Posts

Showing posts from 2018

Nashukuru Niliandika Kitabu Hiki

Image
Nashukuru niliandika kitabu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Nasema hivi kutokana na jinsi kinavyothaminiwa na watu wanaokitumia. Taarifa hizi ninazipata kutoka kwao. Wiki hii kwa mfano, nimepata mawasiliano kutoka kwa waalimu wawili. Profesa Artika Tyner, kiongozi mojawapo wa Chuo Kikuu cha St. Thomas ameniandikia kuwa anahitaji nakala za kitabu hii, nami nimempelekea. Niliwahi kumwongelea katika blogu hii, baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza. Tangu tukutane, amekuwa mpiga debe wangu wa dhati. Namshukuru. Nimepata pia ujumbe kutoka kwa Profesa Barbara Zust wa Chuo cha Gustavus Adolphus kunialika kwenda kuongea na wanafunzi anaowapeleka Tanzania katika programu ambayo imedumu miaka mingi. Kama ilivyo kawaida yake, ananiomba nikaongee na wanafunzi kuhusu masuala yaliyomo katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Kama kawaida, watakuwa wameskisoma na wanasubiri fursa ya kuniuliza masuali. Miaka yote nimefurahi kukutan

Kumbukumbu ya Matengo Folktales Kutajwa Katika "Jeopardy."

Image
Kipindi kama hiki, mwaka jana, kitabu cha Matengo Folktales kilitajwa katika kipindi maarufu cha televisheni kiitwacho Jeopardy." Ilikuwa tarehe 23 Novemba, nami niliandika taarifa katika blogu hii. Tukio hili la kushtukiza lilinifungua macho nikatambua kuwa "Jeopardy" ni maarufu sana hapa Marekani. Bado sijui taarifa za kitabu changu zilifikaje kule, ila ninafurahia kuwaambia waMarekani taarifa hizo kila ninaposhiriki matamasha ya vitabu.

Vitabu Kama Zawadi ya Sikukuu

Image
Kwa watu wengi, huu ni wakati wa maandalizi ya sikukuu ya Krismasi. Pamoja na mengine, ni kununua zawadi kwa ajili ya ndugu, marafiki na kadhalika. Hapa Marekani, vitabu ni zawadi mojawapo inayothaminiwa. Hapa kushoto ni picha niliyopiga tarehe 16 Novemba katika duka la vitabu la Barnes and Nobel mjini Burnsville. Inaonyesha kabati la vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka. Nilipiga picha hiyo kwa sababu kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , kipo hapo. Kimekuwepo kwa wiki nyingi. Bila shaka kuna wateja wanaoingi na kuchungulia kwenye kabati hilo ili kupata wazo juu ya kitabu cha kununua, kwani tayari kimependekezwa na watu wazoefu wa vitabu. Utamaduni wa kuvihesabu vitabu kama zawadi muafaka kwa sikukuu au mazingira yeyote mengine unanivutia, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii. Ninatamani utamaduni huu uote mizizi katika nchi yangu. Nawazia furaha watakayokuwa nayo watoto kwa kupewa vitabu kama zawadi, kwa sababu ninajua kuwa watot

Nimeongea na Lumen Christi Book Club

Image
Miezi kadhaa iliyopita, nilipata mwaliko wa kwenda Lumen Christi Catholic Community kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Aliyenialika ni Jackie ambaye alikuwa amekisoma kitabu hicho. Alisema kwamba jumuia ya waumini hao wana klabu yao ya usomaji vitabu, na kwa sasa wamejikita katika vitabu vinavyohusu Afrika. Nilipoingia ukumbini, niliona meza imepangwa vizuri karibu na mlandoni, yenye vitabu vyangu na vya waandishi wawili ambao tunafahamiana: Maria Nhambu ambaye alizaliwa Tanzania, na Afeworki Ghorghis, jaji mstaafu wa mahakama kuu ya Eritrea. Baada ya Jackie kunitambulisha, nilielezea kifupi nilivyokulia Tanzania, katika utamaduni wa wa-Matengo, na hatimaye nilivyokutana na utamaduni wa Marekani, nilipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, na kufikia kuwa mshauri kwa vyuo vinavyopeleka wanafunzi Afrika, kama nilivyoandika katika utangulizi wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Difference s. Kati

