Showing posts with label Half Price Books. Show all posts
Showing posts with label Half Price Books. Show all posts

Saturday, July 1, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ninaamini kuwa kila mtu ana kitu anachokipenda sana. Kuna watu wanaopenda sana soka. Ni mashabiki ambao daima wanafuatilia mechi. Wako tayari kukopa hela ili waende uwanjani kuangalia mechi. Wengine wanapenda bia. Katika baa za Tanzania, nimeona watu wanaokunywa na kuandikiwa deni walipe baadaye. Kama huku kupenda kitu namna hii ni ugonjwa, basi vitabu ndio ugonjwa wangu. Ndio maana katika blogu hii ninaandika mara kwa mara habari za vitabu.

Mtu anaweza kuuliza, inakuwaje katika ulimwengu huu wa vitabu pepe, tuko watu ambao tunaendelea kung'ang'ania vitabu vya jadi? Je, hatuoni udhia wa kubeba vitabu hivyo, na pia udhia wa kuvitafutia sehemu ya kuviweka, badala ya kutumia kifaa cha kuhifadhia vitabu pepe, ambacho kinaweza kubeba mamia ya vitabu au zaidi? Ukweli ni kwamba, mazoea yana taabu. Sio rahisi kuachana na mazoea.

Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi, nilipita katika duka la vitabu la Half Price Books, mjini Apple Valley. Kama kawaida, niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Ernest Hemingway au vitabu juu ya Hemingway. Sikuona kipya, nikaelekea sehemu vinapouzwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Hapo nilichagua vitabu vinne.

Kitabu kimoja ni Gilgamesh: A Verse Narrative, cha Herbert Mason. Wafuatiliaji wa fasihi simulizi za kale wanafahamu juu ya Gilgamesh, mtu maarufu katika masimulizi ya watu wa himaya ya Sumer, katika nchi ambayo leo inaitwa Iraq, na pia nchi zingine za Mashariki ya Kati. Masimulizi haya hatimaye yaliandikwa, katika lugha kadhaa za wakati ule, kwa hati iitwayo "cuneiform," ambayo ni tofauti kabisa na hizi hati tunazotumia leo, kama vile ya ki-Rumi, au ki-Arabu. Ugunduzi wa maandishi yale ulitokana na juhudi za wana akiolojia.

Lakini baada ya ugunduzi, hakuna aliyeweza kusoma hati ya "cuneiform." Baadaye sana siri ya hati hii iligunduliwa na usomaji wake ukawezekana. Tafsiri za masimulizi ya Gilgamesh zikaanza. Kwa upande wangu, kwa miaka mingi nimefundisha masimulizi ya Gilgamesh kwa kutumia tafsiri ya N. K. Sandars. Nilifahamu, hata hivyo, kwamba ziko tafsiri zingine pia. Kwa hivyo, leo niliona ninunue hii tafsiri ya kishairi ya Herbert Mason.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni A Play of Giants, ambayo ni tamthilia ya Wole Soyinka. Nimesoma na kufundisha maandishi ya Soyinka kwa miaka mingi, kuanzia tamthilia, riwaya, mashairi na insha. Ninavyo vitabu vyake kadhaa, lakini si A Play of Giants. Hata hivyo, nilifahamu tangu zamani kuwa tamthilia hii inawaumbua madikteta wa Afrika. Sasa nitaisoma.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Theban Plays of Sophocles. Ni tafsiri ya David R. Slavitt ya tamthilia tatu za Sophocles. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa u-Griki ya kale. Ninazo tatsiri tofauti za tamthilia hizo, lakini niliamua kununua hii pia. Ni jambo bora kusoma tafsiri mbali mbali za kazi ya fasihi, kwani kila tafsiri inaleta ladha tofauti na hata tofauti za ujumbe.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Speaking of Books: The Best Things Ever Said About Books and Book Collecting, kilichohaririwa na Rob Kaplan na Harold Rabinowitz. Hicho sikuwahi hata kukisikia, lakini nilivyoangalia ndani, nilivutiwa. Ni mkusanyiko wa kauli za watu mbali mbali kuhusu vitabu, usomaji, uandishi, waandishi, wasomaji, na kadhalika. Nilikuwa ninafahamu baadhi ya mambo ambayo yamewahi kusemwa kuhusu vitabu, kama vile kauli ya Ernest Hemingway, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Kutokana na kupendezwa kwangu na mambo hayo, niliona ninunue kitabu hiki.

Thursday, March 16, 2017

Nimenunua "Two Thousand Seasons" (Ayi Kwei Armah)

Leo nilienda St. Paul, na wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley kuangalia vitabu katika duka la Half Price Books, kama ilivyo kawaida yangu. Hilo duka lina maelfu ya vitabu, na wateja wanapishana humo tangu asubuhi hadi jioni.

Kila ninapoingia katika duka la vitabu, ninajikuta nikianza kuangalia kama kuna vitabu vipya juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Leo sikuona kitabu kipya juu ya Hemingway, nikaenda sehemu nyingine humo dukani, kwenye kona kabisa, ambapo sikosi kupitia.

