Posts

Showing posts from March, 2009

Vitabu Vyangu Vimeingia Longitude Books

Siku chache zilizopita, nilileta ujumbe kuwa kampuni ya Longitude Books , inayouza vitabu kwa wasafiri na watalii, iliniulizia namna ya kupata vitabu vyangu. Mara baada ya kuwajibu, wamefanya hima na kuvijumlisha vitabu hivyo katika orodha yao. Huu ni mfano wa jinsi wenzetu walivyo makini katika kuzichangamkia fursa. Niliwaambia kuwa vitabu hivi vinapatikana lulu.com kwa bei ya dola 12, na wao wajipangie bei ya kuviuza kwa wateja wao. Wameamua kuuza kwa dola 19.95. Ukitaka kuvitafuta vitabu hivyo hapa Longitude Books , andika Mbele katika kidirisha cha "Search" halafu bonyeza " Go ."

Watanzania Wanaoishi Baa

Watanzania wengi wanaishi baa. Ingawa wana nyumba, au wamepanga vyumba, wanatumia muda mwingi zaidi baa kuliko kwenye makazi hayo. Wakitoka ofisini au sehemu nyingine ya kazi, wanaelekea baa. Wanakaa hapo hadi usiku, wakati baa inapofungwa. Wanakwenda nyumbani kulala tu, na asubuhi sana wanaamka tena na kwenda kazini. Jioni wanapotoka kazini, wanaelekea baa. Siku hadi siku, maisha yao ni hayo. Kwa nini watu wanaishi baa? Bila shaka kila mtu anayeishi baa ana sababu zake. Katika kuongea na watu kijuu juu, inaonekana wako wanaoamini kuwa baa ni mahali pa kubadilishana mawazo ya maana. Sina hakika kuwa ulabu unaboresha mawazo. Wengine inaonekana wanaishi baa kwa vile nyumbani hakukaliki. Wako baa kama wakimbizi. Hata kama sina ufahamu wa kutosha, naona kuna haja ya kulitafakari suala hili la Watanzania wanaoishi baa.

Kila Mtu na Lwake: Tutafika?

Najiuliza kama njia ya kufanikiwa katika jamii yetu ya kiTanzania ni ya kushirikiana au ni ya kila mtu na lwake. Mara moja moja huwa nahudhuria mikutano ya wajasiriamali na wafanya biashara hapa Marekani, ingawa mimi ni mwalimu. Huwa nasoma pia vitabu na majarida kuhusu ujasiriamali na uendeshaji wa biashara. Kwenye hii mikutano, watu wanaongelea shughuli zao, wanabadilishana uzoefu na kuelimishana. Baada ya hapo, watu hupenda kubadilishana anwani na simu, ili waweze uwasiliana zaidi. Mimi mwenyewe nimewahi kuombwa nielezee shughuli zangu, maana ninajaribu kujiimarisha kama mjasiriamali, kwenye shughuli ya kutoa ushauri katika masuala yahusuyo tamaduni ili kuwawezesha wafanya biashara, wajasiriamali, na wengine kufanikiwa wanaposhughulika na watu wa tamaduni mbali mbali. Ni jambo la kufurahisha kwamba, baada ya kujieleza, nimeona watu walivyo wepesi kunipa ushauri, kuniunganisha na wengine, na kadhalika. Kitu wanachozingatia katika shughuli hizi ni kujenga na kutumia mtandao. Hii dh

Vitabu kwa Watalii

Leo nimepata ujumbe kutoka Longitude Books , kampuni maarufu ya kiMarekani inayouza vitabu kwa watalii na wasafiri wengine. Wanaulizia namna ya kupata vitabu vyangu. Wanasema wameambiwa na jumuia ya Stanford Alumni Travel waviweke vitabu hivi katika orodha yao kwa ajili ya wasafiri wanaokwenda Tanzania. Longitude Books wanahitaji vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales na katika ujumbe wao wanasema "we'd like to be able to include Africans and Americans and Matengo Folktales in our mix of recommendations for travelers to Tanzania....We're working on more family and exchange programs and both books will enhance our offerings." Kwangu hii ni habari njema. Ni faraja kuona kuwa kazi ninayofanya inatambuliwa. Hilo si jambo geni hapa Marekani. Vitabu vyangu vinatambuliwa na kutumika sehemu mbali mbali. Kinachosikitisha ni kuwa kwa miaka kadhaa nimejaribu kuwasiliana na waTanzania wanaohusika na sekta ya ut