Nimepeleka Vitabu kwa wa-Matengo

Image
Mwezi Julai mwaka huu nilikwenda Tanzania, nikiwa nimechukua vitabu vingi. Baadhi ni vile nilivyoandika mwenyewe, ambavyo niliviwasilisha katika maduka ya Kimahama, na A Novel Idea. Nilichukua pia nakala 16 za Matengo Folktales kwa ajili ya kuzipeleka kwa wa-Matengo, wilayani Mbinga, katika mkoa wa Ruvuma. Ninasema hivyo, na kutaja kabila langu, nikijua kwamba kwetu wa-Tanzania, hii ni kauli tata, isiyopendeza, kwani inaashiria upendeleo au ubaguzi kwa msingi wa kabila. Utamaduni wa Tanzania, uliojengwa na chama cha TANU, hauafiki ubaguzi wa makabila au wa aina nyingine. Sasa kwa nini nimetoa kauli hiyo? Kwa nini niliamua kupeleka nakala hizi za Matengo Folktales kwa wa-Matengo? Napenda kuthibitisha kwamba nilifanya jambo muafaka. Matengo Folktales ni mkusanyo wa hadithi za jadi ambazo nilizirekodi nyumbani u-Matengo miaka ya sabini na kitu. Nilizirekodi katika kaseti, kisha nikachagua hadithi kumi na kuzitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliandika uchambuzi wa kila hadithi na nika

Minnesota Black Authors Expo Imekaribia

Image
Bado siku sita tu hadi maonesho yaitwayo Minnesota Black Authors Expo yatakapofanyika. Hii ni mara ya pili kwa maonesho haya kufanyika. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana. Waandaaji waliniomba niwemo katika jopo la waandishi watakaoongelea masuala mbali mbali ya uandishi wa vitabu. Nilikubali. Jopo linategemewa kuwa kivutio kikubwa katika tamasha hilo.

Waandishi Marafiki Tumekutana

Image
Tarehe 13 mwezi huu, nilishiriki tamasha la vitabu liitwalo Deep Valley Book Festival mjini Mankato, jimbo hili la Minnesota. Nilishahudhuria mara tatu tamasha hili linalofanyika mara moja kwa mwaka. Nilijua kuwa mmoja wa waandishi ambao walikuwa mbioni kushiriki ni rafiki yangu Becky Fjelland Brooks anayeonekana pichani kushoto. Becky ni mwalimu katika South Central College hapa Minnesota. Tulianza kufahamiana wakati yeye na Profesa Scott Fee wa Minnesota State University Mankato waliponialika kwenda kuongea na wanafunzi waliokuwa wanawaandaa kwa safari ya masomo Afrika Kusini. Watu wengi walihudhuria mhadhara wangu kuhusu tofauti za tamaduni, na nakala nyingi za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences zilinunuliwa. Baada ya hapo, nimepata mialiko ya kwenda kuongea na wanafunzi hao kila mara wanapoandaliwa safari ya Afrika Kusini. Mwalimu Becky ni mmoja wa wale wa-Marekani ambao wanaipenda Afrika na wanajibidisha kuwaelimisha wenzao kuhusu Afri

Kitabu Bado Kiko Dukani Barnes and Noble

Image
Juzi nilienda Apple Valley na Burnsville kuangalia maduka ya vitabu, kama nilivyoandika katika blogu hii. Kule Burnsvile, mji jirani na Apple Valley, nilitaka kuingia katika duka la Barnes and Noble ambamo kitabu changu kilikuwa kimewekwa sehemu maalum ya vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Sikujua kama ningekikuta, kwani sijui utaratibu wanaofuata katika kuvionesha vitabu hivyo sehemu hiyo. Nilidhani labda vinawekwa kwenye kabati hili kwa wiki moja hivi. Nilishangaa kukiona kitabu changu bado kipo, na kimewekwa juu zaidi ya pale kilipokuwepo kabla. Hapa kushoto ni picha niliyopiga wiki iliyopita, na kulia ni picha niliyopiga juzi. Ninafarijika na kufurahi kukiona hapa. Ninasubiri siku ya kwenda kukiongelea, kama nilivyodokeza.

Vitabu Nilivyonunua Leo

Image
Leo niliamua kutembelea maduka ya vitabu kwenye miji ya Apple Valley na Burrnsville hapa Minnesota. Apple Valley, kwenye duka la Half Price Books,   nilinunua vitabu vitatu bila kutegemea. Nilipita sehemu ya vitabu vya Hemingway, ambapo sikuona kitabu kigeni kwangu. Nilienda sehemu ya bei nafuu, nikanunua vitabu vitatu. Kimoja ni Essays and Poems cha Ralph Waldo Emerson, kilichohaririwa na Tony Tanner. Kwa miaka mingi nimefahamu jina la Emerson. Nilifahamu kuhusu insha yake "Self Reliance," ingawa sikuwa nimewahi kuisoma. Nilifahamu pia kuwa ameathiri sana falsafa na uandishi, sio tu Marekani, bali kwingineko. Kwa hali hiyo, sikusita kununua kitabu hiki, hasa baada ya kuona kuwa kina mashairi ya Emerson. Sikujua kuwa alitunga mashairi. Kitabu kingine nilichonunua ni Collected Poems cha Edna St. Vincent Millay. Huyu ni mwandishi ambaye sidhani kama niliwahi kusikia hata jina lake. Lakini nilipoona hiki kitabu kikubwa sana chenye kurasa 757 na nyongeza ya kurasa 32, na h