Hapo, katikati ya msitu wa vitabu, niliona kitabu cha Ayi Kwei Armah, Two Thousand Seasons. Sikutegemea kukuta kitabu cha Armah. Nilikichukua hima, huku nikikumbuka enzi za ujana wangu Tanzania, kwani ni wakati ule ndipo nilianza kusikia habari za Ayi Kwei Armah.

Tangu nikiwa mwanafunzi sekondari, nilikuwa nafuatilia sana fasihi ya ki-Ingereza. Somo la fasihi ni somo nililolipenda na kuliweza sana. Nilipoingia Chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973, ndipo nilipofahamu kuwa Ayi Kwei Armah alikuwa anaishi Dar es Salaam. Alikuwa anafundisha chuo cha ualimu Chang'ombe, lakini tulishangaa kwa jinsi alivyokuwa hatumwoni kokote, hata chuo kikuu. Tulitegemea angejihusisha na chuo kikuu, lakini sidhani kama aliwahi hata kukanyaga pale.

Jambo hilo lilitushangaza, hasa kwa kuzingatia umaarufu wake kama mwandishi katika Afrika na ulimwenguni. Tulisoma riwaya yake, The Beautyful Ones Are Not Yet Born, na mimi binafsi nilisoma pia Fragments, Why are we So Blest?, na Two Thousand Seasons. Ayi Kwei Armah tulimfahamu pia kutokana na insha yake, "African Socialism: Utopian or Scientific?"

Nilijua tangu wakati ule kuwa wahakiki walikuwa wanalumbana kuhusu uandishi wa Armah. Baadhi walilalamika jinsi anavyoielezea Ghana katika The Beautyful Ones Are Not Yet Born. Anaelezea uozo wa kina namna. Wahakiki na wasomaji walishangaa kwa nini aliamua kuanika uozo huo machoni pa ulimwengu.

Two Thousand Seasons inahusu biashara ya utumwa iliyosababisha mamilioni ya wa-Afrika kupelekwa bara la Amerika kama watumwa. Armah kwa kushughulikia mada hii, alikuwa anaendeleza jadi ya waandishi wenzake wa Ghana, kama vile Ama Ata Aidoo katika tamthilia zake mbili: Dilemma of a Ghost na Anowa.

Saturday, May 14, 2016

Nimepita Tena Katika Duka la Half Price Books

Leo alasiri nilikwenda eneo la Minneapolis, mwendo wa maili 40, kwa shughuli binafsi. Ilikuwa siku nzuri, ya jua la wastani na hali ya hewa ya kupendeza. Wakati wa kurudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaamua kupitia katika duka la Half Price Books. Nilitaka hasa kuangalia kama kuna chochote juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Kufuatilia vitabu juu ya Hemingway imeshakuwa mazoea kwangu, wala siwezi kujizuia.

Ninajua kuwa sitakikuta kitabu kipya kilichoandikwa na Hemingway. Inafahamika kwamba miswada yote ya vitabu vya Ernest Hemingway imeshachapishwa. Kinachotokea ni kuwa yanachapishwa matoleo mapya ya vitabu vyake, kama vile matoleo yanayohaririwa na mjukuu wake, Sean Hemingway, ambavyo Mzee Patrick Hemingway, mtoto wa Ernest Hemingway, anaviandikia utangulizi.

Maandishi mapya kabisa ya Ernest Hemingway yanayochapishwa ni barua zake. Kuna mradi wa kukusanya barua zote za Ernest Hemingway tangu utotoni mwake. Wahariri wa mradi huu ni maprofesa Sandra Spanier na Robert W. Trogdon, ambao wamebobea katika utafiti juu ya Ernest Hemingway. Hadi sasa majuzuu matatu yamechapishwa, na kila juzuu ni mkusanyo wa barua za miaka michache. Inatarajiwa kuwa mradi huu ambao utachukua miaka mingi, utatoa majuzuu yatachapishwa 17.

Vitabu vingine vipya ambavyo vinaendelea kuchapishwa ni matokeo ya utafiti juu ya maisha na maandishi ya Ernest Hemingway. Tangu zamani, kumekuwa na watafiti wengi wanaojishughulisha na utafiti huu, na vitabu ambavyo wamechapisha na wanaendelea kuchapisha ni vingi. Si rahisi kwa mtu yeyote kufuatilia suala hili kikamilifu, lakini ninakuwa na duku duku ya kuona kuna vitabu gani vipya juu ya Hemingway katika duka la vitabu.

Nimefurahi leo kukikuta kitabu juu ya Hemingway ambacho sikuwa hata nimekisikia, The True Gen: An Intimate Portrait of Hemingway by Those Who Knew Him kilichoandikwa na Denis Brian. Katika kukipitia, niliona kuwa kitabu hiki ni taswira ya Hemingway inayotokana na kumbukumbu za watu waliomfahamu. Niliamua hapo hapo kukinunua. Baada ya kufika nyumbani, nimeanza kukisoma.  Kuna maelezo ya watu wengi, kuanzia wale waliokuwa watoto wakienda shule na mtoto Ernest Hemingway hadi waandishi, wake zake, na watu wengine.

