Posts

Showing posts from March, 2012

Changamoto za Kuendesha Blogu

Kuenesha blogu sio kazi rahisi. Kuna changamoto nyingi. Kwa mfano, wakati mwingine unashindwa kujua uandike nini. Huna wazo kichwani. Wakati mwingine unaandika ukijiuliza kama kweli uchapishe hicho unachoandika. Unajua fika kuwa chochote unachochapisha, kinasambaa duniani dakika hiyo hiyo. Kuna pia upande wa wasomaji, yaani hao tunaowaita wadau wa blogu. Binafsi, nawakaribisha wadau wanaotembelea blogu yangu. Unapoandika makala kwenye blogu yako, huwezi kujua watu wataipokea vipi. Kila mtu ni tofauti na mwingine. Kinachomridhisha au kumpendeza huyu kinaweza kumuudhi mwingine. Ufanyeje hapo? Huwezi kumridhisha kila mtu, na kwa upande wangu siandiki kwa lengo la kumridhisha yeyote. Najaribu tu kuelezea kilichomo akilini au moyoni mwangu wakati ninapondika. Kuna pia wadau wanaoandika maoni. Hapo pana changamoto. Kuna watoa maoni ambao wanamshambulia au kumbeza mwendesha blogu. Je, ni sahihi kwa mwendesha blogu kuyafuta maneno yao yasionekane kwenye blogu? Bin

Profesa Anapotinga Baa

Kwa siku hizi ambazo nimekuwepo hapa Dar, nimekuwa nikitinga kwenye baa hii au ile, ingawa sinywi ulabu. Watu wengi hapa nchini wananifahamu kutokana na kuona taarifa zangu mtandaoni. Huko kwenye baa, wengine huambiwa na wenzao mimi ni nani. Wadau wakishagundua kuwa mimi ni profesa, hupenda kuanzisha mijadala nami. Wanadadisi mambo mengi, yakiwemo yale ya Marekani. Nimejikuta nikilumbana na wadau wa aina aina, wakiwemo wale ambao wamelewa chakari. Ni burudani ya aina yake kuwashuhudia hao waliolewa chakari wakijibidisha kutema umombo ili ijulikane kuwa nao wamo. Sasa, katika hizi siku zijazo, nataka kuanza kuwaambia hao marafiki zangu kuwa kwa kweli, mahali ambapo profesa anapaswa kuwepo ni maktabani, darasani, au sehemu ya utafiti wake. Anapaswa kuwa anatumia muda wake mwingi katika kusoma na kuandika makala na vitabu, si kukaa kaunta akitema cheche kwa wadau wa konyagi, Tusker, na Kilimanjaro za baridi. Wadau kwenye baa hawatambui hilo. Hatari mojawapo ni kuwa watu wanadhani mtu k

Kunywa Maji Badala ya Ulabu

Image
Kwa siku kadhaa sasa, nikiwa katika kutumia dawa nilizoandikiwa na daktari, ni marufuku kukata ulabu. Badala yake, kinywaji changu ni maji tu. Nikikaa mahali, hata baa, kinywaji changu ni maji tu. Mwanzoni, nilidhani itakuwa adhabu kali kuziangalia chupa za bia baridi katika joto hili la Dar es Salaam bila kunywa hata glasi moja. Lakini nimegundua kuwa kunywa maji kuna raha yake. Ningejiona shujaa iwapo ningeweza kuendelea hivyo hivyo maisha yote.

Nimetua Safari Resort Dar es Salaam

Image
Jana, Jumamosi, nilitua Safari Resort, eneo la Kimara, Dar es Salaam. Ilikuwa mchana, nami nilitamani kwenda tena mahali hapa, ambapo nilipapenda kuanzia miaka ya 1976, nilipoanza kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hapo kushoto unaiona Safari Resort, ukiwa kwenye barabara iendayo Morogoro. Hapo ndipo getini, palivyo siku hizi. Miaka ile, Safari Resort ilikuwa inavuma sana. Gwiji wa Muziki King Kikii alikuwa akiimba hapa na bendi yake,na kukonga nyoyo za wa-Tanzania kupita maelezo. Sikwenda Safari Resort kuchapa ulabu. Wiki hii natumia dawa kutibu tatizo la afya lililonipata. Kwa hivi, sinywi bia kabisa. Nanywa maji tu. Hata hivyo, nimegundua kuwa kwenda sehemu za starehe kama hizo na kuishia kunywa maji haimaanishi kuwa unakaa hapa ukiwa na majonzi. Sio lazima ukienda mahali kama hapa upige ulabu hadi upotee njia, au uanzishe varangati ya kufa mtu, kama tufanyavyo wa-Tanzania. Maji yanatosha, na bado