Nimeshiriki Tamasha la Vitabu la Deep Valley

Image
Leo nilienda Mankato, Minnesota, kushiriki tamasha la vitabu liitwalo Deep Valley Book Festival. Hii ilikuwa mara yangu ya nne kushiriki tamasha hilo. Ilikuwa fursa ya kuongea na watu kwa undani kuhusu mambo mbali mbali. Kuna watu kadhaa ambao nawakumbuka zaidi. Mmoja aliniambia kuwa ana binti yake ambaye anafundisha ki-Ingereza kama lugha ya kigeni. Hapa Marekani somo hilo linajulikana kama English as a Foreign Language. Hufundishwa kwa wahamiaji ambao wanahijtaji kujia lugha hiyo, ambayo ndio lugha rasmi ya hapa Marekani. Nilichangia mada hiyo kwa kuelezea jinsi sgughuli ya kufundisha ESL inavyofungamana na suala la tamaduni. Hufundishi tu muuno, sarufi, istilahi, bali pia utamaduni wa mazungumzo. Mama mmoja mzee, mwandishi, ambaye meza yake ilikuwa mbele yangu, alifika kunisalimia na kuongea. Nilimwuliza ameandika kuhusu nini, akaniambia kitabu chake kinahusu changamoto aliyopitita kufuatia binti yake kujitokeza kama mwenye silika ya mapenzi ya jinsia yake. Nilivyomwelewa huyu

Mchakato wa Kwenda Kuongelea Kitabu

Image
Leo nimepata ujumbe kutoka kwa Dan, ambaye hivi majuzi alikipigia debe kitabu changu,  Africans and Americans: Embracing Cultural Differences,  katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Anaendelea na juhudi yake. Ameandika: Happy to spread the word about your book. Let me know if you are ever interested in doing a talk at our store. I can connect you with our manager. Tafsiri yangu : Ninafurahi kukitangaza kitabu chako. Nijulishe iwapo utapenda kuja kukiongelea katika duka letu. Nitaweza kukuunganisha na meneja wetu. Kuwaalika waandishi kuongelea vitabu vyao ni utamaduni wa kawaida hapa Marekani. Ni fursa ya mwandishi kukutana na watu wanaotaka kujua mambo kama  historia ya mwandishi, changamoto za uandishi, falsafa na mawaidha yake kuhusu uandishi, na kadhalika. Vinakuwepo vitabu vya mwandishi, kwa watu kuvinunua na yeye kuvisaini. Wa-Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Naambiwa Niongeze Bei ya Kitabu

Image
Katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki, ninakutana na mambo mengi, zikiwemo tabia na mitazamo ya wateja. Moja ambalo linanigusa zaidi ni pale mteja anaposhauri niongeze bei ya kitabu changu. Hiyo imetokea mara kadhaa, kuhusiana na vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultual Differences na Matengo Folktales . Vitabu hivi ninaviuza kwenye matamasha kwa dola 14 kila kimoja. Kwa kujua kwamba watu wengine wanatoa  noti ya dola 20 au noti mbili za dola kumi kumi, ninajitahidi kuwa na chenji. Ajabu ni kwamba watu wengine hawasubiri chenji, na wengine wanakataa. Wanachotaka ni kitabu waende zao. Ninakumbuka watu waliowahi kutoa noti ya dola 20 bila kutaka chenji. Mmoja wa hao, nilipojiandaa kumpa chenji, alisema hiyo chenji ni shukrani yake kwangu kwa kuandika kitabu. Tarehe 4 mwezi huu nilikutana na jambo jingine kabisa. Mama moja, Jackie, ambaye nimemfahamu miezi michache iliyopita na akasoma hivi vitabu vyangu viwili, alinialika kwenye mhadhara wa rafiki yake Mar

Nimenunua Tena Tungo Zote za Shakespeare

Image
Tarehe 24 Septemba, nimenunua tena kitabu cha tungo zote za William Shakespeare.  Nilikinunua katika duka la Half Price Books mjini Apple Valley nilipotoka Burnsville kuangalia kitabu changu kama nilivyoelezea katika blogu hii. Ingawa tayari nina vitabu vinne vyenye tungo zote za Shakespeare, sikuona tatizo kununua hiki pia. Kuwa na nakala mbali mbali za kitabu cha tungo za Shakespeare kuna mantiki nzuri kwa sababu tungo hizo zimehaririwa kwa namna mbali mbali. Hii imekuwa ni sehemu ya historia ya uchapishaji wa tungo za Shakespeare. Mara kwa mara neno linaloonekana kwenye nakala fulani si lile linaloonekana kwenye nakala nyingine au limeandikwa kwa namna tofauti na lilivyo katika nakala nyingine. Hali hiyo ni ile inayoonekana katika miswada ya tungo za zamani, sehemu mbali mbali ulimwenguni, ikiwemo za huku kwetu, kama zile za Liongo Fumo. Tofauti hazikwepeki, kwa sababu uandishi katika enzi za Shakespeare ulikuwa tofauti na wa leo. Leo kitabu kikichapishwa, tunategemea ni nak

Nimekikuta Kitabu Changu Barnes and Noble

Image
Baada ya kusikia kwamba kitabu changu kimewekwa sehemu maalum katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoandika katika blogu hii, leo nimeenda Burnsville kuangalia. Hapa kushoto linaonekana duka hilo, ambalo nimelitembelea mara kadhaa. Hapa kushoto ndio mwonekano wa kabati ambapo huwekwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka. Kitabu changu kinaonekana hapo chini. Duka lolote la Barnes and Noble huwa na vitabu vingi sana. Ni kama maktaba. Kwa hiyo, kitabu kuuzwa humo si jambo la ajabu. Hakunaajabu yoyote kwa kitabu changu kuuzwa Barnes and Noble. Kama nilivyoandika juzi, kitab changu hich kimekuwepo kwenye mtandao wa Barnes and Noble kwa muda mrefu. Kitu cha pekee ni uamuzi wa mhudumu wa duka kukipendekeza kwa wateja, kama inavyooneka hapa chini ya kitabu: Short and sweet. A wonderful read about the differences between Africans and Americans. I feel wiser to the world after reading it. Tafsiri yangu: Kifupi na kitamu. Andiko la kupendeza ajabu kuhusu tofauti za

Kitabu Kimeingia Barnes and Noble

Image
Kwa wasomaji wa vitabu hapa Marekani, jina la Barnes and Noble si geni, kwani ni jina la kampuni inayomiliki maduka mengi ya vitabu yaliyoko nchi nzima. Maduka ya Barnes and Noble ni maarufu kiasi kwamba watu wanapoongelea maduka ya vitabu, huwazia kwanza Amazon na Barnes and Noble. Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mhudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville, mwendo wa nusu saa kutoka hapa ninapoishi. Ameandika: Hi Joseph. Just letting you know I put your book on the staff recommendation display at the Barnes and Noble Burnsvill e where I work. The book about cultural differences between Africans and Americans. I really enjoyed it! Tafsiri yangu: Jambo Joseph. Nakufahamisha tu kwamba nimeweka kitabu chako sehemu vinapoonyeshwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville ambapo ninafanya kazi. Kile kitabu juu ya tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani. Nilikifurahia sana! Bwana huyu aliyeniandikia ujumbe alikuwa mhudumu wa duka

Mdau Wangu Mpya

Image
Juzi, tarehe 8, nilikwenda Coon Rapids, Minnesota, kuhudhuria uzinduzi wa jarida liitwalo L Magazine. Jarida hilo linalohusu zaidi masuala ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, limeanzishwa na Bi Bukola Oriola mwenye asili ya Nigeria anayeishi hapa Minnesota. Kati ya watu waliohudhuria ni Dr. Artika Tyner, rafiki wa karibu wa Bi Oriola. Dr. Tyner ni "Vice President for Diversity and Inclusion" wa Chuo Kikuu cha St. Thomas.  Anaonekana pichani akiwa ameshika tuzo alizopewa hiyo juzi kwa mchango wake kwa jamii. Alipotambulishwa kwangu kwenye meza nilipoweka vitabu vyangu, tuliongea kiasi kuhusu shughuli zake na zangu. Alinunua vitabu vyangu, zikiwemo nakala 9 za Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Vile vile alielezea hamu yake ya kuendelea kuwasiliana nami ili tutafakari namna ya kushirikiana katika programu zinazohusu Afrika na watu wenye asili ya Afrika yaani wanadiaspora. Nilitambua kuwa Dr. Tyner ni mmoja wa waMarekani Weusi ambao w

