Saturday, March 31, 2012

Changamoto za Kuendesha Blogu

Kuenesha blogu sio kazi rahisi. Kuna changamoto nyingi. Kwa mfano, wakati mwingine unashindwa kujua uandike nini. Huna wazo kichwani. Wakati mwingine unaandika ukijiuliza kama kweli uchapishe hicho unachoandika. Unajua fika kuwa chochote unachochapisha, kinasambaa duniani dakika hiyo hiyo.

Kuna pia upande wa wasomaji, yaani hao tunaowaita wadau wa blogu. Binafsi, nawakaribisha wadau wanaotembelea blogu yangu. Unapoandika makala kwenye blogu yako, huwezi kujua watu wataipokea vipi. Kila mtu ni tofauti na mwingine. Kinachomridhisha au kumpendeza huyu kinaweza kumuudhi mwingine. Ufanyeje hapo?

Huwezi kumridhisha kila mtu, na kwa upande wangu siandiki kwa lengo la kumridhisha yeyote. Najaribu tu kuelezea kilichomo akilini au moyoni mwangu wakati ninapondika.

Kuna pia wadau wanaoandika maoni. Hapo pana changamoto. Kuna watoa maoni ambao wanamshambulia au kumbeza mwendesha blogu. Je, ni sahihi kwa mwendesha blogu kuyafuta maneno yao yasionekane kwenye blogu? Binafsi, naona ni bora watu wawe na fursa kamili ya kujieleza. Tatizo tu ni jinsi wengi wao wanavyojificha chini ya kivuli cha anonymous. Mimi mwenye blogu najitambulisha wazi, na hata ninapoancika maoni kwenye blogu za wengine ninajitambulisha wazi, hata pale ninapoandika jambo linalowaudhi watu. Sielewi kwa nini wengine wasifanye hivyo hivyo.

Lakini je, mdau akiandika matusi dhidi ya mtu mwingine, au akimdhalilisha mtu mwingine, ni sahihi kuruhusu hayo kwenye blogu yako? Suali hili lilijitokeza katika kikao changu na Mwenyekiti Mjengwa siku chache zilizopita.

Nilijifunza mawili matatu kutoka kwake. Ninajua kuwa endapo blogu yangu itaendelea na kuwa maarufu kama ya Mjengwa, changamoto za aina hii zitanipata.

Nakaribisha uzoefu na maoni ya wanablogu wengine, na ya wadau.

5 comments:

Anonymous said...

Mimi (anonymous) nadhani kila blog ina watu wake wenye hadhi fulani.Kwa mfano hii blog yako Prof si rahisi kukuta ni sehemu ya wahuni wasio kuwa na nidhamu au wale watu wenye kujihisi ni lazima atoe maoni kwa kila kinachoandikwa.Unaweza ukaandika makala humu na watu wachache wakatoa maoni yao kistaarabu hata kama mtu atatofautiana na ww. Lakini makala hiyo hiyo ikatolewa kwenye blog nyegine utakuta jinsi watu wanavyo respond differentely.Hapo basi ndipo utakapo ona tofauti ya blog na watu wake.Si kila anonymous ataandika kumtukana mtu na si kila anyeandika jina lake huandika kiustaarabu bila ya kumtukana mtu. Hayo ni maoni yangu"anonymous"

Mbele said...

Asante, anonymous, kwa mchango wako murua. Nimeguswa na kila ulilosema.

Christian Sikapundwa said...

Profesa unacho kisema ndicho kilicho kwa baadhi ya watu,na ukweli usiyofichika kwamba ninapoandika nambo fulani ili wadau wa blog yangu wasome,ni kila mmoja atapokea aonavyo yeye,wengine watapendezwa nayo na wengine hawatapendezwa nayo.Lakini ahtuwezi kutumia mtandao huu ati kwa kuwa wengine wanachukizwa,ili mradi maadili ya matumizi ya mitandao inafuatwa.
Kuhusu kutumia lugha chafu kwenye mitandao ni ukosefu wa maadili,kwanini blog zitumike kuchafua wengine? Haipendezi.
Juma pili ya matawi njema.

Yasinta Ngonyani said...

Prof. Ulichosema ni kweli kabisa na kama alivyosema asiye na jina hapo juu kwamba inategemea na mtu na mtu sio hao wasio na majina tu ndio wanaoandioka lugha chafu ...na ni kwalöi utakuta mimi nineandika mada haileti changamoto lakini mada hiyohiyo mwingine anaichukua na kuiweka kibarazani kwake na inapokelewa na watu vingine kabisa....

www.mwana-dikala.bogspot.com said...

Prof. Unachosema ni kweli. Binadamu tumezaliwa, na kulelewa katika mazingila tofauti. Aidha tunatofautiana ki elimu,imani, exposure na MTAZAMO. Ndio maana mtu mmoja anaweza kuiona glasi ya maji ikiwa NUSU imejaa na mwingine akaiona glasi hiyo ikiwa NUSU tupu. Glasi ni ileile kinachogomba ni mtazamo tu. Ni vizuri kuwaelewa watu na kuwachukulia jinsi walivyo.Ni vizuri kuonya, kukemea na kushauri kwa lugha nzuri. Hata hivyo tabia ya kutoa maoni ya matusi na kashfa dhidi ya watu wengine ni ukosefu wa ustaarabu na uduni wa kufikiri. Ni muhimu kumtendea mwingine unavyopenda kutendewa nawe.MWANADIKALA

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...