Mbwa aliyezua tafrani Zanzibar apelekwa New York

Leo nimeona makala, "Mbwa aliyezua tafrani Zanzibar apelekwa New York," ambayo imenigusa kwa namna ya pekee, kwa vile inahusu tofauti baina ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani. Masuala hayo nayashughulikia sana, katika utafiti, ufundishaji, uandishi, warsha, na mazungumzo na watu mbali mbali. Makala hii imenigusa kwa namna ya pekee kwa kuwa inahusu habari iliyotokea Zanzibar. Nilishaenda Zanzibar, kwa kuombwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kutoa mihadhara kuelezea jinsi mimi kama Mwafrika ninavyoiona Marekani. Mihadhara hiyo niliitoa Zanzibar na Pemba. Nilizungumzia tofauti za utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani, nikitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Suala la mbwa nimeliongelea katika kitabu hiki. Na niliposoma makala hii, nilipata hisia kuwa laiti kama hao wawekezaji wangekuwa wamekisoma, kwani walikuja kweye utamaduni ambao si wao, na walikuwa na wajibu wa kuzingatia utamaduni wa wenyeji. Makosa ya ain

Mishahara Haitoshi

Katika nchi yetu ya Tanzania, watu wanalalamika muda wote kuwa mishahara haitoshi. Gharama ya maisha ni kubwa kuliko mishahara. Hata kwa kuzingatia mahitaji muhimu tu, watu wengi wana haki ya kusema kuwa mishahara haitoshi. Malalamiko ya mishahara kuwa haitoshi yanasikika duniani kote. Hapa Marekani, shida kubwa inayowakabili watu ni kulipa bili na madeni mbali mbali. Marekani ni nchi ya madeni. Kutodaiwa popote ni sifa nzuri katika utamaduni wa Tanzania. Lakini Marekani, sifa inakuja kutokana na umakini wa kulipa madeni. Mishahara ya Wamarekani wengi inaishia kwenye kulipa madeni. Kwa hivi, nao wanalalamika kuwa mishahara haitoshi. Wako Watanzania ambao wana mishahara ambayo ingeweza kutosheleza mahitaji muhimu. Tatizo ni kuwa dhana ya mahitaji muhimu ina utata. Tunaweza kusema mahitaji hayo ni chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, na usafiri. Lakini, katika utamaduni wetu, orodha ya mahitaji muhimu ni kubwa zaidi ya hiyo. Kumlipia ada mtoto wa shangazi ni wajibu. Kuchangia gh

Busara za Kipanya

Image
Kati ya watu maarufu sana Tanzania ya leo ni mchoraji wa vikatuni vya Kipanya. Tovuti yake hii hapa . Ujumbe wa Kipanya katika katuni inayoonekana hapa unatukumbusha mambo ya msingi. Tunapoongelea masuala ya nchi yetu, au wahusika wanapopanga mipango mbali mbali, walengwa wakuu wanakuwa hao wanaoishi vijijini, ambao ndio asilimia kubwa ya wananchi, au walengwa wanakuwa hao wa mijini, ambao ndio wapangaji wa hiyo mipango?

Ushauri kwa Viongozi wa Serikali - Awamu ya Nne

Nimesoma makala, ambayo imeandikwa na H.S. Kasori, nikavutiwa sana na anayosema kuhusu Mwalimu Nyerere. Miaka yote tangu nilipoanza kuyafahamu masuala ya siasa, nimemwona Mwalimu Nyerere kuwa mtu wa aina hiyo anayoongelea Kasori. Pamoja na masuala mengine yote katika blogu yangu hii, ninajitahidi kutaja na kujadili mchango wa Mwalimu Nyerere. Ni muhimu tuendelee kufanya hivyo, kwani mchango wa Mwalimu Nyerere kwa Taifa letu na dunia ni mkubwa sana. Kuna upotoshaji mwingi kuhusu Mwalimu Nyerere. Naamini kuna pia juhudi inafanywa nchini Tanzania kuzimisha na kufifisha fikra za Mwalimu Nyerere. Hayo nitaendelea kuyaongelea katika blogu hii. Mimi ni Mtanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote. Msimamo wangu kuhusu vyama vya siasa Tanzania ninautoa katika baadhi ya makala zangu ndani ya blogu hii. Naileta hapa makala ya Kasori kwa vile nimevutiwa na yale anayosema kuhusu Mwalimu Nyerere. Nawakaribisha kusoma makala ya Kasori, "Ushauri kwa Viongozi wa Serikali - Awamu ya Nne&q