The 2018 Minnesota Black Author's Expo

Image

Vitabu Nilivyonunua Nairobi

Image
Nilisafiri tarehe 15 Julai kwenda Tanzania. Nilishukia Nairobi, kwa shughuli binafsi, ikiwemo kununua vitabu vya ki-Swahili. Kitabu nilichotamani zaidi ni Sauti ya Dhiki cha Abdilatif Abdalla ambacho nilitaka kukisoma kwa makini kuliko nilivyowahi kufanya kabla. Ninawazia pia kutafsiri kwa ki-Ingereza baadhi ya mashairi. Nilivyoingia tu katika duka la vitabu la Textbbook Center, Kijabe Street, nilikitafuta kitabu cha Sauti ya Dhiki . Nilikiona, kikiwa na jalada tofauti na lile la mwaka 1973. Nilinunua pia Kichwamaji , Kaptula la Marx , Mzingile , na Dhifa , vya Euphrace Kezilahabi; Mashetani , tamthilia ya Ebrahim Hussein, na Haini , cha Adam Shafi. Tangu zamani, nimekuwa na baadhi ya vitabu vya Kezilahabi, Ebrahim Hussein, na Adam Shafi. Ninafurahi kujipatia vile ambavyo sikuwa navyo. Hata hivi, nimegundua kuwa sasa nina nakala mbili za Mashetani na mbili za Kichwamaji .

Maongezi ya Kina Leo na Msomaji Wangu

Image
Leo nimekuwa na maongezi ya kina na msomaji wangu, mchungaji ambaye nilishamtaja katika blogu hii. Tulikutana mjini Hastings, Minnesota, tukaongeaa kwa saa mbili na robo. Tulikuwa tumeahidiana kwamba nikasaini nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho mchungaji alikuwa anampelekea mtu fulani wa karibu. Tuliongea sana kuhusu shughuli zetu za kuelimisha na kuhamasisha jamii ya watu weusi juu ya masuala ya kujitambua. Mchungaji ameendelea kunifahamisha kuwa kitabu changu kinamsaidia kujitambua kama mtu mwenye asili ya Afrika, ingawa ana pia asili ya ki-Cherokee na ki-Faransa. Anataka kitabu hiki kitumike kuwaelimisha vijana wa-Marekani Weusi, waweze kujitambua na kujivunia walivyo na silika za u-Afrika, ili wasiwe wanabezwa na wazungu. Nami naelewa vizuri tatizo lilivyo kwa hao vijana. Wanashinikizwa kubadili mwenendo, lugha, na mambo yao mengine, ili wafuate ya wazungu. Mashuleni wanashinikizwa, kudhibitiwa, na kuadhibiwa kwa mien

Nimehudhuria Mhadhara Kuhusu Frantz Fanon

Image
Jioni hii nilikuwa St. Paul kuhudhuria mhadhara juu ya Frantz Fanon uliotolewa na Dr. Moustapha Diop. Mhadhara uliandaliwa na Nu Skool, jumuia ya wa-Marekani Weusi ambayo nimewahi kuiongelea katika blogu hii. Niliona ni lazima nikahudhurie mhadhara huu, ambao mada yake ilikuwa "Becoming Fanon: A Portrait of the Decolonized" kwa kuzingatia umuhimu wa fikra za Fanon katika harakati za ukombozi sehemu mbali mbali za dunia, hasa ukombozi wa fikra. Nilikutana  na fikra za Fanon kwa mara ya kwanza nilipokuwa mwanafunzi chuo kikuu cha Dar es Salaam, katika idara ya Literature, miaka ya 1973-76. Aliyetufundisha ni mwalimu Grant Kamenju, na vitabu vya Fanon alivyotumia ni The Wretched of the Earth na Black Skin White Masks . Katika kufundisha fasihi ya Afrika, ninaona umuhimu wa kurejea katika fikra za Fanon mara kwa mara. Sielewi utakosaje kurejea kwenye fikra za Fanon. Katika mhadhara wake, Dr. Diop alielezea kifupi maisha ya Fanon, akajikita zaidi katika kufafanua jinsi

Vitabu Vinapobebana

Image
Nadhani kila msomaji wa vitabu anatambua manufaa na raha ya kusoma vitabu vya aina mbali mbali. Hivi ninavyoandika, ninakaribia kumaliza kusoma Riding the Waves of Culture: Understanding Diversity in Global Business , kitabu ambacho nilikitaja siku kadhaa katika blogu hii. Nimekifurahia sana kitabu hiki, kwa jinsi kinavyoongelea masuala ya tofauti za tamaduni, mada ambayo ninashughulika nayo sana. Kinanifanya nielewe undani wa yale niliyoandika katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Kwa mfano, sura ya kitabu hiki iitwayo "How We Manage Time," imenipa msamiati wa kuelezea yale niliyoelezea katika sura iitwayo "Time Flies But Not in Africa." Nimeelewa kwamba msimamo wetu wa-Afrika ni "synchronic" au "polychronic" na msimamo wa wa-Marekani ni "sequential." Tofauti zetu ambazo nimezielezea katika kitabu changu zimejengeka katika mitazamo hiyo miwili. Nitoe mfano. Kama ninavyoeleza katika kitabu changu, sisi t

