hii, ya watu wengi kuwemo maktabani wakati wa alasiri, Jumamosi, niliwazia hali ya Tanzania. Nilijiuliza ni wapi katika Tanzania unaweza kuona hali hii, tena Jumamosi mchana. Ni wapi unaweza kuwaona watu wa rika mbali mbali wamejaa maktabani wanajisomea. Hata huyu dada Latonya  niliyekutana naye jana hapo nje ya maktaba alikuwa anakuja maktabani na akina dada wenzake.

Ningekuwa na uwezo, ningebadili mioyo ya wa-Tanzania, wawe kama hao wa-Marekani, wenye kupenda kusoma. Ningehamasisha ujenzi wa maktaba zaidi. Kwa mji kama Dar es Salaam, ningependa ziwepo maktaba Sinza, Kinondoni, Buguruni, Kigamboni, Kawe, Kimara, Ukonga na sehemu zingine. Ingekuwa ni Marekani, mji wa ukubwa wa Dar es Salaam ungekuwa na maktaba nyingi. Lakini, miaka hamsini na zaidi tangu tupate uhuru, maktaba ni hiyo hiyo moja. Si jambo la kujivunia.

Saturday, May 9, 2015

Neno Jingine Kuhusu Uandishi na Uchapishaji

Mimi ni mwandishi wa vitabu. Ninaandika vitabu vya tahakiki ya fasihi, juu ya masuala ya jamii, fasihi simulizi, na masuala ya athari za tofauti za tamaduni, hali halisi ya uandishi wa vitabu, mbinu za kujichapishia vitabu. Naandika kuhusu utangazaji na uuzaji wa vitabu, na kuhusu hali halisi ya usomaji wa vitabu Tanzania na ughaibuni.

Ninatoa ushauri kwa wengine kupitia blogu hii na katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Yeyote anayetaka kujifunza kutoka kwangu anaweza kufanya hivyo, bila kipingamizi. Lakini namtegemea aanze kwa kusoma nilichoandika, mawasiano ya ziada yafuate baadaye.

Siwezi kuwasiliana na kila mtu na kuongelea hata yale ambayo tayari nimeshaandika. Nina kazi yangu na majukumu mengine kila siku. Nikisema niwasiliane na kila mtu hata kwa yale ambayo nimeshaandika, nitashindwa kufanya kazi zangu zinazoniwezesha kuishi, kulipia nyumba, matibabu, na mahitaji mengine.

Labda niache kazi niliyoajiriwa kufanya, nijiajiri kama mshauri. Ikiwa hivyo, kila anayetafuta ushauri kwangu atatakiwa alipie. Ndivyo wanavyofanya watoa ushauri. Nami ujuzi na uzoefu ninao, kama inavyodhihirika katika taarifa ninazoandika katika blogu hii ya hapakwetu na blogu ya ki-Ingereza.

Suali ambalo ninaulizwa tena na tena ni kuhusu mikakati ya kuchapisha miswada. Ni wazi kuwa watu bado wana fikra za jadi kuhusu uchapishaji. Nawashauri waondokane na fikra za kuwateemea wachapishaji. Badala yake, waingie katika ulimwengu wa kujichapishia vitabu.

Wafanyeje au waanzie wapi ndio aima ya masuala ninayoongelea katika blogu na katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Kama mtu anataka mafanikio, ni lazima awekeze katika elimu inayohusiana na shughuli anayotaka kufanya. Kununua vitabu na kuvisoma ni uwekezaji, sawa na uwekezaji wa kununua trekta ya kilimo au nyavu za kuvulia samaki.

 Suala la kujichapishia vitabu ni tata, hasa kwa upande wa wanataaluma. Jadi iliyopo katika kuchapisha vitabu vya kitaaluma au makala za kitaaluma imekuwa ya kuzingatia umuhimu wa wanataaluma tofauti na mwandishi kufanya uhakiki na udhibiti wa andiko kabla ya kuchapishwa. Ninapangia kuandika zaidi kuhusu suala hilo.  

Friday, January 23, 2015

Kwa Anayewazia Kuchapisha Kitabu

Wazo la kuchapisha kitabu linawavutia watu wengi. Ni wazo lenye ndoto za mafanikio.Wako wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawapa umaarufu. Kuna wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea fedha nyingi. Wengi, labda wote, wanaamini kuwa wakisha chapisha kitabu, kazi yao inakuwa imemalizika; kinachobaki ni kungojea matokeo, kama vile umaarufu na fedha.

Ni bora mtu anayewazia kuchapisha kitabu ajielimishe zaidi kuhusu jambo hili, nami hupenda kuchangia yale ninayoyafahamu, kwa kadiri ya uwezo wangu. Vipengele ni vingi, lakini hapa nitaongelea vichache tu.

Mtu uandike kitabu kutokana na kujua kuwa una jambo la kusema kimaandishi. Uwe una jambo ambalo linakuelemea akilini mwako na kukusukuma uandike. Msukumo utoke ndani ya nafsi yako. Ukishaandika kitabu kwa msingi huo, utajisikia una raha sawa na mtu aliyetua mzigo. Kuridhika kwako ndilo jambo mihimu. Mengine yanafuata baadaye.

Huenda kitabu chako kitawavutia watu wakakinunua na kukisoma, au huenda kisiwavutie. Lakini sidhani kama hili ni tatizo lako, maadam umeshakidhi haja ya kutua mzigo uliokuwemo akilini mwako, na sasa uko huru kuwazia mambo mengine. Uhuru huu ni jambo muhimu.

Katika miaka yangu ya kuandika, na hata kuchapisha vitabu, nimekuwa nikisoma kuhusu uandishi, uchapishaji na uuzaji wa vitabu. Kitu kimoja mihimu nilichojifunza ni kuwa kuandika na kuchapisha kitabu sio mwisho wa kazi yako kama mwandishi. Kuna kazi kubwa mbele yako, kazi ya kuutangazia ulimwengu kuhusu kuwepo kwa kitabu chako, na kazi ya kukiuza kitabu chako.

Watafiti na waandishi wa masuala hayo wanasisitiza kuwa wajibu wa kuuza kitabu ni yako wewe mwandishi. Kabla ya kuanza kusoma mawazo haya, niliamini, kama wengi wanavyoamini, kwamba kazi ya kutangaza na kuuza kitabu ni ya mchapishaji. Kumbe, hata kama mchapishaji anaweza kuchangia katika jukumu hilo, mwandishi unawajibika sana, na pengine zaidi kuliko mchapishaji.

Kwa upande wa Tanzania, kwa hali ilivyo, tatizo kubwa ni kwamba utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ni hafifu sana. Watu wengi wanadhani kusoma vitabu ni shughuli ya wanafunzi, na hivi vitabu viwe vimo katika mitaala ya shule.

Kujisomea vitabu bila shinikizo la shule au mitihani ni utamaduni ambao unakosekana. Hii ni sababu moja inayonifanya nitoe angalizo kuwa mtu unaweza kuchapisha kitabu na kisiwe na wasomaji.

Masuala haya ya uandishi na uuzaji wa vitabu nimeyaelezea katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, na katika makala mbali mbali katika blogu hii. Ninaendelea kujielimisha kuhusu masuala hayo, na nitaendelea kuandika.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...