Mkulima wa Msoga, Msoma Vitabu

Image
Jana nimekutana tena na Gilbert Mahenge, mkulima wa Msoga, Bagamoyo, ambaye tumeshakuwa marafiki. Nilishaandika habari zake hapa , nikimnadi kuwa ni msomaji makini wa vitabu. Alikuja tukakutana Dar es Salaam, katika hoteli ya Deluxe, Sinza. Lengo kubwa la kukutana lilikuwa kuongelea shughuli za kampuni yangu ya Africonexion , tukazama katika kutafakari changamoto zinazotokana na utandawazi wa leo, na fursa zake. Mahenge alishasoma kitabu changu cha CHANGAMOTO , kama nilivyoelezea kabla. Anapenda kuyanukuu niliyoandika. Basi, hiyo jana, nilimletea vitabu vyangu vingine viwili avione, yaani Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , Matengo Folktales , na Notes on Achebe's Things Fall Apart . Ili kuzuia malalamiko na maulizo miongoni mwa wasomaji wa blogu hii, niseme tu kuwa vitabu hivi vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 na 0717 413 073. Tulipokuwa tunaongelea masuala ya changamoto za malengo na maendeleo ya mtu binafsi, nilitaja suala la mtu kuwa n

Nimeugua Dar es Salaam; Natibiwa Hapa Hapa, Sio India

Nimeugua Dar kuanzia siku chache zilizopita. Nimejikuta nikiwashwa hasa mikononi, miguuni, na mgongoni. Kwa siku mbili sikuweza kulala usiku. Katika kuulizia watu, nikaambiwa ni "allergy." Na mhudumu mmoja kwenye duka la madawa maeneo ya Sinza aliniambia niende Magomeni, kwenye hospitali ya Dr. Ole. Nilienda hapo. Wakati wa kuchukuliwa damu ili ipimwe, mpimaji alinipiga mchapo kuwa isije ikawa nimewekewa sumu ya unga. Akazidi kutonya, huku akijifanya ananyunyizia unga mezani, kuwa kaunga kidogo tu kanatosha. Nami nilijibu kuwa mtu huwezi kujua, kwani Bongo haina dogo. Tukawa tunacheka. Ni kweli daktari alipochunguza ripoti ya upimaji amegundua nina "allergy," na akanielezea sababu zake. Pia alisema kuna bakteria katika damu. Aliniandikia sindano na vidonge vya aina mbali mbali. Alisema kuwa hiyo dozi itafuta kabisa hili tatizo. Nimedundwa sindano jana na vidonge nikaanza. Tayari nimeshaanza kujisikia nafuu. Naendelea vizuri kabisa. Nimeleta habari hii binafsi kw

Nimetua Kunduchi Beach Hotel

Image
Jana mchana nilichukua dala dala nikaenda zangu Kunduchi Beach Hotel. Kuanzia maeneo ya Lugalo na kwenda mbele, kuna shughuli kubwa ya ujenzi wa barabara. Napenda kupunga upepo sehemu za ufukweni. Napenda pia kuandika taarifa za sehemu hizo, kama nilivyofanya kuhusu Matema Beach na Mbamba Bay .

Nimetua Bongo, Na "Laptop" Yangu Imetoweka

Nimetua Bongo kutokea ughaibuni tarehe 3 Machi. Wiki moja baadaye, "laptop" yangu imeibiwa hapa Dar es Salaam, eneo la Sinza. Ilikuwa ni Apple mpya. Nilikuwa nimeipakia maandishi yangu mengi, miswada na ripoti za utafiti wa kuanzia 1993. Ninachohitaji ni haya maandishi. Huu ni mchango wa taaluma ambao natoa kwa wa-Tanzania na walimwengu. Miswada ya vitabu viwili nilitaka kuchapisha hapa Tanzania wakati huu, kwa manufaa ya wanafunzi, walimu, na jamii. Hii "laptop" ukiifungua inakupa jina la Joseph Mbele, na unahitaji "password" ili kuweza kuitumia. Habari ndio hiyo. Hivi sasa najiona kama mkulima mwenye ari ya kulima, lakini jembe hana. Nakala za miswada ziko ofisini Marekani. Lakini mimi nilipania kufanya kazi kubwa kwa wiki hizi nitakapokuwa hapa Tanzania. Nimekwama.

Mgomo wa Madaktari: Tusidharau Wakunga na Uzazi Ungalipo

Niko Dar es Salaam, kuanzia Machi 3, na kuanzia siku mbili zilizopita, kumekuwa na mgomo wa madaktari, kufuatia madai yao kuwa serikali haijatekeleza makubaliano yaliiyofikiwa wiki chache zilizopita. Nimesikiliza kauli za Waziri Mkuu Pinda pia. Ninachoweza kusema, kwa ufupi kabisa ni kuwa serikali ya Tanzania imeamua kukiuka busara ya wahenga kwamba tusidharau wakunga na uzazi ungalipo. Ni jambo la ajabu na la kutisha kwa serikali au nchi kugombana na madaktari. Kwamba Tanzania imefikia hapo ni dalili tosha za kutowepo busara za kiuongozi. Madai ya madaktari, tangu mwanzo nayaafiki. Madai hayo ni pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi mahospitalini, uwepo wa vifaa, madawa, na kadhalika. Vipato vya madaktari navyo ni duni sana. Tafsiri yangu ni kuwa madai ya madaktari hayahusu maslahi yao binafsi tu, bali maslahi ya wagonjwa. Tanzania, nchi yenye rasilimali nyingi, yenye serikali ambayo inafuja mali kwa namna mbali mbali, inaweza kabisa kutekeleza madai ya madaktari. Nitoe mfa