Mwalimu Mwingine Aongelea Kitabu Changu

Image
Ni jadi yangu kuwatambua wasomaji wanaosema neno kuhusu vitabu vyangu. Ni namna ya kuwashukuru kwa kutumia muda wao kukisoma kitabu na kutumia tena muda kuandika maoni yao. Ninatambua kwamba wanafanya hivyo kwa hiari, na wangeweza kutumia muda wao kwa namna nyingine. Ninawashukuru. Wiki hii amejitokeza mwalimu Khalid Kitito, ambaye amekitumia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika ufundishaji wake hapa Marekani, akaandka maoni kwenye mtandao wa PublicReputation : Africans and Americans written by Joseph Mbele is an excellent book to read about cultural differences between Americans and Africans. He examined the deep culture and not surface culture. It brings out clearly the understanding as to why Americans and Africans have different perspective of time, relationships, work, family, love, respect among others. I used it to teach in my Culture and Identity Class and found it useful. The book provided a forum for insightful discussions and at the

Tunasoma "Homegoing," Riwaya ya Yaa Gyasi

Image
Tarehe 4 Juni, nilianza kufundisha kozi ya kiangazi hapa chuoni St. Olaf juu ya fasihi ya Afrika (African Litterature). Nimefundisha kozi hiyo mara kadhaa miaka iliyopita. Baada ya mimi kutoa utangulizi siku mbili za mwanzo, tulianza kusoma riwaya ya Yaa Gyasi iitwayo Homegoing . Yaa Gyasi alizaliwa Ghana akakulia hapa Marekani. Nilikutana naye katika tamasha la Hemingway mjini Moscow, katika jimbo la Idaho akiwa ni mgeni rasmi wa tamasha kufuatia riwaya yake kushinda tuzo ya PEN/Hemingway kwa mwaka 2017. Homegoing , inaturudisha nyuma karne tatu zilizopita, kwenye nchi ambayo leo ni Ghana. Tunaona jamii inavyoishi mila na desturi zake na mahusiano ya watu, lakini tunaona pia shughuli ya biashara ya utumwa. Tunaona jinsi watu walivyokuwa wakitekwa kufanywa watumwa na wengi kupelekwa pwani kwenye kasri ya Cape Coast kuhifdhiwa humo katika mazingira ya ovyo kupindukia, wakisubiri kuvushwa bahari kwenda Marekani. Homegoing inafaa kusomwa sambamba na tamthilia ya The Dilemma of

Vitendea Kazi vya Kampuni Yangu

Image
Mwaka 2002, nilianzisha na kusajili kampuni ambayo niliita Africonexion , kama nilivyoandika katika blogu hii. Nilisajili kama kampuni binafsi, usajili ambao hapa Marekani hujulikana kama "sole proprietorship." Niliamua kuanzisha na kusajili kampuni hii ya kutoaelimu na ushauri wa masuala ya utamaduni kwa kuwa tayari nilikuwa na uzoefu wa shughuli hizo, nikihudumia vyuo, makanisa, mashirika, jumuia na watu binafsi. Shughuli zangu hizi zimekuwa na mafanikio makubwa, kwa maana kwamba nimewasaidia watu kuelewa na kuepukana na mambo ambayo yanaweza kusababisha migogoro na kutoelewana. Wale ambao tayari walishakumbana na migogoro na kutoelewana nimewasaidia kufahamu kwa nini walijikuta katika migogoro na kutoelewana. Lakini mimi mwenyewe nimefanikiwa pia kujifunza mengi katika shughuli zote hizo. Napenda kuelezea siri moja kubwa ya mafanikio haya. Siri hiyo ni kujielimisha kwa kutumia vitabu. Vitabu ndio vitendea kazi vyangu. Sichoki kununua na kusoma vitabu. Kulingana na shu

Nimekutana na Msomaji Mpya

Image
Jana jioni nilikutana na msomaji mpya wa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilikuwa mjini St. Paul kuhudhuria darasa la Nu Skool, ambayo ni jumuia ya wa-Marekani Weusi wanaokutana mara moja kwa mwezi kutafakari na kujadili masuala mbali mbali. Kwa kawaida, kunakuwepo na mtoa mada na kunakuwepo na masuali ya watu kuyajadili. Wakati mwingine inaonyeshwa filamu ya kuelimisha, ambayo inafuatiliwa na mjadala pia. Mada ya mkutano wa jana ilikuwa "The Language of Black America." Jana hiyo, tulipokuwa tumemaliza darasa na baadhi yetu tukawa tunaendelea kuongea na kutambulishana, mama moja aliniambia kuwa anasoma kitabu changu na kuwa kinamgusa sana. Mama huyu m-Marekani Mweusi alisema kuwa mambo ninayoelezea yanamwezesha kujitambua ni nani kiasili. Alisema anakisoma kitabu kidogo kidogo kwa makusudi ili kuupata ujumbe vizuri, bila pupa. Alisema kuwa, katika maisha yake kama m-Marekani Mweusi alikuwa na hisia mbali mbali, lakini hakuelewa ch

Mtanzania Afundishaye ki-Swahili Marekani Akifurahia Kitabu

Image
Mimi kama mwandishi ninathamini maoni ya wasomaji juu ya maandishi yangu. Msomaji anapokuwa ametumia muda wake kusoma na kutafakari nilichoandika, halafu akatumia muda wake kuandika maoni, kwangu si jambo dogo. Ninashukuru. Katika blogu hii nina jadi ya kuwatambua wadau hao. Hivi karibuni, nimeona andiko la Filipo Lubua katika ukurasa wake wa facebook kuhusu kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Huyu anafundisha ki-Swahili katika Chuo Kikuu cha Pittsburgh hapa Marekani. Anasema kwamba anakitumia kitabu hiki katika kozi juu ya Afrika Mashariki, na anasema ni kitabu kinachovutia sana. Ananishukuru kwa kukiandika kitabu hiki rahisi kusomeka juu ya mitazamo yetu, yaani sisi wa-Afrika na wenzetu wa-Marekani. Anasema kuwa wanafunzi wake wamo katika program ya masomo ambayo watasoma Tanzania. Watakuwa Dar es Salaam na Iringa kwa wiki yapata tano. Katika mawasiliano ya ziada, mwalimu Lubua amesisitiza kuwa hiki kitabu muhimu sana hasa katika kufundishia

Nimeshiriki Amani Festival 2018

Image
Tarehe 5 nilikuwa Carlisle, Pennsylvania, kushiriki katika tamasha liitwalo Amani Festival, ambalo nilishiriki mara ya mwisho mwaka 2005. Nilipata fursa ya kuonyesha baadhi ya vitabu vyangu na kuongea na watu mbali mbali, akiwemo mama mmoja ambaye alifanya kazi Afrika Kusini kwa miaka mitatu. Nilipata pia fursa ya kuhojiwa na mwandishi wa gazeti la Carlisle liitwalo  The Sentinel . Kama kawaida, nilipanga vitabu mezani, na hicho kikawa kivutio. Watu wanafika hapo, na inakuwa ni fursa ya kuongea mambo mengi, kuhusu vitabu na yatokanayo. Huyu mama alipopita mezani pangu alinyooshea kidole kitabu cha Matengo Folktales akisema "I have read that book!" akimaanisha amesoma kitabu hicho. Nilishangaa, nikaanzisha mazungumzo naye. Aliniambia kuwa alinunua kitabu hiki na kusainiwa nami miaka iliyopita, nikajua kuwa ni yapata miaka kumi na tano iliyopita, ambapo nilishiriki tamasha hili. Aliniambia kuwa yeye na mumewe ni wa kanisa moja hapa ambalo lin

Wadau Niliokutana Nao Wikii Hii

Image
Katika siku saba zilizopita, nimekutana na wadau wengi wa vitabu vyangu.  Kwanza, nilipata barua pepe kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni m-Marekani anayefundisha ki-Ingereza Mwanza kwa kujitolea. Ameandika kuhusu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences : Nimemaliza kitabu chako kuhusu tofauti za tamaduni zetu na nilikifurahia sana. Ulinichekesha mara nyingi. Aidha ukanieleza mambo mengi. Aprili tarehe 28, niliongea na wanafunzi wa somo la Global Semester ambao watasafiri na kukaa sehemu mbali mbali za dunia, ikiwemo Arusha, Tanzania, ambako watakaa kwa mwezi moja. Profesa wao aliniomba nikawaeleze masuala ya tofauti za tamaduni. Yeye mwenyewe amesoma  Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Tarehe 28 Aprili, nilikuwa Rochester, Minnesota, kushiriki tamasha la kimataifa linaloandaliwa kila mwaka na Rochester International Association. Hapo nilikutana na hao ndugu wawili wanaoonekana pichani hapa juu. Huyu wa kushoto ni daktari katika  h

Madaktari Wanafundishia Kitabu Hiki

Image
Nilivyoandika kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, sikuwazia kingetumika kwa namna nyingi kama ilivyotokea baadaye. Kilichonishtua zaidi ni pale waalimu wa uuguzi wa chuo cha Gustavus Adolphus walipoamua kukitumia kufundishia, wakaanza, kila wanapofundisha kozi hiyo, kunialika kuongea na wanafunzi. Baada ya muda si mrefu, Dr. Randy Hurley  mwanzilishi na mhusika mkuu wa  na programu ya hospitali ya Ilula, mkoani Iringa, alinialika kuhutubia mkutano wa mwaka wa wadau wa hospitali hiyo. Ulikuwa ni mkutano wa kuchangisha fedha za kuendelezea programu. Hapo ndipo nikajua kuhusu programu ya kuelimisha wauguzi ambayo inafanyika Ilula, ikiwahusisha wa-Marekani na wa-Tanzania. Nilijua kuwa wanatumia kitabu changu, bali sikuwa na taarifa zaidi. Lakini siku chache zilizopita nimeona jinsi kitabu hicho kinavyotajwa katika  silabasi mpya ya kozi yao. Wanafunzi wanahimizwa kukisoma. Kwa kuwa mimi si mtaalam wa masuala ya uuguzi na matibabu, nilijiuliza masu

