Wageni Kutoka Tanzania


Wiki hii nimekuwa na bahati hapa Minnesota ya kukutana na wageni wawili kutoka Tanzania. Mgeni wa kwanza, Ndugu Charles Mpanda kutoka Arusha, tulionana tarehe 25 mjini Rochester, tukapiga picha inayoonekana hapa kushoto. Habari ya tukio hili niliandika hapa. Nitaandika zaidi katika blogu hii ya "hapakwetu."


Leo nimeenda mjini New Prague, kuonana na mgeni mwingine, Fr. Setonga, ambaye naonekana naye katika hiyo picha ya chini. Fr. Setonga tumewasiliana kwa miaka mingi kidogo, kwa simu na barua pepe, ila hatukuwahi kuonana. Leo imekuwa bahati ya kuonana.

Tumeongelea masuala mbali mbali, kuhusu dini yetu, kuhusu juhudi na mafanikio ya Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu, sehemu mbali mbali duniani, kwa karne hadi karne, kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu. Hii inatokana na msimamo wa Kanisa Katoliki wa kuthamini sana elimu. Kwangu mimi niliyesomeshwa katika shule za Kanisa Katoliki, ni jambo la kujivunia na kushukuru kwamba walinifundisha maadili na nidhamu ya kazi ya kiwango cha juu kabisa, pamoja na kuzingatia vipaji na uwezo tunapata kutoka kwa Mungu, na kwa ajili ya kuwahudumia wengine.

Tuligusia mfano hai wa jinsi Kanisa Katoliki linavyokazana kufungua matawi ya chuo kikuu cha Mtakatifu Augustin nchini Tanzania. Nilimdokezea Fr. Setonga kuwa ninawazia kwenda kufundisha katika chuo hiki, kama njia moja ya kutoa shukrani kwa Kanisa.

Kati ya mambo mengine tuliyoongelea kwa undani, tukakubaliana, ni umuhimu wa sisi waumini wa Tanzania kuwa wafadhili wa kanisa letu na shughuli zake mbali mbali. Itakuwa ni faraja na jambo la kujivunia iwapo tutabeba majukumu ambayo aghalabu yamebebwa na wafadhili kutoka nchi za nje, hasa Ulaya na Marekani.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini