Baada ya kumaliza kitabu cha Half of a Yellow Sun, darasa langu la fasihi ya Afrika tumekuwa tukisoma Abyssinian Chronicles , riwaya ya Moses Isegawa. Moses Isegawa ni kijana aliyezaliwa na kukulia Uganda. Lakini mwaka 1990 aliondoka Uganda akaenda kuishi Netherlands, akiwa amechukua uraia wa nchi ile. Nilikuwa nimesikia habari za kitabu chake hiki kwa miaka kadhaa. Nilinunua nakala, ila sikupata fursa ya kukisoma, ingawa nilikipitia juu juu. Hata hivyo katika kukipitia hivyo, niliona wazi kabisa kuwa ni kitabu murua, kilichoelezea kwa ufasaha na mvuto mkubwa maisha ya leo ya watu wa Uganda, kuanzia kijijini hadi mjini. Nilipokuwa naandaa kozi yangu hii, miezi michache iliyopita, niliamua kitabu hiki kiwemo katika orodha yangu. Tumesoma karibu kurasa 100 tu, wakati kitabu kina kurasa 480. Kiasi tulichosoma kimetupa fursa ya kuongelea dhamira mbali mbali zinazojitokeza, kama vile mila na desturi za arusi, masuala ya wahusika, na sanaa. Kwa upande wangu, nimekuwa nikiwaambia w