Mdau Amechagua Kitabu

Image
Jana nimeona taarifa iliyonigusa kwa namna ya pekee. Mdau ameweka mtandaoni picha inayoonekana kushoto, akiwa ameambatanisha ujumbe: "Decided to bring some required reading with me." yaani anasema ameamua kubeba vitabu muhimu vya kujisomea. Hakusema kama anasafiri, lakini ujumbe wake unaashiria hivyo. Niliguswa kuona kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ni kimojawapo alichochagua, nikaandika "I am humbled that you have my "Africans and Americans" book on your list," yaani "nimeishiwa nguvu kuona kuwa umetaja kitabu changu katika orodha yako." Jibu aliloandika ni "Yes! I'm learning a lot. It's funny too. Thanks for the enlightenment," yaani "Ndio! Ninajifunza mengi. Kitabu kinachekesha pia. Asante kwa uelimishaji." Nimeguswa kwa namna ya pekee kwa sababu mdau huyu, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto, ni mtu mwenye ushawishi katika jamii, kama nilivyowahi kuelezea katika blog

Tamasha la Kimataifa Rochester Lawadia

Image
Tarehe 28 Aprili,  Rochester International Association (RIA)  itafanya  tamasha la kimataifa . Tamasha hilo hufanyika kila mwaka. Nitashiriki nikiwa na  vitabu vyangu  na nitaongelea shughuli zangu kama mwalimu na  mtoa ushauri wa masuala ya tamaduni. Ninaona heshima kuwa mwanabodi wa bodi ya RIA, na kushiriki kupanga mipango na matukio yenye maana na umuhimu katika dunia ya leo ambayo inazidi kuwa kijiji.

Mialiko kwa Mwandishi wa Kitabu

Image
Kutokana na mawasiliano kutoka kwa waandishi chipukizi Tanzania ninafahamu kuwa hao ni miongoni mwa wasomaji wa blogu yangu hii ambamo ninaandika mara kwa mara kuhusu vitabu. Mbali na kuviongelea vitabu, nimekuwa nikiandika kuhusu uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu kutokana na uzoefu wangu. Leo ninapenda kuongelea kipengele cha mialiko kwa mwandishi wa kitabu, jadi ninayoiona hapa Marekani, mwandishi kualikwa kuzungumza sehemu mbali mbali baada ya kuchapisha kitabu. Mada hii nimeigusia kwa kiasi fulani katika blogu hii Hata hivyo, nimeona niongezee neno. Kama wewe ni mfuatiliaji wa blogu yangu hii, utakuwa unafahamu kuwa ninapata mialiko mara kwa mara kuongelea mada zinazohusiana na vitabu vyangu: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Suali ni je, kwa nini watu wanialike badala ya wao kusoma tu nilichoandika? Wananialika nikawasomee? Jibu ni hapana. Kinachowafanya wanialike ni kutambua kwao, baada ya kusoma kitabu, kwamba wana m

Taarifa Tatu Kuhusu Kitabu Changu

Image
Blogu hii ni mahali ambapo ninajiwekea kumbukumbu zangu, sambamba na mambo mengine. Jana na leo zimekuwa siku za pekee, kwani nimefikiwa na taarifa tatu kuhusu kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Jana jioni, nilikutana na bwana moja mwenye asili ya ki-Somali aliyejitambulisha kama kiongozi mojawapo wa shule za Minneapolis. Tulipotambulishwa, alianza kunielezea kuwa alishasoma kitabu changu, akagusia jambo mojawapo analolikumbuka kuhusu dhana ya uzuri wa maumbile yetu. Huo ulikuwa ni ujumbe moja kuhusu kitabu changu. Ujumbe mwingine nimepata leo kutoka Nairobi kwa muasisi na mkurugenzi wa taasisi iitwayo IIHT Tulifahamiana alipokuwa anafanya kazi jimboni Illinois hapa Marekani baada ya kuhitimu shahada ya uzamifu. Aliwahi kuendesha semina kwa washiriki yapata 100. Alikuwa ameagiza nakala za kitabu changu kwa washiriki wote wa semina na alinialika kuhutubia. Baada ya kupoteana kwa miaka yapata kumi, nilimtafuta mtandaoni. Nilimwandikia kumsalimia,