Kama ilivyo kawaida, nilipokuwa hapo dukani Half Price Books niliwaona watu wengi humo wakizunguka zunguka kuangalia vitabu na kuvinunua. Wazazi wengi walikuwa na watoto wao. Kama kawaida, inavutia kuwaona watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa katika utamaduni wa kupenda vitabu.

Sikukaa sana humo. Baada ya kununua kitabu changu, niliona niwahi nyumbani nikaanze kukisoma.


Monday, December 8, 2014

Vitabu Nilivyonunua Juzi

Juzi, Jumamosi,  nilienda Minneapolis, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation, ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la Half Price Books, ambalo nimeliongelea mara kadhaa katika blogu hii.

Ingawa ilikuwa jioni sana,  watu walikuwa wengi humo dukani: watu wazima, vijana, na watoto. Nami nilijichanganya nao, nikaangalia angalia sehemu zenye vitabu vya fasihi. Nilinunua vitabu vinne, ambavyo nitavielezea leo.

Lakini kabla ya kuelezea vitabu hivi, napenda kujikumbusha kitu kimoja kilichonigusa, wakati nimesimama katika foleni ya kulipia vitabu. Mbele yangu walikuwepo baba na mama na watoto wadogo wawili wasichana. Walikuwa wameshaweka vitabu vyao kwenye kaunta ya kulipia, huku wakiwaelezea wale watoto jinsi watakavyowasomea vitabu. Kati ya vile vitabu kwenye kaunta, niliviona viwili vikubwa vikubwa vya Harry Potter. Muda wote wale watoto walikuwa na furaha na msisimko. Kwa mara nyingine tena, nilishuhudia jinsi wenzetu wanavyowalea watoto wao katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.

Kitabu kimojawapo nilichonunua ni Much Ado About Nothing, ambayo ni tamthilia ya Shakespeare iliyohaririwa na Barbara A. Mowat na Paul Werstine. Wasomaaji wa Shakespeare wanajua kuwa tamthilia zake zimehaririwa na wahariri mbali mbali katika hii miaka 500 tangu kufariki kwake.

Tamthilia za Shakespeare, ambazo ni 37, hupatikana pia zikiwa zimekusanywa katika kitabu kimoja kikubwa sana. Ingawa ninazo nakala za kitabu hiki--nakala mbili hapa Marekani na nyingine Tanzania--huwa napenda, mara moja moja kununua hivi vitabu vya tamthilia moja moja, kwa vile ni rahisi kubeba katika mkoba na kwenda navyo popote.

Kitabu kingine nilichonunua ni The Pickwick Papers, kilichotungwa na Charles Dickens. Wengi wetu tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu tunamkumbuka Dickens na riwaya zake, kama vile Oliver Twist na A Tale of Two Cities. Binafsi, nilimpenda sana Dickens, na nilisoma vitabu vyake kadhaa. Nimewahi kumwongelea Dickens katika blogu hii.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Hemingway on Hunting. Nimenunua toleo lililochapishwa na The Lyons Press, mwaka 2001. Kitabu hiki ni mkusanyo wa maandishi ya Ernest Hemingway yanayohusu uwindaji. Mhariri wake ni Sean Hemingway, mjukuu wa mwandishi mwenyewe. Pia kuna utangulizi mfupi ulioandikwa na Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Sean amekusanya maandishi kutoka katika vitabu  kama vile Green Hills of Africa, For Whom the Bell Tolls, Across the River and into the Trees, na pia makala na barua mbali mbali alizochapisha Ernest Hemingway katika magazeti.

Ingawa mengi ya maandishi hayo ninayo, niliona ni vema kuwa na kitabu hiki ambacho kinahusu hili suala la uwindaji. Ningependa kusema pia kuna kitabu cha aina hiyo hiyo, ambacho ni mkusanyo wa maandishi ya Hemingway kuhusu uvuvi, na kingine kuhusu uandishi. Hemingway, katika falsafa na nadharia zake, aliongelea uhusiano baina ya  uandishi na uwindaji.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Minaret, riwaya iliyotungwa na Leila Aboulela, ambaye alikulia Khartoum na anaishi Dubai na Aberdeen. Ni mwandishi maarufu, ambaye ameshajitwalia tuzo kadhaa kwa uandishi wake. Ingawa nimesikia habari zake kwa miaka kadhaa, sikuwahi kusoma kitabu chake hata kimoja. Leila Aboulela anajulikana kwa umahiri wake kisanaa, pia kwa jinsi anayowaelezea suala la wanawake katika u-Islam kwa mtazamo tofauti na ilivyozoeleka. Nina dukuduku ya kusoma Minaret, kwa kuanzia, na nitapenda pia kusoma riwaya zake zingine.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...