Kiu ya Kusoma Vitabu

Daima nina kiu ya kusoma vitabu.  Sio rahisi unikute sina kitabu. Hii sio tu kwa vile mimi ni mwalimu. Ni tabia ambayo nilijengeka nayo tangu nikiwa kijana mdogo.

Kuwa mwalimu kumenipa motisha zaidi ya kusoma sana vitabu. Wakati huu ninapoandika, wanafunzi wangu na mimi tumemaliza kusoma Half of a Yellow Sun kilichoandikwa na Chimamanda Ngozi Adichie. Sote tumekifurahia sana. Lakini, mwandishi huyu amechapisha hivi karibuni na kitabu kingine kiitwacho Americanah, ambacho tayari kinazungumziwa sana miongoni mwa wapenda vitabu. Kwa hivi, nami najipanga kujipatia kitabu hiki, nikisome.

Kitabu kingine ambacho tumekimaliza katika darasa tofauti siku chache zilizopita ni Midnight's Children cha Salman Rushdie.  Kitabu hiki ni kama chemsha bongo, kwa jinsi kilivyotumia mbinu mbali mbali za kuelezea maisha ya mhusika mkuu Saleem Sinai. Maisha hayo yamefungamana na historia ya India, tangu dakika ile India ilipopata uhuru, usiku wa manane, mwaka 1947. Rushdie amechanganya matukio ya historia na ubunifu wake wa ajabu katika kitabu hiki.

Midnight's Children ni kitabu kinachokutegemea msomaji uwe na ufahamu fulani wa mila, desturi na dini za India, hasa u-Hindu, u-Islam, u-Kristu, na u-Parsi. Uwe na ufahamu fulani wa historia ya India hasa katika karne ya ishirini, inayojumlisha viongozi maarufu kama Mahatma Gandhi, Jawaharlal Nehru, Muhammad Ali Jinnah, na Indira Gandhi. Ujue mazingira yaliysababisha kuzaliwa kwa nchi mbili za India na Pakistan, na mgogoro wa Kashmir, ambao bado unaendelea. Kwa bahati nzuri, katika miaka niliyofundisha hapa chuoni St. Olaf, nimefundisha sana fasihi ya India na hayo yote niliyoyataja.

Tulipofikia ukurasa wa mwisho wa kitabu hiki, tulijisikia kama washindi wa mashindano magumu. Kwa upande wangu, baada ya kupambana na Midnight's Children hadi mwisho, nimejawa na hamasa ya kusoma kitabu kingine cha Rushdie Satanic Verses, ambacho nilikinunua zamani, nikajaribu kukisoma, bila kufika mbali. Ninahisi kuwa kwa kusoma Midnight's Children nimejiandaa vilivyo kukabiliana na Satanic Verses. Au labda nianzie na kitabu chake kiitwacho The Enchantress of Florence, ambacho nimekuwa nacho kwa miaka kadhaa, bila kukisoma.

Ni jambo jema kujaribu kusoma maandishi mbali mbali ya mwandishi yeyote, sio kitabu kimoja tu. Kwa mfano, kwa upande wa Tanzania, utawakuta watu wakitaja kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai lakini hawajui kuwa mwandishi huyu amechapisha vitabu vingine pia, na makala nyingi, kuhusu u-Islam na fasihi.

Vile vile, wengi wakisikia jina la Salman Rushdie, wanalihusisha na kitabu cha Satanic Verses tu. Huu nao ni uzembe, kwani mwandishi huyu amechapisha vitabu vingi, kuanzia riwaya hadi insha kuhusu masuala mbali mbali ya sanaa, siasa na utamaduni. Kumtendea haki Rushdie ni lazima tusome maandishi yake mbali mbali.

Akili zetu zinapaswa ziwe na duku duku isiyoisha ya kujua mambo. Njia moja kuu ya kujaribu kukidhi kiu hii ni kusoma sana vitabu. Hapo utaona kwamba, tofauti na imani ya jamii yetu ya Tanzania, wajibu wa kusoma vitabu ni wa watu wote, sio wanafunzi tu.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini